“Novemba 24–30: ‘Yeye “Ametia Muhuri Huduma Yake na Kazi Zake kwa Damu Yake Mwenyewe,”’: Mafundisho na Maagano 135–136,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Mafundisho na Maagano 135–136,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Novemba 24–30: Yeye “Ametia Muhuri Huduma Yake na Kazi Yake kwa Damu Yake Mwenyewe”
Mafundisho na Maagano 135–136
Adhuhuri ya Juni 27, 1844, iliwakuta Joseph na Hyrum Smith katika jela kwa mara nyingine, wakiwa wameandamana na John Taylor na Willard Richards. Waliamini walikuwa hawana hatia ya jinai yoyote, lakini walijisalimisha chini ya ulinzi, wakitumaini kutunza usalama wa Watakatifu waliokuwa Nauvoo. Hii haikuwa mara ya kwanza kwamba maadui wa Kanisa walikuwa wamemuweka Nabii Joseph ndani ya gereza, lakini wakati huu alionekana kujua kwamba asingerudi akiwa hai. Yeye na marafiki zake walijaribu kufarijiana kwa kusoma kutoka katika Kitabu cha Mormoni na kuimba nyimbo za dini. Kisha milio ya risasi za bunduki ilisikika, na ndani ya dakika chache maisha ya duniani ya Joseph Smith na kaka yake Hyrum yalifika mwisho.
Na bado haikuwa mwisho wa sababu tukufu waliyokuwa wameikumbatia. Na ilikuwa siyo mwisho wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo. Kulikuwa na kazi zaidi ya kufanya na ufunuo zaidi ambao ungeliongoza Kanisa kusonga mbele. Mwisho wa uhai wa Nabii haukuwa mwisho wa kazi ya Bwana.
Ona Watakatifu, 1:521–52.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Mafundisho na Maagano 135; 136:37–39
Joseph na Hyrum Smith walitia muhuri ushuhuda wao kwa damu yao.
Fikiria jinsi ambavyo ungeweza kujisikia kama ungekuwa unaishi Nauvoo wakati Joseph na Hyrum Smith walipouawa (ona Watakatifu, 1:554–55). Ni kwa jinsi gani ungeweza kujaribu kuelewa tukio hili la majonzi? Mafundisho na Maagano 135, iliyochapishwa miezi mitatu baadaye pengine ingesaidia. Unapopekua sehemu hii, zingatia kitu ambacho kingekuletea wewe uelewa na hakikisho. Ungesema nini kwa mtu ambaye anakuuliza, “Kwa nini Mungu anaruhusu Nabii Wake auawe?” (ona Mafundisho na Maagano 136:37–39).
Ungeweza pia kupekua sehemu ya 135 kwa ajili ya maneno au vifungu ambavyo vingekuvutia wewe kuwa mwaminifu kwa Kristo hadi mwisho, kama Joseph ana Hyrum walivyokuwa.
Ona pia Mafundisho na Maagano 5:21–22; “Kukumbuka Kifo cha Kishahidi; katika Ufunuo katika Muktadha, 299–306; Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2011), 522–23, 529–40; “Testimony of the Book of Mormon” (video), Maktaba ya Injili.
Joseph Smith alikuwa nabii na shahidi wa Yesu Kristo.
Mafundisho na Maagano 135:3 inataja baadhi ya mambo ambayo Joseph Smith aliyakamilisha “katika kipindi kifupi cha miaka ishirini.” Ni kwa jinsi gani mambo haya yamekuathiri wewe na uhusiano wako na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo? Zingatia jinsi gani wewe ungekamilisha mojawapo ya sentensi kama hii: Kwa sababu ya kile ambacho Bwana amekifanya kupitia Joseph Smith, Mimi … Unaweza pia kuandika na kushiriki ushuhuda wako juu ya Joseph Smith pamoja na wengine.
Njia nyingine ya kujifunza kuhusu misheni ya Joseph Smith ni kujaribu kuandika taarifa ya kifo au maneno ya kumsifu. Ungesema nini ili kujenga imani katika Kristo na injili Yake iliyorejeshwa? Ungeweza kutaka kujumuisha matukio muhimu au mafanikio yanayopatikana katika Mafundisho na Maagano 135 au yale yaliyotajwa katika nyenzo hapo chini.
Yesu Kristo amefunua kweli nyingi kuhusu Yeye Mmwenyewe na Upatanisho Wake kupitia Joseph Smith. Zingatia kutafakari uzoefu ulionao katika kujifunza Mafundisho na Maagano mwaka huu. Je, ni kweli gani zilizokuwa za kipekee kwako? Unaweza kushiriki kweli hizi na familia yako, darasa au washiriki wa akidi au watu wengine unapojifunza wiki hii. Je, kweli hizi zinakusaidiaje wewe uelewe na usogee karibu zaidi na Mwokozi?
Ona pia “Joseph Smith: The Prophet of the Restoration” (video), Maktaba ya Injili; Tad R. Callister, “Joseph Smith—Nabii wa Urejesho,” Liahona, Nov. 2009, 35–37; “Sifa kwa Aliyenena na Bwana,” Nyimbo za Dini, na. 17; Topics and Questions, “Joseph Smith,” Maktaba ya Injili.
Muziki Unaohusiana
Kuimba nyimbo za dini au kutazama video zifuatazo kungeweza kumwalika Roho Mtakatifu au kuvutia majadiliano kuhusu kazi ya Nabii Joseph Smith na dhabihu za Watakatifu walioendelea baada yake.
“Msafiri kwa Miguu” (Nyimbo za Dini, na. 19). Akiwa katika Jela ya Carthage, John Taylor aliimba wimbo huu.
