“Njia Tatu za Kuvumilia Maisha na Kuyafurahia,” Liahona, Septemba 2024.
Vijana Wakubwa
Njia Tatu za Kuvumilia Maisha na Kuyafurahia
Baba wa Mbinguni anatutaka tupate shangwe katika maisha tuliyopewa.
Ni lini ilikuwa mara yako ya mwisho kwako kuwa na furaha ya kweli?
Je, swali hilo lilikuwa gumu kujibu?
Wakati wa nyakati zenye changamoto, tunaweza kuzama sana katika majaribu yetu kiasi kwamba hatuwezi kabisa kukumbuka vile shangwe ilivyo. Kama vile Dada Reyna I. Aburto, Mshauri wa Pili wa zamani katika Urais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi, alivyolielezea: Mawingu meusi yanaweza … kujitengeneza katika maisha yetu, kitu ambacho kinaweza kutuziba kwenye nuru ya Mungu na hata kutusababisha tujiulize ikiwa nuru hiyo bado ipo kwetu.”
Kwa wengi wetu vijana wakubwa, maisha wakati mwingine yanaweza kuhisi kama kitu tu cha kuvumilia—kitu cha kuhangaikia mpaka mwishowe tupokee baraka tulizoahidiwa.
Kile ambacho wakati mwingine tunasahau ni kwamba pia ni kitu cha kufurahia. Baraka ya furaha ya milele inaweza kuanza sasa.
Hapa kuna njia chache ambazo kupitia hizo tunaweza kuwasha upya nuru na shangwe katika maisha yetu.
Kumbuka Kweli Rahisi
Badala ya kuyafundisha macho yetu kuona gizani, tunaweza kupekua miale ya nuru ambayo injili ya Yesu Kristo huleta katika maisha yetu.
Rais Russell M. Nelson ametukumbusha sisi kwamba “shangwe huja kutoka kwa Yesu Kristo, na kwa sababu ya [Yesu Kristo]. Yeye ndiye chanzo cha shangwe yote.” Wakati unapohangaika ili kupata nuru katika maisha yako, kumgeukia Yesu Kristo daima kunapaswa kuwa hatua ya kwanza.
Unaweza pia kumwomba Baba wa Mbinguni ili akusaidie ukumbuke umuhimu wa utambulisho wako wa kiungu.
Mzee Gary B. Sabin wa Sabini alifundisha: “Ni muhimu kwa furaha yetu kwamba tukumbuke kwamba sisi ni wana na mabinti wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo.” Kwa kweli kujua kwamba Mungu anakujua na anataka kilicho bora kwako kunaweza kuangaza maisha yako.
Licha ya changamoto unazokabiliana nazo, kukumbuka kanuni hizi za injili za msingi zinaweza kukusaidia ualike nuru ya Mwokozi katika maisha yako.
Tafuta Ni Kipi Hukuletea Furaha
Wakati mwingine inaweza kuwa vigumu kukumbuka kwamba furaha yetu daima haionekani kuwa sawa na furaha ya kila mtu. Kwa kweli, kama vijana wakubwa, ni vigumu kukosa kulinganisha maisha yetu na ya wale wanaotuzunguka. Lakini kumbuka kwamba wewe una udhibiti juu ya furaha yako mwenyewe.
Jiulize mwenyewe: ni kipi kinafanya wewe uwe na furaha?
Ni kipi hukufanya utabasamu?
Kama vile wakati huo Rais Dieter F. Uchtdorf alivyopendekeza alipokuwa Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, “Punguza kasi na chukua muda wa ziada ili kujifahamu vyema wewe mwenyewe.” Tafuta uzuri katika vitu vidogo vidogo: Nenda matembezini. Tembelea hekalu. Jisajili kwa ajili ya mradi wa huduma. Tafuta jambo jipya ulipendalo au anza pale ulipokuwa umeachia lile la zamani.
Mzee Richard G. Scott (1928–2015) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wakati mmoja alizungumza kuhusu jinsi ubunifu unavyoweza kunururisha maisha yetu: “Chagua kitu kama vile muziki, dansi, kuchonga sanamu, au ushairi. Kuwa mbunifu kutakusaidia ufurahie maisha. Huzalisha roho ya shukrani. Hukuza talanta fiche, hunoa uwezo wako wa kiakili, kutenda, na kupata dhumuni la maisha. Huondoa upweke na huzuni kubwa. Hutia nguvu mpya, huamsha shauku, na huleta ladha kwenye maisha.”
Kupata kile kinachoujaza moyo wako kwa furaha kunaweza kuwasha upya nuru katika maisha yako wakati unapokuwa umekwama.
Fokasi kwenye Kile Kilicho Muhimu Zaidi
Kama maisha yanakuzidia sana na unahisi kama yanachukua nguvu zako zote ili tu kumaliza siku, chukua dakika chache za utulivu ili kufokasi juu ya kile kilicho muhimu zaidi.
Ili kufanya hivyo, Rais Uchtdorf alipendekeza kwamba “turahisishe maisha yetu kidogo.” Fokasi tena maisha yako kwenye upendo wa Baba wa Mbinguni na zawadi nzuri ya Upatanisho wa Kristo. Weka vipaumbele kwenye uhusiano na familia yako, marafiki zako, na wewe mwenyewe.
Pigana na uhasi kwa uchanya, giza kwa nuru ya Yesu Kristo na Injili Yake.
Kama vile Rais Nelson alivyotuhimiza: “Hebu tusivumilie tu kipindi hiki cha sasa. Hebu tukumbatie siku zijazo kwa imani!” Wakati ukivumilia magumu ya maisha, jifunze kufurahia uzuri wake pia. Furaha ya milele ambayo injili huahidi haianzi wakati fulani katika siku za usoni—inaanza sasa.