“Julai 21–27: ‘Kwani yule Aliyepewa Vingi Kwake Huyo Vitatakiwa Vingi’: Mafundisho na Maagano 81–83,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 81–83,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Julai 21–27: Kwani Yule “Aliyepewa Vingi, Kwake Huyo Vitatakiwa Vingi”
Mafundisho na Maagano 81–83
Mnamo Machi 1832, Bwana alimwita Jesse Gause kuwa mshauri wa Joseph Smith katika Urais wa Ukuhani Mkuu (sasa ukiitwa Urais wa Kwanza). Mafundisho na Maagano 81 ni ufunuo kwa Kaka Gause kuhusu wito wake mpya. Lakini Jesse Gause hakutumikia kwa uaminifu, kwa hiyo Frederick G. Williams aliitwa kujaza nafasi yake. Jina la Kaka Williams lilichukua nafasi ya jina la Kaka Gause katika ufunuo huu.
Hicho kinaweza kuonekana kama kipengele kidogo, lakini kinadokeza ukweli muhimu: mengi ya mafunuo katika Mafundisho na Maagano yameelekezwa kwa watu mahususi, lakini daima tunaweza kutafuta njia za kuyatumia kwetu wenyewe (ona 1 Nefi 19:23). Tunaposoma ushauri wa Bwana kwa Frederick G. Williams wa “kuyaimarisha magoti yaliyo dhaifu” tunaweza kuwafikiria watu ambao tungeweza kuwaimarisha (Mafundisho na Maagano 81:5). Tunaposoma mwaliko wa Bwana kwa washiriki wa Taasisi ya Muungano wa “jifungeni wenyewe kwa agano hili” tunaweza kufikiria maagano yetu wenyewe. Na tunaweza kusoma ahadi Yake, “Mimi, … ninafungwa wakati ninyi mnapofanya ninayosema,” kama vile Yeye anazungumza nasi (Mafundisho na Maagano 82:10, 15). Tunaweza kufanya hivi kwa sababu, kama Bwana alivyotangaza, “Lile nisemalo kwa mmoja ninalisema kwa wote” (mstari wa 5).
Ona “Newel K. Whitney and the United Firm,” “Jesse Gause: Counselor to the Prophet,” Revelations in Context,, 142–47, 155–57.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Mafundisho na Maagano 81:4–5; 82:18–19
“Utakuwa umefanya mema makuu kwa wanadamu wenzako.”
Katika vifungu kadhaa vya maneno katika Mafundisho na Maagano 81–83, Bwana anatualika tuwasaidie watu walio na uhitaji karibu nasi. Fikiria kuwekea alama vifungu vya maneno unapovipata. Mojawapo ya mifano yenye maelezo sana iko katika Mafundisho na Maagano 81:4–5. Haya ni baadhi ya maswali ya kukusaidia utafakari mistari hii:
-
Ni zipi baadhi ya njia ambazo kupitia kwao mtu anaweza kuwa “dhaifu”? Inamaanisha nini “kuwasaidia” wao? Ni lini huduma kama ya Kristo ya wengine ilinisaidia wakati nilipohisi kuwa mdhaifu?
-
Ni nini kingeweza kusababisha mikono ya mtu kuwa “imelegea” kisitiari? Ni kwa jinsi gani ninaweza “kuiinua” mikono hiyo?
-
“Magoti dhaifu” ingeweza kumaanisha nini? Ni kwa jinsi gani yataimarishwa?
Ni kwa jinsi gani Mwokozi anafanya mambo haya kwa ajili yako?
Pengine kujifunza mstari huu kumemleta akilini mtu fulani ambaye ungeweza “kumsaidia,” “kumwinua,” au “kumuimarisha.” Utafanya nini ili kumhudumia mtu huyo?
Nini kingine unachojifunza kuhusu huduma kwa wengine katika Mafundisho na Maagano 82:18–19? Ungeweza pia kutazama video “Teachings of Thomas S. Monson: Rescuing Those in Need” (ChurchofJesusChrist.org). Ni jinsi gani waumini wa kata ya Askofu Monson walionesha kile mistari hii inachokifundisha?
Ona pia Yakobo 2:17–19; Mosia 18:8–9; “Works of God” (video), ChurchofJesusChrist.org.
Mwokozi amenipatia vingi na anataka vingi kutoka kwangu.
Kusoma mstari huu kungeweza kukusukuma upitie tena kile ambacho Mungu amekupa—baraka za kimwili na kiroho. Kumbuka hili unaposoma sehemu ya 82 iliyosalia. Ni kipi unahisi Mungu anahitaji kutoka kwako?
