Liahona
Njia ya uanafunzi
Septemba 2024


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Njia ya uanafunzi

Fokasi ya urais wa Eneo la Kati la Afrika ni kutuhimiza tuwe wanafunzi wazuri zaidi wa Yesu Kristo kadiri tunavyofanya yote yaliyo ndani ya uwezo wetu kuishi kulingana na maagano tuliyoyafanya na Baba yetu wa Mbinguni kwenye ubatizo na ndani ya Hekalu.Ibada hizi zinatufunga kwa Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo.

Nabii Mormoni katika Kitabu cha Mormoni alijifafanua kama Mwanafunzi wa Kristo (3 Nefi 5:13). Neno mwanafunzi linatokana na neno la Kilatini lenye maana anayejifunza. Mwanafunzi wa Yesu Kristo ni yule ambaye amefanya agano la kujichukulia juu yake jina la Yesu Kristo, kumkumbuka daima na kushika amri Zake. Mwanafunzi ni mtu anayejifunza na kujaribu kila siku kuwa zaidi kama Mwokozi Yesu Kristo. Mwanafunzi ni mtu anayejaribu kujifunza, kufikiri, kuhisi, na kutenda kama vile Mwokozi Yesu Kristo anavyofanya. Moja ya nyimbo zangu pendwa za watoto ni “Ninajaribu kuwa kama Yesu” (Nyimbo za Dini 78, Kitabu cha Nyimbo za Watoto) kwa sababu maneno hunikumbusha kile inachomaanisha kuwa mwanafunzi.

Sitasahau kamwe somo ambalo mke wangu kipenzi Dada Mutombo alinifunza mnamo siku ya kwanza ya ndoa yetu. Ninaikumbuka Jumapili ile kama vile ilikuwa jana. Hatukuwa na chakula nyumbani kwetu na hakukuwa na pesa ya kununua chakula. Kama mume mpya niliyeoa, hakika nilitaka kumpa mahitaji mke wangu mpya, lakini sikuwa na rasilimali za kutimiza hilo. Nilijihisi mpweke.

Nilimtazama mke wangu akiwa amelala juu ya godoro ambalo tulikuwa tumeliweka sakafuni kwa sababu hatukuwa na pesa ya kununua kitanda. Alikuwa amechoka na mwenye njaa. Niliamua kumtembelea rafiki yangu mwema ili kutafuta suluhisho la jaribu langu. Nilimwacha mke wangu ndani ya chumba chetu kidogo chenye mita mbili za mraba na kwenda kumwona rafiki yangu. Aliniambia kwamba hakuwa na pesa za kunisaidia lakini alinipa dola moja ya kutumia kwenye usafiri wa kunifikisha nyumbani. Niliona hili kama jibu la sala yangu ya dhati kwa Baba yangu wa Mbinguni, nikiomba msaada na uungaji wake mkono. Niliamua kutembea kwenda nyumbani na kutumia dola kununua chakula kwa ajili ya mke wangu kwa sababu hiyo ndiyo ilikuwa pesa pekee niliyokuwa nayo.

Nikiwa njiani kurudi nyumbani, nilitumia dola kununua kipande kidogo cha nyama na mkate na kuviweka ndani ya mfuko mweusi wa plastiki. Nilifurahi kwamba sasa nilikuwa na chakula cha kumpa mke wangu na niliharakisha kwenda nyumbani. Ilikuwa baada ya saa 3:00 usiku wakati nilipofika nyumbani, na kipenzi changu Nathalie alikuwa amechoka, amenyongonyea, na mwenye njaa, na pengine akijiuliza kuhusu siku za usoni. Je, unaweza kupata taswira ya kwenda nyumbani bila chakula kwenye siku yako ya kwanza ya maisha ya ndoa? Nilipofika nyumbani, kwa ujasiri nilimpa mke wangu chakula, nikisema, “kipenzi, nimepata chakula kiasi kwa ajili yako, tafadhali amka .“Aliamka na kuchukua mfuko wa plastiki na kuona kipande cha nyama na mkate. Aliuliza, “umepata wapi pesa ya kununua chakula hiki? Nilimwambia.

