“Septemba 15–21: ‘Baada ya Taabu Kubwa … Huja Baraka’: Mafundisho na Maagano :102-105,: Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 102–105,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
September 15–21: “Baada ya Taabu Kubwa … Huja Baraka”
Mafundisho na Maagano 102–105
Watakatifu wa Kirtland walivunjwa mioyo kusikia kwamba kaka na dada zao wa Jackson County, Missouri, walikuwa wakifukuzwa kutoka kwenye nyumba zao. Lazima ilikuwa inatia moyo, wakati huo, wakati Bwana alipotangaza kwamba “ ukombozi wa Sayuni” hauna budi “kuja kwa uwezo” (Mafundisho na Maagano 103:15). Kwa ahadi hiyo katika mioyo yao, wanaume zaidi ya 200 na takriban wanawake na watoto 25 walijisajili katika kile walichokiita Kambi ya Israeli, baadaye ikijulikana kama Kambi ya Sayuni. Kazi yake ilikuwa kutembea kwenda Missouri na kuikomboa Sayuni.
Kwa washiriki wa Kambi, kuikomboa Sayuni kulimaanisha kuwarejesha Watakatifu kwenye ardhi yao. Lakini punde kabla Kambi haijawasili Jackson County, Bwana alimwambia Joseph Smith kuisitisha na kuivunja Kambi ya Sayuni. Baadhi ya washiriki wa Kambi walitatizwa na kukasirika; ilionekana kwamba safari ilikuwa imeshindikana na ahadi za Bwana hazikutimia. Wengine, hata hivyo, waliiona kitofauti. Wakati watakatifu waliofukuzwa hawakupata tena ardhi na nyumba zao, uzoefu uliwaletea kiwango cha “ukombozi” kwa Sayuni, na “ulikuja kwa uwezo.” Washiriki waaminifu wa Kambi ya Sayuni, wengi wao ambao baadaye walikuwa viongozi wa Kanisa, walishuhudia kwamba uzoefu uliongeza kwa kina imani yao katika uweza wa Bwana, kwenye wito mtakatifu wa Joseph Smith, na katika Sayuni—si tu Sayuni ambayo ni mahali bali Sayuni ambayo ni watu wa Mungu. Badala ya kutilia shaka thamani ya kazi hii iliyoonekana kutofanikiwa, walijifunza kwamba kazi halisi ni kumfuata Mwokozi, hata wakati ambapo hatuelewi kila kitu. Hivi ndivyo Sayuni, hatimaye, itakavyokombolewa.
Ona Saints, 1:194–206; “The Acceptable Offering of Zion’s Camp,” katika Revelations in Context, 213–18.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Mafundisho na Maagano 102:12–23
Je, ni nini dhumuni la mabaraza ya uumini?
Sehemu ya 102 ina mihutasari ya mkutano wa Kirtland, Ohio, ambapo baraza kuu la kwanza la Kanisa lilianzishwa. Katika mstari wa 12–23, Bwana anaelezea taratibu zinazofuatwa na mabaraza makuu wakati wanapofanya mabaraza ya uumini kwa wale waliofanya makosa makubwa.
Rais M. Russell Ballard alifundisha, “Waumini wakati mwingine huuliza kwa nini mabaraza ya [uumini] ya Kanisa yanafanyika. Kusudi lina sehemu tatu: kuokoa roho ya mvunja sheria, kumlinda asiye na hatia, na kulinda usafi, uadilifu, na jina zuri la Kanisa” (Nafasi ya Kuanza Upya: Mabaraza ya Nidhamu ya Kanisa na Urejesho wa Baraka,” Ensign,. Sept. 1990, 15).
Ona pia Topics and Questions, “Membership Councils,” Maktaba ya Injili.
Mafundisho na Maagano 103:1–12, 36; 105:1–19
Sayuni inaweza kujengwa tu juu ya kanuni za uadilifu.
Kwa nini Watakatifu walipoteza ardhi yao ya ahadi huko Missouri? Yaweza kuwa kulikuwa na sababu nyingi—angalau moja, Bwana alisema, ilikuwa ni “uvunjaji sheria wa watu wangu.” Kama isingekuwa hivyo, Sayuni “ingeweza kukombolewa” (Mafundisho na Maagano 105:2). Unaposoma Mafundisho na Maagano 103:1–12, 36; 105:1–19, unaweza kuona baadhi ya vitu ambavyo vilizuia kuanzishwa kwa Sayuni katika Missouri na vingine ambavyo vingeweza kusaidia. Unajifunza nini ambacho kinaweza kukusaidia uanzishe Sayuni katika moyo wako, nyumba yako, na jamii yako?
Mafundisho na Maagano 103:12–13, 36; 105:1–6, 9–19
Baraka zinakuja baada ya majaribu ya imani.
Katika njia nyingi, kushiriki katika Kambi ya Sayuni ilikuwa jaribu la imani. Safari ilikuwa ndefu, hali ya hewa ilikuwa ya joto, na chakula na maji vilikuwa wakati mwingine haba. Na baada ya yote waliyovumilia, Kambi ya Sayuni bado haikufanikiwa katika kuwarudisha Watakatifu kwenye ardhi yao. Fikiria kama ungekuwa na fursa ya kumwandikia barua mshiriki wa Kambi ya Sayuni ambaye imani yake katika Bwana ilikuwa imeyumbishwa kwa uzoefu wake. Ni nini ungesema ili kumtia moyo mtu huyu? Unapata kweli zipi katika Mafundisho na Maagano 103: 5–7, 12–13, 36; 105:1–6, 9–19 ambazo zingeweza kusaidia?
