Njoo, Unifuate
Juni 2–8: “Kujishughulisha kwa Shauku katika Kazi Njema” Mafundisho na Maagano 58–59


“Juni 2–8: ‘Kujishughulisha kwa Shauku katika Kazi Njema’: Mafundisho na Maagano 58–59,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)

“Mafundisho na Maagano 58–59,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025

Independence, Missouri, miaka ya 1830

Independence, Missouri, 1831, na Al Rounds

Juni 2–8: “Kujishughulisha kwa Shauku katika Kazi Njema”

Mafundisho na Maagano 58–59

Wakati wazee wa Kanisa mwanzoni walipoona eneo la mji wa Sayuni—Independence, Missouri—haikuwa kile walichotegemea. Baadhi walifikiri wangekuta jumuiya iliyositawi, yenye bidii pamoja na kundi lenye nguvu la Watakatifu. Badala yake, walikuta makazi machache yaliyojitenga, yasiyo na ustaarabu waliouzoea na yaliyokaliwa na wakazi walowezi wenye fujo badala ya Watakatifu. Ilionekana kwamba Bwana hakuwaomba tu kuja Sayuni—Yeye aliwataka wao kuijenga Sayuni.

Wakati matarajio yetu hayalandani na uhalisia, tunaweza kukumbuka kile Bwana alichowaambia Watakatifu mnamo 1831: “Hamuwezi kuona kwa macho yenu ya asili, kwa wakati huu, mipango ya Mungu wenu … na utukufu utakaofuata baada ya taabu kubwa” (Mafundisho na Maagano 58:3). Ndiyo, maisha yamejaa taabu, hata uovu, lakini tunaweza bado “kutekeleza haki nyingi; kwa uwezo ulio ndani [yetu]” (mistari 27–28).

Ona pia Saints, 1:127–33.

ikoni ya kujifunza

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Mafundisho na Maagano 58:1–5; 59:23

“Baada ya taabu kubwa huja baraka.”

Watakatifu walitumaini kwamba wakati wa kipindi cha maisha yao, Jackson County ingesitawi kuwa Sayuni, mahali ambapo Watakatifu wote wangeweza kukusanyika. Hata hivyo, muda wao katika Jackson County ulikuwa umejaa taabu. Ndani ya miaka michache, walilazimishwa kuondoka na “kusubiri kwa kipindi kifupi kwa ajili ya ukombozi wa Sayuni” (Mafundisho na Maagano 105:9).

Unajifunza nini kuhusu taabu au changamoto kutoka kwenye maneno ya Bwana katika Mafundisho na Maagano 58: 1–5? Kwa nini unadhani baadhi ya baraka huja tu baada ya taabu? Ni baraka zipi umezipokea baada ya taabu?

Ni kipi unachojifunza kutoka Mafundisho na Maagano 59:23 ambacho kinakuletea tumaini?

Mafundisho na Maagano 58:26–29

Ninaweza “kutekeleza haki nyingi” kwa “hiari yangu wenyewe.”

Kama sehemu ya kujifunza kwako mistari hii, ungeweza kutengeneza orodha ya baadhi ya mambo ambayo kwayo “unajishughulisha kwa shauku.” Je, yote ni “kazi njema”? Tafakari kile unachoweza kufanya ili “kutekeleza haki nyingi”—na zingatia kuweka malengo ya kufanya hivyo.

Kwa nini unadhani Bwana anakutaka ufanye “mambo mengi kwa hiari [yako] wenyewe”? Matokeo yangekuwa yapi ikiwa “ungelazimishwa katika mambo yote”? Ni kipi 2 Nefi 2:27 inaongeza kwenye uelewa wako wa kanuni hii?

Ona pia Dale G. Renlund, “Chagueni Hivi Leo,” Liahona, Nov. 2018, 104–6.

Mafundisho na Maagano 58:42–43

ikoni ya seminari
Bwana hunisamehe ninapotubu.

