“Juni 30–Julai 6: ‘Hakuna Silaha Iliyotengenezwa dhidi Yenu Itakayofanikiwa’: Mafundisho na Maagano 71–75,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 71–75,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Juni 30–Julai 6: “Hakuna Silaha Iliyotengenezwa dhidi Yenu Itakayofanikiwa”
Mafundisho na Maagano 71–75
Tangu alipokuwa mvulana mdogo, Joseph Smith alipitia ukosoaji—hata maadui—wakati alipojaribu kuifanya kazi ya Mungu. Lakini yaweza kuwa ilikuwa vigumu hasa mwishoni mwa 1831, wakati Ezra Booth alipoanza kukemea Kanisa hadharani, kwa sababu kwenye hili mkosoaji alikuwa muumini wa zamani. Ezra alikuwa amemwona Joseph akitumia nguvu za Mungu kumponya mwanamke. Alikuwa amealikwa kumsindikiza Joseph kwenye utafiti wa kwanza wa ardhi ya Sayuni huko Missouri. Lakini tangu hapo alikuwa amepoteza imani yake na, katika jaribio lake la kumkosoa Nabii, alichapisha mfululizo wa barua kwenye gazeti la Ohio. Na juhudi zake zilionekana kufaulu, kwa sababu “hisia zisizo za kirafiki … zilijitokeza dhidi ya Kanisa” katika eneo hili (Mafundisho na Maagano 71, kichwa cha habari cha sehemu). Ni nini waumini wanapaswa kufanya katika hali sawa na hiyo? Wakati hakuna jibu moja sahihi kwa kila hali, inaonekana kwamba mara nyingi—ikijumuisha suala hili mnamo 1831—sehemu ya jibu la Bwana ni kutetea ukweli na kusahihisha uongo kwa “kutangaza injili” (mstari wa 1). Ndiyo, kazi ya Bwana daima itapata ukosoaji, lakini mwishoni, “hakuna silaha iliyotengenezwa dhidi [yake] itakayofanikiwa” (mstari wa 9).
Ona “Ezra Booth and Isaac Morley,” katika Revelations in Context, 134.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Roho ataniongoza ninapotangaza injili ya Mwokozi.
Inaweza kuwa usumbufu wakati watu wanapokosoa au kudhihaki imani yako katika Mwokozi, injili yake, au Kanisa Lake. Hilo linapotokea, unafanya nini? Jambo sawa na hilo lilitokea Ohio mnamo 1831 (ona kichwa cha habari cha sehemu ya Mafundisho na Maagano 71). Bwana aliwaambia Joseph Smith na Sidney Rigdon kufanya nini kuhusu hilo katika Mafundisho na Maagano 71? Pengine ungeweza kuorodhesha maelekezo ambayo Bwana aliwapa na baraka alizoziahidi.
Kama nyongeza ya kujifunza sehemu ya 71, ungeweza pia kuchunguza jinsi Mwokozi alivyowajibu wakosoaji Wake wakati wa huduma Yake duniani. Hapa kuna baadhi ya mifano: Mathayo 22:15–22; 26:59–64; Yohana 10:37–38. Unajifunza nini kutoka Kwake? Ni umaizi upi wa ziada unaupata kutoka Mathayo 18:15; Waefeso 4:31–32; 2 Timotheo 3:12; Yakobo 1:19?
Ni kwa jinsi gani ushauri Wake ungetumika kwenye hali unazokabiliana nazo leo? Ungeweza kufikiria njia za amani za kusahihisha uongo kwa maneno yako mwenyewe. Kwa mfano, ungeweza kuanza kwa kuonyesha heshima kwa maoni ya mtu mwingine, na kisha ungeweza kushiriki kwa unyenyekevu na kwa njia ya upole kile unachoamini kuhusu Yesu Kristo na mafundisho Yako. Ili kujiandaa kwa ajili ya matukio kama haya, pengine ungeweza kufanyia mazoezi mbinu hii kwa marafiki zako au wanafamilia.
Ona pia Topics and Questions, “Helping Others with Questions,” Maktaba ya Injili; Dallin H. Oaks, “Kuwapenda Wengine na Kuishi kwa Tofauti,” Liahona, Nov. 2014, 25–28; Jörg Klebingat, :Wanafunzi Jasiri katika Siku za Mwisho,” Liahona, Mei 2022, 107–10.
Bwana hunibariki kupitia huduma ya viongozi kama maaskofu.
Wakati Newel K. Whitney alipoitwa kuhudumu kama askofu, majukumu yake yalikuwa tofauti kidogo na yale ya maaskofu wa leo. Kwa mfano, Askofu Whitney alisimamia uwekaji wakfu wa mali na ruhusa ya kufanya makazi katika ardhi ya Sayuni huko Missouri. Lakini unaposoma kuhusu wito wake katika Mafundisho na Maagano 72, ungeweza kugundua baadhi ya miunganiko kwenye kile maaskofu wanachofanya leo—angalau katika roho, ikiwa si mahususi, kwenye majukumu yao.
Kwa mfano, ni kwa njia zipi “unatoa hesabu ya usimamizi” kwa askofu wako? (mstari wa 5). Katika siku yetu “ghala ya Bwana” inaweza kujumuisha michango, huduma, na talanta za waumini wa kata (ona mistari 10, 12). Ni kwa jinsi gani unachangia kwenye ghala hilo?
