Vitabu vya Maelekezo na Miito
4.Uongozi na Mabaraza katika Kanisa la Yesu Kristo


“4. Uongozi na Mabaraza katika Kanisa la Yesu Kristo,” Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho (2021)

“4. Uongozi na Mabaraza katika Kanisa la Yesu Kristo,” Kitabu cha Maelezo ya Jumla.

mkutano wa baraza la kata

4.

Uongozi na Mabaraza katika Kanisa la Yesu Kristo

4.0

Utangulizi

Kama kiongozi katika Kanisa, umeitwa kwa msukumo kupitia watumishi wa Bwana waliopewa mamlaka. Unayo haki ya kusaidia katika kazi ya Baba wa Mbinguni ya “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Unafanya hili kwa kuwahimiza waumini kushiriki katika kazi ya wokovu na kuinuliwa kwa ajili yao wenyewe, familia zao, na wengine (ona sura ya 1). Utapata shangwe unapowatumikia watoto wa Mungu.

Kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo, utawahudumia wengine mara kwa mara mmoja mmoja. Pia utakuwa na fursa ya kushika uongozi katika mikutano na shughuli zote za Kanisa. Kwa nyongeza, unaweza kutoa huduma muhimu kupitia mabaraza. Hizi zinaweza kujumuisha mikutano ya urais, mikutano ya baraza la kata, na mingine. Sehemu ya 4.3 na 4.4 inatoa miongozo kwa ajili ya mabaraza yenye tija. Mambo yote mahususi kuhusu mikutano ya baraza yamebainishwa katika sura ya 29.

Huduma yako iliyowekwa wakfu inahitaji dhabihu ya muda, lakini usitelekeze mahitaji yako mwenyewe na mahitaji ya familia yako. Omba mwongozo wa Roho Mtakatifu kukusaidia kuweka usawa na kutimiza wajibu wako (ona Mosia 4:27).

4.1

Lengo la Uongozi katika Kanisa

Viongozi wanawahimiza waumini kushiriki katika kazi ya Mungu kwa kuwa “wafuasi wa kweli wa … Yesu Kristo” (Moroni 7:48). Ili kufanya hili, viongozi kwanza wanajitahidi kuwa wafuasi waaminifu wa Mwokozi kwa kufuata mafundisho Yake na mfano Wake (ona Luka 18:22). Kisha wanaweza kuwasaidia wengine kukaribia zaidi kwa Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu. Katika mchakato wa kuwasaidia wengine, wanakuwa wafuasi wazuri zaidi wao wenyewe (ona Mosia 18:26; Mafundisho na Maagano 31:5).

Kuwa mfuasi mwaminifu ili kuwasaidia wengine kuwa wafuasi waaminifu ndilo lengo nyuma ya kila wito katika Kanisa. Kila wito unajumuisha fursa za kutumikia, kuongoza, na kuwaimarisha wengine.

4.2

Kanuni za Uongozi katika Kanisa

Wakati wa huduma Yake duniani, Mwokozi aliweka mfano wa uongozi kwa ajili ya Kanisa Lake. Kiini cha lengo Lake, kilikuwa kufanya mapenzi ya Baba Yake wa Mbinguni na kuwasaidia wengine kuelewa na kuishi injili Yake (ona Yohana 5:30; Mosia 15:7). Aliwapenda wale Aliowaongoza na alionesha upendo huo kwa kuwahudumia (ona Yohana 13:3–5).

Mwokozi aliongeza uwezo wa wengine kwa kuwapa majukumu na fursa za kukua (ona Mathayo 10:5–8; Yohana 14:12). Aliwatia moyo na kuwasahihisha kwa uwazi na upendo (ona Yohana 21:15–17).

Bwana alisema, “Acha kila mtu na ajifunze wajibu wake, na kutenda kazi katika ofisi ambayo ameteuliwa, kwa bidii yote” (Mafundisho na Maagano 107:99). Maneno haya yanatumika kwa wote ambao wanapokea jukumu la kutumikia na kuongoza katika Kanisa la Mwokozi.

Tafuta mwongozo wa Bwana ili kukusaidia kujifunza na kutimiza majukumu ya wito wako. Unapojifunza maandiko, tafuta kanuni za uongozi ambazo Mwokozi alionyesha na kufundisha. Kutumia kanuni katika sura hii pia kutakusaidia kuongoza katika njia inayofaa zaidi katika Kanisa la Mwokozi.

4.2.1

Jiandae Kiroho

Yesu alijiandaa Mwenyewe kiroho kwa ajili ya misheni Yake ya duniani (ona Luka 4:1–2). Vivyo hivyo wewe pia unajiandaa kiroho kwa kusogea karibu na Baba wa Mbinguni kupitia sala, kusoma maandiko, na utiifu kwa amri Zake. Kuwafuata manabii Wake pia kunakusaidia kujiandaa kiroho (ona Mafundisho na Maagano 21:4–6).

