“Kapteni Moroni na Pahorani,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Kapteni Moroni na Pahorani
Nguvu kutoka kwa Mungu
Wanefi na Walamani walikuwa vitani. Moroni alikuwa kapteni wa jeshi la Wanefi. Viongozi wa Wanefi hawakutuma askari wa kutosha au chakula. Moroni alikasirika na kuandika barua kwa Pahorani, kiongozi wa Wanefi.
Katika barua yake, Moroni alimuuliza Pahorani kwa nini hakutuma msaada. Moroni alifikiri Pahorani hakujali kuhusu watu na alitaka tu mamlaka. Moroni alitaka watu wake wawe huru.
Pahorani alihuzunika kwamba majeshi hayakuwa na msaada. Alitaka kumsaidia Moroni, lakini hakuweza. Baadhi ya Wanefi walikuwa wakipigana dhidi yake.
Wanefi hao waliitwa watu wa mfalme. Walitaka kuwa na nguvu kwa ajili yao wenyewe na kuwatawala watu. Walikuwa wamechukua serikali kutoka kwa Pahorani.
Pahorani alitaka kuendelea kuwaongoza Wanefi ili aweze kuwasaidia. Kama Moroni, alitaka Wanefi wamfuate Mungu na wawe na uhuru wao. Alitamani kwamba wasipigane na mtu yeyote. Lakini alikuwa tayari kupigana ikiwa itasaidia kuwaweka watu wake salama.
Pahorani aliwaomba Wanefi wamsaidie kupigana kulinda familia zao, uhuru wao, na haki yao ya kumwabudu Mungu. Alijua kwamba Roho wa Mungu angekuwa pamoja nao wakati walipochagua kupigania kile kilicho sahihi. Wanefi wengi walikuja kumsaidia Pahorani kuilinda nchi yao.
Pahorani alimwandika Moroni barua. Hakuwa amemkasirikia Moroni. Alimwambia Moroni kila kitu kinachoendelea. Alimuomba Moroni aje na amsaidie kupigana na watu wa mfalme. Pahorani alijua kwamba kama wangemfuata Mungu, hawakuhitaji kuogopa. Mungu angewalinda na kuwasaidia.
Moroni alijawa na tumaini kwa sababu ya imani ya Pahorani. Lakini alikuwa na huzuni kwamba baadhi ya Wanefi walikuwa wakipigana na watu wao wenyewe na hawakumtii Mungu. Moroni alichukua jeshi na kwenda kumsaidia Pahorani. Aliinua bendera ya uhuru kila mahali alipokwenda. Maelfu ya Wanefi waliamua kupigana ili kulinda uhuru wao.
Moroni na Pahorani waliwashinda watu wa mfalme na majeshi yao. Pahorani akawa kiongozi wa Wanefi tena. Moroni alituma watu wengi kusaidia majeshi ya Wanefi. Pia aliwatumia majeshi chakula Sasa kwamba Wanefi walikuwa na umoja, walishinda vita vingi. Walichukua miji mingi ya Wanefi kutoka kwa Walamani.