“Sauti za Urejesho: Tafsiri ya Kitabu cha Mormoni,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Tafsiri ya Kitabu cha Mormoni,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Sauti za Urejesho
Tafsiri ya Kitabu cha Mormoni
Mnamo Aprili 1829, mwezi ambao sehemu ya 6–9 ya Mafundisho na Maagano zilipokelewa, kazi kubwa ya Joseph Smith ilikuwa kutafsiri Kitabu cha Mormoni. Hatujui maelezo mengi kuhusu mchakato wa kimiujiza wa kutafsiri, lakini tunajua ya kwamba Joseph Smith alikuwa mwonaji, akisaidiwa na vyombo ambavyo Mungu alikuwa amevitayarisha: mawe mawili angavu yaliyoitwa Urimu na Thumimu na jiwe lingine lililoitwa jiwe la mwonaji.
Wakati alipoombwa baadaye kutoa maelezo ya jinsi rekodi hii ilivyotafsiriwa, Joseph alisema “kwamba haikukusudiwa kuueleza ulimwengu kila kitu.” Mara kwa mara alisema kiurahisi tu kwamba kilitafsiriwa “kwa karama, na uwezo wa Mungu.”
Maelezo yafuatayo, kutoka kwa mashahidi walioshuhudia kwa macho yao mchakato wa kutafsiri, wanaunga mkono ushahidi wa Joseph.
Emma Smith
“Wakati mume wangu alipokuwa anatafsiri Kitabu cha Mormoni, niliandika sehemu yake, alipokuwa anatoa imla ya kila sentensi, neno kwa neno, na alipofika kwenye majina halisi hakuweza kuyatamka, au maneno marefu, alitaja herufi, na wakati nilipokuwa nikiziandika, kama nilifanya makosa katika tahajia, angenisimamisha na kusahihisha tahajia yangu ingawa ilikuwa haiwezekani kwa yeye kuona jinsi nilivyokuwa nayaandika wakati ule. Hata neno Sarah hakuweza kulitamka mara ya kwanza, lakini ilibidi atoe herufi zake, na nililitamka kwa ajili yake.”
“Mabamba mara kwa mara yaliwekwa kwenye meza bila jaribio lolote la kuyaficha, yalifungwa kwenye kitambaa kidogo cha kitani cha meza, ambacho nilimpa kuyafungia. Mara moja nilihisi mabamba, wakati yalipowekwa mezani, nikifuatisha mipaka yake na maumbo yake. Yakionekana kuwa ya kupindika kiurahisi kama karatasi nene, na yangetoa sauti kama ya chuma wakati ncha zake ziliposogezwa kwa kidole gumba, kama vile wakati mwingine unaposogeza ncha za kitabu. …
“Imani Yangu ni kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha uhalisia mtakatifu—sina wasiwasi hata kidogo juu ya hilo. Nimeridhika kwamba hakuna mtu ambaye angeweza kutolea imla uandikaji wa miswada ile isipokuwa alikuwa ameongozwa kiungu; kwani, wakati nikiwa kama mwandishi wake, [Joseph] alitoa imla kwangu saa baada ya saa; na wakati wa kurejea baada ya chakula, au baada ya shughuli, mara moja angeanzia pale alipoachia, bila kuangalia muswada au kutaka sehemu yake kusomwa kwake. Hili lilikuwa jambo la kawaida kwake kufanya. Isingekuwa rahisi kwa mtu mwenye elimu kufanya hivyo; na, kwa mtu mjinga na asiye na elimu kama alivyokuwa, ilikuwa ni haiwezekani kabisa.”
Oliver Cowdery
“Niliandika kwa kalamu yangu mwenyewe Kitabu cha Mormoni chote (isipokuwa kurasa chache) kama yalivyotoka kutoka kwenye mdomo wa nabii, alipokuwa anakitafsiri kwa karama na uwezo wa Mungu, kwa njia ya Urimu na Thumimu, au, kama vinavyoitwa na kitabu, vikalimani vitakatifu. Niliona kwa macho yangu, na kushika kwa mikono yangu, mabamba ya dhahabu ambayo kwayo kitabu kilitafsiriwa. Pia niliona vikalimani hivyo.”