“Novemba 3–9: ‘Sauti ya Furaha kwa Walio Hai na Wafu: Mafundisho na Maagano 125–128,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 125–128,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Novemba 3–9: “Sauti ya Furaha kwa Walio Hai na Wafu”
Mafundisho na Maagano 125–128
Mnamo Agosti 1840, Jane Neyman aliyekuwa anaomboleza alimsikiliza Nabii Joseph Smith akizungumza kwenye mazishi ya rafiki yake Seymour Brunson. Mwana kijana wa Jane aliyeitwa Cyrus pia alikuwa amefariki dunia karibuni. Kuongezea kwenye huzuni yake ulikuwa ni ukweli kwamba Cyrus alikuwa bado hajabatizwa, na Jane alikuwa na wasiwasi hii ingemaanisha nini kwa nafsi yake ya milele. Joseph alikuwa amejiuliza jambo kama hilo kuhusu mpendwa kaka yake Alvin, ambaye pia alikufa kabla ya kubatizwa. Kwa hiyo Nabii aliamua kushiriki na wote mazishini kuhusu kile ambachoBwana alifunua kwake kuhusu wale ambao wanakufa bila kupokea ibada za injili—na kile tunachoweza kufanya ili kuwasaidia.
Mafundisho ya ubatizo kwa ajili ya wafu yaliwasisimua Watakatifu; mawazo yao yaligeuka mara moja kwa wanafamilia wengine waliofariki. Sasa kulikuwa na matumaini kwa ajili yao! Joseph alishiriki furaha yao, na kwenye barua akifundisha mafundisho haya, alitumia lugha ya furaha, na ya shauku kuelezea kile Bwana alichomfundisha kuhusu wokovu wa wafu: “Acheni milima ishangilie kwa shangwe, nanyi mabonde yote lieni kwa sauti; nanyi bahari zote na nchi kavu yatajeni maajabu ya Mfalme wenu wa Milele! (Mafundisho na Maagano 128:23).
Ona Watakatifu,, 1:415–27; “Barua kuhusu Ubatizo kwa ajili ya wafu,” katika Ufunuo katika Muktadha, 272–76.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Bwana ananitaka niitunze familia yangu.
Baada ya kurudi kutoka misheni huko Uingereza—moja ya misheni nyingi alizohudumu—Brigham Young alipokea wito mwingine muhimu kutoka kwa Bwana. Aliamriwa “kuishughulikia vizuri familia [yake]” (mstari wa 3), ambayo iliteseka wakati yeye alipokuwa hayupo. Unaposoma sehemu hii, fikiria kwa nini wakati mwingine Bwana anahitaji dhabihu katika huduma zetu. Unaweza kufanya nini ili kuishughulikia vizuri familia yako?
Ona pia “Fanya Matunzo Mahsusi ya Familia Yako,” katika Ufunuo katika Muktadha, 242–49.
Ninaweza kumtegemea Bwana wakati wa nyakati ngumu.
Mashitaka ya uongo na vitisho vya kukamatwa vilimlazimisha tena Joseph Smith kujificha katika mwezi wa Agosti 1842. Na bado maneno aliyoyaandika kwa Watakatifu muda huu (sasa Mafundisho na Maagano 127) yamejaa matumaini na furaha. Je, mistari 2–4 inakufundisha nini wewe kuhusu Mungu? Kuhusu kukabili upinzani wa kejeli? Ni kifungu gani cha maneno kutoka kwenye mistari hii kingekusaidia wewe unapohisi kuteseka? Fikiria kuandika jinsi gani Bwana anavyokusaidia katika “maji ya kina kirefu” ya maisha yako.
Mafundisho na Maagano 127:5–8; 128:1–8.
“Chochote kile unachokiandika duniani kitaandikwa mbinguni.”