Tafuta ufunuo ili kuelewa mahitaji ya wale unaowaongoza na jinsi ya kutimiza kazi ambayo Mungu amekuita kufanya. Kupitia juhudi zako za kukaribia karibu na Bwana, unaweza kupokea mwongozo katika maisha yako binafsi, kwenye majukumu ya familia, na kwenye wito wa Kanisa.

Bwana pia ameahidi kutunuku karama za kiroho kwa wale wanaozitafuta (ona Mafundisho na Maagano 46:8). Kwa unyenyekevu unapomwomba Baba wa Mbinguni ili kupokea karama hizi, Yeye ataongeza uwezo wako wa kuongoza na kuwainua wale unaowatumikia.

4.2.2

Wahudumie Watoto Wote wa Mungu

Yesu aliwahudumia watu yeye binafsi, akijitoa kuwainua na kuwafundisha wale waliojiona wapweke, wasio na matumaini, au wamepotea. Kwa maneno na matendo Yake, aliwaonyesha watu kwamba Yeye aliwapenda. Yeye alitambua asili takatifu na ustahili wa milele wa kila mtu.

Wapende watu unaowatumikia kama Yesu alivyofanya. Omba “kwa nguvu zote za moyo” ili ujazwe upendo Wake (Moroni 7:48). Jenga urafiki wa dhati. Wafikie wale ambao wanaweza kuwa wapweke, wanahitaji faraja, au wana mahitaji mengine. Upendo wako utayabariki maisha yao na kuwasaidia watu watamani kuja kwa Kristo.

Wasaidie watu binafsi wazidishe uongofu wao na kuimarisha imani yao katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Wasaidie wajiandae kufanya maagano wakati wanapopokea ibada yao inayofuata. Wahimize watunze maangano waliyoyafanya na washiriki baraka za toba. Wasaidie wajue kwamba wanaweza kuendelea kuelekea kutimiza uwezekano wao wa kiungu bila kujali changamoto zinazowakabili.

4.2.3

Fundisha Injili ya Yesu Kristo

Viongozi wote ni walimu. Jitahidi kufuata mfano wa Mwokozi kama mwalimu (ona sura ya 17; Kufundisha katika Njia ya Mwokozi). Kupitia maneno na vitendo vyako, fundisha mafundisho ya Yesu Kristo na kanuni za injili Yake (ona 3 Nefi 11:32–33; Mafundisho na Maagano 42:12–14). Mafundisho ya kufaa yanahamasisha watu kuimarisha uhusiano wao na Mungu na kuishi injili, wakipiga hatua kuelekea uzima wa milele.

Kufundisha katika njia ya Mwokozi ni zaidi ya kuzungumza; kunajumuisha kusikiliza na kuuliza maswali kama Yeye alivyofanya (ona Mathayo 16:13–17).

Walimu wenye weledi pia ni wanafunzi wenye bidii. Fanya mafunzo ya neno la Mungu kuwa kipaumbele kikubwa katika maisha yako. Elewa kwamba kujifunza ni mchakato wa maisha yote. Tafuta kujifunza kutoka kwa wengine, ikiwa ni pamoja na wale unaowafundisha. (Ona Mafundisho na Maagano 88:122.)

Fundisha kutoka kwenye maandiko na maneno ya manabii wa siku za mwisho (ona Mafundisho na Maagano 52:9). Kumbuka kwamba “kuhubiri neno [kuna] matokeo yenye nguvu zaidi kwa akili za watu kuliko … kitu kingine chochote” (Alma 31:5).

Tafuta ushawishi wa Roho wakati unapojiandaa na unapofundisha. Roho Mtakatifu anapeleka ukweli katika mioyo na akili za wale unaowafundisha (ona 2 Nefi 33:1).

Wafundishe waumini waweke msimamo wa kujifunza injili kwa sala wao binafsi na familia zao.

Kama umeitwa au umepangiwa kuongoza katika mkutano wa Kanisa au shughuli, hakikisha kwamba mafundisho yanaadilisha na ni sahihi (ona Mafundisho na Maagano 50:21–23).

4.2.4

Ongoza katika Haki

Bwana alifunua kwamba “kuna umuhimu wa kuwepo kwa marais, au maafisa viongozi” katika Kanisa Lake (Mafundisho na Maagano 107:21). Wale ambao wanashikilia funguo za ukuhani wanaongoza katika maeneo yao ya uwajibikaji, kama vile akidi, au kata.

Vikundi vingine katika Kanisa, vikijumuisha Muungano wa Usaidizi, Wasichana, Watoto, na Shule ya Jumapili pia vinaongozwa na afisa kiongozi. Viongozi hawa wanaitwa na kutawazwa na kupewa mamlaka yaliyonaibishwa na yule anayeshikilia funguo za ukuhani au mtu yeyote aliyemruhusu kufanya hivyo (ona 3.4.3).

