“Kiambatisho B: Kwa ajili ya Darasa la Watoto—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Mafundisho na Maagano 2025 (2025)
“Kiambatisho B,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani 2025
Kiambatisho B
Kwa Ajili ya Darasa la Watoto—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu
Katika miezi ambayo ina Jumapili tano, walimu wa Darasa la Watoto wanahimizwa kubadili ratiba ya muhtasari wa Njoo, Unifuate wa Jumapili ya tano kwa shughuli moja au zaidi za kujifunza.
Kanuni na Ibada za Injili ya Yesu Kristo
Mafundisho ya Kristo hutufundisha jinsi ya kurudi kwa Mungu.
Wakati Yesu Kristo alipowatokea watu katika Mabara ya Amerika, aliwafundisha mafundisho Yake. Alisema kwamba tunaweza kuingia katika ufalme wa Mungu ikiwa tuna imani, tutatubu, kubatizwa, kupokea Roho Mtakatifu na kuvumilia hadi mwisho (ona 3 Nefi 11:31–40; Mafundisho na Maagano 20:29). Shughuli zilizo hapa chini zinaweza kukusaidia uwafundishe watoto kwamba kanuni na ibada hizi zitatusaidia tumkaribie zaidi Mwokozi katika maisha yetu yote.
Ili kujifunza zaidi kuhusu mafundisho ya Kristo, ona 2 Nefi 31.
Shughuli Yamkini
-
Wape watoto picha ambazo zinawakilisha imani katika Yesu Kristo, toba, ubatizo, na uthibitisho (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 1, 111, 103, na 105). Soma au kariri na watoto makala ya nne ya imani, na waombe kuzishikilia juu picha zao wakati kanuni au ibada hiyo inapotajwa. Wasaidie watoto waelewe jinsi kila kanuni na ibada hizi zinavyotusaidia tuwe zaidi kama Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
-
Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto waelewe kwamba imani, toba, ubatizo na uthibitisho si matukio ya mara moja bali huathiri ukuaji wetu wa kiroho katika maisha yetu yote? Kwa mfano, unaweza kuwaonesha picha ya mbegu na mti mkubwa (au chora vitu hivi ubaoni). Wasaidie wafikirie mambo yanayosaidia mbegu ikue na kuwa mti mkubwa, kama vile maji, udongo na mwanga wa jua. Wasaidie waone kwamba haya ni kama mambo tunayofanya ili kuwa karibu zaidi na Mungu katika maisha yetu yote—kujenga imani yetu katika Yesu Kristo, kutubu kila siku, kuishi maagano yetu ya ubatizo, kula sakramenti, na kumsikiliza Roho Mtakatifu.
-
Shiriki pamoja na watoto hadithi kuhusu fataki kutoka kwenye ujumbe wa Mzee Dale G. Renlund “Je, Kutubu Kunanisaidia Vipi Nihisi Furaha?” Rafiki, Des. 2017, 12–13, au Liahona, Des. 2017, 70–71; ona pia video “Repentance: A Joyful Choice” [Maktaba ya Injili]). Katika sehemu mbalimbali wakati wa hadithi, waalike watoto wafikirie jinsi ambavyo Mzee Renlund yawezekana alihisi. Kwa nini tunahisi furaha tunapotubu? Shiriki pamoja na watoto furaha na upendo ambao umeuhisi wakati ulipomwomba Baba wa Mbinguni akusamehe.
Ubatizo
Yesu Kristo aliweka mfano kwangu wakati alipobatizwa.
Japokuwa Yesu hakuwa na dhambi, alibatizwa ili aweke mfano kamili wa utiifu kwa Baba wa Mbinguni (ona 2Nefi 31:6–10).
Ili kujifunza zaidi kuhusu ubatizo, ona Mafundisho na Maagano 20:37; Topics and Questions, “Baptism,” Maktaba ya Injili.
