“Sauti za Urejesho: Familia ya Joseph Smith,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Familia ya Joseph Smith,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Sauti za Urejesho
Familia ya Joseph Smith
Kila mmoja wetu anaathiriwa kwa kina na maisha yetu ya kifamilia, na Joseph Smith hakuwa tofauti. Msimamo wa kidini wa wazazi wake na desturi vilipanda mbegu za imani ambazo zilifanya Urejesho uwezekane. Shajara ya Joseph Smith inarekodi shukrani hii: “Maneno na lugha havitoshelezi kuelezea shukrani niliyonayo kwa Mungu kwa kunipa uzazi wa heshima sana.”
Nukuu zifuatazo kutoka kwa mama yake, Lucy Mack Smith; kaka yake William Smith; na Nabii mwenyewe zinatupa mtazamo wa mara moja kwenye ushawishi wa kidini katika nyumba ya akina Smith.
Lucy Mack Smith
“[Yapata mwaka 1802], nilikuwa mgonjwa. … Nilijiambia mwenyewe, sijajitayarisha kufa kwani sijui njia za Kristo, na ilionekana kwangu kama vile kulikuwa na korongo la upweke na giza kati yangu na Kristo ambalo sithubutu kujaribu kulivuka. …
“Nilimtazamia Bwana na niliomba na kumsihi Bwana kwamba angeyanusuru maisha yangu ili niweze kuwalea watoto wangu na kufariji moyo wa mume wangu; hivyo nilijilaza usiku kucha. … Nilifanya ahadi na Mungu [kwamba] kama angeniacha niishi ningefanya bidii kupata ile dini ambayo ingeniwezesha kumtumikia kwa usahihi, bila kujali ingekuwa katika Biblia au kama ingeweza kutafutwa, hata kama ingeweza kupatikana kutoka mbinguni kwa sala na imani. Hatimaye sauti ilizungumza nami na kusema, ‘Omba na utapata, bisha na utafunguliwa. Acha moyo wako ufarijiwe. Unamwamini Mungu, niamini na mimi pia.’ …
“Kutoka wakati huu na kuendelea nilipata nguvu endelevu. Nilisema japo kidogo juu ya mada ya dini ingawa ilijaza fikra zangu zote, na nilifikiri kwamba ningefanya bidii yote mara nitakapoweza kumtafuta mtu fulani mwenye kumcha Mungu aliyejua njia za Mungu kunifundisha mambo ya Mbinguni.”
William Smith
“Mama yangu, ambaye alikuwa mwanamke mcha Mungu sana na mwenye kupenda ustawi wa watoto wake, kote hapa na baada ya hapa, alitumia kila uwezo ambao upendo wake wa mzazi ungeweza kupendekeza, kutufanya tujishughulishe katika kuomba kwa ajili ya wokovu wa nafsi zetu, au (kama neno lilivyokuwa wakati huo) ‘katika kupata dini.’ Alitushawishi kuhudhuria mikutano, na takribani familia yote ikapenda jambo hilo, na kuwa watafutaji wa ukweli.”
“Siku zote tulikuwa na sala za familia kwa kadiri ninavyoweza kukumbuka. Ninakumbuka vizuri baba alikuwa na desturi ya kubeba miwani yake katika mfuko wa fulana yake, … na wakati sisi wavulana tulipomwona akipapasa miwani yake, tulijua ile ilikuwa ishara ya kuwa tayari kwa ajili ya sala, na kama hatukugundua mama angesema, ‘William,’ au yeyote yule aliyekuwa mzembe, ‘jitayarishe kwa ajili ya sala.’ Baada ya sala kulikuwa na wimbo ambao tungeimba.”
Joseph Mkubwa na Lucy Smith walifundisha familia yao kusoma maandiko.
Joseph Smith
“Sasa ninasema, kwamba [baba yangu] kamwe hakufanya tendo la uchoyo ambalo lingesemekana si la ukarimu, katika maisha yake, kwa ufahamu wangu. Nilimpenda baba yangu na kumbukumbu yake; na kumbukumbu ya matendo yake mema, huja kwa uzito mkubwa juu ya akili zangu; na mengi ya maneno yake ya ukarimu na ya mzazi kwangu, yameandikwa juu ya kibao cha moyo wangu. Matakatifu kwangu, ni mawazo ambayo ninayahifadhi ya historia ya maisha yake, ambayo yamezunguka akili zangu na yamepandikizwa, kwa kufuatilia kwangu mwenyewe tangu nilipozaliwa. … Mama yangu pia ni mmoja wa waadilifu, na bora zaidi ya wanawake wote.”