“Julai 14–20: ‘Nitawaongoza’: Mafundisho na Maagano 77–80,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 77–80,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Julai 14–20: “Nitawaongoza”
Mafundisho na Maagano 77–80
Chini ya miaka miwili baada ya Kanisa la Yesu Kristo kurejeshwa, lilikuwa na zaidi ya waumini 2,000 na lilikuwa linakua kwa kasi. Mnamo Machi 1832 Joseph Smith alikutana na viongozi wengine wa Kanisa “kujadili shughuli za Kanisa”: hitaji la kuchapisha mafunuo, kununua ardhi ya kukusanyikia, na kuwatunza masikini (ona Mafundisho na Maagano 78, kichwa cha habari cha sehemu). Ili kukidhi mahitaji haya, Bwana aliita idadi ndogo ya viongozi wa Kanisa kuunda Taasisi ya Muungano, kundi ambalo lingeunganisha nguvu zao kwenye “kuendeleza kazi” ya Bwana (mstari wa 4) katika maeneo haya. Lakini hata katika maswala kama hayo ya utawala, Bwana alifokasi kwenye mambo ya milele. Hatimaye, lengo la kiwanda cha uchapishaji au ghala—sawa na kila kitu kingine katika ufalme wa Mungu—ni kuwaandaa watoto Wake kupokea “mahali katika ulimwengu wa selestia” na “utajiri wa milele” (mstari wa 7, 18). Na ikiwa baraka hizo ni ngumu kuzielewa kwa sasa, katikati ya maisha yaliyojaa shughuli nyingi za kila siku, Yeye anatuhakikishia, “Changamkeni, kwa kuwa nitawaongoza” (mstari wa 18).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Mungu hutoa elimu kwa watu ambao wanatafuta kuipata.
Kadiri Joseph Smith na Sidney Rigdon walivyofanya kazi kwenye tafsiri yenye mwongozo ya Biblia, walikuwa na maswali kuhusu kitabu cha Ufunuo, kama vile watu wengi walivyo na maswali. Na kama Joseph alivyojua vyema, wakati alipopungukiwa na hekima, yeye angeweza kumwomba Mungu. Umaizi alioupata upo katika Mafundisho na Maagano 77. Unaposoma sehemu hii, fikiria kuandika umaizi wako juu ya sura zinazohusika katika kitabu cha Ufunuo. Unajifunza nini kutokana na kujifunza kwako kuhusu kupokea ufunuo?
Taasisi ya Muungano ilikuwa nini?
Taasisi ya Muungano ilianzishwa ili kusimamia uchapishaji na maswala ya biashara ya Kanisa huko Ohio na Missouri. Iliundwa na Joseph Smith, Newel K. Whitney, na viongozi wengine wa Kanisa ambao waliunganisha rasilimali zao ili kukidhi mahitaji ya kimwili ya Kanisa linalokua. Kwa bahati mbaya, Taasisi ya Muungano iliangukia kwenye madeni na ilisambaratika mnamo 1834 wakati madeni yalipokuwa makubwa.
Ona pia “Newel K. Whitney and the United Firm,” katika Revelations in Context, 142–47; Church History Topics, “United Firm (‘United Order’),” Maktaba ya Injili.
Ninaweza kusaidia “kuendeleza kazi” ya Kristo na Kanisa Lake.
Bwana alimwambia Joseph Smith na viongozi wengine wa Kanisa kwamba kusimamia ghala na kiwanda cha uchapishaji kungesaidia “kuendeleza kazi, ambayo mmeahidi wenyewe” (Mafundisho na Maagano 78:4). Ni nini ungesema ni “kazi” ya Kanisa la Mwokozi? Tafakari hili unaposoma Mafundisho na Maagano 78:1–7. Ni zipi baadhi ya njia tofauti tofauti ambazo kupitia hizo unaweza kusaidia kuendeleza kazi hiyo—ikijumuisha kwenye familia yako?
Ona pia Kitabu cha Maelekezo ya Jumla, 1.2.
Mafundisho na Maagano 78:17–18
Bwana ataniongoza.
Kwa nini unadhani Bwana wakati mwingine huwaita wafuasi Wake “watoto wadogo”? (Mafundisho na Maagano 78:17). Ni lini umewahi kuhisi kuwa sawa na mtoto mdogo, pengine kwa sababu ya kitu ambacho “bado hujakielewa” au “huwezi kukistahimili”? (mstari wa 17–18). Unapata nini katika mistari hiii ambacho kinaweza kukusaidia wewe “uchangamke” (mstari wa 18) kwenye nyakati sawa na hizo? Fikiria kupata picha zako mwenyewe wakati ulipokuwa mtoto, na tafakari jinsi ambavyo umekua kiroho tangu wakati huo. Au fikiria kitu fulani ambacho kilikuwa kigumu kwako wakati ulipokuwa kijana mdogo lakini sasa ni rahisi. Ni kwa jinsi gani Baba wa Mbinguni bado anakutaka wewe uwe kama mtoto? (ona Mosia 3:19). Ni kwa jinsi gani Yeye “anakuogoza wewe”?
Ninaweza kupokea vitu vyote kwa shukrani.
Ili kujiandaa kujifunza Mafundisho na Maagano 78:19, ungeweza kutengeneza orodha ya vitu vizuri ambavyo vimetokea kwako leo. Kisha tengeneza orodha ya vitu ambavyo havionekani sana kama baraka kwako. Tafakari orodha hizi unaposoma Mafundisho na Maagano 78:19. Ni tofauti ipi inaletwa katika maisha yako kama unapokea “vitu vyote” kwa shukrani—hata vitu ambavyo havingeonekana kama baraka?
