Kitabu cha Mormoni Kiliniletea Amani, Liahona, 2024.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Kitabu cha Mormoni Kiliniletea Amani
Nilikuja kuelewa kwamba Kitabu cha Mormoni kilitamanika kwa ajili ya kubadilisha maisha yangu na kunileta karibu zaidi na Yesu Kristo.
Mwishoni mwa mwaka 2013, vijana wawili waliovaa mashati meupe na tai walianza kumtembelea dada yangu mara mbili kwa wiki. Nilijua mara moja walikuwa wanatoka kwenye kanisa. Kwangu mimi, kuwa sehemu ya kanisa haikuwa katika mipango yangu, kwa hiyo niliamua kutozungumza nao.
Kwa kila matembezi yao, nilihakikisha sipo nyumbani wakati walipowasili. Hata hivyo, kuna kitu cha kipekee, kilivuta usikivu wangu. Daima walibeba kitabu cha rangi ya bluu. Nilikuwa sijakiona kamwe hapo awali, na kilionekana kigeni kwangu.
Siku moja sebuleni, dada yangu alianza kuniambia kuhusu kitabu hiki. Ghafula, vijana wale wawili waliwasili. Bahati mbaya, nisingeweza kujificha. Walituona tukiwa na kile kitabu cha bluu—Kitabu cha Mormoni—na wakaaanza kuniuliza ninajua nini kumhusu Yesu Kristo.
Nilipokuwa ninawasikiliza wamisionari kutoka siku ile na kuendelea, nilivutiwa na jinsi walivyounganisha mafundisho yao na Kitabu cha Mormoni. Matokeo yake, kitabu cha rangi ya bluu kikawa si kigeni tena kwangu.
Bado nilikuwa na mashaka sana kukihusu kitabu hicho, lakini nilianza kukisoma. Nilikuja kuelewa kwamba Kitabu cha Mormoni hakikuwa mbadala wa Biblia bali kilikuwa cha kutamanika kubadilisha maisha yangu na kunileta karibu sana na Yesu Kristo. Nilijifunza kwamba Kitabu cha Mormoni kiini chake ni Mwokozi. Mafundisho yake yalinisaidia mimi kujua Yeye ni nani na Baba wa Mbinguni ni nani.
Kitabu cha Mormoni punde kilinisaidia kuwa mtu bora, mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo. Pia kilinisaidia kuboresha mtazamo wangu nilipokabiliana na changamoto kila siku. Kutokana na uzoefu wangu kwa kukijifunza, ninajua kinawasaidia watu kuja kwa Kristo na kuishi injili (ona Moroni 10:32). Hutuhimiza sisi kufuata mafundisho ya Kristo na kuyatumia katika maisha yetu ya kila siku. Kinatupa sisi elimu kwamba sisi ni wana na mabinti wa Mungu. Kinaleta amani.
Baada ya wiki kadhaa za kukutana na wamisionari na kusoma Kitabu cha Mormoni, nilibatizwa. Ninatoa ushuhuda wangu kwa moyo wangu wote kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli na kwamba kukisoma huleta tumaini na nuru katika nyakati za giza, hutusaidia kuhisi upendo na ulinzi wa Bwana. Mimi ninashukuru kuwa na Kitabu cha Mormoni katika maisha yangu.