“Aprili 28–Mei 4: ‘Sheria Yangu ya Kulitawala Kanisa Langu’: Mafundisho na Maagano 41–44,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 41–44,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Aprili 28–Mei 4: “Sheria Yangu ya Kulitawala Kanisa Langu”
Mafundisho na Maagano 41–44
Kanisa lilikua kwa haraka katika mwaka 1830 na 1831, hasa kwa ongezeko la haraka la waumini wapya huko Kirtland, Ohio. Kukua huku kuliwasisimua na kuwatia moyo Watakatifu, lakini pia kulileta baadhi ya changamoto. Je, unawezaje kukiunganisha kikundi kinachopanuka kwa haraka cha waaminio? Hususani, unafanya nini wanapokuwa wanaleta mafundisho na desturi kutoka kwenye imani zao za zamani? Kwa mfano, wakati Joseph Smith alipowasili Kirtland mapema Februari 1831, aliwakuta waumini wapya wakishirikiana mali yao pamoja katika kujaribu kwa dhati kuiga Wakristo wa Agano Jipya (ona Matendo ya Mitume 4:32–37). Bwana alifanya baadhi ya masahihisho muhimu na ufafanuzi juu ya mada hii na nyinginezo. Alifanya hili hasa kupitia ufunuo uliorekodiwa katika Mafundisho na Maagano 42 ambayo Yeye aliuita “sheria yangu ya kulitawala kanisa langu” (mstari wa 59). Katika ufunuo huu, tunajifunza kweli ambazo ni muhimu katika kukuza Kanisa la Bwana katika siku za mwisho. Na tunajifunza kwamba tunayo mengi zaidi ya kujifunza: “Ikiwa utaomba,” Bwana ameahidi, “nawe utapokea ufunuo juu ya ufunuo, maarifa juu ya maarifa” (Mafundisho na Maagano 42:61).
Ona pia Saints, 1:114–19.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
“Yeye ambaye huipokea sheria yangu na kuitenda, huyo ndiye mwanafunzi wangu”
Ilipofika mapema 1831, Watakatifu walikuwa wanaanza kukusanyika huko Ohio. Wakiwa na hamu ya kupokea sheria ambayo Mungu aliahidi kuifunua pale (ona Mafundisho na Maagano 38:32). Lakini kwanza, Bwana alifundisha jinsi wanafunzii wake wanavyopaswa kujiandaa kupokea sheria Yake. Ni kanuni gani unazozipata katika Mafundisho na Maagano 41:1–6 ambazo zingeweza kuwasaidia Watakatifu kupokea sheria ya Mungu? Ni kwa jinsi gani kanuni hizi zinakusaidia kupokea maelekezo kutoka Kwake?
Ona pia “A Bishop unto the Church,” katika Revelations in Context, 77–83.
Bwana ananipa mimi amri kwa sababu ananipenda.
Watakatifu walichukulia ufunuo unaopatikana katika Mafundisho na Maagano 42:1–72 kuwa mojawapo ya zile zilizo muhimu zaidi ambazo Nabii alizipokea. Ulikuwa mojawapo ya mafunuo ya kwanza kuchapishwa. Kwa miaka mingi Watakatifu waliuita tu “sheria.” Wakati sehemu hii haijumuishi amri au sheria zote za Mungu, ni muhimu kutafakari kwa nini kanuni hizi zilikuwa muhimu kwa Kanisa lililorejeshwa hivi karibuni. Kwa nini ni za muhimu kwetu sisi leo?
Kwa sababu sehemu ya 42 kwa kiasi ni ndefu, ungeweza kufikiria kujifunza sehemu ndogo ndogo, kama ifuatavyo. Tambua kanuni zinazofundishwa katika kila mstari, na fikiria jinsi gani sheria hizi ni ishara ya upendo wa Bwana kwa watu Wake.
Kwa nini Mungu hutupatia sheria na amri? Ni kwa njia gani wewe umeweza kubarikiwa kwa kujua na kufuata amri?
Mafundisho na Maagano 42:30–42
“Wakumbuke maskini.”
Kama sehemu ya sheria iliyofunuliwa katika sehemu ya 42, Bwana aliwafundisha Watakatifu Wake jinsi gani wao wangeweza, kama wafuasi wa Kristo wa zamani, kuwa na “mali shirika” (Matendo ya Mitume 2:44; 4 Nefi 1:3), na “pasiwe na maskini miongoni mwao” (Musa 7:18). Unajifunza nini kutoka Mafundisho na Maagano 42:30–42 kuhusu jinsi gani Watakatifu waliishi sheria ya kuweka wakfu? (Kuweka wakfu maana yake kutenga kitu kwa ajili ya matumizi matakatifu.)
Ingawaje “vitu vyote havitumiki kwa usawa” leo mahekaluni Watakatifu wa Siku za Mwisho, wanafanya maagano ya kuishi sheria ya kuweka wakfu. Unawezaje kuweka wakfu kitu kile ambacho Mungu amekupatia ili kuwabariki watu walio katika uhitaji? Pengine kuimba wimbo kama “Because I Have Been Given Much” (Nyimbo za Dini, na. 219) unaweza kukupatia mawazo.
