Liahona
Nabii Hutuongoza kwa Yesu Kristo
Septemba 2024


“Nabii Hutuongoza kwa Yesu Kristo,” Liahona, Septemba 2024.

Nabii Hutuongoza kwa Yesu Kristo

Nabii anajua njia kwa sababu yeye anamjua Yesu Kristo, ambaye ni “njia, kweli, na uzima” (Yohana 14:6).

Kielelezo cha Mwokozi akiwa na kondoo upande wa nyuma

Kumtafuta yule Mmoja, na Liz Lemon Swindle, isinakiliwe

Siku moja nilikuwa ninakula chakula cha mchana katika mkahawa wa Jengo la Kanisa la Utawala pamoja na wenzangu watatu katika Sabini. Wakati tulipokuwa tukila, Rais Russell M. Nelson alikuja kwenye meza yetu akiwa na bakuli lake la supu na kusema, “Naomba nijiunge nanyi?”

“Bila shaka, Rais!,” sote tulisema. Ni nani hangependa kula chakula pamoja na nabii?

Wakati tukila, Rais Nelson alishiriki uzoefu mchache alioupata katika nchi nyingi alizotembelea na kuzungumza kuhusu watu waliomvutia. Alikuwa mpole sana, mwenye hekima, na ukarimu.

Tulipomaliza kula, nilimgeukia Rais Nelson na kusema, “Rais, sijui kama nitakuwa na fursa ya kuketi meza moja nawe muda wowote karibuni. Lakini jioni ya leo, ninaenda kumwona mke wangu na watoto na kuwaambia kwamba nilikula chakula cha mchana pamoja na nabii. Ninajua wataniuliza, ‘Amekuambia utuambie nini sisi?’ Rais, Ungependai nimwambie nini mke wangu na watoto?

Rais Nelson aliniangalia kwa dakika chache. Nilikuwa na hamu ya kusikia kile ambacho yeye angesema! “Nina maneno mawili kwa ajili yako,” alisema. “Iambie familia yako kwamba nimesema, ‘Zishikeni Amri.’”

Sisi sote tumeshasikia ushauri kutoka kwa Rais Nelson hapo awali, lakini katika muda huu, nilihisi ushuhuda binafsi wenye nguvu kwamba Rais Nelson kwa kweli alikuwa nabii. Nilimshukuru, na baadaye siku hiyo niliwaambia familia yangu kile kilichokuwa kimenitokea. Watoto wangu baadaye walitengeneza vibandiko vya “Zishikeni Amri” na kuviweka kwenye jokofu letu na vioo ili kutukumbusha kile Rais Nelson alichosema.

Tangu wakati huo, nimekuwa nikitafakari ushauri huu wa Rais Nelson. Tunaposhika amri, tunaonyesha upendo wetu kwa ajili ya Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tunasogea karibu na Wao na kukaa katika upendo Wao. (Ona Yohana 14:21; 15:10.)

Uzoefu huu na nabii umenithibitishia ukweli wa kiroho wa kina na muhimu. Katika darasa la Watoto tunaimba, “Mfuate nabii, yeye anaijua njia.” Yeye anaijua njia! Nabii anaijua njia kwa sababu yeye anamjua Mwokozi, ambaye ndiye “njia, kweli, na uzima” (Yohana 14:6). Tunapomfuata nabii, tunaongozwa kwa Yesu Kristo.

Wajibu Mtakatifu wa Manabii

Bwana ametoa wajibu muhimu na mtakatifu kwa manabii kote hapo kale na katika siku yetu. Tunasoma katika maandiko kwamba “hakika Bwana Mungu hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake” (Tafsiri ya Joseph Smith, Amosi 3:7 [katika Amosi 3:7, tanbihi a]).

Katika kitabu cha Ezekieli, tunajifunza zaidi kuhusu kile kinachohitajika kutoka kwa manabii. Bwana alimwambia nabii Ezekieli “Nimekuweka [kama] mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.” (Ezekieli 33:7).

Manabii, kama walinzi juu ya mnara, wana jukumu maalumu la kuwa mdomo wa Bwana na kutangaza kile Yeye alichokifunua kwao. Bwana anahitaji manabii Wake kuwa wanaume wa imani , wanaume wa uadilifu, na wanaume ambao ni shupavu.

kielelezo cha Samweli Mlamani juu ya ukuta

Kielelezo cha Samweli Mlamani na Dan Burr

Samweli Mlamani, kwa mfano, alionyesha msimamo wake kamili kwa Yesu Kristo wakati aliposimama juu ya ukuta na kutangaza kwa Wanefi mambo ambayo Bwana alikuwa ameyaweka ndani ya moyo wake (ona Helamani 13:4).

“Na tazama, malaika wa Bwana amenitangazia,” Samweli alisema, “na alileta habari njema kwa nafsi yangu. Na tazama, nilitumwa kwenu niwatangazie pia, ili mpate habari njema; lakini tazama mmekataa kunisikiliza” (Helamani 13:7).

Ni ajabu kwangu kwamba Samweli kwa ukakamavu alishuhudia juu ya ukweli—hata wakati ambapo Wanefi “walimtupia mawe … na … walimshambulia kwa mishale wakati alipokuwa amesimama juu ya ukuta” (Helamani 16:2). Tunaona ushupavu huu kwa manabii, waonaji, na wafunuzi leo.

Kuufanya Ulimwengu kuwa Mahali Bora

Sio muda mrefu, nilikutana na wenza wanandoa wakati wa mkutano wa kigingi katika Nashville, Tennessee, Marekani. Mke amekuwa muumini wa Kanisa maisha yake yote. Mume hakuwa muumini wa Kanisa.

