Aprili 7–13: ‘Pazeni Sauti Zenu … ili Kutangaza Injili Yangu’: Mafundisho na Maagano 30–36” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 30–36,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Aprili 7–13: “Pazeni Sauti Zenu … ili Kutangaza Injili Yangu”
Mafundisho na Maagano 30–36
Parley P. Pratt alikuwa muumini wa Kanisa kwa takribani mwezi mmoja wakati alipoitwa “nyikani” kuhubiri injili (Mafundisho na Maagano 32:2). Thomas B. Marsh alikuwa muumini kwa muda mfupi kuliko huo wakati alipoambiwa, “Saa ya huduma yako imewadia” (Mafundisho na Maagano 31:3). Orson Pratt, Edward Partridge, na wengine wengi kadhalika walikuwa ndio kwanza wamebatizwa wakati miito ya misheni yao ilipokuja. Labda kuna somo hapo katika mpangilio huu kwa ajili yetu leo: kama unajua vya kutosha kukubali injili ya urejesho kwa ubatizo, unajua vya kutosha kuishiriki na wengine. Ndiyo, daima tunataka kuongeza ufahamu wetu wa injili, lakini Mungu kamwe hajasita kuwaita “wasio na elimu” kuhubiri injili Yake (Mafundisho na Maagano 35:13). Kwa kweli, Yeye anatualika sisi sote, “Fungueni vinywa vyenu na kutangaza injili yangu” (Mafundisho na Maagano 30:5). Na tunafanya hivyo vizuri sana sio kwa kupitia hekima yetu wenyewe na uzoefu bali “kwa uwezo [wa] Roho” (Mafundisho na Maagano 35:13).
Ona pia “The Faith and Fall of Thomas Marsh,” “Ezra Thayer: From Skeptic to Believer,” “Orson Pratt’s Call to Serve,” katika Revelations in Context, 54–69.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Nimeitwa kuwa shahidi wa Yesu Kristo.
Kama una wito rasmi kama mmisionari au la, unaweza kuwa shahidi wa Yesu Kristo “nyakati zote, katika mambo yote, na mahali pote” (Mosia 18:9). Unapojifunza Mafundisho na Maagano 30–36, andika kile unachojifunza kuhusu fursa zako za kushiriki injili. Ungeweza kutengeneza orodha ya mambo ambayo Bwana ameyataka kwako na orodha nyingine ya ahadi ambazo Bwana hufanya unaposhiriki injili (kwa mfano, ona Mafundisho na Maagano 30:8; 31:3–5; 32:1, 5; 35:13–15, 24). Ungeweza pia kutafuta kanuni ambazo zinaweza kukusaidia kushiriki injili. Unapata nini ambacho kinakuvutia “kutangaza habari njema ya shangwe kuu”? (Mafundisho na Maagano 31:3).
Mzee Gary E. Stevenson alifundisha kwamba kutangaza injili “kunaweza kukamilishwa kupitia kanuni za kawaida, zenye kueleweka kwa urahisi, zilizofundishwa kwa kila mmoja wetu tangu utoto wetu: upendo, shiriki na alika” (“Penda, Shiriki, Alika,” Liahona, Mei 2022, 85). Zingatia kujifunza ujumbe wake wakati ukifikiria kuhusu jamaa, marafiki na familia. Mawazo gani yanakuja kwako kuhusu jinsi unashiriki nao “kile ambacho [wewe] unapenda kuhusu injili ya Yesu Kristo? Ni katika njia gani unaweza kuwaalika “kuja na kuona,” “kuja na kuhudumu,” na “kuja na kuwa sehemu ya”? Unapoimba au kusikiliza “Nitakwenda Utakako” (Nyimbo za Dini, na. 154) au wimbo unaohusiana na huo, ungeweza kujiuliza mwenyewe, Je, Bwana anataka niseme nini na kuwa ili kushiriki injili Yake?”
Ona pia Marcos A. Aidukaitis, “Inua Moyo Wako na Ushangilie,” Liahona, Mei 2022, 40–43; Topics and Questions, “Inviting All to Receive the Gospel of Jesus Christ,” “Ministering as the Savior Does,” Maktaba ya Injili; “Inviting All to Come unto Christ: Sharing the Gospel” (video), Maktaba ya Injili.
Mafundisho na Maagano 31:1–2, 5–6, 9, 13
Bwana anaweza kunisaidia katika uhusiano wa familia yangu.
Familia katika miaka ya 1830 zilipambana na maswala mengi sawa na yale ambayo familia zinakabiliana nayo leo. Je, ni mwongozo na ahadi gani Bwana alizotoa kwa Thomas B. Marsh kuhusu familia yake katika Mafundisho na Maagano 31? (Ona hususani mstari wa 1–2, 5–6, 9, 13). Ni kwa jinsi gani maneno yake yanaweza kukusaidia katika uhusiano wa familia yako?
Kwa maelezo zaidi kuhusu Thomas B. Marsh, ona Saints, 1:79–80, 119–20.
Mafundisho na Maagano 32–33; 35
Bwana huniandaa mimi kwa kazi ambayo Yeye anataka niifanye.
Kujifunza maisha ya watu walioelezewa katika Mafundisho na Maagano 32–33; 35 kunaweza kukusaidia kutambua jinsi gani Bwana anakutayarisha kwa ajili ya kazi Yake. Kwa mfano, ungeweza kusoma kuhusu uhusiano kati ya Parley P. Pratt na Sidney Rigdon katika “Sauti za Urejesho: Waongofu wa Mwanzo.” Uhusiano huu uliwabariki vipi watoto wa Mungu? (ona Mafundisho na Maagano 35).
