“Januari 6–12: “Sikilizeni, Enyi Watu”: Mafundisho na Maagano 1,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 1,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Januari 6–12: “Sikilizeni, Enyi Watu”
Mafundisho na Maagano 1
Mnamo Novemba 1831, Kanisa lililorejeshwa la Yesu Kristo lilikuwa na mwaka mmoja na nusu tu. Ingawa lilikuwa linakua, lilikuwa bado kundi lisilojulikana la waumini wanaoishi katika miji midogo, wakiongozwa na nabii aliye katika umri wa miaka katikati ya ishirini. Lakini Mungu aliwafikiria waumini hawa kuwa ni watumishi Wake, na wajumbe Wake, na Yeye alitaka mafunuo aliyowapa yahubiriwe kwa ulimwengu.
Mafundisho na Maagano 1 ni utangulizi wa Bwana au dibaji, ya mafunuo haya. Kwa uwazi inaonesha kwamba japokuwa idadi ya waumini wa Kanisa ilikuwa ndogo, hapakuwa na chochote kidogo kuhusu ujumbe ambao Mungu alitaka Watakatifu Wake washiriki. Ni “sauti ya onyo” kwa ajili ya “wakazi wote wa dunia,” ikiwafundisha kutubu na kuanzisha “agano la milele” la Mungu (mstari wa 4, 8, 22). Watumishi wanaobeba ujumbe huu ni “wadhaifu na wa kawaida.” Lakini watumishi wanyenyekevu ndiyo wale tu Mungu anaowaita—wakati ule na sasa—kulileta Kanisa “kutoka lisikoonekana na kutoka gizani” (mstari wa 23, 30).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
“Sikilizeni, Enyi Watu”
Dibaji inatambulisha kitabu. Inaainisha dhamira na makusudi ya kitabu na kusaidia wasomaji kujiandaa kusoma. Unaposoma sehemu ya 1—“dibaji” ya Bwana kwenye Mafundisho na Maagano (mstari wa 6)—tafuta dhamira na makusudi Bwana aliyotoa kwa ajili ya mafunuo Yake. Je, wewe unajifunza nini ambacho kitakusaidia katika kujifunza kwako Mafundisho na Maagano mwaka huu? Kwa mfano, unaweza kutafakari inamaanisha nini “kusikia sauti ya Bwana” katika mafunuo haya (mstari wa 14) au “kuchunguza amri hizi” (mstari wa 37).
Ona pia utangulizi kwa Mafundisho na Maagano.
Mafundisho na Maagano 1:4–6, 23–24, 37–39
Bwana anazungumza kupitia watumishi Wake, ikijumuisha manabii watakatifu wa siku za mwisho.
Sehemu ya 1 inaanza na kumalizika kwa tangazo la Bwana kwamba Anazungumza kupitia watumishi Wake wateule (ona mstari wa 4–6, 23–24, 38). Andika kile unachojifunza kutoka kwenye ufunuo huu kuhusu:
-
Bwana na sauti Yake.
-
Kwa nini manabii wanahitajika katika siku yetu.
Je, unahisi kushawishiwa kufanya nini kama matokeo ya kile unachokitafuta?
Ni lini umesikia sauti ya Bwana kupitia sauti ya watumishi Wake? (Ona mstari wa 38).
Ungeweza pia kufikiria kwamba rafiki ambaye hajui kuhusu manabii walio hai anasoma sehemu ya 1 pamoja na wewe. Je, ni maswali gani yawezekana rafiki yako akawa nayo? Ni mistari gani ungetaka kujadiliana na rafiki yako ili kumsaidia kuelewa jinsi gani unavyohisi kuhusu kuwa na manabii katika siku yetu?
Yawezekana ukapendelea kujua kwamba wakati baraza la wazee lilipokutana katika mwaka 1831 ili kuzungumza kuhusu uchapishaji wa mafunuo ya Joseph Smith, baadhi ya watu walipinga wazo hilo. Waliona aibu kwa ajili ya udhaifu wa Joseph katika kuandika, na walikuwa na wasiwasi kwamba kuchapisha ufunuo huo kungeweza kukasababisha matatizo zaidi kwa Watakatifu (ona Watakatifu, 1:140–43). Ikiwa ungekuwa wewe ni mshiriki wa baraza hili, je, ungetatuaje mashaka haya? Je, ni utambuzi gani unaupata katika sehemu ya 1 ambayo ingeweza kusaidia? (ona, kwa mfano, mstari wa 6, 24, 38).
Fikiria kujumuisha wimbo kama “Msikilize Nabii” (Nyimbo za Dini, na. 16) katika kujifunza na kuabudu kwako. Tafuta kirai katika wimbo ambacho kinafundisha kanuni hizo hizo kama mistari katika sehemu ya 1.
Ona pia Mada na Maswali, “Manabii,” Maktaba ya Injili.
Mafundisho na Maagano 1:12–30, 34–36
Urejesho unanisaidia mimi kukabiliana na changamoto za siku za mwisho.
