“Kiambatisho A: Kwa ajili ya Wazazi—Kuwaandaa Watoto Wako kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Kiambatisho A,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025
Kiambatisho A
Kwa ajili ya Wazazi—Kuwaandaa Watoto Wako kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu
Kwa sababu Yeye anakupenda, anakuamini na anajua uwezekano wako, Baba wa Mbinguni amekupatia wewe fursa ya kuwasaidia watoto wako kuingia na kupiga hatua kwenye njia Yake ya agano, njia ya kuelekea kwenye uzima wa milele (ona Mafundisho na Maagano 68:25–28). Hii inajumuisha kuwasaidia wajiandae kufanya na kuyashika maagano matakatifu, kama vile agano la ubatizo na maagano yanayofanyika hekeluni. Kupitia maagano haya, watoto wako watakuwa kwa shangwe wamejifunga wao wenyewe kwa Mwokozi, Yesu Kristo.
Kuna njia nyingi za kuwaandaa watoto wako kwa ajili ya safari hii kwenye njia ya agano, na Baba wa Mbinguni atakusaidia ugundue njia iliyo bora zaidi ya kuwasaidia. Unapotafuta mwongozo wa kiungu, weka akilini kwamba siyo kujifunza kote kunafanyika wakati wa masomo yaliyopangiliwa. Ukweli ni kwamba, sehemu ya kitu kinachofanya kujifunza nyumbani kuwe na nguvu sana ni fursa ya kujifunza kwa mfano na kupitia nyakati ndogo ndogo na za kawaida kabisa—nyakati ambazo hujitokeza katika njia ya asili katika mtiririko wa maisha ya kila siku. Kama vile kufuata njia ya agano kulivyo mchakato endelevu, wa maisha yote, ndivyo ilivyo kujifunza kuhusu njia ya agano. (Ona “Nyumba na Familia,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi [2022], 30–31.)
Hapa chini kuna baadhi ya mawazo ambayo yanaweza kuongoza kwenye mwongozo zaidi wa kiungu. Unaweza kupata mawazo ya ziada kwa ajili ya kuwafundisha watoto wa umri wa Msingi katika “Kiambatisho B: Kwa Ajili ya Watoto—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu.
Ubatizo na Uthibitisho
Nefi alifundisha kwamba “lango ambalo [sisi] tutaingilia kwenye” njia ya agano “ni toba na ubatizo kwa maji” (2 Nefi 31:17). Jitihada zako za kuwasaidia watoto wako wajiandae kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho zinaweza kuweka miguu yao kuwa thabiti kwenye njia ya agano. Jitihada hizi zinaanza kwa kufundisha kuhusu imani katika Yesu Kristo na toba. Pia zinajumuisha kufundisha jinsi gani tunafanya upya maagano yetu ya ubatizo kwa kula sakramenti kila wiki.
Hapa kuna baadhi ya nyenzo zinazoweza kukusaidia: 2 Nefi 31; toleo maalumu la jarida la Rafiki kuhusu ubatizo; Topics and Questions, “Baptism,” Maktaba ya Injili.
-
Wakati wowote unapokuwa na uzoefu ambao unaimarisha imani yako katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, ushiriki na mtoto wako. Wasaidie waelewe kwamba imani ni kitu ambacho kinaweza kuendelea kukua na kuwa imara zaidi na zaidi katika maisha yote. Ni baadhi ya mambo gani ambayo mtoto wako anaweza kufanya ili kukuza imani imara katika Kristo kabla hawajabatizwa?
-
Mtoto wako anapofanya uchaguzi usio sahihi, zungumza kwa furaha kuhusu zawadi ya toba. Na wakati wewe unapofanya uchaguzi usio sahihi, shiriki furaha ambayo inakuja wakati unapotubu. Shuhudia kwamba kwa sababu Yesu Kristo aliteseka na kufa kwa ajili ya dhambi zetu, tunaweza kutubu kila siku, tukasamehewa, na kupokea nguvu ya kubadilika. Wakati mtoto wako anapoomba msamaha, msamehe bure na kwa shangwe.