Ni kwa jinsi gani Bwana amekubariki wewe na familia yako kupitia huduma ya askofu?
Ona pia Quentin L. Cook, “Maaskofu—Wachungaji juu ya Kundi la Bwana,” Liahona, Mei 2021, 56–60.
Nina fursa nyingi za kushiriki injili ya Mwokozi.
Wakati Joseph Smith na Sidney Rigdon waliporejea kutoka kwenye jukumu lao la umisionari (ona Mafundisho na Maagano 71), Bwana aliwaambia waendelee na kutafsiri Biblia (ona Mwongozo wa Maandiko, “Tafsiri ya Joseph Smith (TJS),” Maktaba ya Injili). Lakini hilo halikumaanisha Yeye aliwataka wao wasitishe kushiriki injili. Hata hivyo, kushiriki injili ni sehemu ya maisha ya mwanafunzi.
Unaposoma Mafundisho na Maagano 73, zingatia jinsi unavyoweza kufanya kushiriki injili kuwe “endelevu” (mstari wa 4)—au sehemu ya—uhalisia wa maisha yako kati ya majukumu yako mengine.
“Fanya kazi kwa nguvu zako … kutangaza ukweli.”
Ufunuo katika sehemu ya 75 ulikuwa umeelekezwa kwa watu ambao walikuwa wametoa majina [yao] kwenda kutangaza injili ya “Mwokozi” (mstari wa 2). Njia moja ya kujifunza ufunuo huu ni kutengeneza orodha mbili: (1) jinsi ya kushiriki injili kwa ufanisi na (2) jinsi ambavyo Bwana hutubariki na kutusaidia tunapofanya hivyo.
Unadhani inamaanisha nini “kukaa bure ” au “kuwa mzembe” katika kushiriki injili? Inamaanisha nini “kufanya kazi na nguvu zako zote”? (mstari wa 3).
Ona pia “Nitakwenda Utakako,” Nyimbo za Dini, na. 154.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Ninaweza kutetea ukweli kwa kushiriki ushuhuda wangu.
-
Unaweza kutumia kichwa cha habari cha sehemu ya Mafundisho na Maagano 71 au “Sura ya 25: Joseph Smith na Sidney Rigdon Wanaenda Misheni” (katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 96, au video inayohusiana katika Maktaba ya Injili) kuwafundisha watoto wako kuhusu hali ambayo ilitoa uvuvio wa sehemu ya 71. Kisha wasaidie wagundue katika mstari wa 1 kile Bwana alichowataka Joseph na Sidney wafanye kuhusu “hisia zisizo za urafiki” kwa Kanisa. Ni kwa jinsi gani Yeye alisema Angewasaidia? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa kama Joseph na Sidney?
-
Mngeweza pia kuimba wimbo ambao unawapa msukumo watoto wako kuwa wakweli kwa Mwokozi kama vile “Stand for the Right: (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 159). Wasaidie watoto wako wafanye mazoezi jinsi ya kushiriki kile wanachojua kumhusu Yesu Kristo.
Bwana amemwita askofu anisaidie.
-
Kusoma Mafundisho na Maagano 72:2 pamoja kungeweza kutoa fursa za kujadili kwa nini Bwana hutupatia maaskofu (ona pia “Sura ya 17: Maaskofu wa Kwanza wa Kanisa,” katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 64–66, au video inayohusiana katika Maktaba ya Injili). Wewe na watoto wako mngeweza kutafuta picha au vitu ambavyo vinawakilisha majukumu ya askofu. Picha na ukurasa wa shughuli mwishoni mwa muhtasari huu vinatoa baadhi ya mawazo. Kisha mngeweza kuzungumza pamoja kuhusu maaskofu unaowajua na jinsi ambavyo Bwana amebariki familia yako kupitia huduma yao.
Ninaweza kutoa juhudi yangu bora kwa Bwana.
-
Ili kuzungumza kuhusu tofauti kati ya kuwa “mzembe” na “kufanya kazi kwa nguvu [zetu] zote,” pengine ungechagua baadhi ya vitendo vya huduma au kazi za nyumbani na kuwaalika watoto wako wafanye maonyesho ya kuzifanya kwa uzembe na kuzifanya kwa nguvu zao zote. Unaposoma “wala mskae bure” katika Mafundisho na Maagano 75:3, watoto wako wangeweza kuonesha jinsi ambavyo wangeweza kufanya kazi kwa uzembe. Unaposoma “lakini fanya kazi kwa nguvu zako zote,” wangeweza kuonesha jinsi ya kufanya kazi kwa bidii. Kwa nini ni muhimu kwamba tufanye kwa uwezo wetu wote wakati tunapomtumikia Bwana?
-
Katika ujumbe wake “Kanuni Mbili za Uchumi Wowote” (Liahona, Nov. 2009, 55–58), Rais Dieter F. Uchtdorf alisimulia hadithi mbili kuhusu kazi. Pengine ungeweza kuzishiriki na watoto wako na kuzungumza kuhusu jinsi inavyokuwa kujua kwamba tumefanya kazi kwa bidii na tumefanya kwa uwezo wetu wote.