“Aprili 14–20: ‘Mimi Ni Yeye Aliye Hai, Mimi Ni Yule Aliyeuawa’: Pasaka,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Pasaka,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
April 14–20: “Mimi Ni Yule Aliye Hai, Mimi Ni Yule Aliyeuwawa”
Pasaka
Aprili 3, 1836, ilikuwa Jumapili ya Pasaka. Baada ya kusaidia kuhudumia sakramenti kwa Watakatifu katika Hekalu la Kirtland lililokuwa limewekwa wakfu karibuni, Joseph Smith na Oliver Cowdery walipata sehemu tulivu nyuma ya pazia na waliinamisha vichwa vyao katika sala ya kimya. Kisha, kwenye siku hii takatifu wakati Wakristo kila sehemu walikuwa wanasherehekea Kufufuka kwa Yesu Kristo, Mwokozi aliyefufuka alitokea katika hekalu Lake, akitangaza, “Mimi ni yeye aliye hai, Mimi ni yule aliyeuawa” (Mafundisho na Maagano 110:4).
Inamaanisha nini kusema kwamba Yesu Kristo ni “yeye aliye hai”? Haimaanishi tu kwamba aliinuka kutoka kaburini siku ya tatu na kuonekana kwa wafuasi Wake huko Galilaya. Inamaanisha kwamba anaishi leo. Anazungumza kupitia manabii leo. Analiongoza Kanisa Lake hivi leo. Anaponya nafsi zilizojeruhiwa na mioyo iliyovunjika leo. Kwa hiyo tunaweza kurudia maneno ya Joseph Smith yenye ushuhuda wenye nguvu: “Baada ya shuhuda nyingi ambazo zimetolewa juu Yake, huu ni ushuhuda … ambao tunatoa juu yake: Kwamba yu hai!” (Mafundisho na Maagano 76:22). Tunaweza kusikia sauti yake katika mafunuo haya, ushahidi wa mkono Wake katika maisha yetu, na kuhisi “neno hili hufariji: ‘Najua Kristo yu Hai!’” (Nyimbo za Dini, na. 68).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Yesu Kristo yu hai.
Wengi wetu hatujamwona Yesu Kristo kama ambavyo Nabii Joseph Smith alivyomwona. Lakini tunaweza kujua, kama alivyomwona, kwamba Mwokozi yu hai, kwamba Yeye anajua mafanikio yetu na mapambano yetu na kwamba Yeye atatusaidia katika nyakati za uhitaji. Fikiria ushuhuda wako wewe mwenyewe juu ya Kristo aliye hai unapotafakari maswali hayo hapo chini na jifunze taarifa zinazoambatana nayo.
-
Yesu Kristo ni nani? Kwa nini tunamwabudu Yeye (ona “Kristo Aliye Hai: Ushuhuda wa Mitume”).
-
Je, Roho ananifundisha nini kuhusu uzoefu wa Joseph Smith na wengine ambao walimwona Mwokozi? Je, shuhuda zao zinaimarishaje ushuhuda wangu? (ona Mafundisho na Maagano 76:11–14, 20–24; 110:1–10; Joseph Smith—Historia ya 1:17).
-
Ninajifunza nini kuhusu huduma na uungu wa Mwokozi kutokana na maneno Yake mwenyewe? (ona Mafundisho na Maagano 29:5; 38:7).
-
Mwokozi anawezaje kunisaidia mimi leo? (ona Isaya 53:3–5; Waebrania 2:17–18; Mosia 3:7; Alma 7:11–13; 36:3; Etheri 12:27; Musa 5:10–12).
Katika video “My Spiritual Goal,” msichana anaamua kukariri “Kristo Aliye Hai” (Maktaba ya Injili). Ni kitu gani kinakuvutia wewe kuhusu uzoefu wake? Je, unahisi kushawishika kufanya nini ili kupokea kweli zilizoko katika “Kristo Aliye Hai” moyoni na akilini mwako?
Ili kujifunza zaidi kuhusu jinsi gani Mwokozi anatubariki sisi leo, ungeweza kujifunza, kusikiliza, au kuimba “Najua Kristo Yu Hai” (Nyimbo za Dini, na. 68). Ingeweza kuwa ya kuvutia kutafuta kweli katika wimbo huu ambazo pia zinafundishwa katika Mafundisho na Maagano 6:34; 84:77; 98:18; 138:23.
Ona pia Topics and Questions, “Jesus Christ,” Maktaba ya Injili.
Kwa sababu ya Yesu Kristo, mimi nitafufuka.
Joseph Smith alijua jinsi inavyokuwa kuomboleza kifo cha wapendwa, ikijumuisha baba yake na wawili kati ya kaka zake. Joseph na Emma walizika watoto wao sita, kila mmoja akiwa na umri mdogo wa miaka chini ya miwili. Kutokana na mafunuo ambayo Mungu aliyatoa, Joseph na Emma walipata mtazamo wa milele.
Tafuta kweli kuhusu mauti na mpango wa Mungu wa milele katika Mafundisho na Maagano 29:26–27; 42:45–46; 63:49; 88:14–17, 27–31; 93:33–34. Ni kwa jinsi gani kweli hizi zimeathiri jinsi unavyokichukulia kifo? Ni kwa jinsi gani zinaathiri jinsi unayoishi?
