“Sauti za Urejesho: Waongofu wa Mwanzo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Waongofu wa Mwanzo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Sauti za Urejesho
Waongofu wa Mwanzo
Hata kabla Kanisa halijaanzishwa mnamo Aprili 1830, Bwana alitangaza, “Shamba ni jeupe tayari kwa mavuno” (Mafundisho na Maagano 4:4). Maelezo haya yalithibitika kuwa kweli katika miezi ambayo ilifuata, wakati watafutaji wengi wa ukweli waliongozwa na Roho wa Mungu kutafuta Kanisa la Urejesho la Yesu Kristo.
Wengi wa hawa waongofu wa mwanzo walikuwa wamehusika na kujenga msingi wa Urejesho, na hadithi zao za uongofu ni zenye thamani kwetu leo. Imani waliyoonesha ni imani ile ile tunayohitaji ili kuwa waongofu kwenye injili ya Yesu Kristo.
Abigail Calkins Leonard
Wakati Abigail Calkins Leonard alipokuwa katika umri wa miaka ya thelathini, alitaka kusamehewa dhambi zake. Mara chache alisoma Biblia, na watu kutoka makanisa ya Kikristo walimtembelea nyumbani kwake, lakini alikuwa amekanganyikiwa kuhusu nini kilichotofautisha kanisa moja na jingine. “Asubuhi moja, alisema, “Nilichukuwa Biblia yangu na nilikwenda msituni, nilipopiga magoti.” Aliomba kwa bidii kwa Bwana. “Mara moja ono lilipita mbele ya macho yangu,” alisema, “na madhehebu tofauti yalipita moja baada ya jingine, na sauti iliniita, ikisema: ‘Haya yamejengwa kwa ajili ya kupata faida.’ Kisha, na mbele zaidi, niliweza kuona mwanga mkubwa, na sauti kutoka juu ilisema: ‘nitawainua watu, ambao nitafurahia kuwamiliki na kuwabariki.’” Muda mfupi baadaye, Abigail alisikia kuhusu Kitabu cha Mormoni. Japokuwa alikuwa bado hana nakala ya kitabu hicho, alitafuta “kujua ukweli wa kitabu hiki, kwa karama na uweza wa Roho Mtakatifu,” na “mara moja alihisi uwepo wake.” Mwishowe wakati alipoweza kusoma Kitabu cha Mormoni, alikuwa “tayari kukipokea.” Yeye na mume wake, Lyman, walibatizwa mwaka 1831,
Thomas B. Marsh
Wakati Thomas B. Marsh alipokuwa kijana mkubwa, alijifunza Biblia na alijiunga na kanisa la Kikristo. Lakini hakutosheka, mwishowe kujiondoa kutoka makanisa yote. “Nilikuwa na kipimo cha roho ya unabii,” alisema, “na nilimwambia [kiongozi wa kidini] kwamba nilitegemea kanisa jipya lingeinuka, ambalo litakuwa na ukweli katika usafi wake.” Sio muda mrefu baada ya haya, Thomas alipata msukumo wa kiroho kuacha nyumba yake huko Boston, Massachusetts, na kusafiri magharibi. Baada ya kuwa kwa miezi mitatu huko New York magharibi bila kupata kile alichokuwa akikitafuta, alianza kurudi nyumbani. Akiwa njiani, mwanamke alimwuliza Thomas kama alikuwa amesikia kuhusu “Kitabu cha Dhahabu kilichogunduliwa na kijana anayeitwa Joseph Smith.” Akiwa amevutiwa na wazo hili, Thomas mara moja alisafiri kwenda Palmyra na alikutana na Martin Harris kwenye duka la kupiga chapa, ndio kwanza kurasa 16 za kwanza za Kitabu cha Momoni zikiwa zinatoka kwenye mashine ya uchapishaji. Thomas aliruhusiwa kuchukuwa nakala ya kurasa hizo 16, na alizipeleka nyumbani kwa mkewe, Elizabeth. “Alipendezwa sana” na kitabu, anakumbuka, “akikiamini kuwa ni kazi ya Mungu.” Thomas na Elizabeth baadaye walihamia New York na watoto wao na walibatizwa. Kwa maelezo zaidi kuhusu Thomas B. Marsh, ona Mafundisho na Maagano 31.)
Parley na Thankful Pratt
Kama Thomas Marsh, Parley na Thankful Pratt waliitikia msisimko wa kiroho kuacha mashamba yao yaliyostawi Ohio kwa nia ya kuhubiri injili kama walivyoielewa kutoka kwenye Biblia. Wakati Parley alipomwambia ndugu yake, “Roho wa mambo haya aligusa akili yangu kwa nguvu mno hivi karibuni kiasi kwamba sikuweza kupumzika.” Wakati walipofika mashariki ya New York, Parley alipata msukumo wa kubaki kwa muda katika eneo. Thankful, waliamua, wangeendelea bila yeye. “Nina kazi ya kufanya katika jimbo hili la nchi,” Parley alimwambia, “na ni kitu gani hicho, au ni muda gani itachukuwa kukifanya, mimi sijui, lakini nitakuja wakati kitakapokuwa kimefanyika.” Ilikuwa pale ambapo Parley kwa mara ya kwanza alisikia juu ya Kitabu cha Mormoni. “Nilihisi mvuto wa ajabu katika kitabu hiki,” alisema. Aliomba nakala na kusoma usiku mzima. Ilipofika asubuhi, alijua kitabu kilikuwa cha kweli, akakithamini “zaidi ya utajiri wote wa ulimwengu.” Ndani ya siku chache tu Parley alibatizwa. Kisha alirudi kwa Thankful, ambaye pia alibatizwa. (Kwa maelezo zaidi kuhusu Parley P. Pratt, ona Mafundisho na Maagano 32.)
Sidney na Phebe Rigdon
Akiwa njiani kutoka New York kwenye misheni huko Missouri, Parley Pratt na watenda kazi wenzake walipumzika huko Mentor, Ohio, nyumbani kwa Sidney na Phebe Rigdon—marafiki wa zamani wa Parley aliowajua kutoka huko Ohio. Sidney alikuwa mchungaji wa Kikristo, na Parley hapo mwanzo alikua muumini wa mkusanyiko wa watu wake na alimfikiria kama mshauri wa kiroho. Parley kwa shauku aliwaambia rafiki zake kuhusu Kitabu cha Mormoni na Urejesho wa injili ya Yesu Kristo. Sidney mwenyewe alikuwa akitafuta urejesho wa Kanisa la kweli ambalo alilipata limeelezwa katika Agano Jipya, ingawa alikuwa mwenye kushuku kuhusu Kitabu cha Mormoni hapo mwanzo. “Lakini nitakisoma kitabu chako,” alimwambia rafiki yake Parley, “na nitajaribu kuhakikisha, kama kitakuwa ufunuo kutoka kwa Mungu au la.” Baada ya wiki mbili za kujifunza na sala, wote yeye na Phebe waliridhika kitabu kilikuwa cha kweli. Lakini Sydney pia alijua kwamba kujiunga na Kanisa kungekuwa dhabihu kubwa kwa familia yake. Ni dhahiri angepoteza kazi yake kama mchungaji, pamoja na hadhi yake ya kijamii katika jumuiya. Wakati yeye na Phebe walipojadili uwezekano huu, Phebe alitamka “nimehesabu gharama, na … ni tamanio langu kufanya mapenzi ya Mungu, iwe kwa uzima au iwe kwa kifo.”