Unaposoma Mafundisho na Maagano 127:5–8; 128:1–8, tafuta sababu za kwa nini Bwana alimpa Joseph Smith maelekezo mahususi kuhusu kuandika ubatizo kwa ajili ya wafu. Hii inakufundisha nini kuhusu Bwana na kazi Yake? Je, ni kwa jinsi gani unahisi maelekezo haya yangeweza kutumika kwa kumbukumbu za familia yako mwenyewe, kama vile kwenye shajara binafsi?
Mafundisho na Maagano 128:5–25
Wokovu wa mababu zangu ni wa muhimu kwa wokovu wangu
Ni wazi kutokana na kile Mungu alichokifunua kupitia Joseph Smith kwa nini mababu zetu ambao hawakubatizwa katika maisha haya wanatuhitaji: tunabatizwa kwa ajili yao ili wao waweze kuchagua kuipokea au kuikataa ibada hii. Lakini nabii pia alifundisha kwamba wokovu wa mababu zetu ni “muhimu na wa lazima kwa wokovu wetu.” Unaposoma Mafundisho na Maagano 128:15–18, fikiria kwa nini iko hivyo.
Mstari wa 5 unafundisha kwamba ibada ya ubatizo kwa ajili ya wafu ilikuwa “imeandaliwa kabla ya kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu.” Ukweli huu unakufundisha nini kuhusu Mungu na mpango Wake? Ujumbe wa Mzee Dale G. Renlund “Historia ya Familia na Kazi ya Hekaluni: Kuunganishwa na Uponyaji” unaongeza nini kwenye uelewa wako? (Liahona, Mei 2018, 46–49).
Joseph Smith alitumia maneno kama “nguvu ya kuunganisha,” “kiungo unganishi,” na “muungano kamili” wakati anafundisha kuhusu ibada za ukuhani na ubatizo kwa ajili ya wafu. Tafuta maneno haya na yale yanayofanana na haya unaposoma Mafundisho na Maagano 128:5–25. Je, unaweza kufikiria vitu unavyoweza kutumia ili kufafanua maelezo haya, kama vile mnyororo au kamba? Kwa nini maneno haya ni mazuri kuelezea mafundisho haya?
Kufikiria maswali yafuatayo kunaweza pia kusaidia katika kujifunza kwako mistari hii:
-
Kwa maoni yako, ni kwa nini ubatizo kwa ajili ya waliokufa ufikiriwe kama “mada tukufu zaidi kuliko mada zote zilizo kwenye injili ya milele”? (mstari wa 17). Je, ni uzoefu upi umekusaidia wewe ujisikie kwa njia hii?
-
Ni katika hali gani ulimwengu unaweza kulaaniwa kama hakuna “muunganiko … kati ya mababu na watoto”? (mstari wa 18).
-
Nini kinakuvutia kuhusu maneno ya Joseph Smith katika mistari 19–25? Je, mistari hii inaathiri vipi jinsi wewe unavyofikiria kuhusu Yesu Kristo?, kuhusu huduma za hekaluni kwa ajili ya mababu zako? (Ona pia “Come, Rejoice,” Nyimbo za Dini, na. 9
Baada ya kujifunza mistari hii, unaweza kuhisi kuvutiwa kufanya kitu kwa ajili ya mababu zako. Mawazo katika FamilySearch.org yangeweza kusaidia.
Mkusanyiko wa “Inspirational Videos” katika “Temple and Family History” katika Maktaba ya Injili unaweza kukupa msaada wa kiutendaji, hadithi zenye mwongozo wa kiungu na jumbe kutoka kwa viongozi kuhusu historia ya familia.
Ona pia Kevin R. Duncan, “Sauti ya Furaha!,” Liahona, Mei 2023, 95–97.
“Utoaji Mtukufu na wa Ajabu.”
