Liahona
Jinsi Gani Changamoto Zilinisaidia Nijenge Upya Msingi Wangu wa Imani
Septemba 2024


“Jinsi Gani Changamoto Zilinisaidia Nijenge Upya Msingi Wangu wa Imani,” Liahona, Septemba 2024.

Vijana Wakubwa

Jinsi Gani Changamoto Zilinisaidia Nijenge Upya Msingi Wangu wa Imani

Baada ya changamoto kali za kiakili, kimwili na kiroho, niligundua inamaanisha nini kupata uponyaji kupitia Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

picha ya mwandishi pamoja na Hekalu la Salt Lake likiwa upande wa nyuma

Nilikuwa nikihudumu kama mmisionari huko Ufaransa wakati ulimwengu ulipoangushwa na UVIKO-19 iliitupa nchi yote katika vizuizi vikali vya kutotoka nje. Nimesumbuka na msongo wa mawazo maisha yangu yote, kwa hiyo nilikuwa na hofu kwamba mazingira ya kufungiwa yangenisabishia kupatwa na msongo wa mawazo. Lakini wiki ya kwanza ya karantini—wiki iliyoelekea mkutano mkuu wa kihistoria wa Aprili 2020—ilikuwa mojawapo ya wiki ya kiroho zaidi katika maisha yangu.

Nikitazama nyuma, uzoefu huu niliopata wiki hiyo nilihisi Bwana alikuwa ananiimarisha kwa ajili ya dhoruba.

Mzee Gary E. Stevenson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitoa mahubiri katika mkutano huo kuhusu marekebisho ambayo yangefanywa kwenye misingi ya Hekalu la Salt Lake. Alifananisha utengezaji huo mpya na maisha yetu wenyewe na kutuomba tufikirie swali hili:

“Je! ni mambo gani ya msingi ya tabia yangu ya kiroho na kihisia ambayo yataniruhusu mimi na familia yangu kubaki thabiti na pasipo kuondoshwa, hata kustahimili matetemeko ya ardhi na matukio ya ghasia ambayo hakika yatatokea katika maisha yetu?”

Nilipokuwa nasikiliza mahubiri yake, Roho alinitia kwenye fikra kwamba, kama hekalu hili, nilikuwa ninaenda kuvunjika kwa namna fulani wakati wa kipindi kijacho cha maisha yangu. Lakini pia nilihisi kwamba kama nitamgeukia Bwana wakati wa changamoto hizi, Yeye angenisaidia mimi kuimarisha msingi wangu wa imani.

Kuhisi Kuvunjika

Kama ilivyotarajiwa, punde nipatwa na msongo wa mawazo, na haikuwa muda mrefu nilijiona kuwa niko kwenye mtego wa mduara usio na mwisho wa mawazo ya kujiua. Nilihisi kuvunjika kiakili, kihisia, na kiroho.

Baada ya miezi miwili ya karantini, mambo yakawa mazuri kidogo. Shukrani kwa mabadiliko katika hali yangu, kama vile tiba ya dawa za msongo wa mawazo na mwisho wa kufungwa, nilianza kujisikia vizuri kiakili. Lakini punde baadaye, nilianza kujisikia mgonjwa na nikaona uvimbe mara tatu chini ya koo langu.

Hapo mwanzo nilipuuza uvimbe huu, lakini wakati dalili zangu zilipozidi, ilikuwa wazi kwamba nisingeweza kubakia katika eneo la misioni. Nilirudi nyumbani, ambapo upesi niligunduliwa kuwa na saratani ya damu—lymphoma ya Hodgkin.

Kwa sababu dawa zangu za msongo wa mawazo zilikuwa na athari ya kuleta ganzi kwenye hisia, nilihisi kutojali sana nilipoanza tiba ya kemikali ya miezi sita.

Lakini hata hivyo, nilianza kuvunjika kimwili.

picha ya mwandishi pamoja na Hekalu la Salt Lake likiwa upande wa nyuma

Kujenga Upya Msingi Wangu wa Kiroho

Mwaka mmoja baada ya tibakemikali kuisha, nilianza kujisikia vyema kimwili. Nilirudi chuoni na kufanya mipango. Lakini kuugua maumivu kiroho na ganzi niliyohisi kwenye misioni yangu na wakati wa tibakemikali sasa ilikuwa imebadilika kuwa hisia ya kawaida ya kutojali kuhusu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

Nilikuwa ninasumbuka na hisia zangu kuhusu kile nilichokuwa nimepitia na kuhisi kama Wao walikuwa wamenitelekeza wakati nilipokuwa chini.

Lakini Baba wa Mbinguni alijua ni njia ipi nilihitaji kuchukua ili niweze kupona.

Nilihisi kama nilikuwa ninapambana na vifusi na mabaki ya imani yangu ambayo wakati fulani ilikuwa imara na utu wangu ambao wakati fulani ulikuwa mchangamfu. Nilihisi kutounganika kabisa na mimi mwenyewe. Moyo wangu ulilainika kwa majaribio ya Bwana ya kunifikia, lakini kiroho nilihisi hatia, wasiwasi, na nisiyestahili kwa sababu ya kutojali kwangu juu ya injili.

Baada ya kutafakari juu ya afya yangu ya kiroho kwa miezi michache, nipata msukumo wa kufanya mabadiliko madogo ya kiroho katika maisha yangu. Nilikuwa nimepuuza maumivu kwa muda, lakini nilitaka kutatua uchungu niliohisi katika nafsi yangu kwa sababu ya changamoto niliyokuwa nimepata.

Punde niliweza kuona mkono wa Mungu katika maisha yangu. Bila kujua ni ganzi kiasi gani ya kiroho nilikuwa ninaihisi, marafiki na wapendwa wangu walileta mada ya uponyaji. Mmoja wao hata alishiriki mahubiri ya ibada kutoka kwa Elaine S. Marshall.