Kila afisa kiongozi anatumikia chini ya maelekezo ya mtu anayeshikilia funguo za ukuhani (ona 3.4.1). Muundo huu unatoa utaratibu na mipaka dhahiri ya majukumu na uwajibikaji katika kufanya kazi ya Bwana.

Afisa kiongozi anaweza kunaibisha kwa mtu mwingine uteuzi wa kuongoza kwa muda. Kwa mfano, kama rais wa Muungano wa Usaidizi atakuwa hayupo kwenye mkutano wa Muugano wa Usaidizi wa jumapili, atamteua mshauri wake wa kwanza kuongoza mkutano. Kama mshauri wa kwanza atakuwa pia hayupo, rais atamteua mshauri wake wa pili kuongoza.

Kiongozi anayeongoza katika vikundi vya Kanisa, mkutano, au shughuli anahakikisha kwamba malengo ya Bwana yamefanikishwa. Katika kufanya hivi, kiongozi anafuata kanuni za injili, sera za Kanisa, na maelekezo ya Roho Mtakatifu.

Wale wanaoongoza wanafuata mfano wa Yesu Kristo katika kutumikia kwa upole, unyenyekevu, na upendo msafi (ona Yohana 13:13–15). Wito au jukumu la kuongoza halimfanyi mtu anayelipokea kuwa wa muhimu zaidi au mwenye thamani zaidi kuliko wengine (ona Mafundisho na Maagano 84:109–10).

Kama umeitwa au umepangiwa kuongoza, fuata mafundisho ya Mwokozi kwamba “na mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu” (Mathayo 20:27; ona mstari wa 26–28). Shauriana na wengine na tafuta umoja katika kuelewa mapenzi ya Bwana na kufanya kazi Yake (ona Mafundisho na Maagano 41:2; ona pia 4.4 katika kitabu hiki cha maelezo jumla).

Sio busara kutamani kuongoza katika kikundi chochote katika Kanisa la Bwana (ona Mafundisho na Maagano 121:37). Bali, kwa unyenyekevu na kwa uaminifu tumikia katika nafasi ambayo umeitwa. Jitahidi kutimiza kazi ya Bwana na jicho lako likiwa kwenye utukufu Wake (ona Mafundisho na Maagano 4:5). Amini kwamba Bwana atakupa wewe fursa za kukua na kuwabariki watoto wa Baba wa Mbinguni.

mkutano wa kata

4.2.5

Naibisha Majukumu na Hakikisha Uwajibikaji

Mwokozi aliwapa wafuasi Wake majukumu na wajibu wenye maana (ona Luka 10:1). Pia aliwapa fursa ya kuwajibika kwa kazi waliyopewa kufanya (Ona Luka 9:10.)

Kama kiongozi, unaweza kuwasaidia wengine kukua kwa kunaibisha majukumu kwao. Kwa njia hii utawasaidia pia kupokea baraka ambazo zinakuja kutokana na kutumikia. Jitahidi kushirikisha waumini wote katika kufanya kazi ya Mungu.

Kunaibisha pia kunaweza kufanya huduma yako iwe ya kufaa zaidi. Kama utajaribu kufanya kazi nyingi, “kwa hakika utadhoofika” (Kutoka 18:18). Tafuta mwongozo wa Roho kuhusu jukumu gani la kunaibisha ili uweze kufokasi kwenye vipaumbele vyako vya juu.

Kunaibisha ni zaidi ya kuwapangia wengine jukumu. Pia kunajumuisha kumfundisha na kumwamini mtu mwingine kutimiza kazi. Kwa kawaida kunajumuisha mambo yafuatayo:

  • Kutana na mtu umwalike kumtumikia Bwana katika jukumu. Msaidie mtu aelewe jukumu na lengo la jukumu hilo, ikiwa ni pamoja na jinsi huduma yake itakavyowabariki wengine.

  • Shaurianeni pamoja kuhusu jukumu, nani mwingine angeweza kuhusika, na lini lingepaswa kukamilika. Hakikisha kwamba mtu huyo anaelewa na yuko radhi kulikubali jukumu. Onyesha ujasiri katika uwezo wake.

  • Mtie moyo mtu huyo kuomba msukumo kuhusu jinsi ya kutimiza jukumu. Onesha imani yako na msaidie mtu huyo kufanikiwa. Toa mwelekeo na usaidizi kama inavyotakiwa.

  • Baada ya kila kipindi fulani mwombe mtu atoe taarifa juu ya jukumu. Kubali juhudi kubwa za mtu yule, na onyesha shukrani kwa kile alichokifanya.

