Liahona
Mungu Alikuwa na Kitu Bora kwa ajili Yetu
Septemba 2024


Mungu Alikuwa na Kitu Bora kwa ajili Yetu, Liahona, Septemba 2024.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Mungu Alikuwa na Kitu Bora kwa ajili Yetu

Wakati wamisionari waliponifundisha kwamba mimi ni mtoto wa Mungu, nilijua Yeye alikuwa na baraka zaidi ghalani kwa ajili ya familia yangu na mimi.

picha ya mwandishi akiongoza kwaya

Picha kutoka kwa mwandishi

Nilikulia katika kijiji kidogo, huko Ufilipino vijijini. Familia yangu ilikuwa masikini. Katika Ufilipino kama huna pesa, huwezi kwenda shule. Licha ya kikwazo hicho, mimi nilikuwa kijana mwenye ndoto nyingi.

Niliwaambia wazazi wangu nilitaka kuwa daktari au mwalimu au mtaalamu wa aina fulani, lakini daima waliniambia niache kuota ndoto. Hatukuwa na pesa kwa ajili yangu kwenda chuoni. Wazazi wangu walitaka niridhike na nisikatishwe tamaa na maisha yangu.

“Kuwa mtaalamu siyo kwa ajili yetu sisi,” wao walisema. Hawakuamini kwamba kitu chochote bora kilikuwa ghalani kwa ajili ya familia yetu kuliko kile tulichokuwa nacho tayari.

Lakini hilo lilikuwa kabla ya kujiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Tuliishi mbali na jiji lolote, lakini wamisionari walitupata na waliendelea kurudi. Walifanya dhabihu ya kuifundisha familia yangu, lakini walibadilisha maisha yetu milele.

Wakati tulipojiunga na Kanisa, nilijifunza kwamba mimi nilikuwa mtoto wa Mungu mwenye uwezekano wa kukua na kujifunza na kuwa (ona Musa 1:39; “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Maktaba ya Injili). Kwa elimu ya injili, nilijua ilikuwa ni wakati wa kuinua hali ya familia yangu. Hatukuwa tu tena watu masikini kutoka kijiji kidogo—sisi ni wana na mabinti wa Mungu wa thamani wanaostahili baraka ambazo Yeye ameahidi kwa wafuasi Wake waaminifu.

Wamisionari walileta injili katika maisha yangu, injili ilileta muziki katika maisha yangu, na muziki ulinipatia udhamini wa kuhudhuria chuo. Nilipata shahada ya elimu ya shule ya upili na kisha shahada ya muziki, nikijikita katika kuongoza kwaya. Sasa ninafundisha muziki katika Chuo Kikuu cha Liceo de Cagayan na kuendesha Klabu ya Glee ya Shule Upili ya Liceo U. Pia ninaongoza kwaya ya waumini wa Kanisa. Misheni yetu ni kushiriki ukweli juu ya Mungu kupitia muziki.

Kuhitimu kutoka chuo kikuu kumenipa maisha mapya. Mimi sijui ningekuwa wapi leo bila injili ya Yesu Kristo.

Kila mtu anastahili nafasi ya kujifunza, kama mimi nilivyojifunza, kwamba wanaye Baba wa Mbinguni na kwamba Yeye amewabariki kwa uwezekano wa kukua na kujifunza na kuwa.