“Yesu Anashiriki Sakramenti,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni (2023)
Yesu Anashiriki Sakramenti
Daima kumkumbuka Yeye
Baada ya Yesu kuwaponya wagonjwa na kuwabariki watoto wadogo, Alianzisha sakramenti kwa watu wote waliokusanyika kumsikiliza Yeye. Aliwaomba wanafunzi Wake walete mkate na divai.
Yesu alimega mkate na kuubariki. Aliwapa wanafunzi kuula. Aliwaomba wanafunzi kutoa mkate kwa watu wote.
Yesu alisema kila mtu aliyemwamini na kubatizwa anapaswa kula mkate. Wanapofanya hivyo, wanapaswa kukumbuka mwili Wake. Aliwakumbusha watu kuhusu wakati walipohisi alama za misumari katika mikono na miguu Yake na jeraha ubavuni Mwake.
Kisha Yesu akawapa wanafunzi divai ili wanywe. Aliwaomba wanafunzi kutoa divai kwa watu wote.
Yesu alisema kila mtu aliyetubu na kubatizwa anapaswa kunywa divai. Alimuomba kila mtu aliyekunywa divai akumbuke damu Yake. Aliwakumbusha kwamba Alitoa damu Yake wakati alipoteseka na kufa kwa ajili yao.
Yesu alisema kwamba kula mkate na kunywa divai ilikuwa ni amri. Kwa kula mkate na kunywa divai, watu walimwonyesha Baba wa Mbinguni kwamba walitaka kutii amri Zake na kumkumbuka Yesu. Yesu alisema watabarikiwa kwa Roho Mtakatifu kama wangefanya mambo haya.
Baada ya watu kula mkate na kunywa divai, walijazwa na Roho Mtakatifu. Kisha watu wakamsifu Yesu.