“Sifa kwa Aliyenena na Bwana,” (Nyimbo za Dini, na. 17; ona pia video). Maneno ya wimbo huu wa dini yaliandikwa kama heshima kwa Joseph Smith.
“Njooni Enyi Watakatifu” (Nyimbo za Dini, na. 20; ona pia video).
“Faith in Every Footstep” (ona video).
Ninaweza kukamilisha mapenzi ya Bwana ninapofuata ushauri Wake.
Baada ya Joseph Smith kufa, Watakatifu walifukuzwa kutoka Nauvoo. Sasa walikabiliwa na safari ya maili 1,300 (kilomita 2,100) inayopitia nyika korofi. Brigham Young, Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alikuwa na mashaka kuhusu jinsi ambavyo Watakatifu wangepona kwenye safari hiyo. Katika makazi ya muda yaliyoitwa Winter Quarters, aliomba kwa ajili ya mwongozo. Majibu ya Bwana yameandikwa katika sehemu ya 136. “Kwa kuwasaidia Watakatifu kukumbuka kwamba tabia yao kwenye safari ilikuwa muhimu kama vile mwisho wa safari yao, ufunuo huu ulisaidia kubadilisha uhamiaji huu kutoka ulazima usio wa muhimu mpaka kwenye uzoefu muhimu wa kiroho wa pamoja” (“Hili Litakuwa Agano Letu,” katika Ufunuo katika Muktadha, 308).
Weka hili akilini unapojifunza sehemu ya 136. Ni ushauri gani unaupata ambao ungeweza kusaidia kugeuza jaribu gumu katika maisha yako “kuwa uzoefu muhimu … wa kiroho”? Unaweza pia kutafakari jinsi ushauri huu unavyoweza kukusaidia ukamilishe mapenzi ya Bwana katika maisha yako mwenyewe, kama ulivyowasaidia Watakatifu wa mwanzo katika safari yao.
Ona pia “Hili Litakuwa Agano Letu,” katika Ufunuo katika Muktadha, 307 307–14; “Njooni Enyi Watakatifu,” Nyimbo za Dini, na. 20; Mada za Historia za Kanisa, “Urithi wa Uongozi katika Kanisa,” Maktaba ya Injili.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
(Mafundisho na Maagano 135:1–2, 4-5).
Joseph Smith na Hyrum Smith walitoa maisha yao kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo.
-
Fanya muhtasari wa Mafundisho na Maagano 135:1 kwa ajili ya watoto wako au shiriki “Sehemu ya 57: Nabii Ameuawa” (katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 201–5, au video inayohusiana katika Maktaba ya Injili). Hii ingeweza kuwa fursa nzuri kwa wewe na watoto wako kushiriki hisia zenu kuhusu dhabihu Joseph na Hyrum waliyoifanya kwa ajili ya Mwokozi na injili Yake.
-
Mafundisho na Maagano 135:4–5 inaeleza kwamba Hyrum Smith alisoma kifungu kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni kabla hajaenda katika Jela ya Carthage. Wewe na watoto wako mngeweza kusoma kifungu hiki pamoja (ona Etheri 12:36–38). Je, ni kwa jinsi gani mistari hii ilimfariji Hyrum? Shiriki maandiko ambayo hukupa wewe faraja wakati ukiwa na hofu au huzuni.
-
Wewe na watoto wako mngeweza kutazama picha za manabii (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 7, 14, 67) na kuzungumza kuhusu baadhi ya vitu ambavyo Mungu anawataka manabii kuvifanya. Manabii hawa walitoa dhabihu ya nini kwa ajili ya Mwokozi?
Joseph Smith alikuwa nabii na shahidi wa Yesu Kristo.
-
Ili kuwasaidia watoto wako wakumbuke na washukuru jinsi gani Bwana ametubariki kupitia misheni ya Joseph Smith, mngeweza kuonyesha vitu ambavyo vinawakilisha mambo ambayo Joseph aliyafanya, kama vile Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, au picha ya hekalu (ona pia ukurasa wa shughuli ya wiki hii). Halafu watoto wako wangeweza kutafuta katika Mafundisho na Maagano 135:3 kwa ajili ya baadhi ya vitu ambavyo Joseph Smith alifanya ili kutusaidia sisi tuje karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Waalike watoto wako kushiriki kwa nini wanashukuru kwa ajili ya mambo haya.
Bwana anaweza kunibariki ninapokuwa napambana.
-
Fikiria kuweka picha ya Hekalu la Nauvoo upande mmoja wa chumba na tengeneza kibanda rahisi cha makazi upande mwingine. Waalike watoto wako kukusanyika karibu na picha, na waambie kuhusu Watakatifu ambao walipaswa kuondoka Nauvoo baada ya kufa kwa Joseph Smith (ona sehemu ya 58, 60, na 62 katika Hadithi za Mafundisho na Maagano, 206–8, 211–16, 222–24, au video inayohusiana nayo katika Maktaba ya Injili). Sisitiza imani ambayo Watakatifu hawa walikuwa nayo katika Yesu Kristo, na waalike watoto wako watembee kuelekea kwenye makazi ili kuwakilisha kuelekea Winter Quarters. Wangeweza kuimba wimbo kama “To Be a Pioneer” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 218–19) wanapotembea.
-
Elezea kwamba katika Mafundisho na Maagano 136, Bwana alitoa ushauri ili kuwasaidia Watakatifu katika safari yao kwenda Bonde la Salt Lake. Wasaidie watoto wako watafute kitu katika ufunuo huu ambacho kinaweza kuwapatia ujasiri kwa ajili ya safari hii (ona mistari 4, 10–11, 18–30). Je, Ushauri huu utatusaidiaje sisi kwa majaribu yanayotukabili leo?