Liahona
Gamenti ya Ukuhani Mtakatifu
Septemba 2024


“Gamenti ya Ukuhani Mtakatifu,” Liahona, Sept. 2024.

Gamenti ya Ukuhani Mtakatifu

Kama sehemu ya endaumenti ya hekaluni, tumepewa ukumbusho mtakatifu wa kimwili wa maagano yetu —ishara ya Mwokozi Mwenyewe.

Adamu na Hawa wakitembea pamoja

Maelezo kutoka kwa Adamu na Hawa, na Douglas M. Fryer

Bila kujali maandalizi waliyopewa na hakikisho walilojaribu kulikumbuka, lazima ilikuwa mshtuko wa kushangaza kwa Adamu na Hawa kuacha Bustani yao ya kiparadiso ya Edeni na kuingia katika ulimwengu ulioanguka.

Kwa ufahamu wa dhati, waligundua kile ilichomaanisha kuachilia utulivu wao, maisha yasiyo na wasiwasi kwa ajili ya ulimwengu wa upinzani na jasho, miiba na huzuni—ikifuatiwa hatimaye na kitu kinachoitwa kifo. Hawangeweza kujua mwanzoni maana ya haya yote, lakini punde walijua kwamba kila siku inaweza kuleta maumivu mapya. Hakika, maumivu makali zaidi ya yote yalikuwa ni kutambua kwamba wangekabiliana na haya yote wakiwa wametenganishwa na Baba yao wa Mbinguni—“wamefungiwa nje ya uwepo wake,” Musa baadaye angeandika.

Kutokana na utengano huu na upweke katika ulimwengu wa baridi, wenye kuchosha, ilikuwa faraja iliyoje kwa Adamu na Hawa kukumbuka jambo moja: kwamba ahadi zilikuwa zimefanywa—ni kitu kitakatifu na cha milele kinachoitwa maagano. Walikuwa wameahidi kuwa watamtii Baba siku zote za maisha yao, na Yeye alikuwa ameahidi kumtoa Mwokozi, ambaye angepunguza maumivu yao na huzuni, kulipia makosa yao, na kuwarudisha salama kwenye uwepo Wake.

Lakini ni kwa jinsi gani watu hawa wangekumbuka kile walichoahidi? Ni kwa jinsi gani wangebaki na ufahamu wa hali yao ya hatari—ufahamu wakati wote, mchana na usiku?!

Ukumbusho wa Maagano Yao

Kwa ukumbusho kama huo Yeye aliwapa “mavazi ya ngozi.” Hii ilikuwa zawadi isiyo kifani na kwa wakati muafaka. Baada ya kula tunda lililokatazwa, Adamu na Hawa waliweza kufahamu mara moja kwamba walikuwa uchi. Kwanza, walijaribu kujifunika uchi wao kwa majani ya mtini. Kisha, wakiogopa kwamba haikutosha, walijaribu kujificha kutoka kwa Bwana. (Juhudi kama hiyo ya kipumbavu ilikuwa ushahidi kwamba maisha ya duniani yalikuwa yakiingia!) Kutoka wakati ule hadi sasa, Baba mwenye upendo amewaalika watoto Wake kuja Kwake, kutoka mafichoni. Na kama vile kwa mavazi ya ngozi wakati huo na mavazi mbalimbali ya nguo tangu wakati huo, Yeye kwa rehema Yake hajatuacha uchi lakini amewavisha watiifu katika “joho la haki,” ukumbusho wa ahadi na maagano yetu. “Gamenti hizi za wokovu” zinaashiria zawadi iliyo kuu zaidi ya zote, Upatanisho wa Yesu Kristo.

