Njoo, Unifuate
Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani


“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani,” Njoo, Unifuate——Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)

“Kutumia Njoo, Unifuate,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025

wanandoa wakijifunza pamoja

Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani

Nyenzo Hii Ni Kwa Ajili ya Nani?

Nyenzo hii ni kwa ajili ya mtu yeyote anayetaka kujifunza Mafundisho na Maagano—kama mtu binafsi, kama familia na katika madarasa ya Kanisa. Kama hukuwa ukijifunza maandiko mara kwa mara huko nyuma, nyenzo hii inaweza kukusaidia uanze. Kama tayari una mazoea mazuri ya kujifunza maandiko, nyenzo hii inaweza kukusaidia upate uzoefu mwingi wenye maana.

Watu Binafsi na Familia Nyumbani

Mahali pazuri pa kujifunza injili ni nyumbani. Walimu wako kanisani wanaweza kukusaidia, na unaweza kupata uhamasisho kutoka kwa waumini wengine wa kata. Lakini kunusurika kiroho, kila mmoja wetu anahitaji kulishwa kutokana na “neno jema la Mungu” (Moroni 6:4: ona pia Russell M. Nelson, “Maneno ya Ufunguzi,” Liahona, Nov. 2018, 6–8).

Tumia nyenzo hii katika njia yoyote ambayo inakusaidia wewe. Miuhtasari hii inaonyesha baadhi ya kweli za milele zinazopatikana katika Mafundisho na Maagano. Pia inapendekeza mawazo na shughuli ili kukusaidia wewe kujifunza maandiko wewe binafsi, pamoja na wanafamilia, au pamoja na marafiki. Unapojifunza, fuata mwongozo wa Roho ili kupata kweli za milele ambazo zinaleta maana kwako. Tafuta jumbe za Mungu kwa ajili yako, na kufuata misukumo unayopokea.

Walimu na Wanafunzi Kanisani

Kama unafundisha darasa la Msingi, vijana au darasa la watu wazima la Shule ya Jumapili, akidi ya Ukuhani wa Haruni, au darasa la Wasichana, unahimizwa kutumia miuhtasari katika nyenzo hii unapojiandaa kufundisha. Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani ni mtaala kwa ajili ya darasa lako la Jumapili. Mawazo katika nyenzo hii yamesanifiwa kwa ajili ya kujifunza nyumbani na kanisani. Unapojiandaa kufundisha, anza kwa kuwa na uzoefu wako mwenyewe katika maandiko. Maandalizi yako muhimu zaidi yatatokea wakati unapopekua maandiko na kutafuta mwongozo binafsi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Unaweza pia kujifunza ukiwa na mahitaji ya watu unaowafundisha katika akili yako. Tafuta kweli za milele. Njoo, Unifuate inaweza kukusaidia wewe kutambua baadhi ya kweli hizi na kujifunza jinsi maandiko yanaweza kutumika katika maisha yako.

Kumbuka kwamba kujifunza injili, katika ubora wake, ni inapokuwa kitovu chake ni nyumbani na kusaidiwa na Kanisa. Kwa maneno mengine, jukumu lako kubwa ni kuwasaidia watu unaowafundisha katika juhudi zao za kujifunza na kuishi injili nyumbani. Usijali kuhusu kuwa na maudhui ya kipekee ya kuwapa wao darasani. Badala yake, wape fursa ya kushiriki uzoefu wao, mawazo, na maswali kuhusu vifungu vya maandiko walivyosoma nyumbani. Waalike washiriki kweli za milele walizozipata. Hii ni muhimu zaidi kuliko kusoma tu kiasi fulani cha maelezo.

Madarasa ya Shule ya Jumapili ya Vijana na Watu Wazima

Moja ya sababu kuu ya sisi kukutana katika madarasa ya Shule ya Jumapili ni kusaidiana na kutiana moyo pale tunapojitahidi kumjua na kumfuata Yesu Kristo. Njia rahisi tunayoweza kufanya hivyo ni kuuliza swali kama vile “Roho Mtakatifu amekufundisha nini wiki hii wakati ulipojifunza maandiko ukitumia Njoo, Unifuate?” Majibu ya swali hili yangeweza kuongoza kwenye majadiliano yenye maana ambayo yanajenga imani katika Yesu Kristo na Injili Yake.

