“Septemba 29–Oktoba 5: ‘Ni Nyumba Yako, Mahali pa Utakatifu Wako’: Mafundisho na Maagano 109–110,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 109–110,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Septemba 29–Oktoba 5: “Ni Nyumba Yako, Mahali pa Utakatifu Wako”
Mafundisho na Maagano 109–110
Milango kwenye Hekalu la Kirtland haikutakiwa kufunguliwa mpaka saa 2:00 asubuhi ya Machi 27, 1836. Lakini Watakatifu waliotegemea kuhudhuria huduma za kuwekwa wakfu walianza kujipanga mapema hata kabla ya saa 1:00 asubuhi. Sehemu ya watakaozidi na kisha kikao cha pili vilihitajika ili kumwingiza kila mmoja aliyefika. Na haikuwa walio hai tu waliokuwa na hamu ya kuwepo. Mashahidi wengi walishuhudia kwamba waliwaona malaika ndani ya hekalu na hata kwenye paa, wakati na baada ya kuwekwa wakfu. Hakika ilionekana kwamba “majeshi ya mbinguni” yalikuwa yamekuja “kuimba na kupaza sauti” pamoja na Watakatifu wa Siku za Mwisho (“Roho wa Mungu,” Nyimbo za Dini, na. 2).
Kwa nini shangwe kuu—pande zote mbili za pazia? Baada ya karne kadhaa, kumekuwa na nyumba ya Bwana tena duniani. Bwana alikuwa anatimiza ahadi Yake ya kuwabariki Watakatifu Wake “kwa uwezo utokao juu” (Mafundisho na Maagano 38:32). Na hii, Yeye alitamka, “ni mwanzo tu wa baraka” (Mafundisho na Maagano 110:10). Enzi tunayoishi sasa—na uharakishaji wa kazi ya hekaluni na ibada zinazopatikana kwa mamilioni ya walio hai na wafu—ilikuwa na mwanzo wake huko Kirtland, wakati “pazia juu ya dunia [lilikuwa] linaanza kufunguka” (“Roho wa Mungu”).
Ona pia Watakatifu, 1:232–41.; “Nyumba kwa ajili ya Mungu Wetu,” katika Ufunuo katika Muktadha, 169–72.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Bwana ananipa baraka nyingi kupitia maagano ya hekaluni.
Hekalu la Kirtland lilikuwa tofauti na mahekalu tunayoyajua leo. Hapakuwa na madhabahu na hapakuwa na kisima cha ubatizo, kwa mfano. Lakini baraka zinazoelezwa katika sehemu ya 109, sala ya kuweka wakfu kwa ajili ya Hekalu la Kirtland, zinapatikana pia katika nyumba ya Bwana leo. Rejelea mistari ifuatayo ili kutafuta baadhi ya baraka hizi, na tafakari jinsi zinavyoweza kusaidia kuimarisha uhusiano wako na Baba yako wa Mbinguni na Yesu Kristo.
Mistari 5, 12–13 (ona pia Mafundisho na Maagano 110:6–8); katika nyumba ya Bwana, Yeye anaweza kujionyesha mwenyewe kwangu, na ninaweza kuhisi nguvu Zake.
Baraka zingine:
Kama umewahi kuingia katika nyumba ya Bwana, fikiria kuhusu jinsi gani ahadi hizi zimetimizwa katika maisha yako.
Wimbo “Roho wa Mungu” (Nyimbo za Dini, na. 2) uliandikwa kwa ajili ya kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Kirtland—na umekuwa ukiimbwa tangu wakati huo katika uwekwaji wakfu kwa kila hekalu. Zingatia kuimba au kuusikiliza kama sehemu ya kujifunza na kuabudu kwako. Ni baraka gani za hekalu unazipata zimeelezewa katika wimbo huu?
Sala ni mawasiliano na Baba wa Mbinguni.
Sehemu ya 109 ni sala ya kuweka wakfu ambayo Joseph Smith alipewa kwa ufunuo (ona kichwa cha habari cha sehemu hii). Unajifunza nini kuhusu sala kutoka sehemu hii? Kwa mfano, wewe ungeweza kufanya muhtasari wa kile nabii alichokitolea shukrani na baraka zipi aliziomba. Ni nini kingine alichokisema katika sala hii? Unapojifunza, ungeweza kutathmini mawasiliano yako mwenyewe na Baba wa Mbinguni. Unajifunza nini kuhusu Yeye na Mwanaye kutokana na sala hii?
Kama ungetaka kusoma sala za kuweka wakfu mahekalu mengine, ikijumuisha hekalu lililo karibu zaidi na wewe, tembelea ukurasa wa mahekalu kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org.
Mafundisho na Maagano 110:1–10
Bwana anaweza kujidhihirisha Mwenyewe kwangu katika nyumba Yake.
Unaposoma maelezo ya Mwokozi katika Mafundisho na Maagano 110:1–10, ikijumuisha kichwa cha habari cha sehemu, tafakari mistari hii inapendekeza nini kuhusu Yeye.
Je, Yesu Kristo anajidhirihishaje Mwenyewe—au anafanyaje ili Yeye mweyewe ajulikane kwako wewe—katika nyumba Yake? Yeye anakusaidiaje wewe kujua kwamba Anazikubali dhabihu zako?
