“Yesu Anawatembelea Watu,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Yesu Anawatembelea Watu
Kumsaidia kila mtu kumwamini Yeye
Watu wengi hawakuwasikiliza manabii wa Mungu. Lakini baadhi ya watu waliamini kile manabii walichofundisha. Waumini hawa walisubiri ishara za kifo cha Yesu Kristo.
Baada ya Yesu kufa Yerusalemu, ishara zilianza. Katika Amerika, kulikuwa na dhoruba, matetemeko ya ardhi, na moto kwa saa tatu. Miji iliharibiwa, na watu wengi walikufa. Kisha kulikuwa na giza totoro kwa siku tatu.
Giza lilikuwa totoro kiasi kwamba watu hawakuweza kuona jua, mwezi, au nyota. Hawakuweza hata kuwasha moto au mishumaa.
Watu wengi ambao bado walikuwa hai walikuwa na huzuni sana na kuogopa. Walilia na kusikitika kwamba walikuwa hawajatubu mapema.
Ghafla, walisikia sauti. Ilikuwa ni Yesu akizungumza nao. Aliahidi kumponya kila mtu aliyetubu. Yesu aliwaambia Alikuwa amekufa na kurudi tena kuwasaidia watu wote. Watu walishangaa sana kiasi kwamba waliacha kulia. Kulikuwa na ukimya katika nchi kwa saa nyingi.
Yesu alizungumza tena. Aliwaambia watu kwamba Angewasaidia kama wangechagua kumfuata Yeye. Giza liliondoka, na dunia ikaacha kutetemeka. Watu walikuwa na furaha na walimsifu Yesu.
Takribani mwaka mmoja baadaye, watu wengi walikuja hekaluni katika nchi ya Neema. Walizungumza kuhusu Yesu na ishara za kifo Chake. Wakiwa wanazungumza, walisikia sauti tulivu kutoka mbinguni. Mwanzoni, hawakuweza kuielewa. Kisha wakaisikia tena.
Waliposikia sauti mara ya tatu, walitazama kuelekea mbinguni. Alikuwa ni Baba wa Mbinguni akizungumza. Aliwaambia watu wamwone na kumsikiliza Mwanaye. Kisha watu wakamwona mtu katika joho jeupe akishuka chini kutoka mbinguni.
Mtu yule alisimama miongoni mwa watu na kusema, “Mimi ni Yesu Kristo.” Watu walianguka chini. Yesu aliwaambia Yeye alikuwa ameteseka na kufa kwa ajili ya kila mtu. Aliwaalika watu kugusa alama katika mikono Yake, miguu, na ubavu ili kwamba waweze kujua Yeye ni Mwokozi wa ulimwengu.
Watu walienda kwa Yesu mmoja mmoja. Waliona kwa macho yao wenyewe na kuhisi kwa mikono yao wenyewe alama mikononi Mwake, miguuni, na ubavuni Mwake. Wote walijua kwamba Yeye ndiye yule ambaye manabii walisema angekuja. Walijua Yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Watu walianguka miguuni mwa Yesu na kumwabudu.