Njoo, Unifuate
Sauti za Urejesho: Maonyesho ya Kiroho na Hekalu la Kirtland


“Sauti za Urejesho: Maonyesho ya Kiroho na Hekalu la Kirtland,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)

“Maonyesho ya Kiroho na Hekalu la Kirtland,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025

ikoni ya sauti za urejesho

Sauti za Urejesho

Maonyesho ya Kiroho na Hekalu la Kirtland

Picha ya Hekalu la Kirtland

Hapa chini ni maneno ya Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao walikuwa ndani ya Hekalu la Kirtland wakati wa kuwekwa kwake wakfu na katika mikutano mingine ambayo ilifuata. Wengi walifananisha uzoefu wao na kile Watakatifu wa kale walivyohisi wakati walipokuwa “wamevikwa nguvu kutoka juu” kwenye siku ya Pentekoste (Luka 24:49; ona pia Matendo ya Mitume 2:1–4; Mafundisho na Maagano 109:36–37).

Eliza R. Snow

Portrait photograph of Eliza R. Snow seated in a chair.

“Sherehe hizo za kuwekwa wakfu zinaweza kukaririwa, lakini hakuna lugha ya duniani inayoweza kuelezea maonyesho ya kimbingu ya siku hiyo ya kukumbukwa. Malaika waliwatokea baadhi, wakati hali ya uwepo wa kiungu ikiwafikia wote waliokuwepo, na kila moyo ukajazwa na ‘shangwe isiyoelezeka na kujawa na utukufu.’”

Sylvia Cutler Webb

“Moja ya kumbukumbu zangu za mwanzo kabisa zilikuwa kuwekwa wakfu kwa Hekalu. Baba yangu alituchukua juu ya mapaja yake na alituambia kwa nini tulikua tunakwenda na kile ilichomaanisha kuweka wakfu nyumba kwa Mungu. Na ingawa tulikuwa wadogo sana wakati ule, ninakumbuka bayana tukio lile. Ninaweza kutazama nyuma katika miaka iliyopita na kuona kama nilivyoona wakati huo Joseph Nabii, amesimama na mikono yake imeinuliwa kuelekea mbinguni, uso wake ukiwa kijivu kilichofifia, machozi yakitiririka mashavuni mwake alipokuwa akinena kwenye siku ile isiyosahaulika. Karibu wote walionekana kuwa katika machozi. Nyumba ilikuwa imejaa mno, watoto walikuwa kwa kiasi kikubwa wamekaa katika mapaja ya watu wazima; dada yangu alikaa juu ya mapaja ya baba na mimi juu ya mapaja ya mama. Ninaweza kukumbuka hata nguo tulizovaa. Akili zangu zilikuwa changa mno wakati ule kuelewa umuhimu kamili wa yote, lakini jinsi muda ulivyosonga nilianza kufahamu zaidi na zaidi, na ninashukuru sana kwamba nilipata fursa ya kuwa pale.”

Oliver Cowdery

Head and shoulder portrait of Oliver Cowdery in suit and tie.

“Jioni nilikutana na maafisa wa kanisa katika nyumba ya Bwana. Roho alimwagwa kwa wingi—Niliona utukufu wa Mungu, kama wingu kubwa, likija chini na kutua juu ya nyumba, na kuijaza kama upepo mkali upitao wenye nguvu. Niliona vilevile miale ya ndimi, kama vile ya moto ikitua juu ya wengi, … wakati walipozungumza kwa lugha zingine na kutabiri.”

Benjamin Brown

“Maono mengi yalionwa. Mmoja aliona mto au wingu likitua juu ya nyumba, liking’aa kama wakati jua linapong’aa kwenye wingu kama dhahabu. Wawili wengine waliona viumbe watatu wakivinjari vinjari katika chumba wakiwa na funguo zinazong’aa mikononi mwao, na pia mnyororo unaong’aa mikononi mwao.”

Orson Pratt

Portrait engraving of Orson Pratt

“Mungu alikuwa pale, malaika zake walikuwa pale, Roho Mtakatifu alikuwa katikati ya watu … na walikuwa wamejazwa kutoka vilele vya vichwa vyao mpaka nyayo za miguu yao kwa nguvu na mwongozo wa kiungu wa Roho Mtakatifu.”

Nancy Naomi Alexander Tracy

“[Wakati] Hekalu lilipokamilika na kuwekwa wakfu … zilikuwa siku zangu mbili za shangwe kuu katika maisha yangu. Wimbo wa kufaa ambao ulitungwa kwa ajili ya tukio hili ulikuwa ‘Roho wa Mungu Awaka Kama Moto.’ Ilikuwa hakika kweli kwamba ushawishi wa Mbinguni ulitua juu ya nyumba ile. … Nilihisi kwamba mbingu ilikuwa duniani.”

Muhtasari

  1. Katika Edward W. Tullidge, The Women of Mormondom (1877), 95.

  2. Katika Karl Ricks Anderson, Joseph Smith’s Kirtland: Eyewitness Accounts (1996), 182–83.

  3. Oliver Cowdery diary, Machi 27, 1836, Church History Library, Salt Lake City.

  4. Benjamin Brown letter to his wife, Sarah, circa April 1836, Benjamini Brown family collection, Church History Library, Salt Lake City; vituo na herufi kubwa vimeboreshwa.

  5. Orson Pratt, “Remarks,” Deseret News, Jan. 12, 1876, 788.

  6. Katika Richard E. Turley Jr. na Brittany A. Chapman, eds., Wanawake wa Imani katika Siku za Mwisho (2011), 1:442.