“Agosti 18–24, ‘Kanuni yenye Ahadi’: Mafundisho na Maagano 89–92,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 89–92,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Agosti 18–24: “Kanuni yenye Ahadi”
Mafundisho na Maagano 89–92
Kwenye Shule ya Manabii, Nabii Joseph Smith aliwafunza wazee wa Israeli kuhusu kuujenga ufalme wa Mungu duniani. Walijadili kweli za kiroho, walisali pamoja, walifunga, na walijiandaa kuhubiri injili. Lakini kulikuwa na kitu kuhusu mazingira ambacho kingeweza kuonekana si cha kawaida kwetu leo, na hakikuonekana sawa kwa Emma Smith pia. Wakati wa vikao, wanaume walivuta na kutafuna tumbaku, kitu ambacho hakikuwa cha kushangaza kwa wakati huo, lakini iliweka madoa meusi kwenye sakafu za mbao na kuacha harufu mbaya kwenye hewa. Emma alishiriki wasiwasi wake kwa Joseph, na Joseph alimwomba Bwana. Jibu la Bwana lilikuwa ufunuo ambao ulikwenda mbali zaidi ya kuvuta tumbaku na uchafu wa tumbaku. Uliwapa Watakatifu, kwa vizazi vijavyo, “kanuni yenye ahadi”—ahadi ya afya ya kimwili, “hekima,” na “hazina kubwa ya maarifa” (Mafundisho na Maagano 89:3, 19).
Ona pia Saints, 1:166–68.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Bwana alinipa Neno la Hekima ili linisaidie niwe mwenye afya katika mwili na roho.
Wakati wazee katika Shule ya Manabii waliposikia kwa mara ya kwanza Joseph Smith akisoma Neno la Hekima, kwa haraka “walirusha mirija na misokoto ya tumbaku ya kutafuna kwenye moto” (Saints, 1:168). Walitaka kuonesha utayari wao wa kumtii Bwana. Pengine tayari “umerusha” kutoka kwenye maisha yako vitu ambavyo Neno la Hekima linaonya dhidi yake, lakini nini kingine unajifunza kutoka kwenye ufunuo huu? Zingatia mawazo haya:
-
Fikiria ufunuo kama “kanuni yenye ahadi” (mstari wa 3)—kweli za kudumu ambazo zinaongoza ufanyaji maamuzi. Je, ni kanuni zipi unazipata ambazo zinaweza kuongoza maamuzi yako? Ni baraka zipi Bwana anaahidi? (ona mstari wa 18–21). Ni kwa jinsi gani Yeye ametimiza ahadi hizo katika maisha yako?
-
Ni mifano ipi umeiona ya “uovu na njama … katika mioyo ya watu wenye kula njama” kuhusiana na Neno la Hekima? (mstari wa 4). Kwa nyongeza ya ufunuo huu, ni kipi Bwana amekupa ili kikusaidie uepuke na ushinde uovu huu?
-
Ni kipi ufunuo huu unakufundisha kumhusu Bwana? Ni kwa jinsi gani Neno la Hekima linahusiana na Mafundisho na Maagano 29:34–35?
-
Ni kipi unasukumwa kufanya ili kuutunza vizuri mwili wako?
Unaweza kuwa ulipata fursa za kuwaelezea wengine kwa nini unaishi Neno la Hekima—na unaweza kuwa na fursa zaidi katika siku zijazo. Zingatia jinsi gani ungeweza kutumia fursa hizi kushuhudia juu ya Mwokozi, utakatifu wa miili yetu, na kweli zingine za kiroho. Kwa ajili ya mawazo, ona “Mwili wako ni mtakatifu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi, 22–29.
Ona pia 1 Wakorintho 6:19–20; Thomas S. Monson, “Kanuni na Ahadi,” Liahona, Nov. 2016, 78–79; Topics and Questions, “Word of Wisdom,” Maktaba ya Injili; “The Word of Wisdom,” katika Revelations in Context, 183–91; “Addiction,” “Physical Health,” Life Help, Maktaba ya Injili.
Urais wa Kwanza unashikilia “funguo za ufalme.”
Katika sehemu ya 90, Bwana alitoa maelekezo kuhusu “huduma na urais” (mstari wa 12) wa Joseph Smith, Sidney Rigdon, na Frederick G. Williams—washiriki wa kile ambacho sasa tunakiita Urais wa Kwanza. Unajifunza nini kuhusu Urais wa Kwanza kutoka mstari wa 1–17? Fikiria kupitia tena jumbe za hivi karibuni kutoka kwa washiriki wa Urais wa Kwanza. Wanafanya nini ili “kuweka vyema mambo yote ya kanisa hili na ufalme”? (mstari wa 16). Ni kwa jinsi gani unaweza kuonesha kwamba si “kitu rahisi” kwako? (mstari wa 5).
Fikiria kuimba au kusoma maneno ya “Msikilize Nabii” (Nyimbo za Dini,, na. 16) au wimbo mwingine kuhusu manabii ambao unaendana na mafundisho katika mistari hii. Je, ni kwa jinsi gani huduma ya Urais wa Kwanza imekusaidia uwajue Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo?
“Mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida [yangu].”
Tafakari uzoefu wowote uliowahi kuwa nao ambao unashuhudia juu ya ahadi ya Bwana katika Mafundisho na Maagano 90:24. Zingatia kuandika uzoefu wako na kuushiriki pamoja na mwanafamilia au mpendwa wako—pengine mtu anayehitaji hakikisho jipya au kutiwa moyo. Ikiwa una baraka ambazo bado unazisubiri, tafakari kile unachoweza kufanya ili kubaki mwaminifu wakati unaposubiri kuona “mambo yote yakifanyika kwa pamoja kwa faida yako.”