Shughuli Yamkini
-
Onesha picha ya ubatizo wa Mwokozi au mtu mwingine (au ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 35 na ama na. 103 au na. 104). Waombe watoto washiriki utofauti na mfanano uliopo kati ya picha hizo mbili. Someni pamoja Mathayo 3:13–17 au “Sura ya 10: Yesu Anabatizwa” katika Hadithi za Agano Jipya, 26–29 (au video inayohusiana nayo katika Maktaba ya Injili). Waruhusu watoto waonyeshe kwa kidole mambo yaliyo katika picha ambayo yametajwa katika usomaji au video. Waambie watoto kuhusu upendo wako kwa Mwokozi na nia yako ya kumfuata Yeye.
-
Sikilizeni au imbeni wimbo kuhusu ubatizo, kama vile “When Jesus Christ Was Baptized” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,102). Tunajifunza nini kuhusu ubatizo kutoka kwenye wimbo huu? Soma 2 Nefi 31:9–10, na waalike watoto wasikilize ni kwa nini Yesu Kristo alibatizwa. Waalike wachore picha zao wenyewe wakiwa kwenye siku yao ya ubatizo.
Ninaweza kuchagua kufanya agano na Mungu na kubatizwa.
Kujitayarisha kwa ajili ya ubatizo kunamaanisha mengi zaidi ya kujitayarisha tu kwa ajili ya tukio fulani. Inamaanisha kujitayarisha kufanya agano na kisha kulishika agano hilo kwa maisha yote. Tafakari jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto waelewe agano watakalofanya na Baba wa Mbinguni pale watakapobatizwa, ambalo linajumuisha ahadi Anazotoa kwao na ahadi wanazotoa Kwake.
Shughuli Yamkini
-
Eleza kwamba agano ni ahadi kati ya mtu na Baba wa Mbinguni. Tunapojitahidi kutimiza ahadi zetu kwa Mungu, Mungu anaahidi kutubariki. Andika ubaoni Ahadi Zangu kwa Mungu na Ahadi za Mungu Kwangu. Someni pamoja Mosia 18:10, 13 na Mafundisho na Maagano 20:37, na wasaidie watoto watengeneze orodha ya ahadi wanazoziona chini ya vichwa vya habari sahihi (ona pia Dallin H. Oaks, “Agano Lako la Ubatizo,” Rafiki, Feb. 2021, 2–3). Shiriki jinsi ambavyo Baba wa Mbinguni amekubariki wakati unapojitahidi kushika agano lako la ubatizo.
-
Waoneshe watoto picha za vitu ambavyo Yesu Kristo alivifanya wakati wa huduma Yake (kwa baadhi ya mifano, ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 33–49). Waombe watoto wazungumze kuhusu Yesu anafanya nini katika kila picha. Soma Mosia 18:8–10, 13, na waalike watoto wasikilize mambo ambayo wanaahidi kufanya wakati wanapobatizwa (ona pia “Agano la Ubatizo,” Rafiki, Feb. 2019, 7, au Liahona, Feb. 2019, F3). Ahadi hizi zitashawishi vipi matendo yetu ya kila siku? Waalike watoto wachore picha yao wenyewe wakimsaidia mtu fulani kama vile ambavyo Yesu angefanya.
Uthibitsho
Wakati ninapothibitishwa, ninakuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huleta baraka nyingi, ikiwa ni pamoja na fursa kwa watoto kuwa washiriki hai katika kazi ya Mungu.
Ili kujifunza zaidi kuhusu uthibitisho na kipawa cha Roho Mtakatifu, ona Gary E. Stevenson, “Ni Kwa Jinsi Gani Roho Mtakatifu Anakusaidia?,” Liahona, Mei 2017, 117–20; Topics and Questions, “Holy Ghost,” Maktaba ya Injili.
