“Desemba 22–28: ‘Zawadi Isyo na Mfano ya Mwana Mtakatifu wa Mungu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Krismasi,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2025
Desemba 22–28: Zawadi Isiyo na Mfano ya Mwana Mtakatifu wa Mungu
Krismasi
Nabii Joseph Smith alitamka, “Kanuni za msingi za dini yetu ni ushuhuda wa Mitume na Manabii, kuhusu Yesu Kristo, kwamba Alikufa, Akazikwa, na Akafufuka tena siku ya tatu, na kupaa mbinguni; na mambo yote mengine ambayo yanahusiana na dini yetu ni viambatisho vyake” (Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith [2011], 49). Zaidi ya miaka 160 baadaye, maelezo haya yaliwashawishi Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili kuchapisha “Kristo Aliye Hai: Ushuhuda wa Mitume” katika heshima ya kumbukizi ya miaka 2000 ya kuzaliwa Mwokozi (ona Russell M. Nelson, “Kuchota Nguvu za Yesu Kristo katika Maisha Yetu,” Liahona, Mei 2017, 40).
Kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunashangilia kwa baraka ya ufunuo endelevu kupitia manabii na mitume wa sasa. Tuna shukrani kwa maneno yao ya ushauri yenye mwongozo wa kiungu, maonyo, na yenye kutia moyo. Lakini zaidi ya yote, tunabarikiwa kwa shuhuda zao zenye nguvu juu ya Yesu Kristo–—wakati wa Krismasi na mwaka mzima. Haya ni zaidi ya maneno ya kusisimua tu ya waandishi stadi au wazungumzaji wa umma au umaizi kutoka kwa wataalamu wa maandiko. Haya ni maneno ya wateule wa Mungu, walioitwa, na kupewa mamlaka “mashahidi maalumu wa jina la Kristo ulimwenguni kote” (Mafundisho na Maagano 107:23).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
“Hakuna mwingine aliyekuwa na ushawishi mkubwa.”
Utasema nini kuunga mkono kauli kwamba “hakuna mwingine aliyekuwa na ushawishi mkubwa [kama Yesu Kristo] juu ya wote ambao wameishi na ambao bado wataishi juu ya dunia”? Tafuta vifungu katika “Kristo Aliye Hai” ambavyo vinaelezea ushawishi wa kina wa Mwokozi. Je, Yeye amekushawishije wewe?
Tuseme mtu asiyefahamu Ukristo akikuuliza kwa nini tunasherehekea Krismasi. Je, wewe ungemjibu nini? Rejelea “Kristo Aliye Hai” ukiwa na swali hili akilini, na zingatia kuandika mawazo yoyote au misukumo ambayo inakuja kwako.
Ona pia “Why We Need a Savior” (video), Maktaba ya Injili.
“Alifufuka kutoka kaburini.”
Katika “Kristo Aliye Hai,” Mitume wanashuhudia juu ya Kufufuka kwa Mwokozi, wakitaja kutokea mara tatu kwa Bwana aliyefufuka (ona aya ya 5). Zingatia kusoma kuhusu maelezo ya ziara hizi katika Yohana 20; 3 Nefi 11; na Joseph Smith—Historia ya 1:14–20. Unajifunza nini kuhusu Mwokozi kutokana na maneno Yake na vitendo wakati wa kujitokeza huku?
“Ukuhani Wake na Kanisa Lake vimerejeshwa.”
Wakati wa mafunzo yako ya Mafundisho na Maagano mwaka huu, umekuwa na fursa ya kujifunza zaidi kuhusu jinsi “ukuhani wa Mwokozi na Kanisa Lake vilivyorejeshwa.” Je, kweli au kanuni gani zilizorejeshwa zimekuwa hususani zenye maana kwako? Fikiria kurejea baadhi ya maandiko yafuatayo ambayo yanafundisha kuhusu Urejesho: Mafundisho na Maagano 1:17–23; 13; 20:1–12; 65; 110; 112:30–32; 124:39–42; 128:19–21. Tafakari jinsi kweli za injili iliyorejeshwa zinavyokusaidia wewe kumjua na kumpenda Yesu Kristo.
“Siku moja Atarudi duniani.”
Krismasi ni muda wa kutazama nyuma juu ya siku Yesu Kristo alipozaliwa na kungojea kwa hamu siku atakaporudi tena. Unajifunza nini kuhusu kurudi Kwake kutoka aya ya pili kutoka mwisho ya “Kristo Aliye Hai”? Unaweza pia kufikiria kusoma, kuimba, au kusikiliza nyimbo za dini za Krismasi ambazo zinafundisha kuhusu Ujio wa Pili, kama vile “Shangwe Kote” au “Ukaja Usiku Ule” (Nyimbo za Dini, na. 113, 118).
“Yeye ni nuru, uzima, na tumaini la ulimwengu.”
Katika aya ya mwisho ya “Kristo Aliye Hai,” tambua sifa na majina aliyopewa Mwokozi. Zingatia kutumia muda kujifunza kuhusu baadhi ya majina hayo. Kwa mfano:
Nuru: Ni kwa jinsi gani Yesu Kristo ni kama nuru kwako? Ungeweza kufikiria kuchora picha au kupiga picha ambayo kwako wewe, inawakilisha nuru ambayo Yeye hukupatia wewe. Je, unahisi kuvutiwa kufanya nini ili kuishiriki nuru Yake? (Ona pia Yohana 8:12; 3 Nefi 18:24; Mafundisho na Maagano 50:24.)