Gamenti ni Ishara ya Mwokozi

Sasa, fikra hii yote kuhusu Adamu na Hawa na maagano na mavazi, bila shaka, ni zaidi ya zoezi la kiakili tu. Si vigumu kufikiria jinsi Adamu na Hawa walivyojisikia, kwa sababu sisi pia tunakumbana na matatizo katika ulimwengu huu ulioanguka. Sisi pia tumetengwa kutoka kwenye uwepo wa Mungu, na tunajiweka mbali zaidi kila wakati tunapovunja sheria. Kama Adamu na Hawa, tumepewa Mwokozi huyo huyo, Yesu Kristo wa Nazareti, Alfa na Omega, Mwana wa Mungu aliye hai. Kama vile Adamu na Hawa, tumefanya maagano na Mungu. Na, kama sehemu ya endaumenti ya hekaluni, tumepewa ukumbusho mtakatifu wa kimwili wa maagano hayo—ishara ya Mwokozi Mwenyewe. Katika kipindi chetu cha maongozi ya Mungu inaitwa gamenti ya ukuhani mtakatifu.

Tunavaa gamenti ndani ya nguo zetu za nje. Majukumu yoyote niliyo nayo, kazi yoyote ninayofanya katika maisha, wajibu wowote wa maisha yangu ya kila siku yanahitaji, chini yake yote haya ni maagano yangu—daima na milele. Chini yake yote haya ni zile ahadi takatifu ambazo kwazo ninashikilia kwa dhati. Gamenti haijivuniwi au kuonyeshwa mbele ya ulimwengu, wala maagano yangu. Lakini ninaendelea kuyashikilia karibu nami—karibu kadiri ninavyoweza. Ni ya binafsi sana na matakatifu sana.

Katika kukumbuka maagano hayo, ahadi hizo za pande mbili, tunavaa gamenti maisha yetu yote. Desturi hii inaakisi tamanio letu la Mwokozi kuwa ushawishi endelevu katika maisha yetu. Ishara zingine pendwa ni za kipindi fulani pekee. Tunabatizwa mara moja katika maisha yetu. Tunapokea sakramenti mara moja kwa wiki. Tunahudhuria hekaluni kadiri hali zetu zinavyoruhusu. Lakini gamenti ya ukuhani mtakatifu ni tofauti: ishara hii tunaiheshimu kila siku mchana na usiku.

Na hivyo ndivyo maagano yalivyo—hayawekwi kando kwa urahisi au uzembe na hayabadilishwi ili kuendana na ufahari na mitindo ya kisasa ya jamii. Katika maisha ya mfuasi wa Yesu Kristo, njia za ulimwengu lazima zibadilishwe ili kuendana na maagano yetu, si vinginevyo.

Tunapovaa gamenti, tunakuwa, kama Urais wa Kwanza ulivyofundisha, tunavaa ishara takatifu ya Yesu Kristo. Kama ndiyo hivyo, kwa nini tutafute kisingizio cha kuvua alama hiyo? Kwa nini tujinyime sisi wenyewe ahadi ya nguvu, ulinzi, na rehema ambayo gamenti huwakilisha? Kinyume chake, wakati wowote tunapohitaji kuondoa gamenti hii kwa muda, tunapaswa kuwa na hamu ya kuirudisha tena, haraka iwezekanavyo, kwa sababu tunakumbuka vyote viwili ahadi na hatari zinazotoa maana kwa maagano yetu. Zaidi ya yote, tunakumbuka msalaba na kaburi tupu la Kristo.

Wengine wanaweza kusema, “Nina njia zingine za kumkumbuka Yesu.” Na ningejibu, hiyo inapendeza. Njia nyingi zaidi ni bora zaidi. Acha sote tufikirie njia nyingi kadiri tunavyoweza kushika ahadi yetu ya “daima kumkumbuka Yeye.” Lakini kwa kufanya hivyo, itakuwa ukosefu wa werevu kupuuza kwa makusudi ukumbusho ambao Bwana Mwenyewe aliutoa kwa endaumenti, gamenti ya ukuhani mtakatifu.

