“Mpangilio wa Umoja katika Yesu Kristo,” Liahona, Okt. 2024.
Ujumbe wa Kila mwezi katika Liahona, Oktoba 2024
Mpangilio kwa ajili ya Umoja katika Yesu Kristo
Tunapoungana katika Yesu Kristo kama wale watu katika 4 Nefi, hamu yetu ya kuwa na umoja inachukua nafasi ya tofauti zetu na kutuongoza kwenye furaha.
Tunaishi katika zama ambazo wimbi kubwa la kutokuelewana na mabishano linaenea kote ulimwenguni. Vikisaidiwa na teknolojia na watu ambao mioyo yao imepoa, vikosi hivi vya mgawanyiko vinatishia kujaza mioyo yetu kwa dharau na kuharibu mawasiliano yetu kwa ugomvi. Uhusiano wa kijumuiya unavunjika. Vita vinaunguruma.
Kinyume cha hali hii, wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo wanatamani amani na wanashughulika kikamilifu kutafuta kujenga aina tofauti ya jamii—ile ambayo imejengwa juu ya mafundisho ya Yesu Kristo. Kwa sababu hii, Bwana ametuamuru “kuweni na umoja; na kama hamna umoja ninyi siyo wangu” (Mafundisho na Maagano 38:27). Hakika, umoja ni sifa bainifu ya Kanisa la kweli la Yesu Kristo.
Ni kwa jinsi gani tunafanya kazi dhidi ya nguvu za mgawanyiko na ugomvi? Ni kwa jinsi gani tunapata umoja?
Kwa bahati nzuri, 4 Nefi katika Kitabu cha Mormoni inatupatia mfano. Mlango huu kwa ufupi unaandika jinsi watu hawa walivyoishi baada ya Mwokozi kuwatembelea, kuwafundisha, na kuanzisha Kanisa Lake miongoni mwao. Hadithi hii inaonyesha jinsi watu hawa walivyofanikisha umoja wenye furaha na wenye amani, na inatupatia sisi mpangilio tunaoweza kuufuata ili kufikia umoja huo huo sisi wenyewe.
Uongofu
Katika 4 Nefi 1:1, tunasoma: “Wanafunzi wa Yesu walikuwa wameanzisha kanisa la Kristo katika nchi zote zilizokuwa karibu. Na [watu] walikuja kwao, na kwa ukweli walitubu dhambi zao.”
Tunaungana kumzunguka Bwana na Mwokozi Yesu Kristo. Kadiri kila mtu anavyojifunza kuhusu Yesu Kristo, injili Yake, na Kanisa Lake, Roho Mtakatifu anashuhudia ukweli kwenye moyo wa kila mtu. Kila mmoja wetu kisha anaweza kuukubali mwaliko wa Mwokozi wa kuwa na imani Kwake na kumfuata Yeye kwa kutubu.
Hivyo huanza safari ya mtu binafsi ya uongofu—mbali na ubinafsi na tamaa za dhambi na kuelekea kwa Mwokozi. Yeye ni msingi wa imani yetu. Na kila mmoja wetu anapomtegemea Yeye katika kila wazo (ona Mafundisho na Maagano 6:36), Yeye anakuwa nguvu yenye kuunganisha katika maisha yetu.
Maagano
Kumbukumbu katika 4 Nefi inaendelea kusema kwamba wale waliokuja katika Kanisa na kutubu dhambi zao “walibatizwa katika jina la Yesu; na pia walimpokea Roho Mtakatifu” (4 Nefi 1:1). Walikuwa wameingia katika agano—uhusiano maalum, wa kuunganisha—pamoja na Mungu.
Tunapofanya na kushika maagano, tunajichukulia juu yetu jina la Bwana kama watu binafsi. Pia tunajichukulia jina Lake juu yetu kama watu. Wale wote wanaofanya maagano na kujitahidi kuyashika wanakuwa watu wa Bwana, hazina Yake maalum (ona Kutoka 19:5). Hivyo, tunasafiri katika njia ya agano kama watu binafsi na kwa pamoja. Uhusiano wetu wa agano na Mungu unatupa sababu ya pamoja na utambulisho wa pamoja. Tunapojiunganisha wenyewe kwa Bwana, Yeye hutusaidia “kuunganisha mioyo yetu pamoja kwa umoja na kupendana sisi kwa sisi” (Mosia 18:21).
Haki, Usawa, na Kuwasaidia Maskini
Hadithi katika 4 Nefi inaendelea: “Hakukuwa na mabishano na ugomvi miongoni mwao, na kila mtu alimtendea mwingine haki.
“Na vitu vyao vyote vilitumiwa kwa usawa miongoni mwao; kwa hivyo hakukuwa na tajiri na masikini, wafungwa na walio huru, lakini wote walifanywa huru, na washiriki wa karama ya mbinguni” (4 Nefi 1:2–3).
Katika shughuli zetu za kidunia, Bwana anatutaka sisi tusipunjane wala kukoseana na tusidanganyane au kufanyiana hila (ona 1 Wathesalonike 4:6). Na tunaposonga karibu zaidi na Bwana, hatutataka kuumizana, lakini kuishi kwa amani, na kumpatia kila mtu kitu anachostahili” .(Mosia 4:13).
Bwana pia ametuamuru kuwajali masikini na wenye shida. Tunapaswa “kuwapa mali [yetu]” ili kuwasaidia, kulingana na uwezo wetu wa kufanya hivyo, bila kuwahukumu (ona Mosia 4:21–27).