Hapa kuna mfano mwingine: Ezra Thayer aliandika kwamba muda fulani kabla ya yeye kubatizwa, alipata ono ambamo “mtu alikuja na kuniletea karatasi lililoviringishwa na kuliwasilisha kwangu, na pia tarumbeta na kuniambia [niipige]. Nilimwambia kwamba sikuwahi [kupiga] chombo chochote maishani mwangu. Alisema unaweza [kuipiga], jaribu. … Ilitoa sauti nzuri ambayo sijawahi kuisikia” (“Revelation, October 1830–B, Revelation Book 1,” utangulizi wa kihistoria, josephsmithpapers.org). Wakati baadaye Joseph Smith alipopokea ufunuo kwa ajili ya Ezra Thayer na Northrop Sweet, uliorekodiwa kama Mafundisho na Maagano 33, Ezra alifafanua ufunuo huo kama lile karatasi lililoviringishwa katika ono lake. Ni kwa jinsi gani Bwana alikuwa akimuandaa Ezra kwa ajili ya kazi ambayo alimtaka aitimize? (ona Mafundisho na Maagano 33:1–13).
Je, ni ushahidi gani tunaouona kwamba mkono wa Bwana ulikuwa katika maisha ya watu hawa waumini wa Kanisa wa mwanzoni? Je, Bwana alimweka nani katika maisha yako ili akusaidie kuja kwa Kristo? Je, ni kwa jinsi gani Yeye anakutaka uwabariki wengine kupitia uaminifu wako, upendo au mwaliko?.
Ona pia “A Mission to the Lamanites,” katika Revelations in Context, 45–49.
Mafundisho na Maagano 33:12–18
Kama nikijenga maisha yangu juu ya injili ya Mwokozi, sitaanguka.
Mafundisho na Maagano 33 ilielekezwa kwa Northrop Sweet na Ezra Thayer, waumini wawili wa Kanisa. Northrop aliacha Kanisa mara baada ya ufunuo huu kutolewa. Ezra alihuduma kwa uaminifu kwa muda fulani, lakini yeye pia hatimaye alianguka. Kusoma kuhusu wao katika sehemu hii kunaweza kukusukuma wewe kufikiria ni imara kiasi gani wewe umejenga “juu ya [ule] mwamba” (mstari wa 13) wa injili. Ni kweli zipi katika mistari hii inaweza kukusaidia kubaki mwaminifu kwa Mwokozi?
Ona pia Helamani 5:12.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Ninapaswa kufokasi zaidi kwenye mambo ya Mungu kuliko mambo ya dunia.
-
Inaweza kuwa ya kupendeza kwa watoto wako kujaribu kufanya majukumu mawili kwa wakati mmoja, kama vile kukariri maneno ya wimbo pendwa wakati wakiandika majina ya watu wote wa familia zao. Kwa nini ni vigumu kufanya vitu viwili kwa wakati mmoja? Mngeweza kisha kusoma Mafundisho na Maagano 30:1–2 pamoja. Ni yapi baadhi ya “mambo ya dunia” ambayo yanaweza kutuvuruga katika kumkumbuka Yesu Kristo na injili Yake? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuendelea kufokasi Kwake?
Mafundisho na Maagano 33:2–3, 6–10
Ninaweza kushiriki injili ya Yesu Kristo.
-
Ili kuwasaidia watoto wako kuelewa Mafundisho na Maagano 33:8–10, unaweza kuwaalika wajaribu kusema kirai na midomo yao ikiwa imefungwa wakati wewe au watoto wengine wabashiri ni kitu gani wao wanasema. Soma mstari wa 8–10 na waalike watoto kufumbua vinywa vyao kila mara wanaposikia kirai “fumbueni vinywa vyenu” kikirudiwa. Kwa nini Baba wa Mbinguni anatutaka tufumbue vinywa vyetu na kushiriki injili pamoja na wengine? Tunaweza kuwaambia nini familia zetu kumhusu Mwokozi na au injili Yake? Mngeweza pia kuimba wimbo kuhusu kushiriki injili, kama vile “We’ll Bring the World His Truth” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 172–73).
-
Fikiria kushiriki uzoefu ambao unao kuhusiana na kanuni au ahadi zilizoko katika Mafundisho na Maagano 30–34. Je, umejifunza nini au kuhisi nini kuhusu Mwokozi wako na kazi Yake unapomtumikia Yeye?
Mafundisho na Maagano 33:12–13
Ninaweza kuyajenga maisha yangu juu ya injili ya Yesu Kristo.
-
Ungeweza kuwatoa watoto wako nje ili kuona msingi wa nyumba yako au jengo la Kanisa na waombe wauelezee. Kwa nini jengo linahitaji msingi imara, madhubuti? Soma pamoja nao Mafundisho na Maagano 33:12–13, na uelezee hisia zako kwa kila mmoja kuhusu kwa nini Bwana anatutaka sisi tujenge maisha yetu juu ya injili Yake. Kwa nini “mwamba” ni neno zuri la kuielezea injili? Je, tunawezaje kujenga maisha yetu juu ya mwamba wa injili? (ona pia Mathayo 7:24–29).