“Mei 19–25: ‘Kile Kilicho cha Mungu Ni Nuru’: Mafundisho na Maagano 49–50,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kasinani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 49–50,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Mei 19–25: “Kile Kilicho cha Mungu Ni Nuru”
Mafundisho na Maagano 49–50
Mwokozi ni “mchungaji wetu mwema” (Mafundisho na Maagano 50:44). Yeye anajua kwamba wakati mwingine kondoo wanatangatanga na nyika ina hatari nyingi. Kwa hiyo kwa upendo anatuongoza hadi kwenye usalama wa mafundisho Yake. Yeye anatuongoza mbali na hatari kama vile “roho za uongo, ambazo zimeenea katika nchi, zikiudanganya ulimwengu” (Mafundisho na Maagano 50:2). Kumfuata Yeye mara zote humaanisha kutupilia mbali mawazo au tamaduni zisizo sahihi. Hiyo ilikuwa kweli kwa Leman Copley na wengine huko Ohio. Walikuwa wameikubali injili iliyorejeshwa lakini bado walishikilia baadhi ya imani ambazo hazikuwa sahihi. Katika Mafundisho na Maagano 49, Bwana alitangaza kweli ambazo zilisahihisha imani za kipindi cha nyuma za Leman kuhusu mada kama vile ndoa na Ujio wa Pili wa Mwokozi. Na wakati waongofu wa Ohio “walipopokea … roho ambazo [hawakuweza] kuzielewa,” Bwana aliwafundisha jinsi ya kutambua madhihirisho ya kweli ya Roho (Mafundisho na Maagano 50:15). Mchungaji Mwema ni mvumilivu kwetu sisi, “watoto Wake wadogo” ambao “lazima tukue katika neema na katika ujuzi wa ukweli” (Mafundisho na Maagano 50:40).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Mafundisho na Maagano 49: 50:24
Yesu Kristo ananitaka nikumbatie kweli za injili Yake.
Kabla ya kujiunga na Kanisa, Leman Copley alikuwa sehemu ya kundi la kidini lililojulikana kama Muungano wa Jumuiya ya Waaminio katika Kuonekana kwa Kristo Mara ya Pili, pia likijulikana kama Shakers. Baada ya mazungumzo na Leman, Joseph Smith alitafuta ufafanuzi kutoka kwa Bwana kuhusu baadhi ya mafundisho ya Shakers. Bwana alijibu kupitia ufunuo katika sehemu ya 49. Baadhi ya imani za Shakers zimetajwa katika kichwa cha habari cha sehemu.
Bwana alifundisha nini katika sehemu ya 49 ili kusahihisha imani za Shakers? Ni ushahidi gani unauona katika ufunuo huu wa upendo Wake na kujali Kwake kwa watu wasio na utimilifu wa ukweli Wake? Ni kwa jinsi gani unaweza kuwafikia wao kwa upendo na kujali?
Je, ni kitu gani kinakuvutia kuhusu maoni ya Bwana katika mstari wa 2? Ungeweza kulinganisha hili na kile ambacho hutokea kama unatazama sehemu moja tu ya sinema, unaangalia kipande kimoja cha chemsha bongo, au unasikia upande mmoja wa hoja. Ni kwa jinsi gani onyo la Bwana linahusiana na Mafundisho na Maagano 50:24? Zingatia kile unachofanya ili upokee nuru zaidi kutoka kwa Bwana.
Ona pia “Leman Copley and the Shakers,” katika Revelations in Context, 117–21.
Mafundisho na Maagano 49:15–17
Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke ni muhimu kwa mpango wa Mungu.
Katika juhudi za kuhujumu mpango wa Baba wa Mbinguni, Shetani hutafuta kusababisha mkanganyiko kuhusu ndoa. Bwana, kwa upande mwingine, huendelea kufunua ukweli kuhusu ndoa kupitia manabii Wake. Unaweza kupata baadhi ya ukweli huu katika Mafundisho na Maagano 49:15–17; Mwanzo 2:20–24; 1 Wakorintho 11:11; na “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Tengeneza orodha ya kweli unazozipata. Kwa nini ndoa ni muhimu sana kwenye mpango wa Mungu?
Mzee Ulisses Soares alifundisha kwamba “injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo inatangaza kanuni ya ushirikiano kamili kati ya mwanamke na mwanamume, kote katika maisha ya duniani na ya milele yote” (“Kwa Ushirikiano na Bwana,” Liahona, Nov. 2022, 42). Unaweza kujifunza ujumbe wake, ukitafuta kanuni “ambazo zinaimarisha ushirikiano kati ya mwanamume na mwanamke.” Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia kanuni hizi katika maisha yako? Kama mtu wa imani nyingine angekuuliza kwa nini ndoa ni muhimu, ungejibu vipi? Je, kwa nini una shukrani kwa ajili ya uelewa huu?
Ona pia Topics and Questions, “Marriage,” “Family,” Maktaba ya Injili; David A. Bednar, “Marriage Is Essential to His Eternal Plan,” Ensign, Juni 2006, 83–84; “Renaissance of Marriage” (video), Maktaba ya Injili.
Mafundisho ya Bwana yanaweza kunilinda kutokana na uongo wa shetani.
