“Yesu Anawafundisha Watu,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Yesu Anawafundisha Watu
Kuwasaidia kujifunza injili Yake
Watu katika Amerika walikuwa na furaha kumwona Yesu Kristo na kumsikia akifundisha. Walikuwa wamesubiri kwa miaka mingi ujio wa Mwokozi.
Yesu aliwafundisha mambo mengi sawa na yale aliyowafundisha watu karibu na Yerusalemu. Aliwafundisha kuwa na imani, kutubu, na kubatizwa. Kama watu wangefanya mambo haya, Mungu angewatumia Roho Mtakatifu. Yesu aliwafundisha jinsi ya kusali. Aliwaomba wawasamehe wengine. Aliwataka wawe mfano kwa wengine.
3 Nefi 11:31–39; 12:22–24, 44; 13:5–14; 17:8; 18:15–24
Yesu aliwaambia watu waende nyumbani na kumwomba Mungu ili awasaidie kuelewa kile alichowafundisha. Alisema atarudi tena siku iliyofuata.
Usiku ule, watu waliwaambia wengine kwamba walikuwa wamemwona Yesu. Walizungumza kuhusu kile alichosema na kukifanya. Watu wengi walisafiri usiku mzima kumwona Yesu.
Siku iliyofuata, watu walikusanyika na wanafunzi kumi na wawili wa Yesu. Wanafunzi waliwafundisha watu kila kitu ambacho Yesu alikuwa amekifundisha. Walipiga magoti ardhini na kusali.
Kisha Yesu alikuja. Alisali kwa ajili ya wanafunzi Wake na kwa ajili ya watu. Wanafunzi pia walisali. Walianza kung’aa kama Mwokozi. Yesu alikuwa na furaha. Wanafunzi walikuwa safi kwa sababu ya imani yao Kwake. Yesu alisali tena, na watu walimsikia akisema mambo ya kushangaza.
Kwa siku chache zilizofuata, Yesu aliwafundisha watu mambo mengi kuhusu mpango wa Baba wa Mbinguni. Pia alishiriki sakramenti pamoja nao. Watu wote katika nchi waliamini katika Yesu Kristo na walibatizwa. Walipokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Watu walisaidiana na kushiriki kila kitu walichokuwa nacho. Walifanya kila kitu Yesu alichowaamuru kukifanya. Waliitwa Kanisa la Kristo. Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walikuwa na furaha sana kwa watu.