Ona pia 1 Wakorintho 15; Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 174–76; Easter.ChurchofJesusChrist.org.
Yesu Kristo alitimiza “upatanisho kamili” kwa ajili yangu mimi.
Njia moja ya kufokasi juu ya Mwokozi wakati wa Pasaka ni kujifunza mafunuo yaliyomo katika Mafundisho na Maagano ambayo yanafundisha kuhusu dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Baadhi zinaweza kupatikana katika Mafundisho na Maagano 18:10–13; 19:16–19; 45:3–5; 76:69–70. Fikiria kutengeneza orodha ya kweli ambazo unazipata katika mistari hii. Ili kuongeza kina cha kujifunza kwako, ungeweza kuongeza kwenye orodha kwa kupekua Luka 22:39–44; 1 Yohana 1:7; 2 Nefi 2:6–9; Mosia 3:5–13, 17–18; Moroni 10:32–33.
Hapa kuna baadhi ya maswali ambayo yangeweza kuongoza kujifunza kwako:
-
Upatanisho wa Yesu Kristo ni Nini?
-
Kwa nini Yesu Kristo alichagua kuteseka na kufa kwa ajili yetu?
-
Ni nini lazima nifanye ili kupokea baraka za dhabihu Yake?
-
Je, ninahisije kumhusu Yesu Kristo baada ya kusoma mistari hii?
Ona pia Mwongozo wa Maandiko, “Upatanisho,” Maktaba ya Injili; “The Savior Suffers in Gethsemane” (video), Maktaba ya Injili.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Kwa sababu ya Yesu Kristo, mimi nitafufuka.
-
Ili kuwafundisha watoto wako kuhusu ufufuko, ungeweza kuanza kwa kuwaonyesha picha za kifo na Ufufuko wa Mwokozi. Waruhusu watoto washiriki kile wanachokijua kuhusu matukio haya. Mngeweza pia kuimba wimbo kama “Did Jesus Really Live Again?” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 64).
-
Fikiria juu ya somo la vitendo ambalo linaweza kuwasaidia watoto kuelewa nini kinatokea wakati tunapokufa (roho zetu na miili yetu hutengana) na wakati tunapofufuka (roho zetu na miili yetu huungana tena, na miili yetu inakuwa mikamilifu na isiyokufa tena). Kwa mfano, nini hutokea tunapoondoa betri kutoka kwenye tochi au kopo la wino kutoka kwenye kalamu ya wino? Nini hutokea wakati vinapounganika tena? (Ona Alma 11:44–45.)
-
Je, watoto wako wanamjua mtu aliaga dunia? Acha washiriki kidogo kuhusu watu hao, na kisha msome pamoja Mafundisho na Maagano 138:17. Zungumzeni kuhusu jinsi gani mnavyohisi kwa kujua kwamba wapendwa wetu watafufuka na kuwa na miili tena.
-
Kama unao watoto wakubwa, unaweza kuwaalika kutafuta kirai kinachonasa ujumbe wa Pasaka katika vipengele vifuatavyo: Mafundisho na Maagano 63:49; 88:14–17, 27; 138:11, 14–17. Wanaweza kufanya vivyo hivyo kwa kutumia video “Because He Lives” (Maktaba ya Injili). Ni kwa jinsi gani tunaweza kushiriki ujumbe huu na wengine?
Nabii Joseph Smith alimwona Yesu Kristo.
-
Wewe na watoto wako mnaweza kuwa na hamu ya kusoma kuhusu nyakati tatu tofauti ambazo Yesu Kristo alijitokeza kwa Joseph Smith na wengine kama ilivyoandikwa katika Joseph Smith—Historia 1:14–17; Mafudisho na Maagano 76:11–24; 110:1–10. Watoto wako wangeweza pia kutazama picha za matukio haya katika ukurasa wa shughuli ya wiki hii. Je, tunajifunza nini kuhusu Yesu Kristo kutoka kwenye kila moja ya matukio haya? Kwa nini ni baraka kujua kwamba Joseph Smith na wengine walimwona Mwokozi aliyefufuka?
Kwa sababu ya Yesu Kristo, ninaweza kusamehewa dhambi zangu.
-
Kweli alizojifunza Joseph Smith kuhusu msamaha kupitia Kristo zinaweza kuwapa watoto wako matumaini kwamba wao wanaweza kusamehewa makosa na dhambi zao. Fikiria kuwaalika watoto wako kutengeneza jedwali lenye vichwa vya habari kama hivi: Mwokozi alifanya nini kwa ajili yangu na Nifanye nini ili kupokea msamaha Wake. Waalike watoto wako kupekua vifungu vifuatavyo ili kupata mambo ambayo yanahusika chini ya vichwa hivi vya habari: Mafundisho na Maagano 18:10–13; 19:16–19; 45:3–5; 58:42–43. Shirikini mmoja na mwingine shangwe na shukrani yenu kwa ajili ya kile Mwokozi alichofanya kwa ajili yetu.
-
Mngeweza pia kutazama video ya “The Shiny Bicycle” pamoja na watoto wako kwenye (Maktaba ya Injili) na shiriki uzoefu wako wakati ulipohisi msamaha wa Mwokozi pale ulipotubu.