“Ono la Kwanza la Joseph Smith,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)
“Ono la Kwanza la Joseph Smith,” Hadithi za Mafundisho na Maagano
1817–1820
Ono la Kwanza la Joseph Smith
Jibu la sala ya unyenyekevu
Mahali ambapo familia ya Joseph Smith waliishi, kulikuwa na makanisa mengi ambayo yalifundisha kuhusu Yesu Kristo. Wote walifundisha mambo tofauti kumhusu Yeye. Joseph hakuwa na uhakika nani alikuwa sahihi. Alijua kwamba alimhitaji Mwokozi, lakini hakujua ni kanisa lipi ajiunge nalo.
Joseph Smith—Historia ya 1:5–6; Saints, 1:9
Joseph aliwaza kuhusu hili kwa muda mrefu. Alitaka kusamehewa dhambi zake. Alitembelea makanisa mengi, lakini bado alihisi kukanganyikiwa.
Joseph Smith—Historia ya 1:8–10; Saints, 1:9–12
Siku moja, Joseph alisoma Yakobo 1:5 katika Biblia. Ilisema kama tunahitaji hekima, tunaweza kumwomba Mungu. Joseph alijua moyoni mwake kwamba hiki ndicho alichohitaji kufanya.
Joseph Smith—Historia ya 1:11–13
Asubuhi ya siku nzuri ya majira ya kuchipua mnamo 1820, Joseph alikwenda msituni karibu na nyumbani kwake. Alitaka kuwa mahali ambapo angeweza kuwa peke yake ili kuomba kwa Baba wa Mbinguni.
Joseph Smith—Historia ya 1:14–15
Joseph alipiga magoti na kuanza kusali. Alipokuwa akifanya hivyo, alihisi nguvu za uovu zikimshika. Alihisi giza likimzunguka. Ilionekana kama mtu alikuwa akijaribu kumzuia asizungumze na Mungu. Joseph alitumia nguvu zake zote kumwomba Mungu amwokoe.
Joseph Smith — Historia ya 1:15–16
Ghafla, Joseph aliona mwanga mkali wa kupendeza ukishuka kutoka mbinguni. Giza liliondoka, na akahisi amani. Katika mwanga Joseph aliwaona Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wakiwa wamesimama juu angani. Baba wa Mbinguni aliliita jina la Joseph. Kisha alimwonyesha Yesu na kusema, “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”
Joseph Smith—Historia ya 1:16–17.
Yesu alimwambia Joseph kwamba dhambi zake zilikuwa zimesamehewa. Joseph alimwuliza Yesu ni kanisa gani ajiunge nalo. Yesu alisema kwamba asijiunge na lolote kati yao.
Joseph Smith—Historia ya 1:18–19; Saints, 1:16
Yesu alisema kwamba kweli muhimu kuhusu injili Yake zilikuwa zimepotea. Alisema angewatuma malaika kufundisha kweli hizi kwa Joseph, ili azishiriki kwa ulimwengu.
Saints, 1:16–17.
Baada ya ono kumalizika, Joseph alijawa na upendo na shangwe. Hakuwa amekanganyikiwa tena. Alijua kwamba Mungu alimpenda. Japokuwa baadhi ya watu walimchukia kwa kusema kwamba alikuwa amewaona Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, Joseph alijua ilikuwa ni kweli.
Joseph Smith—Historia ya 1:20–26; Saints, 1:16