“Mazuri Ambayo Injili Imeniletea,” Liahona, Septemba 2024.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Mazuri ambayo Injili Iliniletea
Kwa sababu ya watu Kanisani, nilimhisi Roho Mtakatifu.
Nilipokuwa nikikua, shujaa wangu alikuwa babu yangu wa upande wa mama, acheii wangu. Alikuwa imara katika imani yake. Nilienda kwenye makanisa mengi tofauti pamoja na yeye lakini dini haikuwa kitu nilichokipenda.
Wakati nilipokutana na Gina, ambaye alikuja kuwa mke wangu, alikuwa muumini mwaminifu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Alinitaka nijifunze kuhusu Kanisa ili tuweze kufunga ndoa hekaluli. Lakini sikutaka hilo. Nilikuwa siyo mtu wa dini sana.
Hatimaye tulifunga ndoa ya serikali. Baada ya kuwa na mtoto, bado sikuwa ninapendelea Kanisa, lakini Gina aliendelea kuhudhuria.
Hatimaye, niliamua ningethibitisha kwamba kanisa lake lilikuwa si la kweli kwa kuhudhuria makanisa mengine. Hii iliendelea kwa miaka kadhaa, lakini popote nilipokwenda, sikusikia faraja.
Kisha, Jumapili moja Gina alipokuwa anamtayarisha binti yetu kwenda kanisani, mimi nilianza kujiandaa kwenda kanisani pia. Aliniangalia na kusema, “Unafanya nini?” Nilijibu, “Najitayarisha kwenda kanisani pamoja nawe.” Alimwangalia binti yetu na kusema, “Jitayarishe upesi! Hatutaki abadili mawazo yake!”
Kwa hiyo, tulienda. Kwa sababu nilimhisi Roho Mtakatifu kupitia watu pale kanisani, watu hao walikuwa muhimu katika uongofu wangu. Baada ya hapo, wamisionari walikuja nyumbani kwetu. Walikuwa wazuri sana, mafundisho waliyonifundisha yalikuwa mazuri kwangu, na Roho aliujaza moyo wangu (ona Moroni 10:4–5).
Nilipomtembelea babu yangu ili kumwambia kile nilichokuwa nimepata, yeye hakufurahia. Lakini nilijua itanibidi nifuate moyo wangu.
Nilijiunga na Kanisa, na punde Gina pamoja nami tuliunganishwa hekaluni. Binti yetu aliunganishwa nasi, na sisi sasa tuna watoto watatu zaidi ambao walizaliwa katika agano.
Ilichukua miaka 10 kwa acheii wangu mwishowe kuheshimu kile sisi tunachoamini katika Kanisa. Katika mahafali ya shule ya upili ya mwanangu, yeye alimwambia kila mtu kwa Kinavajo, “Mimi ninaifurahia familia hii. Ninaunga mkono kile wanacho amini. Watoto wao kwa kweli wanajua jinsi ya kusali.”
Mimi ni muumini pekee wa Kanisa katika familia yangu kubwa, lakini ninajua wao wanakubali kwamba uongofu wangu ni halisi, na wanaona mazuri ambayo injili imeleta kwa mke wangu, watoto wetu, na mimi.