Liahona
Muunganiko wa “Bonjour” kwenye Hekalu la Kinshasa
Septemba 2024


Ujumbe wa Urais wa Eneo

Muunganiko wa “Bonjour” kwenye Hekalu la Kinshasa

Jinsi Mfuko wa Usaidizi wa Patroni wa Hekalu Unavyobariki Maisha

Wakati mwingine vitu vizuri hutokea ambavyo haviwezi tu kuelezewa na kuishia kusema, “mkono wa Bwana ulikuwepo.” Hiyo ndiyo njia pekee ya kuelezea kile kilichotokea katika Hekalu la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mnamo 14 Machi 2024.

“Utukufu kwa Mungu!” alisema Dada Harlaine Odia kwa machozi ya furaha wakati Dada Janeen Redd alipomwonyesha picha hii na kumwambia hadithi ya kile klichotokea siku hiyo:

Dada Harlaine na Dada Redd wanaona picha hii kama ushahidi kwamba mkono wa Bwana unaongoza kazi ambayo wote huifanya katika ofisi za Kanisa za Eneo la Kati la Afrika huko Nairobi, Kenya. Dada Harlaine ni Meneja Mipango wa Eneo. Dada Redd ni mmisionary mwandamizi ambaye anafanya kazi na Dada Harlaine na timu ya wamisionari wawili wadada wengine waandamizi katika Ofisi za Eneo. Timu hii ya wadada hufanya kazi ya kutoa manufaa ya Mfuko wa Usaidizi wa Patroni wa Hekalu (GTPAF) kwa waumini wa Kanisa katika Eneo la Kati la Afrika. Mfuko hutoa usaidizi wa kifedha kwa ajili ya safari, chakula na makazi kwa waumini ili kwamba wapokee baraka zao za hekaluni katika mahekalu yaliyo mbali na makazi yao. Kwa sasa, hekalu linalofanya kazi katika Eneo la Kati la Afrika liko Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mahekalu ya ziada yako katika ujenzi huko Lubumbashi, DRC, na Nairobi, Kenya. Mengine yametangazwa kwa ajili ya ujenzi huko Kananga, DRC; Mbuji-Mayi, DRC na Brazzaville, Jamhuri ya Kongo.

Hivyo, nani yuko katika picha na kwa nini ni muhimu kwa wadada hawa wawili?

Picha inaonyesha wanandoa wapya Nicole Bukasa na Ezi Kalenda wamesimama nje ya Hekalu la Kinshasa kwa shangwe wakisubiri kuunganishwa kwao hekaluni siku hiyo. Walisafiri kwenda Hekaluni pamoja na marafiki wao wanandoa wapya Tresor Tshilombo na mke wake Naomie Mukadi kutoka mji wa mbali wa Lupata, DRC—umbali wa kilometa 1470 (maili 915) kutoka Hekaluni—mwendo ambao wameusafiri mwendo kwa basi la masaa manne mpaka uwanja wa ndege huko Mbuji-Mayi na kisha kwa ndege toka Mbuji-Mayi hadi Kinshasa.

Dada Redd alisafiri hadi Kinshasa kutokea Nairobi pamoja na mumewe, Mzee Jeffrey Redd (ambaye anahudumu kama Mshauri Mwenza wa Sheria katika Ofisi ya Ushauri wa Jumla kwa ajili ya Eneo la Kati la Afrika) pamoja na David Stanford (Mshauri wa Sheria wa Eneo) na mkewe Marie-Laure kwa ajili ya vikao. Wakiwa Kinshasa walipanga kuabudu Hekaluni. Mara akina Redd na akina Stanford walipowasili Hekaluni, salamu frahisi ya “bonjour” ikageuka kuwa mazungumzo ambapo akina Redd na akina Stanford walialikwa kuwa kama mashahidi kwa ajili ya uunganishwaji wa wanandoa hawa wawili wapya.

Ezi, Tresor na Naomie walihudumu kama wamisionari huko Misioni ya Kinshasa DRC West chini ya Rais wa Misioni Francois M. Mukubu. Rais Mukubu sasa ni Rais wa Hekalu la Kinshasa, na ni yeye ndiye aliyefanya ibada ya kuunganishwa ya wanandoa wawili.

Baada ya maswali machache, Dada Redd aligundua kwamba ilikuwa ni timu yake huko Nairobi ambayo imeshughulikia maombi ya wanandoa hawa wawili ya kushiriki katika Mfuko wa usaidizi wa Patroni wa Hekalu wiki chache tu kabla ya kukutana nao ghafla katika Hekalu la Kinshasa. Hakuna anayeijua hadithi hii anaamini kwamba ni kwa bahati tu kwamba akina Redd na akina Stanford walitembea kwenye viwanja vya hekalu katika wakati sahihi wa kuleta muunganiko wa wanandoa ambao awali hawakujulikana kwao, muunganiko ambao ulianzia na salamu rahisi ya “bonjour” iliyofanyika nje ya Hekalu.

Mkono wa Bwana unaongoza kazi Yake. Waumini wengi wa Kanisa watabarikiwa kupokea baraka za hekaluni na kufanya maagano pamoja na Mungu katika Nyumba Yake Takatifu kama wanufaika wa Mfuko wa Usaidizi wa Patroni wa Hekalu.

Na … mtoto wa Nicole na Ezi, ambaye anatarajiwa kuzaliwa mwezi Mei, atazaliwa ndani ya agano.

Kama Dada Harlaine alivyoshangaa, alipoona picha “Utukufu kwa Mungu!”

Waumini wanaotamani kujifunza zaidi kuhusu Mfuko wa Msaada wa Patronni wa Hekalu wanaweza kuwasiliana na Askofu wao au Rais wa Tawi.