-
Mwambie mtoto wako kuhusu ubatizo wako. Onesha picha na shiriki kumbukumbu zako. Zungumza kuhusu jinsi ulivyojisikia, jinsi gani kushika maagano yako ya ubatizo kulivyokusaidia umjue Yesu Kristo vyema zaidi, na jinsi gani maagano yako yanavyoendelea kubariki maisha yako. Mhimize mtoto wako aulize maswali.
-
Panapokuwa na ubatizo katika familia yako au kata yako, nenda na mtoto wako ili aone. Zungumzeni pamoja kuhusu kile ambacho wewe na mtoto wako mlikiona na mlivyojisikia. Kama inawezekana, zungumza na mtu anayebatizwa na muulize maswali kama yafuatayo: “Je, ni kwa jinsi gani ulifanya uamuzi huu? Ulijiandaa vipi?”
-
Wakati wowote unapogundua mtoto wako anafanya kitu alichoahidi kukifanya, mpe pongezi za dhati. Onesha kwamba kutimiza ahadi kunatusaidia tujiandae kushika maagano tunayofanya wakati tunapobatizwa. Ni ahadi gani tunafanya na Mungu wakati tunapobatizwa? Yeye anatuahidi nini sisi? (Ona Mosia 18:8–10, 13.)
-
Zungumza kuhusu jinsi gani kuthibitishwa na kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kulivyokubariki wewe. Kwa mfano, ni kwa jinsi gani umekuwa karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo unapowahudumia wengine na wengine wanapokuhudumia wewe? Msaidie mtoto wako afikirie njia za kuwahudumia na kuwaimarisha wengine akiwa kama muumini wa Kanisa. Pia wasaidie wapate uzoefu na kutambua shangwe inayokuja kutokana na kuhudumu.
-
Wakati wewe na mtoto wako mnapopata tukio takatifu mkiwa pamoja (kama vile kanisani, wakati mkisoma maandiko, au wakati mkimhudumia mtu), waambie kuhusu hisia au mawazo hayo ya kiroho uliyo nayo. Mwalike mtoto wako ashiriki jinsi anavyohisi. Tambua njia tofauti tofauti Roho anavyoweza kuzungumza na watu, ikijumuisha njia ambazo Yeye anazungumza na wewe binafsi. Msaidie mtoto wako atambue na ashiriki nawe nyakati ambapo yaweza kuwa anapata uzoefu wa ushawishi wa Roho Mtakatifu.
-
Angalieni pamoja video kadhaa katika mkusanyiko wa video za Maktaba ya Injili zenye kichwa cha habari “Hear Him!” Zungumzeni pamoja kuhusu njia tofauti ambazo watumishi wa Bwana wanaisikia sauti Yake. Mwalike mtoto wako achore picha au atengeneze video kuhusu jinsi yeye anavyoisikia sauti ya Mwokozi.
-
Fanya sakramenti iwe ni tukio takatifu na la furaha kwa familia yako. Shiriki pamoja na mtoto wako jinsi gani wewe unavyofokasi juu ya Yesu Kristo wakati wa sakramenti. Msaidie mtoto wako atengeneze mpango wa kuonyesha kwamba sakramenti ni takatifu kwao. Kwa mfano, kusikiliza maneno ya sala za sakramenti kunaweza kutukumbusha maagano yetu ya ubatizo.
-
Matoleo mengi ya jarida la Rafiki yanajumuisha makala, hadithi, na shughuli ili kuwasaidia watoto kujiandaa kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho. Mruhusu mtoto wako achague baadhi ili asome na afurahie pamoja nawe. (Ona pia mkusanyiko wa “Preparing for Baptism” katika sehemu ya watoto ya Maktaba ya Injili.)
