“Sauti za Urejesho: Emma Hale Smith,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Emma Hale Smith,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Sauti za Urejesho
Emma Hale Smith
Maneno ya Bwana kwa Emma Smith yaliyorekodiwa katika Mafundisho na Maagano 25 yanafunua jinsi Bwana alivyohisi kumhusu yeye na michango ambayo angeweza kufanya kwenye kazi Yake. Lakini Emma alikuwa mtu wa namna gani? Tunajua nini kuhusu tabia yake, mahusiano yake, nguvu zake? Njia moja ya kuweza kumjua “mwanamke huyu mteule” (Mafundisho na Maagano 25:3) ni kusoma maneno ya watu ambao walimjua binafsi.
Joseph Smith, Mdogo, mumewe Emma
“Pamoja na furaha isiyoelezeka, na ni safari ya furaha iliyoje iliyojaa kifuani mwangu, wakati nilipomchukua kwa mkono wangu, usiku ule, mpendwa wangu Emma—ambaye alikuwa mke wangu, hata mke wa ujana wangu; na chaguo la moyo wangu. Nyingi zilikuwa ngurumo za akili zangu wakati nilipotafakari kwa muda matukio mengi tuliyoitwa kuyapitia. Uchovu, na kazi za taabu, huzuni, na mateso, na furaha na faraja ya mara kwa mara vilitawanyika katika njia zetu na vikapendezesha jukwaa letu. Ee! ni mchanganyiko gani wa mawazo uliijaza akili yangu kwa muda. Tena yuko hapa, hata katika matatizo makubwa, bila kukata tamaa, imara, na bila kutetereka, asiyebadilika, Emma mwenye moyo wa kupenda.”
Lucy Mack Smith, mama mkwe wake Emma
“Emma wakati huo alikuwa kijana, na, kwa asili mwenye ari, moyo wake wote ulikuwa katika kazi ya Bwana, na alihisi kutokupenda kingine chochote isipokuwa kanisa na kusudi la ukweli. Chochote mikono yake ilichopata kufanya, alifanya kwa uwezo wake na hakuuliza maswali ya kichoyo ‘Je, nitanufaika zaidi kuliko yeyote yule?’ Kama wazee wangepelekwa mbali kuhubiri, alikuwa wa kwanza kujitolea huduma zake kusaidia katika kuwapa mavazi kwa ajili ya safari zao, kuacha ufukara wake mwenyewe uwe kile unachoweza kuwa.”
Joseph Smith, Mkubwa, baba mkwe wake Emma
Baraka za kipatriaki za Emma, zilizotamkwa na Joseph Smith, Mkubwa, ambaye alikuwa anahudumu kama patriaki wa Kanisa:
“Emma, mkwe wangu, umebarikiwa na Bwana, kwa ajili ya uaminifu wako na ukweli: utabarikiwa pamoja na mumeo, na kufurahi katika utukufu ambao utakuja juu yake: Nafsi yako imeteseka kwa sababu ya uovu wa binadamu katika kutafuta maangamizo ya mwenza wako, na nafsi yako yote imetolewa katika sala kwa ajili ya ukombozi wake: shangilia, kwani Bwana Mungu wako amesikia maombi yako.
“Umehuzunishwa na ugumu wa mioyo ya nyumba ya baba yako, na umetamani wokovu wao. Bwana ataheshimu kilio chako, na kwa hukumu zake atasababisha baadhi yao kuona upumbavu wao na kutubu dhambi zao; lakini itakuwa kwa mateso kwamba wataokolewa. Utaishi siku nyingi; ndio, Bwana atakutunza mpaka utakapotosheka, kwani utamwona Mkombozi wako. Moyo wako utashangilia katika kazi kubwa ya Bwana, na hakuna yeyote atakayeitwa shangwe yako.
“Utakumbuka siku zote rehema kuu za Mungu wako katika kukuruhusu wewe kuandamana na mwanangu wakati malaika alipotoa kumbukumbu ya Wanefi kwenye uangalizi wake. Umeona huzuni nyingi kwa sababu Bwana amewachukua watoto wako watatu: katika hili wewe hutalaumiwa, kwani anajua tamaa zako safi za kulea familia, kwamba jina la mwanangu liweze kubarikiwa. Na sasa, tazama, ninakuambia, kwamba hivi ndivyo asemavyo Bwana, kama utaamini, bado utabarikiwa katika jambo hili na utapata watoto wengine, kwa ajili ya shangwe na kuridhika kwa nafsi yako, na kwa shangwe ya rafiki zako.
“Utabarikiwa kwa ufahamu, na kuwa na nguvu ya kuelekeza jinsia yako. Fundisha familia yako uadilifu, na njia njema ya maisha kwa watoto wako, na malaika watakatifu watakulinda: na utaokolewa katika ufalme wa Mungu; hivyo ndivyo. Amina.”