Liahona
Ni kwa Jinsi Gani Ninaweza Kuimarisha Ushuhuda Wangu juu ya Nabii?
Septemba 2024


Ni kwa Jinsi Gani Ninaweza Kuimarisha Ushuhuda Wangu juu ya Nabii?,” Liahona, 2024.

Njoo, Unifuate

Helamani 7–16

Ni kwa Jinsi Gani Ninaweza Kuimarisha Ushuhuda Wangu juu ya Nabii?

Mkutano mkuu unaweza kutusaidia kuimarisha shuhuda zetu juu ya manabii walio hai.

Rais Russell M. Nelson akizungumza kwenye mimbari.

Katika kitabu cha Helamani, nabii Samweli Mlamani anashuhudia juu ya Yesu Kristo na anatoa maonyo na mialiko kwa Wanefi (ona Helamani 13-14). Katika siku yetu sisi pia tuna nafasi ya kusikiliza maonyo kwa wakati unaofaa kutoka kwa nabii na viongozi wetu wengine. Kutii mialiko yao hutusaida tufuate njia ya agano.

Mkutano mkuu ni nafasi nzuri ya kusikia maneno ya hivi karibuni kutoka kwa viongozi wenye mwongozo wa kiungu na kusogea karibu na Yesu Kristo. Hapa kuna baadhi ya njia unazoweza kuzingatia kutumia mkutano mkuu ili kuimarisha ushuhuda wako juu ya manabii walio hai.

  1. Kabla ya mkutano mkuu, kwa sala tafakari kwa nini kuwa na nabii ni muhimu kwako. Fikiria kusali ili kupokea uthibitisho kutoka kwa Roho kwamba Rais wa Kanisa wa sasa ni nabii, mwonaji, na mfunuzi wa Mungu aliye duniani leo. “Kujua kupitia ufunuo kwamba kuna nabii aliye hai duniani hubadililisha kila kitu.”

  2. Tafiti inamaanisha nini kumuunga mkono na kumkubali nabii na Viongozi Wakuu wenye Mamlaka. Wakati wa kikao cha mchana cha Jumamosi, shiriki katika kuwakubali wao katika miito yao.

    mtu katika Kituo cha Mikutano akiinua mkono wa kulia kwa ajili ya kura ya kukubali
  3. “Na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu mtajua ukweli wa vitu vyote.” (Moroni 10:5). Unaposikiliza jumbe kutoka kwa viongozi wa Kanisa, kuwa msikivu Roho anapokushuhudia kwamba maneno yao ni ya kweli.

  4. Mojawapo ya wajibu muhimu wa nabii ni kushuhudia juu ya Yesu Kristo na kutufundisha sisi “kuangalia juu kwa Mwana wa Mungu na imani,” (ona Helamani 8:15). Unaweza kutaka kujua nabii na wanenaji wengine wanatufundisha nini kumhusu Mwokozi.

  5. “Kupitia kwa [Rais Russell M. Nelson], tumepokea mialiko isiyohesabika na tumeahidiwa baraka tukufu ikiwa tutamweka Mwokozi wetu, Yesu Kristo kuwa kiini cha maisha yetu.” Fikiria kutengeneza orodha ya mialiko iliyotolewa na nabii na wanenaji wengine wakati wa mkutano mkuu wa hivi karibuni. Rejelea kwenye orodha hiyo ili ikusaidie ujitahidi kuwa zaidi kama Kristo.

  6. Kumbuka mwaliko wa Rais Nelson: “Ninawahimiza mjifunze jumbe za mkutano huu kila mara—hata kwa kurudia—kwa muda wa miezi sita ijayo.” Unaposikiliza au kusoma jumbe hizi tena, wekea alama mambo yanayoonekana kuwa na maana zaidi kwako.

  7. Rais Nelson anatualika “tutafute na kutarajia miujiza.” Unapotii ushauri wa nabii na kufanya mabadiliko katika maisha yako, kuwa makini na baraka unazopokea na miujiza unayoiona (ona Helamani 16:4–5).

Unapofuata hatua hizi ili kukuza ushuhuda wako juu ya nabii, mwonaji, na mfunuzi, vuta kutoka kwenye imani yako katika Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Mungu kwa upendo ametupatia manabii ili kutuongoza kurudi Kwake—manabii wanakuwa kama kinywa Chake cha kufunua mapenzi Yake kwa ulimwengu, (Ona Mafundisho na Maagano 1:38; 21:5–6.) Kama tunachagua kufuata ushauri wa watumishi Wake, tunachagua kumfuata Yeye.