Shughuli Yamkini
-
Alika mtu ambaye alibatizwa na kuthibitishwa hivi karibuni aje darasani na kushiriki kuthibitishwa kwake kulikuwaje. Muombe mtu huyu azungumze kuhusu ilimaanisha nini kwake kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Wasaidie watoto wafikirie njia wanazoweza kutunza agano lao la ubatizo kama waumini wa Kanisa (kama vile kuwatumikia wengine, kuwaalika wengine wajifunze zaidi kuhusu Yesu, kutoa sala katika mikutano na kadhalika). Shiriki jinsi ambavyo kufanya mambo haya kumekusaidia uhisi furaha ya kuwa muumini wa Kanisa la Kristo.
-
Onesha picha ya watu katika Maji ya Mormoni (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 76), na waombe watoto waeleze kile wanachokiona kwenye picha. Simulia hadithi ya Alma na watu wake wakiwa wanabatizwa huko (ona Mosia 18:1–17; “Mlango wa 15: Alma Anafundisha na Kubatiza,” katika Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 43–44, au video inayohusiana kwenye Maktaba ya Injili). Rejea Mosia 18:8–9 na waalike watoto wafanye vitendo ili kuwasaidia wakumbuke mambo ambayo watu walikuwa radhi kufanya kama waumini wa Kanisa la Kristo. Kwa mfano, tunawezaje kuwasaidia wengine “kuchukua hatua mbele ya kufanya maagano na Mungu? (Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” [mkutano wa ibada ya vijana ulimwenguni kote, Juni 3, 2018], Maktaba ya Injili). Shiriki uzoefu wako wakati uliposhuhudia waumini wa Kanisa wakihudumu kwa njia hizi.
Ninapothibitishwa, ninapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Wakati tunapobatizwa na kuthibitishwa, Baba wa Mbinguni anaahidi kwamba “daima Roho Wake apate kuwa pamoja [nasi[” (Mafundisho na Maagano 20:77). Zawadi hii nzuri kutoka kwa Mungu inaitwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
Shughuli Yamkini
-
Soma Mafundisho na Maagano 33:15, na waombe watoto wasikilize zawadi maalumu ambayo Baba wa Mbinguni anatupatia wakati tunapobatizwa na kuthibitishwa. Ili kuwasaidia wajifunze zaidi kuhusu jinsi kipawa cha Roho Mtakatifu kitakavyowasaidia, rejeleeni pamoja Yohana 14:26; Wagalatia 5:22–23; 2 Nefi 32:5; 3 Nefi 27:20. Unaweza pia kurejelea makala isemayo “Roho Mtakatifu Ni …” (Rafiki, Juni 2019, 24–25, au Liahona, Juni 2019, F12–F13).
-
Kabla ya darasa, waombe wazazi wa mtoto mmoja au zaidi washiriki jinsi walivyobarikiwa kwa sababu wana kipawa cha Roho Mtakatifu. Je, ni kwa jinsi gani Yeye anawasaidia? Je, ni kwa jinsi gani wanaisikia sauti Yake?
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu Roho Mtakatifu, kama vile “The Holy Ghost” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 105). Wasaidie watoto waelewe wimbo huu unatufundisha nini kuhusu jinsi Roho Mtakatifu anavyoweza kutusaidia.
Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza nami kwa njia nyingi.
Watoto ambao wanaweza kutambua sauti ya Roho watakuwa tayari kupokea ufunuo binafsi ili uwaongoze katika maisha yao yote. Wasaidie waelewe kwamba kuna njia nyingi ambazo Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza nasi.
Shughuli Yamkini
-
Wasaidie watoto wafikirie njia tofauti tofauti ambazo tunaweza kuzungumza na rafiki anayeishi mbali, kama vile kuandika barua, kutuma barua pepe, au kuzungumza kwenye simu. Wafundishe kwamba Baba wa Mbinguni anaweza kuzungumza nasi katika njia tofauti kupitia Roho Mtakatifu. Tumia ujumbe wa Rais Dallin H. Oaks “Je, ni kwa Jinsi Gani Baba wa Mbinguni Huzungumza Nasi?” ili kuwasaidia watoto waelewe njia tofauti ambazo kupitia hizo Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza kwenye akili na mioyo yetu (Rafiki, Machi 2020, 2–3, au Liahona, Machi 2020, F2–F3).