Waumini wapya wa Kanisa huko Ohio walikuwa na shauku ya kupokea madhihirisho ya kiroho yaliyoahidiwa kwenye maandiko. Shetani, hata hivyo, alikuwa na shauku ya kuwadanganya. Kama wewe ungeombwa kuwasaidia waumini hawa waelewe jinsi ya kutambua madhihirisho ya kweli ya Roho Mtakatifu, ni kanuni zipi katika Mafundisho na Maagano 50 ungezishiriki? (ona hasa mistari 22–25, 29–34, 40–46). Je, ni kwa namna gani Mwokozi alikusaidia ujue tofauti kati ya ukweli na kosa?
Ona pia 1 Wakorintho 14:1–28; 2 Timotheo 3:13–17.
Mafundisho na Maagano 50:13–24
Walimu na wanafunzi wanajengwa pamoja na Roho.
Kuishi injili ya Yesu Kristo kunatoa fursa nyingi za kuwa walimu na wanafunzi, kote nyumbani na Kanisani. Njia moja unayoweza kujifunza Mafundisho na Maagano 50:13–24 ni kuchora picha ya mwalimu na mwanafunzi. Karibu na kila moja, tengeneza orodha ya maneno na virai kutoka kwenye mistari hii ambavyo vinakufundisha jambo kuhusu kujifunza na kufundisha injili. Ni lini ulikuwa na uzoefu ambao ulikufundisha umuhimu wa Roho katika kufundisha na kujifunza? Zingatia kile unachoweza kufanya ili kuboresha juhudi zako kama mwanafunzi na mwalimu wa injili.
Mafundisho na Maagano 50:23–25
“Kile kilicho cha Mungu ni nuru.”
Unapotafakari maneno ya Bwana katika Mafundisho na Maagano 50:23–25, fikiria kuhusu jinsi unavyopokea nuru ya Mungu katika maisha yako na jinsi “unavyofukuza giza”. Kwa mfano, ni kwa jinsi gani mistari hii inaongoza chaguzi zako kuhusu jinsi ya kutumia muda wako? nI burudani gani au ni vyombo vya habari gani unatafuta? mazungumzo yapi unajihusisha nayo? Je, ni maamuzi gani mengine mistari hii inaweza kukusaidia nayo? Wimbo kama vile: “Bwana Ni Nuru” (Nyimbo za Dini, na. 41) unaweza kuhamasisha mawazo ya ziada.
Ona pia, “Tembea katika nuru ya Mungu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi, 16–21.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Mafundisho na Maagano 49:12–14
Ninaweza kumfuata Yesu Kristo.
-
Ili kuwafundisha watoto wako kanuni katika mistari hii, ungeweza kuandaa karatasi nne za michoro ya nyayo na picha nne ambazo zinawakilisha imani katika Yesu Kristo, toba, ubatizo, na kupokea Roho Mtakatifu (ona picha katika ukurasa wa shughuli ya wiki hii). Watoto wako wangeweza kuweka michoro ya nyayo sakafuni zikiwa na picha kando yake. Kisha wangeweza kufanya zamu kutembea kwenye michoro ya nyayo wakati unaposoma Mafundisho na Maagano 49:12–14. Wasaidie waelewe kwamba wakati tunapofanya vitu katika picha hizi, tunamfuata Yesu Kristo.
-
Ungeweza pia kuwaalika watoto wako wafananishe Mafundisho na Maagano 49:12–14 na Matendo ya Mitume 2:38 na makala ya nne ya imani. Ni mifanano ipi wanayoipata? Kwa nini kweli hizi ni muhimu?
Mafundisho na Maagano 49:15–17
Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke ni muhimu kwa mpango wa Mungu.
-
Ili kutambulisha mistari hii, ungeweza kuelezea kwamba Shakers walikuwa kundi la kidini ambalo liliamini watu hawapaswi kuoa au kuolewa (ona kichwa cha habari cha sehemu kwenye Mafundisho na Maagano 49). Waalike watoto wako watafute vitu Bwana alivyovifundisha kuhusu ndoa katika Mafundisho na Maagano 49:15–17. Inamaanisha nini kwamba “ndoa iliamriwa na Mungu”? Pengine mngeweza kusoma pamoja aya tatu za mwanzo za “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Kisha zungumza kuhusu kwa nini ndoa na familia ni muhimu kwa Baba wa Mbinguni.
Mafundisho na Maagano 50:23–25
“Kile kilicho cha Mungu ni nuru”
-
Ili kutambulisha Mafundisho na Maagano 50:23–25, zungumza na watoto wako kuhusu tofauti kati ya nuru na giza. Kwa nini tunahitaji nuru? Mngeweza kusoma pamoja aya ya kwanza ya “Tembea katika nuru ya Mungu” katika Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (ukurasa wa 17) vile vile Mafundisho na Maagano 50:23–25. Zungumza kuhusu njia ambazo kwazo tunapokea nuru ya Mungu na njia ambazo kwazo tunaweza kufukuza giza. Mngeweza kisha kuimba pamoja wimbo kuhusu nuru yao ya kiroho, kama vile “Shine On” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,144).
Mafundisho na Maagano 50:40–46
Yesu Kristo ni Mchungaji wangu Mwema.
-
Baada ya kusoma Mafundisho na Maagano 50:40–46 pamoja, ungeweza kuonesha picha ya Mwokozi iliyopo mwisho wa muhtasari huu na uulize maswali kama haya: Ni kwa jinsi gani mchungaji anahisi kuhusu kondoo Wake? Ni kwa jinsi gani Mwokozi ni kama mchungaji kwetu?