Bila kutaka, niliyasoma.

Kama nesi, Elaine alionyesha usawa kati ya uponyaji kimwili na uponyaji kiroho kwa kusema: “Uponyaji siyo tiba, Tiba ni safi, ya haraka, na inafanyika—mara nyingi kwa aneasthesia . … Uponyaji … mara nyingi ni mchakato wa maisha yote wa kupata nafuu na ukuaji licha ya, labda kwa sababu ya, kuvumilia kimwili, kimhemko, au pambano la kiroho. Unahitaji muda.”

Sifikirii ilikuwa ni bahati nasibu kwamba matibabu ya saratani yangu yalihitaji miezi sita ya tibakemikali. Athari za kemikali ni kali, zenye mabadiliko, na zenye kuhitaji uvumlivu. Cha kushangaza, kujifunza kuuacha mwili wangu kupona kimwili kulinifundisha kanuni muhimu ya uponyaji wa kiroho—jinsi ya kuvuta neema ya Yesu Kristo na kujipa muda na nafasi ya kuponya uhusiano wangu na Yeye na Baba wa Mbinguni.

Kupokea Neema ya Mwokozi

Neema ni msaada wa kiungu, nguvu za kuwezesha na kuimarisha, na uponyaji wa kiroho. Ni zawadi kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni, “inayotolewa kwetu kupitia Upatanisho wa Bwana Yesu Kristo.”

Mfano wangu pendwa wa mtu akipata nguvu ya uponyaji ya Yesu Kristo kupitia Upatanisho Wake ni Alma Mdogo. Alipokuwa amelala katika hali ya kuzimia kwa siku tatu, aliteseka “uchungu wa nafsi iliyolaaniwa,” alikumbuka mafundisho ya baba yake juu ya Yesu Kristo (ona Alma 36:16–17). Alitamani msaada kwanza, na kisha alimgeukia Kristo, ambayo ilibadilisha mwenendo wake na kumruhusu kuponywa kiroho (ona Alma 36:18–22).

Hatua ya kwanza niliyochukua kuelekea uponyaji wa kiroho ilikuwa ni kutafuta hamu ya kuunganika na Mungu. Alma alinifundisha mimi jinsi ya kuanza wakati aliposema, “Kutumia sehemu ya imani, ndiyo, hata ikiwa hamwezi ila kutamani kuamini, acha hamu hii ifanye kazi ndani yenu, hata mpaka mwamini kwa njia ambayo mtatoa nafasi kwa sehemu ya maneno yangu” (Alma 32:27).

Ninashuhudia kutokana na uzoefu binafsi kwamba mafundisho haya ni ya kweli.

Tunaweza kukuza hamu, kupanda mbegu (neno la Mungu), na kuilisha ile mbegu mpaka inakuwa kitu fulani halisi na thabiti. Hatimaye, matunda ya imani yetu katika Yesu Kristo huzaliwa wakati tunapoona mabadiliko katika matendo yetu, maoni yetu, imani zetu, mioyo yetu, akili zetu, na kisha nafsi zetu. Msingi wetu unakuwa umejengwa juu Yake (ona Helamani 5:12).

Sawa na uzoefu wa Alma, hamu yangu ya kumhisi Roho na shangwe ya injili tena vimeanzisha mwenendo mzima ambao ulinichukua kupitia mchakato wa uponyaji. Tangu wakati huo, Mwokozi amenisaidia nitambue hisia zangu zilizopita pale nilipojifunza kuondoa hasira zangu kwa Mungu, Kwake, na udhaifu wangu mwenyewe.

Kwa sababu Yake, sehemu zangu ambazo nilidhania nilikuwa nimezipoteza katikati ya majaribu yangu—kama vile utu wangu, matamanio yangu, na upendo wangu kwa ajili ya injili—vimerudishwa kwangu na vimenifanya nijisikie mzima, mpya, na aliyerejeshwa.

Msingi Imara Zaidi

Uchungu na changamoto vilinibadilisha, lakini nilipopata uponyaji kupitia Yesu Kristo, kwa kweli nilijenga upya msingi wangu wa imani juu Yake. Kadiri muda unavyosonga na mimi ninapona, ninaona kwamba kwa sababu ya Yesu Kristo, ninaweza kujifunza kuwa na shangwe licha ya kusumbuka kwangu. Sasa ninaelewa kwamba sehemu muhimu sana ya kupitia majaribu siyo kile kinachotuvunja au uchungu tunaojisikia—ni kile kinachofuata tunapopitia uponyaji na kujengwa upya kupitia neema ya Mwokozi.

Mzee Patrick Kearon wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: “Marafiki wapendwa ambao mmepatwa na kukosa haki za maisha—mnaweza kuwa na mwanzo mpya na kuanza upya. Katika Gethsemane na Kalvari, Yesu ‘alijuchukulia juu Yake Mwenyewe … maumivu na masumbuko yote tuliyowahi kupata wewe na mimi’ [Russell M. Nelson, “Jina Sahihi la Kanisa,” Liahona, Nov. 2018, 88], na Yeye ameshinda yote!”

Kwa hiyo, kwa wale ambao wanahisi kuvunjika, ninawasihi muwe shupavu, mshikilie, na mumtumainie Bwana na nguvu Zake za uponyaji. Baada ya muda, subira, na hata tamanio dogo, neema Yake inaweza kukubadilisha wewe, kuujenga upya msingi wako, na kukusaidia ujisikie u mzima tena.

Hiyo ndiyo zawadi ambayo Yeye anatoa kwa kila mmoja wetu.

Mwandishi anaishi North Carolina, Marekani.