Yesu Kristo na injili Yake humaanisha kila kitu kwangu. Matumaini na matamanio yangu yote ya milele, kila kitu ninachoshikilia kwa upendo, kinamtegemea Yeye. Yeye ni “mwamba wa wokovu wangu,” njia yangu ya kufika kwa Baba yangu wa Mbinguni, njia yangu pekee ya kurudi kwenye kile nilichokuwa nacho na sasa ninataka kuwa nacho tena, pamoja na mengi zaidi. Zawadi Yake kwetu ni ya ukarimu zaidi ambayo nimewahi kupokea, ambayo ni ya ukarimu zaidi kuwahi kutolewa—iliyonunuliwa kama ilivyokuwa na mateso yasiyo na kikomo, iliyotolewa kwa idadi isiyo na mwisho, iliyotolewa kwa upendo usio na mwisho. Miiba na michongoma, uchungu na maumivu, huzuni na dhambi ya ulimwengu huu ulioanguka, vyote “vimemezwa katika Kristo.”

Kwa hiyo nimevaa gamenti ya ukuhani mtakatifu—kila mchana na usiku kwa namna sahihi tangu nilipopokea endaumenti miaka 64 iliyopita, katika umri wa miaka 19—kwa sababu ninampenda Yeye na kwa sababu ninahitaji ahadi zinazowakilishwa.

Je, kuna maswali kuhusu Uvaaji wa Gamenti?

Baadhi yenu mnaweza kuwa mnasoma makala hii mkitumaini nitajibu swali fulani kuhusu gamenti. Ungeweza kutumainia “Hivyo ndivyo asemavyo Bwana”—au hata “Hivi ndivyo asemavyo mtumishi Wake”—katika jambo lililo ndani ya moyo wako. Swali lako linaweza kutokana na hali binafsi inayohusiana na ajira, mazoezi, usafi, hali ya hewa, staha, vifaa vya usafi, au hata hali ya matibabu.

Baadhi ya majibu ya aina hii ya maswali yanaweza kupatikana katika temples.ChurchofJesusChrist.org na katika sehemu ya 38.5 ya Kitabu cha Maelezo ya Jumla. Wanafamilia na viongozi wanaoaminika wanaweza kutafutwa kwa ajili ya ushauri kuhusu jambo binafsi. Yapo, hata hivyo, maelekezo ya wazi kabisa yaliyotolewa katika ibada za mwanzo, na yupo milele na milele Baba yako wa Mbinguni, ambaye anakujua na kukupenda na anaelewa kila kitu kuhusu hali zako. Angefurahia kuona wewe unamuuliza Yeye maswali haya binafsi.

mnara wa Hekalu la St. George Utah

Picha ya mnara wa Hekalu la St. George Utah

Tafadhali msielewe vibaya. Unapotafuta mwongozo mtakatifu, Roho hatakupa msukumo wa kufanya tofauti na kufuata maelekezo yaliyopokelewa hekaluni na ushauri wa kinabii uliotolewa na Urais wa Kwanza katika kauli yao ya hivi karibuni. Baba mwenye upendo hatakusaidia kuhalalisha kufanya kidogo kuliko unavyoweza kuendana na viwango Vyake vya ibada na staha ambavyo vitakubariki sasa na milele. Lakini je, Yeye anaelewa maswali yako, na atakusaidia upokee baraka za kuheshimu gamenti na kushika maagano yako? Ndiyo! Je, unapaswa pia kushauriana na wataalamu wenye uwezo wa matibabu na afya pale inapohitajika? Bila shaka! Je, unapaswa kupuuza akili ya kawaida au kuangalia zaidi ya lengo? Ninaomba kwamba hutafanya hivyo.

Siwezi kujibu kila swali ulilo nalo. Siwezi hata kujibu kila swali nililo nalo. Lakini ninaweza, kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, kukuahidi msaada wa Mungu mwenye upendo, anayetafuta kila mafanikio na baraka, katika njia ambazo kwa sasa huwezi kuzivumilia au kuzitabiri, unaposhika maagano uliyofanya Naye.