Liahona
Kukusanyika kwa Watakatifu Nchini Rwanda
Septemba 2024


Kurasa za Karibu

Kukusanyika kwa Watakatifu Nchini Rwanda

Mnamo 2002 Nelson na Sapna Samuel walihama kutoka Bangalore, India, kwenda Kigali, Rwanda. Japokuwa kulikuwa na waumini wachache wa kumbukumbu wakiishi Rwanda mnamo miaka ya 1980 na 1990, akina Samwel hawakumpata mtu mwingine yeyote wa kuabudu nao wakati walipowasili mara ya kwanza. Walifanya mikutano wakiwa peke yao kwa miaka kadhaa kabla ya Watakatifu wengine wa Siku za Mwisho kuja Rwanda.

Mwaka 2007 Nelson na Sapna walitoa nyumba yao kama mahala pa kukutania kwa ajili ya kundi dogo lakini lililokuwa likiongezeka la Watakatifu huko Kigali. Mwanzoni, mikutano ilikuwa na watu wachache kiasi kwamba mtu aliyebariki sakramenti angeweza kimyakimya kumtaja kila mtu ambaye angeshiriki sakramenti wakati akimega mkate. Mtoto mchanga wa Samwel akijumuishwa kwenye idadi, kulikuwa na waumini 10 katika kundi hilo dogo. Jean Pierre Ndikumana, Mtakatifu wa Siku za Mwisho Mkongo aliyekuwa akifanya kazi kama daktari huko Butare, alisafiri kwa masaa manne hadi nane ndani ya basi kila wiki ili kufika kwenye huduma. Muumini mwingine Mkongo aliyeitwa Justin pia alihudhuria. Eric na Kathy Hyde, wanandoa wa Marekani, walikuwa na binti na mwana ambao walikuwa vijana pekee Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kundi. Na Fabien Hatangimbabazi, ambaye alijiunga na Kanisa wakati akizuru Marekani na ambaye alikuwa Mrwanda wa kwanza kwenye kundi, alihudumu kwenye mahakama kuu ya nchi.

Japokuwa zuio juu ya usajili wa makanisa mapya nchini Rwanda lilikuwa kikwazo cha kuanzisha rasmi kazi ya umisionari au kupata nyumba ya mikutano, Watakatifu walitamani kuona tawi likianzishwa. Kadiri walivyoendelea kukutana, Bwana aliwakusanya Watakatifu wengine wenye asili ya Rwanda kuja Kigali wakitokea maeneo tofauti tofauti ya dunia.

Yvonne Martin, aliyejiunga na Kanisa huko Scotland, aliwasili mnamo Novemba 2007 na kuanza kushiriki injili na rafiki zake. Jean Marie na Agathe Rumanyika, ambao walikutana na wamisionari huko Missouri kabla ya mambo ya biashara kuwarudisha Kigali, walifika wakati muafaka wa kujitolea nyumba yao na, baadaye, hoteli yao ili kufanyia mikutano wakati kundi lilipokuwa kubwa kuzidi nyumba ya Samwel. Ruth Opar, mmisionari aliyerejea, na Rais wa zamani wa Muungano wa Usaidizi ambaye alijiunga na Kanisa nchini Kenya, alirejea ili kuona ikiwa Kigali ni mahala pazuri kwa ajili ya familia yake kuishi. Tawi la Kigali liliundwa mnamo Machi 16, 2008. Baadaye mwezi huohuo Joshua Opar—mume wa Ruth aliyewahi kuwa askofu—alihamia kwenye tawi akiwa na watoto wao.

Agosti ya mwaka huo waumini wa tawi walisafiri hadi Ziwa Muhazi, takribani saa moja nje ya Kigali, ili kufanya ubatizo wa kwanza nchini. Rafiki wa Yvonne Martin aliyeitwa Damascene Ruhinyura na Mercy Opar, binti wa Ruth na Joshua, walikuwa watu wa kwanza kubatizwa nchini.

Kwa miaka miwili iliyofuatia, tawi dogo lilizidiwa na hitaji la kufundisha na kubatiza. Punde walikuwa wakibatiza waumini wapya 10 kila mwezi. Kati ya hao waliobatizwa walikuwa John Hakizimana, Eric Habiyaremye, Dady Paul Hakizimana, Vincent Munanira, na wengine ambao kila mmoja walipoteza familia zao kwenye vurugu za kikabila za mapema miaka ya 1990 na walikuwa wameishi mitaani au kuhama hama kutoka vituo vya watoto yatima kwa zaidi ya muongo mmoja.

Wavulana hawa waliunda msingi wa akidi ya kwanza ya Ukuhani wa Haruni katika Tawi la Kigali. “Kadiri wavulana hawa walivyojifunza kuwahudumia kaka zao na dada zao,” Rais wa Tawi Eric Hyde alisema, “walijikuta kwamba wanakuwa sehemu ya familia ambayo iliwapenda, na walipata makazi.”

Mwaka 2010 wamisionari wa kwanza waliwasili Rwanda. Brent na Cheri Andrus kutoka Park City, Utah, walianza huduma ya umisionari mnamo Februari mwaka huo. Jukumu lao lilikuwa kuunda mpango wa hatua ya huduma za kibinadamu kwa ajili ya nchi na vilevile kulisaidia tawi dogo lililokuwepo. Kwa makadirio watu 40-50 walikuwa wakikutana eneo la chini la Hoteli ya Okapi iliyomilikiwa na akina Rumanyika.

Kulikuwa na idadi kubwa ya watu ambao hawajabatizwa wakihudhuria huduma za Jumapili, watu ambao walikuwa marafiki na familia za waumini. Mzee na Dada Andrus mara moja walianza kufundisha masomo ya umisionari kabla na baada ya huduma za Jumapili. Mnamo mwezi Juni, ubatizo wa watu kumi na wawili ulifanywa katika nyumba mpya ya mikutano ya tawi huko Kimihurura. Mwezi huo huo akina Hyde waliondoka Rwanda na Joshua Opar aliitwa kuwa rais wa tawi.

Mwaka 2011 mmisionari wa kwanza kutoka Rwanda, Jackson Ndayambaje, aliitwa kuhudumu katika Misioni ya Johannesburg. Hatua nyingine muhimu katika ukuaji wa Kanisa katika miaka hiyo ya mwanzo ilikuwa uanzishwaji wa kazi ya tafsiri ya Kitabu cha Mormoni. Wamisionari wa kwanza vijana hawakuwasili nchini Rwanda hadi mwaka 2012. Katika mwaka huo, tawi la pili la Kigali liliundwa. Tawi la tatu lilianzishwa mwaka 2013.