-
Shiriki uzoefu wakati ambapo Roho Mtakatifu aliwasiliana nawe, ama kupitia mawazo akilini mwako au kupitia hisia moyoni mwako (ona Mafundisho na Maagano 6:22–23; 8:2–3; ona pia Henry B. Eyring, “Fungua Moyo Wako kwa Roho Mtakatifu,” Rafiki, Agosti 2019, 2–3; au Liahona, Agosti 2019, F2–F3). Shuhudia kwa watoto kwamba Roho Mtakatifu anaweza kuwasaidia kwa njia sawa na hizo.
-
Wasaidie watoto watambue nyakati ambazo wanakuwa wamemhisi Roho—kwa mfano, wakati wakiimba wimbo kuhusu Mwokozi au walipokuwa wakiwatendea wengine kwa ukarimu. Wasaidie watambue hisia za kiroho ambazo Roho anazileta, hususani misukumo Yake ya kutenda jambo. Unadhani kwa nini Roho Mtakatifu hutupatia hisia hizi? Wasaidie watoto wafikirie juu ya mambo ambayo tunahitajika tuyafanye ili tumsikie Roho Mtakatifu akizungumza nasi. Zungumza kuhusu kile unachofanya ili kumsikia Roho vizuri zaidi.
Sakramenti
Ninapopokea sakramenti, ninakumbuka dhabihu ya Mwokozi na kufanya upya maagano yangu.
Mwokozi alitupatia sakramenti ili atusaidie tukumbuke dhabihu Yake kwa ajili yetu na tufanye upya maagano yetu.
Ili kujifunza zaidi, ona Mathayo 26:26–30; 3 Nefi 18:1–12; Mafundisho na Maagano 20:77, 79.
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto wapake rangi “Yesu Alitambulisha Sakramenti kwa Wanefi” katika Kitabu cha Kupaka Rangi cha Hadithi za Maandiko: Kitabu cha Mormoni (2019), 26. Waombe waoneshe kile watu wanachofikiria kwenye picha. Wasomee watoto sehemu za 3 Nefi 18:1–12 au “Mlango wa 45: Yesu Kristo Anafundisha kuhusu Sakramenti na Sala,” katika Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 126–27, au angalieni video inayohusiana kwenye Maktaba ya Injili). Je, tunaweza kufanya nini ili tumkumbuke Yesu Kristo wakati wa sakramenti?
-
Waombe watoto wakuambie baadhi ya mambo ambayo wanapaswa kukumbuka kuyafanya siku zote, kama vile kufunga kamba za viatu vyao au kunawa mikono yao kabla ya kula. Kwa nini ni muhimu kukumbuka mambo haya? Soma Moroni 4:3 kwa watoto, na waalike kusikiliza kile tunachoahidi kukumbuka daima wakati tunapokula sakramenti. Kwa nini ni muhimu kumkumbuka Yesu Kristo? Wasaidie watoto waelewe jinsi gani mkate na maji ya sakramenti hutusaidia tukumbuke kile ambacho Yesu amefanya kwa ajili yetu (ona Moroni 4:3; 5:2).
-
Andika ubaoni “Mimi ninaahidi …” Soma sala ya sakramenti kwa watoto (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79). Wakati wanaposikia ahadi tunayoitoa kwa Mungu, pumzika kidogo na uwasaidie wakamilishe sentensi ubaoni kwa ahadi waliyoisikia. Wasaidie waelewe kwamba tunapokula sakramenti, tunafanya ahadi zile zile tulizozifanya wakati wa ubatizo.
-
Inamaanisha nini kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo? Ili kuwasaidia watoto kujibu swali hili, shiriki mfano wa kitu ambacho juu yake tunaweka majina yetu. Kwa nini tunaweka majina yetu juu ya vitu hivi? Kwa nini Yesu Kristo angetaka tuweke jina lake juu yetu? Fikiria kushiriki maelezo haya kutoka kwa Rais Russell M. Nelson: “Kujichukulia juu yetu jina la Mwokozi kunajumuisha kutangaza na kushuhudia kwa wengine—kupitia matendo na maneno yetu—kwamba Yesu ndiye Kristo” (“Jina Sahihi la Kanisa,” Liahona, Nov. 2018, 88).