Nguvu, Mamlaka na Funguo za Ukuhani
Ukuhani ni mamlaka na nguvu za Mungu ambazo kwa hizo Yeye huwabariki watoto Wake. Ukuhani wa Mungu uko duniani leo katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. “Waumini wote wa Kanisa ambao wanashika maagano yao—wanawake, wanaume, na watoto—wanabarikiwa kwa nguvu ya ukuhani wa Mungu katika nyumba zao ili kujiimarisha wao wenyewe na familia zao” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 3.6, Maktaba ya Injili). Nguvu hii itawasaidia waumini katika kuifanya kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa katika maisha yao binafsi na ya familia (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 2.2).
Wakati wanaume na wanawake wanapohudumu katika miito ya Kanisa, wanafanya hivyo kwa mamlaka ya ukuhani, chini ya maelekezo ya wale wanaoshikilia funguo za ukuhani. Watoto wote wa Baba wa Mbinguni—wana na mabinti Zake—watabarikiwa pale wanapokuja kuuelewa vyema ukuhani.
Tunapokea ibada kwa mamlaka ya ukuhani. “Waumini wanaume wa Kanisa wanaostahili wanapokea mamlaka ya ukuhani kupitia utunukiwaji wa ukuhani na kutawazwa kwenye ofisi za ukuhani” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.4). Wale wanaoshikilia ofisi za ukuhani wanaweza kupewa idhini na mtu mwenye kushikilia funguo za ukuhani ili kutekeleza ibada za ukuhani.
Ili kujifunza zaidi kuhusu ukuhani, ona Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 76–79; Russell M. Nelson, “Thamani ya Nguvu ya Ukuhani,” Liahona, Mei 2016, 66–69; “Kanuni za Ukuhani,” mlango wa 3 katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla.
-
Fanya ibada za ukuhani kuwa sehemu thabiti ya maisha ya familia yako. Kwa mfano, msaidie mtoto wako ajiandae kiroho kwa ajili ya sakramenti kila wiki. Mhimize mtoto wako atafute baraka za ukuhani wakati wanapokuwa wagonjwa au wanapohitaji faraja au mwongozo. Ifanye iwe tabia kubainisha njia ambazo Bwana anaibariki familia yako kupitia nguvu za ukuhani.
-
Mnaposoma maandiko pamoja, tafuta fursa za kujadili jinsi Mungu anavyowabariki watu kupitia nguvu Yake. Shiriki uzoefu wako mwenyewe wa wakati ambapo Mungu alikubariki wewe kupitia ukuhani Wake. Kwa mifano ya baraka tunazopokea kutoka kwa Mungu kupitia ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.2, 3.5.
-
Mfundishe mtoto wako kwamba baada ya ubatizo, wanaweza kupokea nguvu za ukuhani kwa kushika agano la ubatizo. Rejeleeni pamoja ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Hazina za Kiroho” (Liahona, Nov. 2019, 76–79). Mwambie mtoto wako jinsi ambavyo ibada za ukuhani zimeleta nguvu ya Mungu katika maisha yako. Kwa ajili ya orodha ya baadhi ya njia ambazo kwazo tunabarikiwa na nguvu za ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.5.
-
Jadilianeni swali hili “Je, Mtumishi wa Bwana yukoje? Someni pamoja Mafundisho na Maagano 121:36–42, na tafuteni majibu. Wakati wowote unapogundua mtoto wako (au mtu mwingine yeyote) akitumia mojawapo ya kanuni au sifa zilizoko katika mistari hii, ibainishe.
-
Wakati wewe au mtoto wako anapotumia funguo kufungua mlango au kuwasha gari, chukua muda huo kulinganisha funguo hizo na funguo zinazoshikiliwa na viongozi wenye ukuhani. (Kwa ajili ya maana ya funguo za ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.4.1). Je, funguo za ukuhani “zinafungua” au “kuwasha” nini kwa ajili yetu sisi? Ona pia Gary E. Stevenson, “Je, Ziko Wapi Funguo na Mamlaka ya Ukuhani?,” Liahona, Mei 2016, 29–32; “Where Are the Keys?” (video) Maktaba ya Injili,
-
Unapokuwa unasimikwa kwa ajili ya wito, mwalike mtoto wako awepo, kama inawezekana. Mruhusu mtoto wako akuone ukitekeleza wito wako. Unaweza hata kutafuta njia sahihi ambazo yeye anaweza kukusaidia. Eleza jinsi unavyoihisi nguvu ya Bwana katika wito wako.
