“Nefi Nabii,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Nefi Nabii
Kupata nguvu kubwa kutoka kwa Bwana
Kundi lililoitwa wezi wa Gadiantoni lilitawala mji wa Zarahemla. Waliahidi kusaidiana kufanya mambo mabaya. Waliwaibia na kuwaumiza watu ili wapate pesa na mamlaka. Wengi wa watu walijiunga na wanyang’anyi. Walitaka kuwa matajiri.
Helamani 6:15–24, 38–39; 7:4–5
Nabii Nefi aliishi Zarahemla. Nefi alisali kwa Mungu kwa sababu alikuwa na huzuni kwamba watu hawakuwa wakifuata amri za Mungu. Nefi aliwaomba watu wakumbuke yote ambayo Mungu aliwafanyia. Lakini watu wengi hawakusikiliza. Walijali zaidi kuhusu fedha na nguvu kuliko kumtii Mungu.
Nefi aliwaonya watu kuhusu wezi. Alisema walihitaji kutubu. Baadhi ya waamuzi wa Wanefi walikuwa wamejiunga na wanyang’anyi. Walimkasirikia Nefi na kusema alikuwa anadanganya. Walitaka watu pia wamkasirikie Nefi.
Nefi alisema kwamba Mungu huwaambia manabii Wake mambo mengi. Nefi aliwaambia kwamba manabii wote walifundisha kuhusu ujio wa Yesu Kristo. Alisema kwamba manabii waliwaonya watu kwamba Yerusalemu ingeangamizwa kama hawangetubu. Aliwasaidia kukumbuka kwamba Yerusalemu iliangamizwa.
Siku iliyofuata, waamuzi walimuuliza Nefi maswali ya kumtega. Nefi aliwaambia kuhusu uovu miongoni mwao. Baadhi ya watu walimwamini Nefi na walijua alikuwa nabii.
Wengine hawakuamini. Kila mmoja alibishana na mwenzake na kisha kuondoka. Nefi alifikiria kuhusu kile Bwana alichokuwa amemfundisha. Alihuzunika kwa sababu ya matendo mabaya ya watu.
Bwana alizungumza na Nefi. Alikuwa na furaha kwamba Nefi alikuwa amewafundisha watu. Kwa sababu ya jinsi Nefi alivyokuwa mtiifu, Bwana alimpa uwezo maalumu juu ya mambo ya duniani na mbinguni. Bwana alijua Nefi angetumia tu nguvu kuwasaidia watu kutubu.
Bwana alimwambia Nefi arudi kwa watu na awaambie watubu. Nefi alienda mara moja. Lakini watu walimkasirikia na hawakusikiliza.
Walijaribu kumweka Nefi gerezani. Lakini Roho wa Mungu alimsaidia Nefi kutoroka.
Nefi aliendelea kufundisha neno la Mungu. Watu bado hawakusikiliza. Walianza kubishana na kupigana wao kwa wao. Wezi walifanya mapigano kuwa mabaya zaidi. Punde, kulikuwa na vita katika kila mji. Watu wengi walikuwa wakiumia au kuuawa. Nefi alikuwa na huzuni. Hakutaka watu waangamizwe kwa vita.
Nefi alimwomba Mungu kusababisha baa kubwa la njaa ili watu wamkumbuke Bwana na kutubu. Hapakuwa na mvua kwa miaka mingi. Ardhi ilikuwa kavu, na mazao hayakukua. Watu walikuwa na njaa. Waliacha kupigana na kuanza kumkumbuka Bwana. Watu walitubu na kuwaondoa wezi.
Watu walimwomba Nefi kumuomba Bwana. Nefi aliona kwamba walikuwa wametubu na wezi walikuwa wameondoka. Alimwomba Bwana atume mvua. Bwana alijibu sala ya Nefi. Mvua ilinyesha, na mazao yakaanza kukua. Watu walimshukuru Mungu. Walijua Nefi alikuwa nabii na alikuwa na uwezo mkubwa kutoka kwa Mungu.