“Sauti za Urejesho: Kambi ya Sayuni,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Kambi ya Sayuni,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Sauti za Urejesho
Kambi ya Sayuni
Kwa sababu Kambi ya Sayuni kamwe haikuwarejesha Watakatifu kwenye ardhi yao huko Jimbo la Jackson, watu wengi walihisi kwamba jitihada zao zilishindwa. Hata hivyo, washiriki wengi wa Kambi ya Sayuni waliangalia nyuma kwenye uzoefu wao na waliona jinsi Bwana alivyokamilisha azma kuu katika maisha yao na katika ufalme Wake. Hapa ni baadhi ya shuhuda zao.
Joseph Smith
Zaidi ya miaka 40 baada ya Kambi ya Sayuni, Joseph Young, ambaye alikuwa mshiriki wa kambi, aliripoti kwamba Joseph Smith alisema yafuatayo:
“Akina kaka, baadhi yenu mna hasira na mimi, kwa sababu hamkupigana Missouri; lakini acha niwaambieni, Mungu hakutaka ninyi mpigane. Asingeweza kuanzisha ufalme wake akiwa na wanaume kumi na wawili wakifungua mlango wa injili kwa mataifa ya dunia, pamoja na wanaume sabini chini ya maelekezo yao ili kufuata katika nyayo zao, isipokuwa awachukue kutoka kundi la wanaume walioyatoa maisha yao, na waliokwishafanya dhabihu iliyo kubwa kama alivyofanya Ibrahimu.
“Sasa, Bwana amejipatia Kumi na Wawili na Sabini wake, na kutakuwepo na akidi zingine za Sabini zitakazoitwa, ambao watafanya dhabihu na hao ambao hawajafanya dhabihu zao na matoleo yao sasa, watazifanya baadaye.”
Brigham Young
“Tulipofika Missouri Bwana alizungumza na mtumishi wake Joseph na alisema, ‘Nimeikubali dhabihu yenu,’ na tulikuwa na fursa ya kurudi tena. Niliporudi marafiki wengi waliniuliza kulikuwa na faida gani katika kuwaita wanaume kutoka kwenye kazi zao kwenda Missouri na kisha kurudi, bila kufanikisha chochote. ‘Imemfaidisha nani?’ waliuliza. ‘Kama Bwana aliamuru ifanyike, alikuwa na maono ya jambo gani katika kufanya hivyo?’ … Niliwaambia ndugu hao kwamba nililipwa vizuri—nililipwa kwa riba kubwa—ndio kwamba kipimo changu kilijazwa mpaka kumwagika kwa ufahamu ambao niliupokea kwa kusafiri na Nabii.”
Wilford Woodruff
“Nilikuwa katika Kambi ya Sayuni pamoja na Nabii wa Mungu. Niliona matendo ya Mungu kwake. Niliona nguvu ya Mungu kwake. Niliona kwamba alikuwa Nabii. Kile kilichodhihirishwa kwake kwa nguvu ya Mungu juu ya misheni ile kilikuwa cha thamani kubwa kwangu na kwa wote waliopokea maelekezo yake.”
“Wakati washiriki wa Kambi ya Sayuni walipoitwa wengi wetu kamwe tulikuwa hatujawahi kuona sura za kila mmoja wetu; tulikuwa wageni kwa kila mmoja wetu na wengi kamwe hawakuwahi kumwona nabii. Tulikuwa tumetawanywa ughaibuni, kama mahindi yanavyochekechwa katika chekecheo, katika taifa zima. Tulikuwa vijana, na tuliitwa mapema siku hiyo kwenda na kuikomboa Sayuni, na kile tulichotakiwa kukifanya ilibidi tukifanye kwa imani. Tulikusanyika pamoja kutoka Majimbo tofauti tofauti pale Kirtland na tulikwenda kuikomboa Sayuni, katika kukamilisha amri ya Mungu kwetu. Mungu alikubali kazi zetu kama alivyofanya kwa kazi za Ibrahimu. Tulikamilisha sehemu kubwa, ingawa waliokengeuka na wasioamini mara nyingi waliuliza swali ‘mmefanya nini?’ Tulipata uzoefu ambao kamwe tusingeweza kuupata [katika] njia nyingine yoyote. Tulikuwa na fursa ya kuuona uso wa nabii, na tulikuwa na fursa ya kusafiri maili elfu pamoja naye, na kuona kazi za roho wa Mungu kwake, na mafunuo ya Yesu Kristo ndani yake na utimizwaji wa mafunuo hayo. Na aliwakusanya kiasi cha wazee mia mbili kutoka taifa zima mapema katika siku hiyo na alituletea tangazo kwa ulimwengu la kuihubiri injili ya Yesu Kristo. Kama nisingeenda na Kambi ya Sayuni nisingeweza kuwa hapa leo [katika Jiji la Salt Lake, nikihudumu katika Akidi ya Kumi na Wawili]. … Kwa kwenda kule tuliwekwa kwenye shamba la mizabibu ili kuihubiri injili, na Bwana alikubali kazi zetu. Na katika kazi zetu zote na mateso, pamoja na maisha yetu mara nyingi yakiwa hatarini, ilitubidi tufanye kazi na kuishi kwa imani.”
“Uzoefu [sisi] tulioupata kwa kusafiri katika Kambi ya Sayuni ulikuwa wa thamani zaidi kuliko dhahabu.”