Kubatizwa na Kuthibitishwa kwa ajili ya Mababu
Mahekalu ni sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake. Ndani ya nyumba ya Bwana, tunafanya maagano matakatifu na Baba wa Mbinguni wakati tunaposhiriki katika ibada takatifu, ambazo zote zinatuelekeza kwa Yesu Kristo. Baba wa Mbinguni ametoa njia kwa watoto Wake wote kufanya maagano na kushiriki katika ibada, ikiwajumuisha wale ambao hawakupokea ibada na maagano hayo katika maisha haya. Mwanzoni mwa mwaka mtoto wako atakapokuwa anatimiza miaka 12, mtoto wako atakuwa amefikisha umri wa kutosha kubatizwa na kuthibitishwa hekaluni kwa niaba ya mababu waliofariki dunia (ona pia 1 Wakarintho 15:29).
-
Nenda kwenye nyumba ya Bwana mara nyingi kadiri hali inavyoruhusu. Zungumza na mtoto wako kuhusu kwa nini unakwenda na jinsi gani hekalu linakusaidia wewe uhisi uko karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
-
Pitieni upya na mjadili maswali ya kibali cha hekaluni pamoja. Unaweza kuyapata kwenye kurasa 36–37 za Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi (2022). Zungumza na mtoto wako kuhusu kile kinachotokea katika mahojiano ya kibali cha hekaluni. Shiriki kwa nini kuwa na kibali cha hekaluni ni muhimu kwako.
-
Someni pamoja Malaki 4:6. Zungumza kuhusu jinsi mioyo yenu inavyoweza kuwageukia babu zenu. Jifunzeni zaidi kuhusu mababu zenu kwa kutafiti pamoja historia ya familia kwenye FamilySearch.org. Watafuteni mababu ambao wanahitaji kubatizwa na kuthibitishwa. Mshauri wa kazi ya hekaluni na historia ya familia wa kata yenu anaweza kuwasaidia.
-
Pitieni upya pamoja baadhi ya nyenzo katika mkusanyiko wenye kichwa cha habari “Hekalu” katika kipengele cha watoto cha Maktaba ya Injili. (Ona pia “Preparing Your Child for Temple Baptisms and Confirmations” on ChurchofJesusChrist.org.)
Kupokea Baraka ya Kipatriaki
Baraka ya kipatriaki inaweza kuwa chanzo cha mwongozo, faraja na uvuvio wa kiungu. Baraka hiyo ina ushauri binafsi kutoka kwa Baba wa Mbinguni kuja kwetu sisi na hutusaidia tuelewe utambulisho wetu na lengo letu la milele. Msaidie mtoto wako ajiandae kupokea baraka ya kipatriaki kwa kumfundisha juu ya umuhimu na asili takatifu ya baraka ya kipatriaki.
Ili kujifunza zaidi, ona Topics and Questions, “Patriarchal Blessings,” Maktaba ya Injili; Julie B. Beck, “Unayo Haki ya Mzaliwa wa Kwanza,” Liahona, Mei 2006, 106–8.
-
Shiriki na mtoto wako uzoefu wako wa kupokea baraka ya kipatriaki. Ungeweza kushiriki mambo kama vile jinsi ulivyojiandaa kuipokea, imekusaidiaje kuja karibu zaidi na Mungu na jinsi ambavyo Yeye ameendelea kukuongoza kupitia baraka hii. Pia ungeweza kumwalika mtoto wako azungumze na washiriki wengine wa familia ambao wamekwisha kupokea baraka zao za kipatriaki.