Ona pia “Because I Have Been Given Much,” Nyimbo za Dini, na. 219.
Amri ni ushahidi wa upendo wa Mungu kwa ajili yetu.
Ikiwa wewe au mtu unayemfahamu amewahi kujiuliza kwa nini Bwana hutoa amri nyingi sana, Mafundisho na Maagano 82:8–10 ingeweza kusaidia. Ni umaizi upi kutoka katika mistari hii ungeweza kukusaidia kumwelezea mtu kwa nini unachagua kufuata amri za Bwana? Ni kipi ungeweza kukilinganisha na amri ambacho kingeweza kusaidia? Ungeweza kupata umaizi wa ziada katika Mafundisho na Maagano 1:37–38; 130:20–21 na video ““Blessed and Happy Are Those Who Keep the Commandments of God” (Maktaba ya Injili). Uzoefu upi umekufunza uzione amri kama baraka?
Fikiria kuhusu baadhi ya amri ambazo Mungu amekupatia. Ni nini amri hizi zimekufundisha kumhusu Yeye na mapenzi Yake? (ona mstari wa 8). Ni kwa jinsi gani maisha yako yameathiriwa kwa kushika amri hizi?
Unajifunza nini kumhusu Bwana kutoka kwenye mstari wa 10? Unadhani inamaanisha nini kwa Bwana “kufungwa”? (ona pia mstari wa 15).
Ni kwa jinsi gani Bwana ametimiza ahadi Zake katika maisha yako? Ni kipi ungeweza kumwambia mtu ambaye hajahisi kupata motisha ya kushika amri kwa sababu hawajapokea baraka walizozitumainia? Je, unapata umaizi wowote wenye msaada katika ujumbe wa Mzee D. Todd Christofferson “Uhusiano Wetu na Mungu”? (Liahona, Mei 2022, 78–80).
Ona pia Topics and Questions, “Commandments,” Maktaba ya Injili.
Bwana hutubariki katika njia Zake za ajabu.
Dada Virginia H. Pearce, aliyekuwa mshiriki wa Urais Mkuu wa Wasichana, alizungumza kuhusu mwanamke ambaye alikuwa na wasiwasi sana juu ya watoto wake waliokuwa wakifanya chaguzi mbaya. Katika hofu, alijaribu kila kitu ambacho angeweza kufikiria ili kupata baraka za Bwana kwa niaba yao. Kama nyongeza kwenye sala ya dhati, aliweka lengo kubwa la kuongeza uhudhuriaji hekaluni na kuhisi kuwa na uhakika kwamba Bwana angetukuza dhabihu hii kubwa kwa kuibadili mioyo ya watoto wake. Mwanamke huyo alisema:
“Baada ya ongezeko la kuhudhuria zaidi hekaluni kwa kipindi cha miaka kumi na kusali siku zote, ninasikitika kusema kwamba chaguzi za watoto wangu hazijabadilika. …
“Lakini mimi nimebadilika. Mimi ni mwanamke tofauti. … Nina moyo mkunjufu sana. Nimejawa na huruma. Hakika ninaweza kufanya mengi na sina hofu, wasiwasi, hatia, lawama, na siogopi. Nimeacha mipaka yangu ya muda na ninaweza kumngojea Bwana. Na ninapokea madhihirisho ya kila mara ya nguvu za Bwana. Yeye hutuma huruma nyororo, jumbe ndogo ndogo ambazo zinathibitisha upendo wake kwa ajili yangu na watoto wangu. Matarajio yangu yamebadilika. Badala ya kutarajia watoto wangu wabadilike, ninatarajia huruma hizi nyororo za kila mara na nimejawa na shukrani kwa ajili ya hizo. …
“Sala zangu zimebadilika. Ninaonesha upendo zaidi na nina shukrani sana. … Bwana hufanya kazi katika njia za ajabu, na kwa kweli nimejazwa na amani ipitayo akili zote” (katika “Prayer: A Small and Simple Thing,” At the Pulpit [2017], 288–89).
“Wajane na yatima watahudumiwa.”
