Hadithi za Maandiko
Joseph na Emma


“Joseph na Emma,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)

“Joseph na Emma,” Hadithi za Mafundisho na Maagano

1825–1828

Joseph na Emma

Wakifanya kazi pamoja ili kuleta Kitabu cha Mormoni kwa ulimwengu

Emma Hale akiwa amekaa kando ya mto karibu na nyumba yake.

Emma Hale alikulia katika familia kubwa huko Pennsylvania, si mbali na New York, ambapo Joseph Smith aliishi. Emma na familia yake walimwamini Mungu. Emma alipenda kusoma, kuimba, kuendesha farasi na kupiga kasia kwenye mto kando ya nyumba yake.

Saints, 1:31–32.

Joseph Smith na baba yake wakitembea kando ya nyumba ya Emma Hale. Emma akitazama nje ya dirisha na kumwona Joseph.

Emma alipokuwa na umri wa miaka 21, Joseph Smith na baba yake walikuja kufanya kazi kwa mmoja wa jirani zake Emma. Baba yake Emma aliwaalika waishi nyumbani kwake.

Joseph Smith—Historia ya 1:56–57; Saints, 1:31–32

Joseph na Emma wakizungumza pamoja nje ya nyumba yao Emma. Wazazi wa Emma wako mlangoni.

Joseph na Emma walipata kujuana. Walipenda kuwa pamoja. Lakini wazazi wa Emma hawakumpenda Joseph. Hawakuamini kwamba alikuwa amemwona malaika.

Saints, 1:32–33.

Emma na Joseph Smith wakiendesha pamoja sleigh iliyokokotwa na farasi.

Takribani mwaka mmoja baadaye, Joseph alimuomba Emma waoane. Emma na Joseph walipendana. Walioana na kwenda kuishi na wazazi wa Joseph huko New York.

Joseph Smith—Historia ya 1:57–58; Saints, 1:34–35

Emma na Joseph Smith wakiendesha gari la farasi ndani ya msitu.

Miaka minne ilikuwa imepita tangu Moroni alipomwambia Joseph kuhusu mabamba ya dhahabu. Ilipofika muda, Emma na Joseph walikwenda kwenye kilima ambapo mabamba yalikuwa yamefichwa.

Joseph Smith—Historia ya 1:59; Saints, 1:36–37

Moroni anamkabidhi mabamba ya dhahabu kwa Joseph Smith

Malaika Moroni alikutana na Joseph juu ya kilima na kumpa mabamba. Alimwambia Joseph kwamba kama angefanya awezavyo kuyatunza mabamba, yangekuwa salama.

Joseph Smith—Historia ya 1:59; Saints, 1:37–38

Joseph Smith akiwa amebeba mabamba ya dhahabu Mwanaume anamkimbiza na kujaribu kuyachukua mabamba.

Watu walikuwa wamesikia kwamba Joseph alikuwa na mabamba ya dhahabu, na baadhi yao walijaribu kuiba mabamba kutoka kwake. Joseph ilibidi atafute mahali pa kuyaficha. Wakati Joseph alipokuwa amebeba mabamba kutoka mahali pa kujificha msituni, baadhi ya wanaume walimshambulia. Aliwaangusha chini na kukimbilia nyumbani kwa wazazi wake.

Joseph Smith—Historia ya 1:60; Saints, 1:38, 40–41

Joseph Smith analeta mabamba ya dhahabu nyumbani na kuwaruhusu familia yake kugusa mabamba.

Wakati Joseph alipoleta mabamba nyumbani, dada yake alimsaidia kuyaweka mezani. Moroni alikuwa amemwambia Joseph asimruhusu yeyote ayaone mabamba, lakini familia yake waliweza kuyagusa mabamba hayo wakati yalipokuwa yamefunikwa na kitambaa.

Saints, 1:41

Emma na Joseph wanahamia katika nyumba mpya.

Mungu alitaka Joseph atafsiri mabamba ya dhahabu ili watu waweze kuyasoma. Lakini watu huko New York waliendelea kujaribu kuiba mabamba. Ilimbidi Joseph aendelee kuyaficha mabamba ili yawe salama. Hivyo Joseph na Emma walihamia nyumba iliyo karibu na ya wazazi wa Emma. Walitumaini wangeweza kutafsiri mabamba hayo kwa amani.

Joseph Smith—Historia ya 1:61–62; Saints, 1:43, 45–46

Joseph Smith akimbusu Emma kwenye paji la uso. Anamsaidia kutafsiri kutoka kwenye mabamba ya dhahabu.

Joseph alianza kutafsiri mabamba. Alitumia vifaa maalumu ambavyo Mungu aliviandaa vimsaidie. Wakati Joseph akitafsiri, Emma aliandika kile alichokisema. Saa baada ya saa walifanya kazi pamoja. Emma alistaajabu. Alijua mume wake alikuwa akitafsiri kwa uwezo wa Mungu.

Joseph Smith—Historia ya 1:35; Saints, 1:49