Kisha ungeweza kualika majadiliano yaliyojikita kwenye mapendekezo ya kujifunza katika Njoo, Unifuate. Kwa mfano, wazo la kujifunza lingeweza kupendekeza kupekua Mafundisho na Maagano 19:15–20, mkitafuta jinsi gani Mwokozi anaelezea mateso Yake. Ungeweza kuwaalika washiriki wa darasa kushiriki jinsi wao walihisi waliposoma maelezo Yake na kuzungumza kuhusu jinsi hili huathiri namna wao wanavyofikiri kumhusu Yeye. Ama mngeweza kutumia sehemu ya muda kujifunza mistari hii pamoja kama darasa.

Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana

Wakati akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana wanapokutana Jumapili, dhumuni lao ni tofauti kiasi fulani na darasa la Shule ya Jumapili. Kama nyongeza ya kusaidiana kujifunza injili ya Yesu Kristo, makundi haya pia yanakutana ili kushauriana pamoja kuhusu kutimiza kazi ya wokovu na kuinuliwa (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 1.2), kama wanavyoelekezwa na urais wao wa akidi au darasa.

Kwa sababu hii, kila mkutano wa akidi au darasa unapaswa kuanza na mshiriki wa urais wa akidi au darasa akiongoza majadiliano kuhusu juhudi zao. Kwa mfano, wangeweza kushauriana pamoja kuhusu juhudi zao za kuishi injili, kuwatumikia watu walio katika shida, kushiriki injili, au kushiriki katika kazi ya hekalu na historia ya familia.

Baada ya muda huu wa kushauriana pamoja, mwalimu anaongoza darasa au akidi katika kujifunza injili pamoja. Viongozi watu wazima au washiriki wa darasa au akidi wanaweza kupangiwa kufundisha. Urais wa darasa au akidi, ukishauriana na viongozi watu wazima, hupanga majukumu haya.

Watu waliopangiwa kufundisha wanapaswa kujiandaa kwa kutumia mapendekezo ya kujifunza katika muhtasari wa kila wiki wa Njoo, Unifuate. Katika kila muhtasari, ikoni hii ikoni ya seminarihuonyesha shughuli ambayo hasa inafaa kwa vijana na inahusiana na kile wanachojifunza katika seminari. Hata hivyo, mapendekezo yoyote katika muhtasari huu yanaweza kutumiwa kama shughuli kwa ajili ya vijana.

Kwa ajili ya mfano wa ajenda za mikutano ya akidi na madarasa, ona kiambatisho D.

Msingi

Maandalizi yako kwa ajili ya kufundisha Msingi huanza kwa kujifunza kwako maandiko wewe binafsi na pamoja na familia yako. Unapofanya hivyo, sikiliza misukumo ya kiroho na umaizi kutoka kwa Roho Mtakatifu kuhusu watoto katika darasa lako la Msingi. Kuwa mwenye kusali. Roho anaweza kukupa mwongozo wa kiungu na mawazo ili uwasaidie wao wajifunze injili ya Yesu Kristo.

Unapojiandaa kufundisha, unaweza kupata mwongozo wa kiungu wa ziada kwa kuchunguza mawazo ya kufundishia katika nyenzo hii. Kila muhtasari katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani una sehemu yenye kichwa cha habari “Mawazo kwa Ajili ya Kuwafundisha Watoto.” Fikiria mawazo haya kama mapendekezo ya kuchochea kupata mwongozo wako wa kiungu. Unawajua watoto katika darasa lako la Msingi—na utapata kuwajua hata vizuri zaidi pale unapochangamana nao darasani. Bwana anawajua pia, na Yeye atakupa mwongozo wa kiungu wa njia iliyo bora zaidi ya kuwafundisha na kuwabariki.

Watoto katika darasa lako wanaweza kuwa tayari wamefanya baadhi ya shughuli hizi katika Njoo, Unifuate pamoja na familia zao. Hiyo ni SAWA. Kurudia rudia ni vyema. Zingatia kuwaalika watoto kushiriki wao kwa wao kile walichojifunza nyumbani. Unapaswa pia kupanga njia za watoto kushiriki hata kama hawakujifunza nyumbani. Watoto hujifunza kweli za injili kwa ufanisi zaidi wakati kweli hizi zinapofundishwa kwa kurudiwa rudiwa kupitia shughuli mbalimbali. Ikiwa unaona kuwa shughuli fulani ya kujifunza inafaa kwa watoto, fikiria kuirudia, hasa ikiwa unawafundisha watoto wadogo zaidi.

Katika miezi ambayo ina Jumapili tano, walimu wa Msingi wanahimizwa kubadilisha muhtasari wa Njoo, Unifuate uliopangwa kwenye Jumapili ya tano kwa shughuli moja au zaidi za kujifunza katika “Kiambatisho B: Kwa ajili ya Msingi—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote Kwenye Njia ya Agano ya Mungu.”