Walikuja kwangu, na yule mume alisema, “Mimi niko tayari kubatizwa.”

Nilifurahia kusikia hilo! Nilimwuliza , “Ni nini kilichobadilika?”

Aliniambia, “Niliposikia ujumbe wa Rais Nelson katika mkutano mkuu, ulinigusa sana. Ndipo nilipojua kwamba yeye alikuwa nabii. Nilipata ushuhuda, na sasa niko tayari kubatizwa.”

Pia namjua mwanamke huko Cape Coast, Ghana, ambaye kwa njia fulani alisikiliza mkutano mkuu. Kamwe hakuwahi kusikia kuhusu Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, lakini akawa ameganda kwa kile alichokuwa ameona na kusikia kutoka kwa manabii, waonaji, na wafunuzi. Baadaye, alilitafuta Kanisa. Alilipata jengo la kanisa na kukutana na wamisionari. Mwishowe, alibatizwa. Hivi karibuni, alinitumia picha zake akiwa hekaluni kupokea endaumenti yake.

Mifano hii miwili inaonyesha jinsi gani ulivyo na nguvu ujumbe wa nabii kwa ulimwengu! Kama wote wangetii ujumbe huu, ulimwengu ungekuwa na amani zaidi. Sisi sote tungefokasi kwenye kile kilicho muhimu zaidi, ikijumuisha kukuza uhusiano na Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, na kujenga familia imara, za milele. Tungekuwa watu bora zaidi kwa sababu tungeshika amri zile kuu mbili za kumpenda Mungu na kumpenda jirani yetu (ona Mathayo 22:37–39). Tungeisogeza mbele Sayuni, jamii ambayo upendo, haki, na maelewano yanashinda, vikiakisi roho ya ufuasi. (ona Mafundisho na Maagano 82:14).

Tunapomfuata nabii, tunaweza kujiamini kwamba tunafanya kile ambacho Mungu angependa tufanye kwa sababu nabii humfuata—na hutusaidia sisi tumfuate—Yesu Kristo. Kwa sababu ya Yesu Kristo, kila kitu maishani kinakuwa cha maana. Tunaweza kuhisi furaha bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu.” Kwa kumfuata nabii, tunaweza kwa kweli kuufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri.

Tafuta Baraka Zilizoahidiwa

Wakati Watakatifu walipofukuzwa kutoka Kirtland, Ohio, Urais wa Kwanza ulimkabidhi mamlaka Oliver Granger kuuza mali za Watakatifu na kulipa madeni ya Kanisa. Oliver, mtu wa kawaida ambaye karibu awe kipofu kwa sababu ya kupigwa na baridi kali, alikubali kazi hii yenye changamoto kwa sababu Nabii Joseph Smith na viongozi wengine walikuwa wamemuomba yeye. Oliver alivumilia magumu mengi, na Bwana alithamini dhabihu yake na juhudi zake.

“Ninamkumbuka mtumishi wangu Oliver Granger,” Bwana alisema. “Tazama, amini ninamwambia yeye kwamba jina lake litakumbukwa katika kumbukumbu takatifu kutoka kizazi hadi kizazi, milele na milele. …

“… Na atakapo anguka atainuka tena, kwani dhabihu yake itakuwa takatifu zaidi kwangu Mimi kuliko mafanikio yake” (Mafundisho na Maagano 117:12–13).

Oliver na mkewe, Lydia, walimuunga mkono nabii, na Bwana alitambua kwamba Oliver alikuwa amefanya vyema kadiri alivyoweza hata kama hakufanikiwa siku zote. Bwana aliangazia thamani ya juhudi zake kuliko mafanikio yake.

Kama mmisionari na hata sasa, sikumbuki kusikia zaidi kuhusu Oliver Granger, lakini jina lake limetajwa katika maandiko kwa sababu alitii maelekezo ya nabii na kupokea baraka zilizo ahidiwa—jina lake ndilo linasikika katika ukumbusho mtakatifu. Tunajifunza kutoka kwa Oliver Granger kwamba hata ingawa maelekezo huja kutoka kwa chanzo kitakatifu (kupitia manabii), hayatoi dhamana ya njia rahisi isiyokuwa na changamoto, bali ahadi ni za uhakika (ona Alma 37:17).

Je! maisha yetu yangekuwaje bila manabii? Nabii aliye hai na Rais wa Kanisa huwakilisha mstari wa moja kwa moja wa mawasiliano kutoka kwa Mungu hadi kwa watu Wake na ndiye mtu wa pekee duniani ambaye hupokea ufunuo wa kuongoza Kanisa lote. Pia hutoa ufunuo endelevu kutoka kwa Mungu ili kutusaidia sisi kuongoza maisha yetu kwenye changamoto za wakati wetu. Kwa kusikiliza ushauri wa nabii, tunaweza kupata amani, shangwe, na mwelekeo katika maisha yetu pale tunapojitahidi kuwa zaidi kama Yesu Kristo. (Ona Mafundisho na Maagano 21:4–6.)

Acha tukumbatie mafundisho na mfano wa manabii wa siku ya leo, tukijua kwamba wao ni vyombo katika mikono ya Mungu vya kutuongoza kwenye baraka za milele. Ninawapenda na kusali kwa ajili yao. Nina shukrani kujua kwamba wao wanapata mwongozo na wanasaidia kutuongoza sisi na familia zetu kwa Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Muhtasari

  1. “Follow the Prophet,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 111–11

  2. Ona Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” Liahona, Mei 2023, 98–101.

  3. Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona,, Nov. 2016, 82.

  4. Ona Boyd K. Packer, “Mdogo wa Hawa,” Liahona,, Nov. 2004, 86.