Rais Gordon B. Hinckley alisema:
“Upatanisho wa Yesu kwa niaba ya wote unawakilisha dhabihu kuu ya uwakilishi. Yeye aliweka mpangilio ambao chini yake akawa mwakilishi wa watu wote Mpangilio huu ambapo ndani yake mtu mmoja anaweza kutenda kwa niaba ya mwingine unatimizwa katika ibada za nyumba ya Bwana. Hapa tunahudumu kwa niaba ya wale waliokufa bila ya ufahamu wa injili. Wao ni uchaguzi wa kukubali au kukataa ibada iliyofanywa. Wanawekwa katika njia iliyo sawa na wale wanaotembea duniani. Waliokufa wanapewa nafasi sawa kama wale walio hai. Tena, ni utoaji mtukufu na wa ajabu ulioje Mwenyezi Mungu amefanya kupitia Ufunuo Wake kwa Nabii Wake” (“Mambo Makuu Ambayo Mungu Ameyafunua,” Liahona, Mei 2005, 82–83).
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Naweza kusaidia kuitunza familia yangu.
-
Ili kuwasaidia watoto wako wajifunze kuwahudumia washiriki wa familia yao, fikiria kushiriki taarifa kuhusu Brigham Young iliyoko katika “Sehemu ya 50: Watakatifu huko Nauvoo” (katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 184, au video inayohusiana katika Maktaba ya Injili) au fupisha Mafundisho na Maagano 126 katika maneno yako mwenyewe. Unaweza kusisitiza kifungu cha maneno “ishughulikie vizuri familia yako” (mstari wa 3) na zungumza na watoto wako kuhusu kile inachomaanisha kuzishughulikia vizuri familia zetu.
-
Inaweza kuwa burudani kwa wewe na watoto wako kuangalia picha za familia (au kuchora picha) mnapozungumza pamoja kuhusu njia tunazoweza kusaidia “kuwashughulikia” washiriki wa familia. Mngeweza pia kuimba wimbo kama vile “Nyumbani ni Mbinguni” (Nyimbo za Dini, na. 168).
Mafundisho na Maagano 128:5, 12
Watoto wote wa Mungu wanahitaji nafasi ya kubatizwa.
-
Waalike watoto wako watafute kutoka Mafundisho na Maagano 128:1 ni somo gani lilijaa katika mawazo ya Joseph Smith. Wangeweza pia kupekua mstari wa 17 ili kutafuta ni somo lipi alilolifikiria kuwa “tukufu zaidi.” Waache waelezee kile walichopata na kuzungumza kuhusu kwa nini somo hili ni la kusisimua.
-
Katika kuongezea kwenye kuwasaidia watoto kujiandaa kwa ajili ya, (na kuishi) maagano yao ya ubatizo, unaweza kuwasaidia wajue jinsi ya kuwasaidia wale ambao hawakufanya maagano haya wakati wa maisha yao. Fikiria kuwaambia watoto wako kuhusu mtu unayemjua aliyekufa pasipo kubatizwa. Kisha mngeweza kusoma pamoja Mafundisho na Maagano 128:5 na angalieni picha ya kisima cha ubatizo cha hekaluni (kama ile iliyoko mwishoni mwa muhtasari huu). Waambie watoto wako vile unavyojisikia kuhusu kubatizwa hekaluni kwa niaba ya wale waliofariki dunia ili kila mmoja apate nafasi ya kufanya maagano na Baba wa Mbinguni.
Baba wa Mbinguni anataka mimi nijifunze kuhusu historia ya familia yangu.
-
Inaweza kuwa burudani kwako na kwa familia yako kutengeneza mnyororo wa karatasi wenye majina ya wazazi, babu na bibi, babu na bibi wakuu, na kuendelea (ona ukurasa wa shughuli ya wiki hii). Kisha mngeweza kushiriki na kila mmoja kile mnachokifahamu kuhusu mababu. Someni pamoja Mafundisho na Maagano 128:18 ili kujua “muunganiko” ni kitu gani ambacho hufanya historia ya familia yetu iwe “nzima na kamili.” Mngeweza pia kuangalia video ya “Courage: I Think I Get It from Him” (Maktaba ya Injili).
-
Shughuli za ziada ili kuwasaidia watoto wako kushiriki katika historia ya familia zinaweza kupatikana katika “The Temple and the Plan of Happiness” katika kiambatisho B au kwenye FamilySearch.org.