Katika Mafundisho na Maagano sehemu ya 1, Bwana anafafanua kwa nini amerejesha Injili Yake. Ona ni sababu ngapi unaweza kuziorodhesha unaposoma mstari wa 12–23. Katika uzoefu wako, ni kwa jinsi gani madhumuni ya Bwana ya Urejesho yanakamilika?
Bwana alijua kwamba siku yetu ingekuwa na changamoto kali (ona mstari wa 17). Unapata nini katika mstari wa 17–30, 34–36 ambacho kinakusaidia wewe kuhisi amani na kujiamini licha ya changamoto hizi?
Ona pia Russell M. Nelson, “Kumbatia Siku za Usoni kwa Imani,” Liahona, Nov. 2020, 73–76.
Bwana hutumia “walio dhaifu na wa kawaida” kutekeleza kazi Yake.
Unaposoma Mafundisho na Maagano 1:19–28, unaweza kutafakari inamaanisha nini kuwa mtumishi wa Bwana. Je, ni sifa gani Bwana anataka watumishi Wake kuwa nazo? Bwana anatekeleza nini kupitia watumishi Wake? Ni kwa jinsi gani unabii katika mistari hii unatimizwa kote ulimwenguni na katika maisha yako?
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Mafundisho na Maagano 1:4, 37–39
Kupitia manabii Wake, Bwana ananionya mimi juu ya hatari ya kiroho.
-
Ili kuanzisha majadiliano kuhusu maonyo kutoka kwa Bwana, ungeweza kuzungumza kuhusu maonyo tunayopokea kutoka kwa watu wengine kuhusu hatari tunazoweza kuziona. Baadhi ya mifano inaweza kujumuisha sakafu yenye kuteleza, dhoruba inayokuja au gari linalokuja kwa kasi. Pengine wewe na watoto wako mngeweza kutazama mifano ya alama za maonyo na kulinganisha maonyo hayo na maonyo ambayo Bwana hutupatia sisi. Kulingana na Mafundisho na Maagano 1:4–6, 37–39, ni kwa jinsi gani Bwana anatuonya sisi? Je, Yeye ametuonya kuhusu nini hivi karibuni? Pengine ungeweza kuangalia au kusoma sehemu za jumbe za mkutano mkuu wa hivi karibuni na kutafuta mifano ya “sauti ya kuonya” ya Mungu.
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu manabii, kama vile ubeti wa mwisho wa “Follow the Prophet” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 111). Shiriki ushuhuda wako kwamba nabii huzungumza neno la Mungu.
Urejesho unanisaidia mimi kukabiliana na changamoto za siku za mwisho.
-
Ili kuhimiza majadiliano kuhusu Mafundisho na Maagano 1:17, wewe na watoto wako mngeweza kufikiria kuwa mnajiandaa kwa safari. Je, mngefungasha vitu gani? Kama mngelijua mapema kwamba mvua ingenyesha au kwamba gari lenu au basi lingepeta pancha, je, ni kwa jinsi gani hilo lingeathiri njia ambayo ninyi mngejiandaa kwa safari hiyo? Someni pamoja mstari wa 17, na zungumzeni kuhusu kitu ambacho Bwana alijua kingekuja kutokea kwetu sisi. Je, Yeye alijiandaaje kwa ajili ya hilo? (Kama ni muhimu, elezea kwamba “janga” ni madhara au kitu cha kuogofya.) Ni kwa jinsi gani amri za Mungu hutusaidia kukabiliana na changamoto za wakati wetu?
Mafundisho na Maagano 1:17, 29
Bwana alimwita Joseph Smith kuwa nabii.
-
Ili kujifunza kuhusu kazi ya Joseph Smith katika kurejesha injili ya Mwokozi, wewe na watoto wako mngeweza kuangalia picha ya Mwokozi na picha ya Joseph Smith (ona picha hizo katika muhtasari huu) na zungumzeni kuhusu Mwokozi ametupatia nini kupitia Joseph Smith. Watoto wako wangeweza kutafuta mifano katika Mafundisho na Maagano 1:17, 29. Waambie watoto wako jinsi gani wewe unajua kwamba Mungu “alimwita mtumishi wangu Joseph Smith, Mdogo, na kusema naye kutoka mbinguni” (mstari wa 17).
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni kanisa la Bwana la “kweli na lililo hai.”
-
Inamaanisha nini kusema kwamba kanisa ni la “kweli na lililo hai”? Ili kuwafanya watoto wako wafikirie kuhusu swali hili, labda ungewaonesha picha za vitu vilivyo hai na vitu visivyo hai-kama vile mmea ulio hai na mmea ulikufa. Je, tunajuaje kitu fulani kiko hai? Kisha mngeweza kusoma mstari wa Mafundisho na Maagano 1:30 na kuzungumza kuhusu inamaanisha nini kwa Kanisa kuwa la “kweli na lililo hai”