“Yesu Anawabariki Watoto,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Yesu Anawabariki Watoto
Kuonyesha upendo Wake kwao
Yesu Kristo aliwafundisha watu mambo mengi. Aliona kwamba walihitaji muda kufikiria kuhusu kile walichojifunza. Aliwaomba waende nyumbani na kuomba kwa Baba wa Mbinguni ili waelewe kile Alichowafundisha. Kisha Yesu aliahidi kuwatembelea tena siku iliyofuata.
Watu walilia kwa sababu walimtaka Yesu abakie zaidi. Yesu aliwapenda watu. Aliweza kuona kwamba imani yao ilikuwa imara sana. Aliwaambia wawalete Kwake watu waliokuwa wagonjwa au waliokuwa wanaumia kwa njia yoyote. Alitaka kuwaponya kila mmoja wao.
Watu walienda Kwake na wanafamilia wao wagonjwa na marafiki. Yesu alimponya kila mmoja wao. Walikuwa na furaha. Walipiga magoti na kuibusu miguu Yake.
Yesu aliwaomba wawalete watoto wao wadogo Kwake. Watu waliwaleta watoto wao na kuwaweka chini karibu na Yesu.
Baada ya watoto wote kuwepo pamoja Naye, Yesu aliwaomba watu kupiga magoti. Alipiga magoti pia. Kisha alisali kwa Baba wa Mbinguni. Alisema vitu vya kushangaza ambavyo maneno Yake hayangeweza kuandikwa. Watu walijawa na furaha.
Yesu aliwaambia watu kwamba walibarikiwa kwa sababu ya imani yao Kwake. Yesu alihisi shangwe nyingi kiasi kwamba alianza kulia.
Kisha Yesu akambariki kila mtoto, mmoja mmoja. Aliomba kwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya kila mmoja wao. Kisha aliwaomba watu wawaangalie watoto wao.
Malaika walikuja kutoka mbinguni na kukusanyika kuwazunguka watoto. Wakati malaika walipowabariki watoto, nuru ya mbinguni iliwazunguka. Katika siku nyingine, Yesu alikutana na watoto na kuwabariki tena. Pia aliwabariki watoto kuweza kuzungumza. Hata watoto wachanga walizungumza. Watoto waliwafundisha wazazi wao mambo ya kushangaza.