-
Rejeleeni pamoja ujumbe wa Mzee Randall K. Bennett’ “Baraka Yako ya Kipatriaki—Maelekezo yenye Mwongozo wa Kiungu kutoka kwa Baba wa Mbinguni” na ujumbe wa Mzee Kazuhiko Yamashita “Ni Lini Upokee Baraka Yako ya Kipatriaki” (Liahona, Mei 2023, 42–43, 88–90). Shirikishaneni kile mlichojifunza kutokana na jumbe hizi kuhusu kwa nini Baba wa Mbinguni anatutaka tupokee baraka ya kipatriaki. Ili kujifunza kuhusu mchakato wa kupokea baraka ya kipatriaki, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 18.17.
-
Kama unao mababu waliopokea baraka za kipatriaki, ingeweza kuwa ya kuvutia kuzisoma baadhi pamoja na mtoto wako. Ili kuomba baraka za mababu waliofariki dunia, ingia katika ChurchofJesusChrist.org, bofya Zana kwenye kona ya juu kulia ya skirini, na chagua Baraka za Kipatraiki.
-
Baada ya mtoto wako kuwa amepokea baraka ya kipatriaki, waalike wanafamilia waliokuwepo waandike hisia zao na wazishiriki hisia hizo kwa mtoto wako.
Kupokea Endaumenti
Mungu anataka kuwapa, au kuwabariki, watoto Wake wote kwa “uwezo utokao juu” (Mafundisho na Maagano 95:8). Tunaenda hekaluni ili kupokea endaumenti yetu binafsi mara moja tu, lakini maagano tunayofanya na Mungu na nguvu za kiroho anazotupatia kama sehemu ya endaumenti hiyo vinaweza kutubariki kila siku ya maisha yetu.
-
Weka picha ya hekalu katika nyumba yako. Mwambie mtoto wako kuhusu hisia unazopata ndani ya hekalu. Zungumza mara kwa mara kuhusu upendo wako kwa Bwana na nyumba Yake na maagano ambayo umefanya humo. Tafuta fursa za kwenda hekaluni pamoja na mtoto wako ili kufanya ubatizo na uthibitisho kwa ajili ya mababu zao.
-
Fanyeni utafiti pamoja kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org. Someni pamoja makala kama vile “About the Temple Endowment” na “Prepare for the House of the Lord.” Mwombe mtoto wako aulize maswali yoyote aliyonayo kuhusu hekalu. Kwa mwongozo kuhusu kile unachoweza kuzungumza nje ya hekalu, ona ujumbe wa Mzee David A. Bednar “Kujiandaa Kupata Kila Kitu Kinachohitajika” (Liahona, Mei 2019, 101–4; ona hususani kipengele chenye kichwa cha habari “Mafunzo na Maandalizi ya Hekaluni Yanayolenga Nyumbani na Kusaidiwa na Kanisa”).
-
Wewe na mtoto wako mnaposhiriki katika au kuwa mashahidi wa ibada zingine (kama vile sakramenti au baraka ya uponyaji), tengeni muda wa kujadili ishara zilizohusika katika ibada hiyo. Je, ishara hizo zinawakilisha nini? Je, ni kwa jinsi gani zinashuhudia juu ya Yesu Kristo? Hii inaweza kumsaidia mtoto wako ajiandae kutafakari maana ya kiishara ya ibada za hekaluni, ambazo pia zinashuhudia juu ya Yesu Kristo.
-
Msaidie mtoto wako atambue jinsi anavyoshika agano la ubatizo lililoelezwa katika Mosia 18:8–10, 13. Pia msaidie mtoto wako atambue jinsi Bwana anavyombariki. Jenga kujiamini kwa mtoto wako katika uwezo wake wa kushika maagano.