Ahadi ya Bwana katika Mafundisho na Maagano 58:42 ya kuwasamehe kikamilifu wale ambao wanatubu inatia msukumo, japo pia inaibua maswali kadhaa: Inamaanisha nini kutubu? Ni kwa jinsi gani nitajua kama nimetubu? Kwa bahati nzuri, Bwana aliendelea, “Kwa hili mnaweza kujua …” (mstari wa 43).

Hapa kuna baadhi ya maswali ya ziada ambayo watu wakati mwingine wanayo kuhusu toba. Je, Roho anakufundisha nini unaposoma nyenzo zilizopendekezwa zilizo hapa chini?

Ni kwa jinsi gani kukiri dhambi zangu kunanisaidia nitubu? Ona Zaburi 32:1–5; Mithali 28:13; Mosia 27:34–37; Alma 39:12–13.

Ninajaribu kuacha dhambi zangu, lakini ninaendelea kufanya makosa. Je, toba yangu bado inastahili? Ona Bradley R. Wilcox, “Ustahili Sio Kukosa Dosari,” Liahona, Nov. 2021, 61–67; “Daily Restoration” (video), Maktaba ya Injili.

5:27

Daily Restoration

Elder Dieter F. Uchtdorf and Church members compare drifting in life to the circles walked by test participants in a dense forest. Shadows creep in off the path, but we can chase away darkness and come back.

Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwa na hakika kwamba Mwokozi amenisamehe? Ona Tad R. Callister, “Upatanisho wa Yesu Kristo,” Liahona, Mei 2019, 85–87, hasa sehemu yenye kichwa cha habari “2 Dhambi.”

Unaweza kupata umaizi zaidi katika “Maswali na Majibu” kuhusu toba katika Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (kurasa 8–9).

Ona pia Topics and Questions, “Repentance,”Maktaba ya Injili.

Mafundisho na Maagano 59

Polly Knight alikuwa nani?

Polly Knight na mumewe, Joseph Knight Mkubwa, walikuwa baadhi ya waaminio wa mwanzo katika wito wa kinabii wa Joseph Smith. Polly na Joseph walitoa usaidizi muhimu kwa Nabii katika kazi ya kutafsiri Kitabu cha Mormoni. Familia ya Knight iliondoka Colesville, New York, ili kukusanyika pamoja na Watakatifu huko Ohio na baadaye waliamriwa kuhamia Jackson County, Missouri. Walipokuwa wakisafiri, afya ya Polly ilianza kuzorota, lakini alikuwa ameweka msimamo wa kuiona Sayuni kabla ya kifo chake. Alikuwa ameishi Missouri siku chache tu wakati alipofariki (ona Saints,, 1:127–28, 132–33). Mafundisho na Maagano 59 ilipokelewa siku ya kifo chake, na mstari wa 1 na wa 2 inaonekana kuwa mahususi kwake.

Mafundisho na Maagano 59:4–19

Amri ni baraka.

Unafikiri inamaanisha nini “kuvikwa taji la … amri”? (mstari wa 4). Zingatia jinsi Bwana anavyokubariki unapojitahidi kutii kila moja ya amri katika mistari 5–19.

Shiriki kile unachojifunza. Katika hali nyingi, umaizi wa kiroho unaoupokea unapojifunza maandiko unaweza kuimarisha imani ya familia yako, marafiki, na washiriki wa kata. Shiriki nao uzoefu wako, hisia, na ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo.

Mafundisho na Maagano 59:9–19

Sabato ni siku ya Bwana.

Baada ya kuahidi kuwabariki Watakatifu katika Sayuni, “kwa amri zisizo haba,” Bwana alitoa msisitizo maalumu kwa amri moja hasa: amri ya kuitakasa “siku Yake takatifu” (Mafundisho na Maagano 59:4, 9). Unapojifunza Mafundisho na Maagano 59:9–19, tafakari kwa nini kuitakasa Sabato kungekuwa muhimu sana kwa Watakatifu hawa wakati walipotafuta kuijenga Sayuni. Kwa nini ni ya muhimu kwako?