Alinitazama na kuuliza swali ambalo sikulitarajia. “Je, umelipa zaka kwenye dola moja uliyopokea?” Nilijibu, “Nathalie, hii ni dola moja tu, unadhani tunapaswa kulipa zaka kwenye kiasi hicho?” Alichukua kipande cha nyama na mkate nilichomnunulia, akakirudisha ndani ya mfuko wa plastiki na kusema kwamba asingekula mkate wa mwanamume ambaye hakumbuki agano lake na Mungu. Ninalia wakati ninapokumbuka uzoefu huu. Nilitubu haraka na kumwahidi mke wangu kwamba kamwe, kamwe nisingerudia kufanya uchaguzi huo mbaya. Alinifunza kile inachomaanisha kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo ambaye anatunza maagano yake na Mungu. Tangu wakati huo nimepata shangwe kuu katika kulipa zaka kamili, kwa uaminifu. Kama vile Rais Nelson alivyosema Kanisa halikuwa na tofauti yoyote kwa sababu nililipa zaka kamili, hata hivyo kuwa mlipa zaka kamili kulinibadilisha kadiri imani yangu katika Mwokozi wangu Yesu Kristo ilivyoongezeka.

Kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo huleta shangwe na amani licha ya changamoto za safari hii ya maisha ya duniani. Ni kuhusu kutoa vyote na pasipo kuacha kitu. Kutoa vyote haimaanishi kwamba yote daima yatakuwa uzoefu wenye mafanikio, bali inamaanisha kwamba tutapata shangwe ambayo ulimwengu hauwezi kuitoa. Shangwe inadumu na inaweza kupatikana kwenye juhudi zetu za kila siku za kukubaliwa na Bwana (M&M 52:15).

Siku za mwanzo za Kanisa, wakati Watakatifu walipofukuzwa kutoka Kirtland, Ohio (Marekani) Oliver Granger alibakizwa nyuma ili auze mali zao zote kwa bei ndogo kadiri ambavyo angeweza. Hakukuwa na uwezekano mkubwa kwamba angefanikiwa, na hakika, hakufanikiwa. Jukumu alilopewa na Urais wa Kwanza wa Kanisa katika kipindi hicho lilikuwa gumu, kama si lisilowezekana. Lakini Bwana alimpongeza kwa juhudi zake ambazo hazikuwa na mafanikio, akisema kumhusu:

“Ninamkumbuka mtumishi wangu Oliver Granger; tazama, amini ninamwambia yeye kwamba jina lake litakumbukwa kuwa takatifu kutoka kizazi hadi kizazi, milele na milele, asema Bwana” (M&M 117:12). Kile kilicho muhimu zaidi kwa Bwana si mafanikio yetu bali dhabihu na juhudi zetu kadiri tunavyoendelea kujaribu kuwa bora zaidi na kufanya vizuri zaidi (M&M 97:8–9).

Kama vile baba wa Mfalme Lamoni ndani ya Kitabu cha Mormoni, ambaye aliyahofia maisha yake wakati Amoni alipoweka upanga wake kwenye shingo yake, alisema, “Ukiniokoa nitakupa chochote utakachoniomba, hata kama ni nusu ya ufalme” (Alma 20:23). Lakini, baadaye baada ya kupokea na kuelewa baraka za upatanisho wa Yesu Kristo na injili Yake, baraka ya kuwa na Mwokozi, alitangaza, “Nitafanya nini ili nipate uzima wa milele ambao umeuzungumzia? Ndio, nitafanya nini ili nizaliwe kwa Mungu, ili hii roho mbovu ing’olewe nje ya mwili wangu, na nipokee Roho yake, ili niwe ze kujazwa na shangwe, ili nisitupiliwe nje siku ya mwisho? Tazama, nitatoa umiliki wangu wote, ndio, nitaacha ufalme wangu, ili nipokee hii shangwe kuu” (Alma 22:15).

Kama wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo hebu tuwe radhi kutoa vyote Kwake kama Yeye alivyotoa vyote kwetu na kwa ajili yetu. Ninajua kwamba yu hai na ni Mwokozi na Mkombozi wangu. Ninajua kwamba upatanisho Wake, huruma Zake nyororo, neema Yake, na tamanio Lake ni kutusaidia tupokee shangwe ya milele. Ninawaalikeni kaka zangu, dada zangu, na rafiki zangu wapendwa kwamba bila kujali chochote, mchague Yesu Kristo katika maisha yako na nyumbani kwenu, ili kwamba sisi sote na watoto wetu tujue ni chanzo kipi tunaweza kutegemea kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu.

Katika jina la Yesu Kristo, Amina.

Tanbihi

  1. Ona “Ninajaribu Kuwa Kama Yesu,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 78–79.

  2. Ona Russell M. Nelson, “Fikiria Mbinguni!” Liahona, Nov. 2023, 119.