Uwezo, Mamlaka na Funguo za Ukuhani
Mungu huwabariki watoto Wake kupitia nguvu za ukuhani.
Watoto wote wa Mungu—wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee—wanapokea nguvu za Mungu pale wanaposhika maagano ambayo wamefanya Naye. Tunafanya maagano haya wakati tunapopokea ibada za ukuhani kama vile ubatizo (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 3.5, 3.6, Maktaba ya Injili). Ili kujifunza zaidi, ona Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 76–79; “Kanuni za Ukuhani,” mlango wa 3 katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla.
Shughuli Yamkini
-
Wasaidie watoto watambue baraka wanazopokea kwa sababu ya ukuhani. Ili kuwapa baadhi ya mawazo, unaweza kuwaonesha video “Baraka za Ukuhani” (Maktaba ya Injili). Fikiria kuorodhesha baraka hizi ubaoni. Kwa nini baraka hizi ni muhimu kwetu? Shuhudia kwamba baraka hizi huja kwetu kwa sababu ya Yesu Kristo na nguvu Yake ya ukuhani.
-
Wasaidie watoto watafute picha ambazo ni kielelezo cha jinsi Mungu anavyotumia nguvu Zake kutubariki sisi. Kwa mfano, wangeweza kutafuta picha ya ulimwengu ambao Yeye aliuumba kwa ajili yetu, mifano ya kuwaponya wagonjwa, na ibada takatifu Yeye alizotoa kwa ajili yetu sisi (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 3, 46, 104, 105, 107, 120). Shiriki kwa nini una shukrani kwa ajili ya ukuhani na baraka ziletwazo na ukuhani. Wasaidie watoto wafikirie juu ya matukio ambapo wao walibarikiwa kwa nguvu za ukuhani wa Mungu.
-
Mojawapo ya njia kuu tunazopokea baraka za nguvu za Mungu katika maisha yetu ni kupitia ibada za ukuhani (ona Mafundisho na Maagano 84:20). Ili kuwasaidia watoto wajifunze ukweli huu, ungeweza kuorodhesha maandiko yafuatayo ubaoni: 3 Nefi 11:21–26, 33 (ubatizo); Moroni 2 (uthibitisho); Moroni 4–5 (sakramenti). Watoto wangeweza kila mmoja kuchagua mojawapo ya vifungu hivi na wabainishe ibada inayoelezwa. Waalike watoto washiriki jinsi ambavyo wao binafsi wamebarikiwa kwa kupokea ibada za ukuhani.
-
Wasaidie watoto waelewe kwamba watapokea nguvu kutoka kwa Mungu pale wanapobatizwa na kushika maagano yao ya ubatizo. Waulize watoto jinsi gani nguvu hii inaweza kuwasaidia.
Kazi ya Mungu inaelekezwa kwa funguo za ukuhani na kutimizwa kwa mamlaka ya ukuhani.
Wakati wowote mtu anaposimikwa kwa ajili ya wito au kupewa kazi ya kusaidia katika kazi ya Mungu, mtu yule anaweza kutumia mamlaka ya Ukuhani aliyokabidhiwa. Kwa nyongeza, wanaume waumini wa Kanisa wenye kustahili wanaweza kutawazwa kwenye ofisi katika ukuhani. Matumizi ya mamlaka yote ya ukuhani ndani ya Kanisa yanaelekezwa na watu wanaoshikilia funguo za ukuhani, kama vile rais wa kigingi, askofu na marais wa akidi. Funguo za ukuhani ni mamlaka ya kuelekeza matumizi ya ukuhani katika kuifanya kazi ya Bwana.