Mafundisho na Maagano 90:28–31
Vienna Jaques alikuwa nani?
Vienna Jaques alizaliwa mnamo Juni 10, 1787, huko Massachusetts. Mwanamke wa imani ambaye alikuwa na kipato kikubwa, Vienna mara ya kwanza alikutana na wamisionari mnamo 1831. Baada ya kupata ushahidi wa kiroho kwamba ujumbe wao ulikuwa wa kweli, alisafiri kwenda kukutana na Nabii huko Kirtland, Ohio, ambapo alibatizwa.
Vienna alitii ushauri wa Bwana kwake katika Mafundisho na Maagano 90:28–31. Uwekaji wakfu wake kwa Bwana, ambao ulijumuisha michango aliyofanya mapema huko Kirtland, vilikuja kipindi muhimu sana kwa kanisa, wakati viongozi walipokuwa wakijaribu kununua ardhi ambapo Hekalu la Kirtland lingejengwa. Vienna alikuwa “mwaminifu, na hakuwa … mvivu” kote katika maisha yake na hatimaye aliweza “kutulia katika amani” (mstari wa 31) huko Salt Lake Valley, ambapo alifariki akiwa na umri wa miaka 96.
“Roho hudhihirisha ukweli.”
Sisi sote tunakutana na jumbe ambazo zina “mambo mengi … ambayo ni ya kweli” na “mambo mengi … ambayo si ya kweli” (Mafundisho na Maagano 91:1–2). Ni ushauri upi unaoupata katika sehemu ya 91 ambao unaweza kukusaidia utambue ukweli katika jumbe unazokutana nazo? Ni kwa jinsi gani Roho alikusaidia ujue tofauti kati ya ukweli na kosa?
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Neno la Hekima hunisaidia niwe mwenye afya katika mwili na roho.
-
Ili kutambulisha sehemu ya 89, pengine wewe na watoto wako mngeweza kuangalia picha ya hekalu au kuimba wimbo kuhusu afya ya kimwili, kama vile “The Lord Gave Me a Temple” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 153), ili kufundisha kwamba miili yetu ni kama mahekalu ya roho zetu. Wasaidie watoto wako waigize jinsi wanavyoweza kuitunza miili yao.
-
Ili kujifunza kuhusu amri za Bwana katika Mafundisho na Maagano 89:10–17), wewe na watoto wako mngeweza kuchora au kuangalia picha za vitu vizuri tunavyoweza kula au tunavyoweza kufanya ili kuiweka miili yetu iwe yenye afya (ona picha na ukurasa wa shughuli mwisho wa muhtasari huu). Ni nini Bwana anatuonya tusitumie? Kwa nini Yeye anatutaka tuitunze miili yetu?
-
Mzee Gary E. Stevenson aliwashauri vijana kupanga mapema kile watakachofanya wakati watakapojaribiwa kwa pombe au madawa ya kulevya. Alifundisha: “Mtaona kwamba majaribu yana uwezo mdogo juu yenu. Mtakuwa tayari mmekwishafanya uamuzi wa jinsi mtakavyojibu na kile mtakachokifanya. Hamtahitaji kufanya uamuzi kila mara” (“Kitabu Chenu cha Mchezo cha Ukuhani,” Liahona, Mei 2019, 48). Baada ya kusoma pamoja Mafundisho na Maagano 89:4 na kauli ya Mzee Stevenson, shauriana na watoto wako kuhusu jinsi wanavyoweza kuamua sasa—kwa maisha yao yote—kuishi Neno la Hekima. Mngeweza hata kuigiza nafasi jinsi ambavyo wangeweza kujibu kama mtu fulani, hata rafiki, akiwapa kitu fulani ambacho ni kinyume na Neno la Hekima. Ni kwa jinsi gani Bwana hutubariki tunapotii Neno la Hekima? (ona mistari 18–21).
Mungu hunipa manabii waniongoze na kunilinda.
-
Ungeweza kuangalia picha za manabii wa kale au kuimba wimbo kama vile “Follow the Prophet” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 110–11). Ni kwa jinsi gani Mungu amewabariki watoto Wake kupitia manabii Wake? Kwa nini tunapaswa kuwasikiliza manabii wa Mungu? (ona Mafundisho na Maagano 90:5). Kisha wewe na watoto wako mngeweza kuangalia picha ya nabii aliye hai na kushiriki baadhi ya vitu ambavyo Bwana amefundisha au kutuonya kuvihusu kupitia nabii huyo. Ni kwa jinsi gani tunaweza kumfuata nabii?
Roho anaweza kunisaidia nijue kipi ni kweli.
-
Ungeweza kufanyia muhtasari kichwa cha habari cha sehemu kwa ajili ya Mafundisho na Maagano 91 ili kuwasaidia watoto wako waelewe kwa nini ufunuo huu ulitolewa. Wangeweza kisha kufikiria sehemu, kama vile katika vyombo vya habari, ambapo tunapata “vitu vingi … ambavyo ni vya kweli” na “vitu vingi … ambavyo siyo vya kweli” (mistari 1–2). Ni nini mstari wa 4–6 inatufundisha kuhusu Roho Mtakatifu? Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu hutusaidia tujue kile kilicho sahihi?