Njoo, Unifuate
Sauti za Urejesho: Gereza la Liberty


“Sauti za Urejesho: Gereza la Liberty,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)

“Gereza la Liberty,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025

ikoni ya sauti za urejesho

Sauti za Urejesho

Gereza la Liberty

Wakati akiwa amefungwa katika Gereza la Liberty, Missouri, Joseph Smith alipokea barua kumtaarifu kuhusu hali ya hatari ya watakatifu wa siku za Mwisho waliokuwa wakifukuzwa kutoka jimboni kwa amri ya gavana. Barua yenye uchungu ilikuja kutoka kwa mke wake Emma. Maneno yake, na jibu la barua ya Joseph, inaonesha vyote mateso yao na imani yao wakati wa kipindi hiki kigumu katika historia ya Kanisa.

Gereza la Liberty

Joseph Smith na wengine walikuwa wameshikiliwa katika gareza hili katika majira ya baridi ya mwaka 1838–39.

Barua kutoka kwa Emma Smith kwenda kwa Joseph Smith, Machi 7, 1839

Kipenzi Mume wangu

Baada ya kupata fursa ya kutuma kupitia rafiki, ninafanya jaribio la kukuandikia, bali sitajaribu kuandika hisia zangu zote, kwani hali uliyopo, kuta, nondo, na komeo, mito inayounguruma, vijito vinavyotiririka, milima inayoinuka, mabonde yanayozama, na mbuga zinazosambaa ambazo zinatutenganisha, na udhalimu wa kikatili ambao kwanza ulikutupa kifungoni na bado unakushikilia huko, pamoja na fikra nyingi zingine, zinaweka hisia zangu mbali kusikoelezeka.

Kama isingekuwa ufahamu wa wewe kutokuwa na hatia, na mwingiliano wa rehema takatifu, nina uhakika kabisa kamwe nisingekuwa na uwezo kuweza kuvumilia vitendo vya mateso ambayo nimevipitia … ; lakini bado ninaishi na bado niko tayari kuteseka zaidi kama ni mapenzi ya ukarimu wa Mbinguni ambayo ninapaswa kuteseka kwa ajili yako.

Sote tuko salama wakati huu, isipokuwa Fredrick ambaye anaumwa sana.

Alexander mdogo ambaye sasa yupo mikononi mwangu ni mmoja wa watoto wanaopendeza uliowahi kuwaona katika maisha yako. Ana nguvu sana kiasi kwamba kwa msaada wa kiti atakimbia kuzunguka chumba kizima. …

Hakuna yeyote bali Mungu anayejua fikra za akili yangu na hisia za moyo wangu nilipoiacha nyumba na mji wetu, na karibia vitu vyote ambavyo tulikuwa navyo isipokuwa Watoto wetu wadogo, na kuanza safari yangu kutoka Jimbo la Missouri, nikikuacha umefungwa katika gereza hilo la upweke. Lakini kumbukumbu ni zaidi kuliko asili ya mwanadamu anavyostahili kuvumilia. …

… Ninatumaini siku nzuri zaidi bado zinakuja kwetu. … [Mimi] siku zote ni wako akupendaye.

Emma Smith

Barua kutoka kwa Joseph Smith kwenda kwa Emma Smith, Aprili 4, 1839

Mpenzi—na mke—nikupendaye.

Usiku wa Alhamisi niliketi chini wakati jua likizama, tulipokuwa tunachungulia kupitia viunzi vya nondo vya gereza hili la upweke, kukuandikia, ili niweze kukujulisha hali yangu. Ni kwamba ninaamini sasa karibia miezi mitano na siku sita tangu nimekuwa chini ya mkunjo wa uso wa mlinzi usiku na mchana, na ndani ya kuta, viunzi vya nondo, na misuguano ya milango ya chuma ya gereza la upweke, lenye giza, na chafu. Kwa hisia kubwa zinazojulikana kwa Mungu pekee naandika barua hii. Tafakari za akili katika hali kama hizi zinaishinda kalamu, au ulimi, au Malaika, kuelezea, au kuchora, kwa mwanadamu ambaye kamwe hajapata kupitia kitu hiki tunachokipitia sisi. … Tunaegemea kwenye mkono wa Yehova, na hakuna mwingine, kwa ajili ya ukombozi wetu, na kama hafanyi, haitafanyika, unaweza kuwa na uhakika, kwani kuna kiu kubwa kwa ajili ya damu yetu katika jimbo hili; sio kwa sababu tuna hatia ya kitu chochote. … Mpenzi wangu Emma, siku zote ninakufikiria wewe na watoto. … Ninataka kumwona Frederick mdogo, Joseph, Julia, Alexander, Joana, na meja mzee [mbwa wa familia]. … Kwa furaha ningeweza kutembea miguu mitupu kutoka hapa kuja kwako, na kichwa wazi, na nusu uchi, ili kukuona na kufikiri ni furaha kubwa, na kamwe sitoona kuwa ni kazi. … Navumilia kwa ushupavu mateso yangu yote, na ndivyo ilivyo kwa wale ambao wapo nami; bado hakuna hata mmoja wetu aliyeasi. Ninakutaka wewe [kutoruhusu] [watoto wetu] wanisahau mimi. Waambie Baba anawapenda kwa upendo mkamilifu, na anafanya yote awezayo ili kuwatoroka hawa wahuni na kuja kwao. … Waambie Baba anasema hawana budi kuwa watoto wazuri, na kumjali mama yao. …

Wako,

Joseph Smith Mdogo.

Muhtasari

  1. Letter from Emma Smith, 7 March 1839,” Letterbook 2, 37, josephsmithpapers.org; tahajia, alama za uandishi, na sarufi vimeboreshwa.

  2. Letter to Emma Smith, 4 April 1839,” 1–3, josephsmithpapers.org; tahajia, alama za uandishi, na sarufi vimeboreshwa.

  3. Joseph na wenzake walikamatwa Oktoba 31, 1838, na kuwekwa chini ya ulinzi mkali mchana na usiku. Baada ya shtaka la mwanzo huko Richmond, Missouri, walipelekwa kwenye Gereza la Liberty mnamo Desemba 1.