Shughuli Yamkini
-
Soma pamoja na watoto Marko 3:14–15, na waoneshe picha ya tukio lililoelezwa hapo (kama vile Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 38). Waulize watoto kama wamewahi kuona mtu akisimikwa kwa ajili ya wito au kutawazwa kwenye ofisi ya ukuhani (au waambie kuhusu uzoefu ambao umekuwa nao). Je, ni kwa jinsi gani hii inafanana na kile ambacho Mwokozi alikifanya kwa Mitume Wake? Wasaidie watoto waorodheshe ubaoni miito au ofisi za ukuhani ambazo zinaweza kutolewa kwa waumini wa Kanisa, kama vile mwalimu au kiongozi katika kikundi. Pembeni ya kila ofisi au wito, unaweza kuandika kile ambacho mtu aliye na ofisi au wito huo ana mamlaka ya kukifanya. Waambie watoto jinsi gani kusimikwa na mtu chini ya maelekezo ya funguo za ukuhani kumekusaidia katika kuhudumu.
-
Waalike watoto wafikirie juu ya kitu fulani kinachohitaji ufunguo, kama vile gari au mlango. Nini kitatokea ikiwa huna ufunguo? Someni pamoja Mafundisho na Maagano 65:2, na toa ushuhuda wako kuhusu umuhimu wa kuwa na funguo za ukuhani. Mnaweza pia kutazama video “Where Are the Keys?” (Maktaba ya Injili) na mtafute kile Mzee Gary E. Stevenson anachofundisha kuhusu funguo za ukuhani.
Hekalu na Mpango wa Furaha
Hekalu ni nyumba ya Bwana.
Mahekalu ni sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake. Katika mahekalu, tunafanya Naye maagano matakatifu, tunapokea baraka ya nguvu ya ukuhani, tunapokea ufunuo, tunafanya ibada kwa niaba ya mababu zetu waliofariki na kuunganishwa na familia zetu kwa milele yote. Haya yote yanawezekana kwa sababu ya Yesu Kristo na dhabihu Yake ya kulipia dhambi.
Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto unaowafundisha watambue utakatifu wa nyumba ya Bwana na wajitayarishe kustahili kushiriki katika ibada za hekaluni? Zingatia kurejelea nyenzo hizi: Mafundisho na Maagano 97:15–17; Russell M. Nelson, “Maneno ya Kuhitimisha,” Liahona, Nov. 2019, 120–22; “Kwa Nini Watakatifu wa Siku za Mwisho Wanajenga Mahekalu,” temples.ChurchofJesusChrist.org.
Shughuli Yamkini
-
Onesha picha ya hekalu moja au zaidi. Waulize watoto ni kitu gani kinafanya hekalu kuwa sehemu maalumu. Onesha kwamba kwenye kila hekalu kuna maandishi haya: “Utakatifu kwa Bwana—Nyumba ya Bwana.” Waulize watoto kile wanachodhani “Utakatifu kwa Bwana” inaweza kumaanisha. Kwa nini hekalu linaitwa nyumba ya Bwana? Je, hii inatufundisha nini kuhusu hekalu? Ikiwa yeyote kati ya watoto hao amewahi kwenda hekaluni, wanaweza pia kushiriki jinsi walivyohisi walipokuwa huko. Ikiwa umewahi kwenda hekaluni, elezea jinsi ambavyo ulihisi uwepo wa Bwana ukiwa huko na zungumza kuhusu kwa nini hekalu ni mahali patakatifu kwako.
-
Someni pamoja Mafundisho na Maagano 97:15–17. Waombe watoto watafute kile ambacho Bwana anatarajia kutoka kwa wale wanaoingia katika nyumba Yake takatifu. Kwa nini tunahitaji kuwa wenye kustahili ili kuingia kwenye nyumba Yake? Kama sehemu ya mazungumzo haya, zungumza na watoto kuhusu kibali cha hekaluni, ikijumuisha jinsi ya kukipata. Unaweza kumwalika mshiriki wa uaskofu ashiriki nao jinsi mahojiano ya kibali cha hekaluni yalivyo na maswali ambayo yanaulizwa.