-
Zungumza kwa uwazi na mara kwa mara kuhusu jinsi maagano yako ya hekaluni yanavyoongoza chaguzi zako na kukusaidia uwe karibu zaidi na Yesu Kristo. Ungeweza kutumia Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 27.2, ili kurejelea maagano tunayofanya hekaluni. Kama wewe umepokea endaumenti, mwambie mtoto wako kuhusu jinsi gani gamenti za hekaluni zinavyokusaidia ukumbuke maagano yako na Yesu Kristo (ona “Nguo Takatifu za Hekaluni” [video], Maktaba ya Injili
Kuhudumu Misheni
Mzee David A. Bednar alifundisha: “Kitu kimoja kilicho muhimu sana unachoweza kufanya ili kujiandaa kwa ajili ya wito wa kuhudumu ni kuwa mmisionari mapema kabla hujaenda misheni. … Kitu muhimu hapa sio kwenda misheni; badala yake, cha muhimu hapa ni wewe kuwa mmisionari na kuhudumu katika maisha yetu yote kwa moyo wetu, nguvu, akili, na uwezo wetu wote. … Unajiandaa kwa ajili ya kazi ya umisionari kwa maisha yote” (“Kuwa Mmisionari,” Liahona, Nov. 2005, 45–46). Uzoefu mtoto wako alionao wa kuwa mmisionari utambariki milele, siyo tu kwa kipindi cha muda fulani atakaohudumu kama mmisionari.
Ili kujifunza zaidi, ona Russell M. Nelson, “Kuhubiri Injili ya Amani,” Liahona, Mei 2022, 6–7; M. Russell Ballard, “Huduma ya Umisionari Imebariki Maisha Yangu Milele,” Liahona, Mei 2022, 8–10; “Matayarisho ya Umisionari: Kuzoea Maisha ya Umisionari,” Maktaba ya Injili.
-
Fanyia mazoezi jinsi ya kushiriki injili katika njia za kawaida. Daima kuwa macho kuona fursa za kushiriki na wengine hisia zako kuhusu Baba wa Mbinguni na Mwokozi na baraka unazopokea kutokana na injili ya Mwokozi iliyorejeshwa na kama muumini wa Kanisa Lake. Waalike wengine waungane na familia yako katika shughuli za Kanisa na za kifamilia.
-
Tafuta fursa za familia yako kukutana na wamisionari. Waalike wawafundishe marafiki zako, au wape nafasi ya kuwafundisha watu nyumbani mwako. Waulize wamisionari kuhusu uzoefu wanaoupata na jinsi gani huduma ya umisionari inavyowasaidia wao kujongea karibu zaidi na Yesu Kristo. Pia waulize kile walichofanya (au wanachotamani wangefanya) ili kujiandaa kuwa wamisionari?
-
Ikiwa ulitumikia misheni, zungumza kwa uwazi na mara kwa mara kuhusu uzoefu wako. Au waalike marafiki au wanafamilia ambao walitumikia misheni wazungumzie uzoefu wao. Ungeweza pia kuzungumza kuhusu njia ambazo umeshiriki injili na wengine maisha yako yote. Msaidie mtoto wako afikirie njia anazoweza kushiriki injili.
-
Mpe mtoto wako fursa za kuifundisha familia yako kanuni za injili. Mtoto wako pia anaweza kufanya mazoezi ya kushiriki imani yake kwa wengine. Kwa mfano, mngeweza kujadili maswali kama “Ni kwa jinsi gani tungeweza kutambulisha Kitabu cha Mormoni kwa mtu ambaye hajapata kukisikia?” au “Ni kwa jinsi gani tungeweza kuelezea uhitaji wetu wa Mwokozi kwa mtu ambaye sio Mkristo?”
-
Msaidie mtoto wako ahisi faraja kuzungumza na watu. Je, ni zipi baadhi ya njia nzuri za kuanzisha mazungumzo? Mhimize mtoto wako ajifunze jinsi ya kusikiliza kile wengine wanachosema, kuelewa kile kilicho katika mioyo yao na kushiriki kweli za injili ambazo zingeweza kubariki maisha yao.
-
Tafuta fursa kwa ajili ya mtoto wako kujifunza kuhusu tamaduni na imani zingine. Wasaidie watambue na kuheshimu kanuni nzuri na za kweli katika imani za wengine.