Ili kujifunza zaidi kuhusu jinsi shukrani kwa Mungu inavyoweza kushawishi maisha yako, chunguza maandiko haya na utengeneze orodha ya kweli unazozipata: Zaburi 107:8–9; Luka 17:11–19; Wafilipi 4:6–7; Mosia 2:19–24; Alma 34:38; 37:37; Mafundisho na Maagano 46:32; 59:7, 15–21.
Zingatia kupekua ujumbe wa Rais Dieter F. Uchtdorf “Shukrani katika Hali Zozote” (Liahona,, Mei 2014, 70–77) kwa ajili ya ushauri kuhusu jinsi ya kuwa na shukrani. Ungeweza kutafuta ushauri kama huo katika video “Rais Russell M. Nelson kuhusu Nguvu za Uponyaji za Shukrani” (Maktaba ya Injili). Ni kwa jinsi gani shukrani huathiri uhusiano wako na Yesu Kristo?
Ona pia “Hesabu Baraka,” Nyimbo wa Dini, na. 137; Topics and Questions, “Gratitude,” Maktaba ya Injili.
Wito wa kumtumikia Mungu ni muhimu zaidi ya mahali ninapotumikia.
Kuhusu Mafundisho na Maagano 80, Mzee David A. Bednar alifundisha, “Pengine moja ya masomo Mwokozi anayotufundisha katika ufunuo huu ni kwamba jukumu la kutumikia mahali fulani ni muhimu na la kipekee lakini ni la pili kwenye wito kwenye kazi” (“Tumeitwa Kwenye Kazi,” Liahona, Mei 2017, 68). Ni uzoefu upi umekusaidia ujifunze kwamba maneno ya Mzee Bednar ni ya kweli? Ni masomo yapi ya ziada unaweza kupata katika Mafundisho na Maagano 79–80 ambayo yangeweza kumsaidia mtu ambaye punde tu amepokea wito?
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Mungu aliumba kila kiumbe hapa duniani.
-
Wewe na watoto wako mnaposoma Mafundisho na Maagano 77:2 pamoja, mngeweza kutazama picha za wanyama, ikijumuisha wadudu na ndege. Watoto wako wangeweza kuonesha picha wakati unaposoma maneno “wanyama,” “vitu vitambaavyo,” na “ndege wa angani.” Shirikini mmoja na mwingine jinsi viumbe wa Mungu wanavyowasaidia mhisi upendo Wake.
Ninaweza kusaidia “kuendeleza kazi” ya Yesu Kristo.
-
Ili kuwasaidia watoto wako wafikirie kuhusu wajibu wao katika kazi ya Bwana, zingatia kusoma pamoja nao Mafundisho na Maagano 78:4 ili kutambua “kazi” ambayo kupitia kwao sisi “tumeahidi wenyewe” (tumeikubali au kuchagua kuiunga mkono) wakati tulipobatizwa. Wasaidie watafute katika maandiko vifungu vya maneno kama haya kwa ajili ya majibu yamkini: Mosia 18:8–10; Mafundisho na Maagano 20:37; Musa 1:39. Watoto wako wangeweza kufurahia kuigiza nafasi jinsi wanavyoweza kusaidia katika kazi ya Bwana. Kwa mfano, inaonekanaje, “kubeba mzigo wa mmoja na wa mwingine” au “kujichukulia juu yetu [wenyewe] jina la Yesu Kristo? Ni kwa jinsi gani hii “inaendeleza kazi” ya Kristo?
Ninaweza kushiriki vile nilivyonavyo pamoja na wengine.
-
Ili kufundisha kile inachomaanisha kuwa “sawa katika vitu vya kidunia” (mstari wa 6), wape watoto wako picha za watu wenye mahitaji (kama vile watu wenye njaa, waliojeruhiwa, au wanaohisi baridi) na vitu ambavyo vingeweza kusaidia (kama vile chakula, bandeji, au blanketi). Kisha watoto wako wangeweza kuoanisha picha na vitu hivyo. Ni kipi tunaweza kushiriki ili kuwasaidia watu walio na uhitaji?
-
Ili kupata baadhi ya muktadha kwa ajili ya sehemu ya 78, soma pamoja na watoto wako sentensi zilizo chini ya picha mbili za kwanza za “Sura ya 28: Nabii Joseph Smith Anakwenda Tena Missouri” (katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 108 au video inayohusiana kwenye Maktaba ya Injili). Kisha watoto wako wangeweza kujifanya wanamsaidia mtu fulani kujenga nyumba, kushiriki chakula, au kuhudumia katika njia nyingine.
Yesu Kristo ataniongoza.
-
Inaweza kuwa burudani kwa watoto wako kuzungumza kuhusu kile inachomaanisha kuwa kiongozi na kisha kuongoza katika shughuli. Baada ya kusoma pamoja Mafundisho na Maagano 78:18, mngeweza kujadili nyakati ambapo tunamwitaji Yesu atuongoze. Zingatieni kuimba wimbo kama vile “I Will Walk with Jesus” (Maktaba ya Injili).
Ninaweza kupokea “vitu vyote kwa shukrani.”
-
Soma pamoja na watoto wako Mafundisho na Maagano 78:19 ili mgundue kile Bwana alichoahidi kwa watu walio na shukrani. Wasaidie watoto wako waelewe kile ambacho “mara mia” humaanisha, pengine kwa kuwaonesha kitu kidogo na kisha vitu100 vya kitu kilekile. Pengine wangeweza kuchora picha za vitu ambavyo wamepokea kutoka kwa Mungu “kwa shukrani.”