Mnamo Aprili 1832, kama ilivyoelekezwa na Bwana, Joseph Smith alisafiri karibu maili 800 kuwatembelea Watakatifu ambao walikuwa wamekusanyika Missouri (ona Mafundisho na Maagano 78:9). Wakati akiwa huko, alitembelea jamii iliyokuwa na wajane kadhaa ambao walikuwa wakilea watoto wao peke yao. Kati yao walikuwa Phebe Peck na Anna Rogers, ambao Nabii aliwafahamu binafsi. Huko Missouri mnamo miaka ya 1830, sheria za nchi ziliwapa wajane haki zenye ukomo kwenye mali za waume zao waliofariki. Unajifunza nini kutoka sehemu ya 83 kuhusu jinsi Bwana anavyohisi kuhusu wajane na yatima? Je, unamfahamu yeyote katika hali hii ambaye angenufaika kutokana na upendo wako na kujali kwako? Ni zipi baadhi ya njia ambazo kupitia kwazo unaweza kushiriki kile ulichonacho na wajane, yatima, akina mama wanaolea watoto peke yao, na wengine walio na uhitaji?
Ona pia Isaya 1:17; Yakobo 1:27.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Ninaweza kusali kwa Mungu “kwa sauti na [ndani] ya moyo wangu.”
-
Unaposoma Mafundisho na Maagano 81:3 pamoja na watoto wako, wasaidie wafikirie sehemu tofauti “hadharani” na faraghani” ambapo wanaweza kusali. Ungeweza pia kusikiliza au kuimba pamoja nao wimbo kuhusu sala, kama vile “A Child’s Prayer” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, na. 144). Shirikini mmoja na mwingine kitu fulani kutoka kwenye wimbo huu ambacho hufundisha ukweli muhimu kuhusu sala. Ungeweza pia kuzungumza kuhusu kuzungumza kwa staha kwa Baba wa Mbinguni.
-
Ili kuwahimiza watoto wako wasali katika mioyo yao, ungeweza kuwapa mioyo ya karatasi na kuwaalika wachore au waandike kitu fulani ambacho wanataka kusali kukihusu kwa Baba wa Mbinguni. Shuhudia kwamba Baba wa Mbinguni anajua kile tunachokifikiria na kukihisi na Yeye anaweza kusikia sala zetu hata kama hatuzisemi kwa sauti. Ungeweza kushiriki nao uzoefu wakati uliposali moyoni mwako na Baba wa Mbinguni akakusikia.
Yesu Kristo ananitaka niwasaidie watu walio na uhitaji.
-
Pamoja na watoto wako, choreni picha za mikono na magoti, na waombe watoto wako watafute sehemu hizi za mwili katika Mafundisho na Maagano 81:5. Bwana anatuomba tufanye nini katika mstari huu? Mngeweza kushiriki mmoja na mwingine baadhi ya njia ambazo kupitia kwazo watu wamekuimarisha wakati ulipohisi kuwa “dhaifu” au “kulegea.” Video “Pass It On” (ChurchofJesusChrist.org) ingeweza kuwapatia watoto wako mawazo kuhusu jinsi ya kuwatumikia wengine. Mngeweza pia kuimba wimbo kuhusu huduma, kama vile “Kuna Lolote Jema Nimefanya” (Nyimbo za Dini, na. 128). Fikiria kuwasaidia watoto wako waweke mpango wa kumsaidia angalau mtu mmoja mwenye uhitaji wiki hii.
-
Ungeweza pia kutumia picha au video kusimulia hadithi rahisi za Yesu Kristo akiwahudumia wengine (ona picha kwenye muhtasari huu; Kitabu cha Sanaa ya Injili,, na. 41, 42, 46, 47, 55; au mojawapo ya Bible Videos katika Maktaba ya Injili). Ni kwa jinsi gani tunaweza kufuata mfano wa Mwokozi wa kuwasaidia wengine?
Baba wa Mbinguni anaahidi baraka tunapojitahidi kumtii Yeye.
-
Wewe na watoto wako mngeweza kuangalia katika Mafundisho na Maagano 82:8–10 kwa ajili ya majibu ya swali “Kwa nini Baba wa Mbinguni hutupatia amri?” Ungeweza kutaka kuwasaidia watoto wako wafikirie mifano ya amri Zake (ona, kwa mfano, Kutoka 20:4–17; Mathayo 22:37–39; Mafundisho na Maagano 89:5–17). Ingeweza kusaidia kama wewe na watoto wako mngepata au kuchora picha zinazowakilisha baadhi ya amri hizo. Ni kwa jinsi gani amri za Baba wa Mbinguni huonesha upendo Wake kwetu?
-
Pengine mchezo rahisi ungeweza kuwasaidia watoto wako wazione amri za Mungu kama baraka, wala si mizigo. Mtu mmoja angeweza kutoa maelekezo ili kumsaidia mtu mwingine, ambaye amefungwa macho, kufanya jambo fulani kama vile kutengeneza sandwichi au kuchora picha. Fikiria jambo la kufurahisha na la ubunifu! Kisha zungumza jinsi amri za Mungu zilivyo kama maelekezo katika mchezo huu.