Ona pia Sharon Eubank, “Ninaomba Atutumie Sisi,” Liahona, Nov. 2021, 53–56; “Sheria,” katika Revelations in Context, 93–95.
Mafundisho na Maagano 42:61, 65–68; 43:1–16
Mungu anatoa ufunuo ili kuliongoza Kanisa Lake—na kuniongoza mimi.
Fikiria kwamba unaongea na muumini mpya wa Kanisa ambaye anafurahia kujua kwamba Kanisa linaongozwa kwa ufunuo. Ni kwa jinsi gani ungeweza kutumia Mafundisho na Maagano 43:1–16 ili kumsaidia kujifunza kuhusu mpangilio wa Bwana wa kuliongoza Kanisa Lake kupitia kwa nabii Wake? Ni kwa jinsi gani ungetumia Mafundisho na Maagano 42:61, 65–68 kufundisha kuhusu kupokea ufunuo binafsi?
Ni nini baadhi ya “mambo ya amani” na mambo ya shangwe uliyopokea kutoka kwa Bwana kupitia Roho Wake?
Ili kujifunza jinsi gani viongozi wa Kanisa wameisikia sauti ya Bwana, ungeweza kuangalia mojawapo ya video katika mkusanyiko wa “Hear Him” katika Maktaba ya Injili. Fikiria kutengeneza video yako mwenyewe, inayoelezea jinsi gani Bwana anawasiliana na wewe.
Ona pia Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili Ya Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2018, 93–96; “Mambo Yote Lazima Yafanyike katika Utaratibu,” katika Ufunuo katika Muktadha, 50–53.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Mwanafunzi ni mtu anayepokea sheria ya Mungu na kuitii.
-
Ili kuwasaidia watoto wako kujua inamaanisha nini kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo, unaweza kuandika Mafundisho na Maagano 41:5 kwenye kipande cha karatasi, ukiacha nafasi wazi pale neno mwanafunzi linapopaswa kuwa. Wanaweza kisha kutazama katika mstari wa 5 kwa ajili ya neno linalokosekana. Kulingana na mstari huu, inamaanisha nini kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo? Ni kwa jinsi gani tunajaribu kuwa wanafunzi bora zaidi wa Kristo?
Ninakuwa mwenye furaha ninapomtii Bwana.
-
Watoto wako wanaweza kufurahia kucheza mchezo ambao unawahitaji wao kusikiliza kwa makini na kufuata maelekezo. Ungeweza kutumia mchezo huu kuzungumza kuhusu inamaanisha nini “kusikiliza, kumsikia na kumtii” Bwana (Mafundisho na Maagano 42:2). Ni maelekezo gani Yeye ametupatia sisi? Je, tunabarikiwaje kwa kutii sheria na amri Zake?
-
Ungeweza kukamilisha ukurasa wa shuhghuli wa wiki hii pamoja na watoto wako. Ungeweza pia kuimba wimbo kuhusu kutii sheria za Mungu, kama vile “I Want to Live the Gospel” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 148). Fikiria kushiriki mmoja na mwingine jinsi kutii sheria za Mungu kumewaletea furaha.
Ninamtumikia Yesu Kristo pale ninapowatumikia wengine.
-
Baada ya kusoma pamoja Mafundisho na Maagano 42:38, wasaidie watoto wako kufikiria njia ambazo wao wanaweza kumhudumia Yesu kwa kuwahudumia wengine. Wanaweza kutafuta mawazo kutoka kwenye video ya “Pass It On” (ChurchofJesusChrist.org). Wanaweza pia kutazama picha za Mwokozi akiwasaidia wengine, kuwaponya wagonywa au kuwa mkarimu kwa watoto (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 42, 47).
-
Unaweza kuwaonyesha watoto wako fomu ya Zaka na Matoleo Mengine na zungumza kuhusu jinsi ya kuitumia kutoa kile tulichonacho ili kuwabariki wengine (ona pia “Zaka na Matoleo Mtandaoni”).
Ni nabii pekee anayeweza kupokea ufunuo kwa ajili ya Kanisa lote.
-
Waalike watoto kufikiria kwamba mtu anasimama kwenye mkutano wa ushuhuda na kuiambia kata kwamba amepokea ufunuo kwa ajili ya Kanisa zima (kwa mfano, ufunuo kwamba hatupaswi tena kula karoti au kwamba tunapaswa kuosha mikono yetu kwa kutumia maziwa badala ya maji.) Anasema kwamba tunapaswa kusikiliza kile anachosema badala ya kumsikiliza nabii. Je, nini kitakuwa si sahihi kuhusu hilo? Kisha mngeweza kujifunza Mafundisho na Maagano 43:1–7 kwa pamoja ili mpate jinsi gani Bwana anatoa amri kwa Kanisa Lake.
-
Ungeweza pia kuonesha picha ya nabii aliye hai na waalike watoto wako washiriki jambo alilofundisha hivi karibuni. Ikiwa wanahitaji msaada, onesha video fupi au soma kifungu cha maneno kutoka kwenye ujumbe wa mkutano mkuu wa hivi karibuni. Kwa nini ni baraka kuwa na nabii aliye hai leo?