Kupokea Ibada ya Kuunganishwa
Ndani ya hekalu, mume na mke wanaweza kufunga ndoa ya milele. Hili linatokea katika ibada inayoitwa “kuunganishwa.” Hata kama ibada hii inaweza kuwa baada ya miaka mingi ijayo kwa mwanao au binti yako, mambo madogo madogo, rahisi na endelevu mnayofanya pamoja wakati wa miaka hiyo yanaweza kumsaidia ajiandae kwa ajili ya baraka hii ya kupendeza.
-
Someni pamoja “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” katika (Maktaba ya Injili). Tangazo hili linafundisha nini kuhusu furaha katika maisha ya familia na kuhusu ndoa zenye mafanikio? Pamoja na mtoto wako, chagueni moja ya kanuni zilizoorodheshwa katika tangazo ili mjifunze. Mnaweza kutafuta maandiko yanayohusiana na kanuni hiyo kutoka katika Mwongozo wa Maandiko. Mnaweza pia kuweka malengo ya kutumia kanuni hiyo kwa ukamilifu zaidi katika familia yenu. Mnapofanyia kazi malengo yenu, jadilini pamoja matokeo ambayo kanuni hiyo huleta katika maisha ya familia.
-
Pamoja na mtoto wako, someni ujumbe wa Rais Dieter F. Uchtdorf “Katika Kuwasifu Wale Wanaookoa” (Liahona, Mei 2016, 77–80). Mnapofika kwenye sehemu yenye kichwa cha habari “Jumuiya ya Vitu vya Kutumia Mara Moja na Kutupa,” mnaweza kutafuta vitu ndani ya nyumba yenu ambavyo vinatumika mara moja na kutupwa na vitu vingine ambavyo si vya kutupwa. Zungumzeni kuhusu jinsi mnavyotumia vitu kwa njia ya utofauti ikiwa mnataka vidumu kwa muda mrefu. Je, hii inapendekeza nini kuhusu jinsi tunavyopaswa kuchukulia uhusiano wa ndoa na familia? Tunajifunza nini kingine kutoka kwenye ujumbe wa Rais Uchtdorf kuhusu jinsi Mwokozi anavyoweza kutusaidia tujenge ndoa na familia imara?
-
Kuwa muwazi kwa mtoto wako kuhusu mambo ambayo wewe na mwenza wako mnajifunza kuhusu kuwa na ndoa ya milele yenye kiini kwa Kristo na jinsi mnavyojaribu kuwa bora. Kama wewe na mwenza wako mmekwisha kuunganishwa hekaluni, mwoneshe mtoto wako kwa mfano jinsi mnavyojitahidi kushika maagano baina yenu wana ndoa pamoja na Bwana. Mwambie mtoto wako jinsi mnavyojitahidi kumfanya Baba wa Mbinguni na Mwokozi kuwa kiini cha uhusiano wenu na jinsi Wao wanavyokusaidieni ninyi (ona pia Ulisses Soares, “Katika Ubia na Bwana,” Liahona, Nov. 2022, 42–45).
-
Wakati maamuzi ya kifamilia yanapohitajika kufanyika, itisha baraza la familia na majadiliano. Hakikisha kwamba maoni ya washiriki wote wa familia yanasikilizwa na kuthaminiwa. Tumia mijadala hii kama fursa ya kuweka mfano wa mawasiliano yenye afya na ukarimu katika uhusiano wa kifamilia, hata wakati ambapo si kila mmoja anaona mambo kwa njia iliyo sawa sawa. (Ona M. Russell Ballard, “Mabaraza ya Familia,” Liahona,, Mei 2016, 63–65.)
-
Wakati kunapokuwa na kutokukubaliana au mfarakano katika familia, onesha uvumilivu na huruma. Msaidie mtoto wako aone jinsi kutatua mfarakano katika njia kama za Kristo kunavyoweza kuwasaidia wao wajiandae kwa ajili ya familia yenye furaha. Someni pamoja Mafundisho na Maagano 121:41–42, na zungumzeni kuhusu jinsi gani kanuni katika mistari hii zinaweza kutumika katika ndoa.