Kila mmoja wetu na “ampende ndugu yake kama vile ajipendavyo mwenyewe” (Mafundisho na Maagano 38:24). Kama tunapaswa kuwa watu wa Bwana na wenye umoja, siyo tu lazima tutendeane sisi kwa sisi kama tulio sawa, bali lazima pia tutazamane kama watu walio sawa na kujisikia katika mioyo yetu kwamba sisi ni watu walio sawa—sawa mbele za Mungu, wenye thamani iliyo sawa na uwezekano wa kuwa ulio sawa.
Utiifu
Somo linalofuata kutoka katika 4 Nefi linakuja katika usemi huu rahisi: “Walifuata amri ambazo walipokea kutoka kwa Bwana wao na Mungu wao” (4 Nefi 1:12).
Bwana alikuwa amewafundisha watu hawa mafundisho Yake, aliwapa amri, na aliwaita watumishi ili kuwasimamia. Moja ya madhumuni Yake katika kufanya hivi ilikuwa ni kuhakikisha kwamba hakungekuwa na mabishano miongoni mwao (ona 3 Nefi 11:28–29; 18:34).
Utiifu wetu kwa mafundisho ya Bwana na watumishi Wake ni muhimu kwenye kuwa wamoja. Hii inajumuisha kujitolea kwetu kutii amri ya kutubu wakati tunapoanguka na kusaidiana pale tunapojitahidi kufanya vizuri zaidi na kuwa bora kila siku.
Kukutana Pamoja
Kisha, tunajifunza kwamba wale watu katika 4 Nefi “[waliendelea] katika kufunga na sala, na kwa kukutana pamoja siku zote kuomba na kusikia neno la Bwana” (4 Nefi 1:12).
Tunahitaji kukutana pamoja. Mikutano yetu ya kuabudu ya kila wiki ni fursa muhimu kwetu ya kupata nguvu, binafsi na kwa pamoja. Tunashiriki sakramenti, kujifunza, kusali, kuimba pamoja, na kusaidiana. Mikusanyiko mingine pia husaidia kuchochea hali ya kuwa wa mahala pale, urafiki, na dhumuni la pamoja.
Upendo
Kumbukumbu katika 4 Nefi kisha inatupatia kile ambacho labda ni ufunguo mkuu kwa haya yote—kitu ambacho bila umoja halisi hakiwezi kupatikana: “Hakukuwa na ubishi katika nchi, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu” (4 Nefi 1:15).
Amani binafsi inafikiwa wakati sisi, katika kujishusha kwa unyenyekevu, tunampenda Mungu. Hii ndiyo amri kuu, na ni ya kwanza. Kumpenda Mungu zaidi kuliko mtu yeyote au kitu kingine chochote ni sharti ambalo huleta amani ya kweli, faraja, kujiamini na shangwe. Tunapokuza upendo wa Mungu na Yesu Kristo, upendo wa familia na jirani kwa kawaida utafuata.
Shangwe kuu zaidi ambayo tutawahi kuipitia itatokea wakati tunapomezwa na upendo kwa Mungu na kwa watoto wote wa Mungu.
Hisani, upendo msafi wa Kristo, ni dawa ya ugomvi. Hisani ni tabia ya msingi ya mfuasi halisi wa Yesu Kristo. Tunapojinyenyekeza sisi wenyewe mbele za Mungu na kusali kwa nguvu zote za mioyo, Yeye atatujalia hisani (ona Moroni 7:48).
Sisi sote tunapotafuta kuwa na upendo wa Mungu kukaa katika mioyo yetu, muujiza wa umoja utaonekana wa kawaida kabisa kwetu.
Utambulisho wa Kiungu
Hatimaye, wale watu katika 4 Nefi walionesha ishara ya umoja ambayo inastahili usikivu wetu: “Hapakuwa na wezi, wala wauaji, wala hakukuwa na Walamani, wala aina yoyote ya vikundi; lakini walikuwa kitu kimoja, watoto wa Kristo, na warithi wa ufalme wa Mungu” (4 Nefi 1:17).
Utambulisho ambao uligawanya watu kwa mamia ya miaka ulipungua kabla ya utambulisho wa kudumu zaidi na wa kuadilisha. Walijiona wenyewe —na kila mtu mwingine—kulingana na uhusiano wao na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Makundi na tofauti vinaweza kuwa vitu vizuri na muhimu kwetu sisi. Lakini utambulisho wetu muhimu zaidi ni ule unaohusiana na asili na dhumuni letu takatifu.
Kwanza na kuu zaidi, kila mmoja wetu ni mtoto wa Mungu. “Pili, kama muumini wa Kanisa, kila mmoja wetu ni mtoto wa agano. Na tatu, kila mmoja wetu ni mfuasi wa Yesu Kristo. Ninawasihi sisi sote tusiruhusu utambulisho mwingine wowote “kuhamisha, kubadilisha, au kuchukua kipaumbele juu ya majina haya matatu ya kudumu.”
Muwe Wamoja
Mungu amewaalika wote waje Kwake. Kuna nafasi kwa ajili ya kila mmoja. Tunaweza kutofautiana katika tamaduni zetu, siasa, makabila, vionjo, na njia zingine nyingi. Lakini tunapoungana katika Yesu Kristo, tofauti kama hizo hufifia katika umuhimu wake na nafasi zake zinachukuliwa na hamu yetu ya kupindukia ya kuwa na umoja—ili kwamba tuweze kuwa Wake.
Yaweke moyoni masomo haya yanayofundishwa katika 4 Nefi. Wakati kila mmoja wetu anapojitahidi kujumuisha vipengele hivi muhimu vya umoja katika maisha yetu, inaweza kusemwa kwetu, kama ilivyokuwa kwao, “Kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu” (4 Nefi 1:16).
© 2024 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, October 2024. Swahili. 19359 743