Mafundisho na Maagano 110:10–16
Mwokozi anaelekeza kazi Yake kupitia funguo za ukuhani.
Kabla tu ya Musa, Elia, na Eliya kutokea katika hekalu ili kurejesha funguo za ukuhani, Yesu Kristo alisema, “Huu ni mwanzo wa baraka ambazo zitamwagwa juu ya vichwa vya watu wangu” (Mafundisho na Maagano 110:10). Unaposoma mistari 11–16, fikiria kuhusu baraka ambazo Mwokozi amemwaga juu yako kupitia kazi iliyoelekezwa kwa funguo hizi. Kwa mfano:
-
Mstari wa 11: Musa na funguo za kukusanywa kwa Israeli (au kazi ya umisionari). Je, ni kwa jinsi gani Bwana amekubariki wewe na familia yako kupitia juhudi za umisionari za Kanisa Lake?
-
Mstari wa 12: Elia na funguo za injili ya Ibrahimu, ikijumuisha Agano la Ibrahimu. Ni kwa jinsi gani Bwana angeweza kukubariki wewe na “vizazi baada yako [wewe]” kwa sababu ya maagano yako? (Ona Russell M. Nelson, “Agano Lisilo na Mwisho,” Liahona, Okt. 2022, 4–11; Mwongozo wa Maandiko, “Elias,” Maktaba ya Injili.)
-
Mistari 13–16: Eliya na nguvu ya kuunganisha inayojidhihirisha kupitia kazi ya hekaluni na historia ya familia. Kwa nini unafikiri Baba wa Mbinguni anataka wewe ujiunganishe kwa mababu zako kupitia ibada za hekaluni? (Ona Gerrit W. Gong, “Mwenye Furaha na Milele,” Liahona, Nov. 2022, 83–86.
Miunganiko gani unaiona kati ya funguo na wajibu wetu katika kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa (kuishi injili ya Yesu Kristo, kuwatunza wale walio katika shida, kuwaalika wote waipokee injili. na kuziunganisha familia kwa ajili ya milele)?
Ni uzoefu gani ambao umekuwa nao kwenye kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa? Je, uzoefu huu unakufundisha nini kuhusu Mwokozi, Kanisa Lake, na kazi Yake?
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Mafundisho na Maagano 109:12–13; 110:1–7.
Hekalu ni nyumba ya Bwana.
-
Wewe na watoto wako mngeweza kuzungumza kuhusu kitu fulani mnachokipenda kuhusu nyumba yenu. Kisha mngeweza kutazama picha ya Hekalu la Kirtlanda na kutumia Mafundisho na Maagano 109:12–13; 110:1–7 ili kuzungumza kuhusu jinsi hekalu hilo lilivyowekwa wakfu na kuwa nyumba ya Bwana (ona pia “Sehemu ya 39: Hekalu la Kirtland linawekwa wakfu,” katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 154, au video inayohusiana katika Maktaba ya Injili). Shiriki na kila mmoja kitu fulani unachopenda kuhusu nyumba ya Bwana.
-
Pengine wewe na watoto wako mngefikiria kwamba rafiki anajaribu kuitafuta nyumba yenu. Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kumsaidia rafiki yetu kujua nyumba yetu ni ipi? Je, tunajuaje kwamba hekalu ndiyo nyumba ya Bwana? (ona Mafundisho na Maagano 109:12–13).
Mwokozi anawabariki watu Wake kupitia funguo za ukuhani.
-
Ungeweza kutumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii au “Sehemu ya 40: Maono katika Hekalu la Kirtland” (katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 155–57, au video inayohusiana katika Maktaba ya Injili) ili kuwasimulia watoto kuhusu viumbe wa mbinguni waliotembelea hakalu hilo. Ungeweza pia kutumia picha iliyo mwishoni mwa muhtasari huu.
-
Ili kujifunza kuhusu umuhimu wa kitu kilichotokea katika Hekalu la Kirtand, wewe na watoto wako mngeweza kuzungumza kuhusu funguo zina kazi gani. Labda watoto wako wangeweza kupeana zamu kushika funguo na kujifanya wanafungu mlango uliofungwa. Wasaidie watafute neno funguo katika Mafundisho na Maagano 110:11–16, na zungumzeni kuhusu baraka ambazo funguo hizi hufungulia. Ungeweza kuelezea kwamba funguo za ukuhani ni ruhusa ya kuliongoza Kanisa Lake. Shiriki shukrani zako kwamba Bwana ametupatia sisi funguo za ukuhani.
Bwana anataka mimi nigeuze moyo wangu uwaelekee mababu zangu.
-
Baada ya Kusoma Mafundisho na Maagano 110:15 pamoja, wasimulie watoto wako kuhusu tukio ambalo lilikusaidia ugeuze moyo wako uwaelekee mababu zako. Mngeweza pia kuimba wimbo pamoja kama: “Family History—I Am Doing It” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 94).
-
Nini kinaweza kusaidia “kugeuza mioyo” ya watoto wako iwaelekee mababu zao? Mnaweza kupata baadhi ya mawazo ya kufurahisha kwenye FamilySearch.org/discovery. Mnaweza kushirikiana kuwatambua mababu ambao wanahitaji ibada za hekaluni. Kwa nini Yesu anatutaka sisi tuifanye kazi hii?