Kisha ungeweza kufikiria kuhusu mfano wa siku za leo wa jaribu kama la Kambi ya Sayuni—kama vile mmisionari ambaye anafanya bidii, lakini hakuna mtu anayejiunga na Kanisa kwa sababu ya juhudi zake. Kulingana na kile unachojifunza, ni kwa jinsi gani ungeweza kumsaidia mmsionari huyo kuona kwamba misheni yake bado imefanikiwa?
Ni kwa jinsi gani Bwana amekubariki wewe “baada ya taabu kubwa”? (Mafundisho na Maagano 103:12).
Ona pia 1 Nefi 11:16–17; Alma 7:11–12; Mafundisho na Maagano 6:33–36; 84:88; 101:35–36; David A. Bednar, “On the Lord’s Side: Lessons from Zion’s Camp,” Ensign, Julai 2017, 26–35, au Liahona, Julai 2017, 14–23; Topics and Questions, “Endure to the End,” Maktaba ya Injili; “Msingi Imara,” Nyimbo za Dini, na. 36.
Je, dhumuni la majaribu ni nini?
Zingatia ushauri wa Mzee Orson F. Whitney kuhusu dhumuni la majaribu: “Hakuna maumivu ambayo tunayapata, hakuna majaribu ambayo tunayapitia ambayo hayana faida. Yanahudumia elimu yetu, kukuza sifa kama vile subira, imani, ustahimilivu, na unyenyekevu. Yale yote tutesekayo na yale yote tuvumiliayo, hasa wakati tuvumiliapo kwa subira, hujenga sifa yetu, hutakasa mioyo yetu, hupanua nafsi zetu, na hutufanya tuwe wapole sana na wenye hisani, wastahiki zaidi kuitwa watoto wa Mungu … na ni kupitia huzuni na mateso, masumbuko na taabu, kwamba tunapata elimu ambayo tulikuja hapa kuipata na ambayo itatufanya tuwe zaidi kama Baba yetu na Mama yetu wa mbinguni” (katika Spencer W. Kimball, Imani Hutangulia Miujiza [1972], 98).
Mafundisho na Maagano 104:11–18, 78–83
Bwana amenifanya kuwa “msimamizi wa baraka za kidunia.”
Kwa kuongezea kwenye majaribu huko Missouri, mnamo 1834 Kanisa lilikabiliwa na matatizo ya kifedha, ikiwa ni pamoja na madeni na matumizi makubwa. Katika sehemu ya 104 Bwana alitoa ushauri kuhusu hali ya kifedha ya Kanisa. Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia kanuni katika mstari wa 11–18 na 78–83 kwenye maamuzi yako mwenyewe ya kifedha?
Ona pia “Treasure in Heaven: The John Tanner Story” na “The Labor of His Hands” (video), Maktaba ya Injili.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Ninaweza kuwa “nuru kwa ulimwengu” kwa kumfuata Yesu.
-
Ungeweza kuwaalika watoto wako kushikilia picha ya balbu ya taa, mshumaa, au chanzo kingine cha mwanga wakati unasoma Mafundisho na Maagano 103:9. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa nuru kwa wengine wakati tunapomfuata Yesu Kristo? Ona pia “Jesus Wants Me for a Sunbeam,” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 60–61).
Mafundisho na Maagano 104:13–18
Bwana ananitaka nishiriki kitu nilichonacho kwa watu walio na uhitaji.
-
Unaweza kutaka kuwapa watoto wako dakika chache ili watengeneze orodha ya baraka ambazo Mungu amewapa (kama vile chakula, nguo, talanta, imani na nyumba). Wahamasishe waorodheshe nyingi kadiri wanavyoweza. Kisha mngeweza kusoma pamoja Mafundisho na Maagano 104:13–18, mkitafuta majibu ya maswali kama haya: Je, ni nani mmiliki wa kweli wa vitu vyote? Je, Yeye anataka sisi tufanye nini kwa vitu hivi? Wewe na watoto wako mngeweza kushiriki uzoefu ambapo mtu fulani alikupa kitu ulichokuwa unakihitaji (ona “the Coat” [video], Maktaba ya Injili].
Bwana atanibariki ninaposhika amri Zake.
-
Mara kadhaa katika sehemu ya 104 Bwana anaahidi “wingi wa baraka” kwa watu wanaotii amri Zake kwa uaminifu. Ili kuwasaidia watoto waelewe kile ambacho “wingi” humaanisha, ungeweza kuchora duara na kuwaomba watoto wako wakusaidie kuzidisha idadi ya duara—wakichora mbili, kisha nne, kisha nane, kisha kumi na sita, na kadhalika. Kila wakati mnapoongeza duara, wasaidie watoto wako wafikirie juu ya baraka ambayo Baba wa Mbinguni amewapatia.
Mafundisho na Maagano 105:38–40
Ninaweza kuwa mpatanishi.
-
Ili kuwasaidia watoto wako wajifunze hadithi za Kambi ya Sayuni, ungeweza kushiriki “Sura ya 36: Kambi ya Sayuni,” (katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 135–39, au video sawa na hiyo katika Maktaba ya Injili). Tua mara kwa mara ili kuzungumza kuhusu masomo tunayoweza kujifunza kutokana na Kambi ya Sayuni—kwa mfano, kwamba Bwana anatutaka tuwe watulivu na tufanye kazi pamoja badala ya kubishana na kupigana (ona pia Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” Liahona, Mei 2023, 98–101).
-
Ungeweza pia kusoma Mafundisho na Maagano 105:38–40 na waombe watoto kusimama kila wakati wanaposikia neno “amani.” Eleza kwamba Bwana aliwataka Watakatifu wafanye amani na watu waliokuwa wakiwafanyia ukatili. Wasaidie watoto wako wafikirie mambo ambayo wangeweza kufanya ili kuwa wapatanishi, na waalike wafanyie maigizo baadhi ya hali hizo.