Uzima: Kwa nini unafikiri uzima ni neno zuri la kumwelezea Yesu Kristo? Ni kwa jinsi gani Yeye anakupa wewe uzima? Je, ni kwa jinsi gani maisha yako yangekuwa tofauti bila Yeye na injili Yake? (Ona pia Yohana 10:10; 1 Wakorintho15:19–23; Mafundisho na Maagano 66:2.)
Tumaini: Unatumainia nini kwa sababu ya Yesu Kristo na injili Yake? Je, unamjua mtu yeyote ambaye anajisikia kukosa tumaini kuhusu baadae yake? Tafakari jinsi utakavyoshiriki pamoja na mtu huyo tumaini unalojisikia katika Yesu Kristo. (Ona pia Warumi 8:24–25; Etheri 12:4; Moroni 7:41.)
Ona pia Topics and Questions, “Jesus Christ,” Maktaba ya Injili.
“Mungu ashukuriwe kwa zawadi [Yake] isiyo na mfano.”
Katika “Kristo Aliye Hai,” Mitume humtaja Mwokozi kama “zawadi” kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni. Kulingana na kile unachokipata katika “Kristo Aliye Hai,” ni kwa jinsi gani ungeikamilisha sentensi hii: “Kupitia Yesu Kristo, Mungu ananipa mimi zawadi ya …” Tafakari kitu unachoweza kufanya ili kuzikumbuka zawadi hizi kwa ukamilifu zaidi.
Jinsi gani kujifunza “Kristo Aliye Hai” kumegusa imani yako katika Mwokozi na upendo wako kwa Mwokozi?
Ona pia Russell M. Nelson, “Zawadi Nne Ambazo Yesu Kristo Anazitoa Kwako” (First Presidency Christmas devotional, Dec. 2, 2018), Maktaba ya Injili; “Excerpts from ‘The Living Christ: The Testimony of the Apostles’” (video), ChurchofJesusChrist.org.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Ninaweza “kutoa ushuhuda [wangu]” ili kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu.
-
Zingatia jinsi utakavyotambulisha kwa watoto wako “Kristo Aliye Hai.” Labda ungeweza kuwasaidia waoneshe kwa kidole kwenye jina Kristo kwenye kichwa cha habari na saini za Urais wa Kwanza na wale Kumi na Wawili. Unaweza kueleza kwamba huu ni ushuhuda wao juu ya Yesu Kristo ambao walitaka kuushiriki na ulimwengu.
-
Mpe kila mtoto kifungu cha maneno kutoka “Kristo Aliye Hai” na waombe watafute au wachore picha ya kifungu hicho. Halafu ungewasaidia watafute kifungu katika “Kristo Aliye Hai.” Unaweza hata kukusanya picha hizo au vifungu na kutengeneza kitabu.
-
Shirikini na kila mmoja jinsi gani mlivyopata ushuhuda juu ya Yesu Kristo. Labda ungepitisha picha ya Mwokozi kwa mzunguko na kupeana zamu kushiriki kitu mnachokijua kuhusu Yeye (ikijumuisha kweli zilizofundishwa katika “Kristo Aliye Hai”).
“Alizunguka huko na huko, akitenda kazi njema.”
-
Wewe na watoto wako mnaposoma aya ya pili ya “Kristo Aliye Hai,” zungumza nao kuhusu baadhi ya mambo ambayo Yesu aliyafanya. Mnaweza pia kutazama picha kutokana na maisha Yake (ona ukurasa wa shughuli ya wiki hii na Kitabu cha Sanaa za Injili). Waalike watoto wako wazungumze kuhusu kitu ambacho Mwokozi anakifanya katika picha hizo. Tunawezaje kuwahudumia wengine kama Yeye alivyofanya? Video ya “Light the World” katika Maktaba ya Injili inaweza kukupa mawazo.
“Yeye ni nuru, uzima, na tumaini la ulimwengu.”
-
Wasaidie watoto wako watafute nyimbo za dini za Krismasi ambazo hutuambia juu ya nuru, uzima, na tumaini ambavyo kuzaliwa kwa Mwokozi kumevileta ulimwenguni—kama vile, “Mji Mwema Bethlehemu” (Nyimbo za Dini, na. 119). Imbeni nyimbo hizo za dini pamoja, na waruhusu watoto waelezee jinsi gani Yesu ameleta nuru, uzima, na tumaini katika maisha yao.
“Mungu ashukuriwe kwa ajili ya zawadi isiyo na mfano ya Mwana Wake mtakatifu.”
-
Ni zawadi gani tumezipokea kwa sababu ya Yesu Kristo? Labda wewe na watoto wako mngezitafuta zawadi hizi katika “Kristo Aliye Hai” au katika wimbo kama “He Sent His Son” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,, 34–35). Kisha wangeweza kufunga zawadi ya kitu fulani kuwakilisha zawadi hizo. Unaweza kupendekeza kwamba watoto wako wafungue zawadi hizo Siku ya Krismasi ili kuwasaidia wamkumbuke Mwokozi na zawadi Yake kwetu sisi.