Liahona
Hadithi Yangu ya Uongofu na Ushuhuda
Septemba 2024


Makala

Hadithi Yangu ya Uongofu na Ushuhuda

Jina langu ni Miamo Siedjouwa Vinick Christian, ninaishi Douala (Cameroon) na mimi ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Nilijiunga na Kanisa nilipokuwa na umri wa miaka 12 na wakati huo niliishi na mama yangu, Kameni Lauris na dada yangu mdogo Awasiri Grâce. Tulikuwa tukihudhuria kanisa la Kipentekoste ambalo lilikuwa mbali sana na nyumbani kwetu. Hii ilifanya iwe vigumu kwetu sisi kuhudhuria huko kila Jumapili kutokana na kukosa pesa ya usafiri.

Mama yangu alikuwa mtu anayempenda Bwana kwa dhati. Wakati ilipokuwa vigumu kwa sisi sote kuhudhuria kwa pamoja, yeye angeniambia mimi niende pamoja na dada yangu mdogo kwenye kanisa jingine karibu na nyumbani kwetu. Tulipokuwa tukitoka hizo Jumapili, ningezurura nje kwenye kanisa la karibu huku nikikadiria muda atakaoutumia mama yangu kuondoka nyumbani! Kisha ningerejea nyumbani bila kuhudhuria kanisa la karibu. Enzi hizo sikupenda dini kabisa kwa sababu sikuelewa mengi kuihusu.

Rafiki wa mama yangu, ambaye alimlea dada yangu mdogo wakati mama yangu akiwa kazini, alitutambulisha kwa Mzee Holland na Mzee Rambeleson.Wamisionari hawa wawili walikuja kututembelea nyumbani. Bado ninakumbuka mara ya kwanza kuhudhuria mkutano wa sakramenti na kuwaona wavulana kama mimi wakishiriki katika kupitisha sakramenti. Baadaye, nilihudhuria Darasa la Watoto na kuona ni wingi wa shangwe kiasi gani watoto wanayo. Nilihisi hisia ya kuwa sehemu yake na kujua kwamba kamwe sitakosa kuhudhuria Jumapili.

Nilipobatizwa, nilitamani mara moja kutoka Darasa la Watoto kwenda Darasa la Wavulana na kuanza majukumu yangu ya kikuhani. Nilianza kumjua vyema Baba yangu wa Mbinguni na utambulisho wangu. Nilisaidia kusafisha jengo siku za Jumamosi na kufika mapema sana siku za Jumapili, wakati mwingine hata kabla milango ya jengo kufunguliwa. Nilipozidi kuwa mkubwa, hamu yangu ya kutumikia misioni iliongezeka pia. Kupitia Seminari na Chuo, niliweza kujiandaa kwa ajili ya misioni yangu na kupata fursa ya kutumikia katika Misioni ya DRC Kinshasa West kuanzia 2021 mpaka 2023. Nina shukrani kwa injili iliyorejeshwa na kwa shangwe iliyoniletea mimi na familia yangu.

Ninajua kwamba Kristo yu hai, na kwamba yuko mkono wa kuume wa Baba yetu wa Mbinguni, kwamba anatujua na kutupenda. Ninajua kwamba Kitabu cha Mormoni ni Ushuhuda Mwingine wa Yesu kristo. Ninajua kwamba tunaongozwa na nabii aliye hai anayepokea ufunuo kutoka kwa Mungu. Katika jina la Yesu Kristo. Amina.