Ndani ya Hekalu tunafanya maagano na Mungu.
Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Yesu Kristo anatualika tufuate njia ya agano ili turejee nyumbani kwa Wazazi wetu wa Mbinguni ili tuwe na wale tunaowapenda” (“Njoo Unifuate,” Liahona, Mei 2019, 91). Wasaidie watoto waelewe kwamba njia ya agano inajumuisha ubatizo, uthibitisho na endaumenti ya hekaluni na kuunganishwa.
Shughuli Yamkini
-
Waombe watoto wakusaidie kurejelea agano lile tunalofanya na Mungu wakati tunapobatizwa na ambalo tunalifanya upya wakati tunapokula sakramenti (ona Mosia 18:10; Mafundisho na Maagano 20:77, 79). Onesha picha ya hekalu na ueleze kwamba Baba wa Mbinguni ana baraka zaidi ambazo Yeye anataka kutupatia ndani ya hekalu.
-
Chora lango linaloongoza kwenye njia. Waulize watoto kwa nini wanadhani inasaidia kuwa na njia ya kutembea. Someni pamoja 2 Nefi 31:17–20, ambapo Nefi analinganisha agano la ubatizo na lango na anatualika tuendelee kwenye njia baada ya ubatizo. Kuna maagano mengi zaidi ya kufanya baada ya ubatizo, ikijumuisha maagano yanayofanywa hekaluni. Eleza kwamba Rais Nelson ameiita njia hii “njia ya agano.”
Hekaluni, tunaweza kubatizwa na kuthibitishwa kwa niaba ya mababu waliofariki.
Injili ya Yesu Kristo hufanya iwezekane kwa watoto wote wa Mungu kurudi kuishi Naye, hata kama watakufa bila kuijua injili. Ndani ya hekalu, tunaweza kubatizwa na kuthibitishwa kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo kwa niaba yao.
Shughuli Yamkini
-
Zungumza kuhusu wakati ambapo mtu alikufanyia jambo ambalo hukuweza kujifanyia mwenyewe. Waalike watoto washiriki uzoefu kama huo. Eleza kwamba tunapoenda hekaluni, tunaweza kupokea ibada takatifu kama vile ubatizo kwa niaba ya wengine ambao wamefariki. Je, ni kwa jinsi gani tunakuwa kama Yesu pale tunapofanya kazi kwa niaba ya wafu? Yeye amefanya nini kwa ajili yetu ambacho hatungeweza kujifanyia wenyewe?
-
Mwalike kijana mmoja au zaidi ambao wamebatizwa kwa niaba ya mababu zao ili waelezee uzoefu wao. Waulize ilikuwaje walipokuwa hekaluni. Wahimize washiriki jinsi walivyojisikia kufanya kazi hii kwa niaba ya mababu zao.
-
Chora mti kwenye ubao, ikijumuisha mizizi na matawi. Waombe watoto wafikirie jinsi gani familia ni kama mti. Andika kwenye mizizi Mababu, andika kwenye matawi wazao, na andika kwenye shina la mti Wewe. Someni pamoja sentensi hii kutoka Mafundisho na Maagano 128:18: “Kwani sisi pasipo wao [mababu zetu] hatuwezi kukamilika; wala wao pasipo sisi hawawezi kukamilika.” Uliza maswali kama yafuatayo: “Kwa nini sisi tunawahitaji mababu zetu? Kwa nini mababu zetu wanatuhitaji sisi? Wazazi wetu, bibi na babu na mababu wengine wametusaidiaje sisi?” Waalike watoto wapekue sehemu iliyosalia ya Mafundisho na Maagano 128:18 kwa ajili ya kifungu cha maneno kinachoeleza jinsi tunavyoweza kuwasaidia mababu zetu.
-
Zingatia kufanya kazi na mzazi wa kila mtoto ili kutafuta jina la babu anayehitaji ibada ndani ya hekalu (ona FamilySearch.org).