Ungeweza pia kutafakari kama wewe unatumia siku ya Sabato katika njia ambayo Bwana aliikusudia. Ni kwa jinsi gani kuitakasa Sabato kunakusaidia ubaki “bila mawaa ya ulimwengu”? (mstari wa 9). Ni nini unaweza kufanya ili kutoa “dhabihu zako za shukrani kwa Aliye Juu Sana”? (mstari wa 10).

sakramenti

Ungeweza pia kugundua kwamba Bwana alitumia maneno kama “kushangilia,” “moyo mkunjufu,” na “kufurahi” ili kufundisha kuhusu siku ya Sabato. Ni kipi hufanya Sabato iwe ya shangwe kwako? Ni kwa jinsi gani ungemwelezea mtu fulani kwa nini unachagua kuitakasa siku ya Bwana?

Unajifunza nini kutoka kwenye wimbo “Kwa Upole Twaimba” (Nyimbo za Dini, na. 78) kuhusu madhumuni na baraka za Sabato?

Ona pia Mwanzo 2:2–3; Isaya 58:13–14; Russell M. Nelson, “Sabato ni Furaha,” Liahona, Mei 2015, 129–32.

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la majarida ya Liahona na Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

ikoni ya 02 ya sehemu ya watoto

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Mafundisho na Maagano 58:26–28

Baba wa Mbinguni amenipa uwezo wa kuchagua.

  • Kusoma pamoja Mafundisho na Maagano 58: 26–26 kunaweza kukupa wewe na watoto wako nafasi ya kuzungumza kuhusu nguvu ambayo Baba wa Mbinguni ametupatia ili kuchagua kutenda mema. Mngeweza kuambiana kuhusu chaguzi tofauti tofauti mlizozifanya na kile kilichotokea kama matokeo. Pengine watoto wako wangependa kuchora picha ya uzoefu wao.

  • Ungeweza kuandika chaguo kwenye upande mmoja wa karatasi na matokeo kwenye upande mwingine na utumie karatasi hii kuonesha kwamba chaguzi zetu na matokeo yake havitengani. Pengine watoto wako wangeorodhesha chaguzi chache na kuzungumza kuhusu matokeo ambayo yanakuja nazo. Kisha mngeweza kusoma pamoja Mafundisho na Maagano 58:27–28 na mzungumze kuhusu chaguzi ambazo “hutekeleza haki nyingi” au matokeo mazuri. Ni kwa jinsi gani Baba wa Mbinguni “hutuzawadia” au kutubariki tunapojitahidi kutenda mema? (mstari wa 28)

Mafundisho na Maagano 59:7; 18–21

“Mshukuru Bwana Mungu wako katika mambo yote.”

  • Zingatia kusoma mistari hii wakati wewe na watoto wako mnaenda matembezini au mkitazama picha za asili, mkigundua vitu ambavyo “vinaridhisha jicho na … kufurahisha moyo” (mstari wa 18). Mngeweza pia kutambua vitu vinavyofahamika katika wimbo kama vile “My Heavenly Father Loves Me” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 228–29). Au ungeweza kuwaalika watoto wako wachore picha za vitu wanavyoshukuru kwavyo na waruhusu wakuambie kuhusu picha zao. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuonesha shukrani zetu kwa vitu hivi?

ndege waimbao na maua

Bwana aliumba vitu vingi vizuri vya kutuleta shangwe.

Mafundisho na Maagano 59:9–12

Sabato ni siku ya Bwana.

  • Kipi tunaweza kufanya siku ya Jumapili ili kumwabudu Bwana na kupata shangwe? Wasaidie watoto wako watafute mawazo katika Mafundisho na Maagano 59:9–12 na katika ukurasa wa shughuli ya wiki hii. Pengine wangeweza pia kupata picha au vitu vinavyowakilisha mambo tunayofanya siku ya Sabato (kama vile picha za sakramenti katika muhtasari huu). Je, ni kwa jinsi gani mambo haya hutusaidia tuhisi kuwa karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo?

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la jarida la Rafiki.

kujiandaa kupokea sakramenti

Kielelezo na Marti Major

ukurasa wa shughuli kwa ajili ya watoto