4.2.6

Watayarishe Wengine kuwa Viongozi na Walimu

Mwokozi aliwatayarisha Mitume Wake kuwa viongozi katika Kanisa Lake. Vivyo hivyo nawe pia wasaidie wengine wajitayarishe kuwa viongozi na walimu. Kazi ya Bwana inalenga juu ya kuwasaidia watu, sio tu kusimamia programu za Kanisa. Programu hizi sio mwisho wa kila kitu. Zipo ili kuwasaidia watu wakue.

Wakati wa kufikiria nani anaweza kutumikia katika miito au majukumu ya Kanisa, kuwa mwenye kusali sana. Kumbuka kwamba Bwana atawastahilisha wale anaowaita. Kile ambacho ni muhimu sana ni kwamba wapo tayari kutumikia, watatafuta kwa unyenyekevu msaada wa Mungu, na wanajitahidi kuwa wenye kustahili. Miito na majukumu vinaweza kuwasaidia wakue kwa kutoa fursa za kutumia imani yao, kufanya kazi kwa bidii, na kuona Mungu akikuza juhudi zao. Toa mwongozo na msaada kwa vijana, waumini wapya, na wengine ambao watahitaji msaada wa ziada katika kutekeleza miito yao.

Wakati mwingine watu wale wale wanaitwa mara kwa mara kwenye nafasi za uongozi. Hii inaweza kuwaelemea wao na familia zao na kuwanyima wengine fursa. Tafuta kuwapa waumini wote fursa za kutumikia na kukua.

Kwa maelezo zaidi kuhusu miito ya Kanisa, ona sura ya 30.

4.2.7

Panga Mikutano, Masomo, na Shughuli zenye Malengo Dhahiri

Tafuta mwongozo wa Roho katika kupanga mikutano, masomo, na shughuli zenye malengo dhahiri. Malengo haya yanapaswa kuwaimarisha watu binafsi na familia, kuwaleta karibu na Kristo, na kusaidia kukamilisha kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa (ona sura ya 1 na 2). Wakati unapanga, fuata kanuni zilizo katika sura ya 20 na 29.

Tengeneza mipango ya muda mrefu kwa ajili ya kikundi chako. Weka kalenda ya mwaka. Fokasi katika kuhimiza ukuaji wa kiroho wa waumini.

4.2.8

Kutathmini juhudi Zako

Mara kwa mara rejelea majukumu yako na ukuaji wako wa kiroho kama kiongozi. Fikiria pia ukuaji wa wale unaowaongoza. Kitengo, akidi ya ukuhani, na viongozi wengine wa vikundi wanaweza kurejea upya viashirio muhimu, ripoti ya robo mwaka , na ripoti zingine katika Leader and Clerk Resources kuona wapi kuna maendeleo na wapi kuna uwezekano wa ukuaji.

Mafanikio yako kama kiongozi yanapimwa kimsingi na dhamira yako ya kuwasaidia watoto wa Mungu kuwa wafuasi waaminifu wa Yesu Kristo. Kwa sababu watu wote wana haki ya kujiamulia, baadhi wanaweza kuchagua kuondoka kwenye njia ya agano. Wakati mwingine hii inaweza kukukatisha tamaa, lakini unapomgeukia Bwana, Yeye atakuinua na kukufariji (ona Alma 26:27). Unaweza kujua kwamba Bwana anapendezwa na juhudi zako wakati unapohisi Roho akifanya kazi kupitia wewe.

4.3

Mabaraza katika Kanisa

Baba wa Mbinguni ameanzisha mabaraza kama sehemu muhimu ya kupokea msukumo, kufanya maamuzi, na kutimiza kazi Yake. Mabaraza yalikuwepo kabla ulimwengu haujaumbwa. Kila mmoja wetu alishiriki katika mabaraza haya kabla ya kuja duniani. (Ona Mafundisho na Maagano 121:32; Ibrahimu 3:22–28.)

Kufuata mpangilo huu, Kanisa la Yesu Kristo linaongozwa na mabaraza kwenye kila daraja. Kwa mfano, Baraza la Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili (ona 5.1.1.1), Urais wa Maeneo (ona 5.2.1), Urais wa vigingi, na uaskofu vyote ni mabaraza. Kwa nyongeza kwenye mabaraza ya kigingi na kata, kila urais wa kikundi cha Kanisa, akidi, au darasa pia ni baraza.

Bwana amewaelekeza viongozi wa Kanisa Lake kushauriana pamoja katika kufanya kazi Yake (ona Mafundisho na Maagano 41:2–3). Mabaraza yanatoa fursa kwa ajili ya washiriki wa baraza kupokea maono wakati wanapotafuta ufunuo kuelewa mahitaji ya watoto wa Mungu na kupanga jinsi ya kusaidia kuyakamilisha.

wanaume wawili wakizungumza

4.4

Kanuni za Mabaraza yenye Tija

Baadhi ya kanuni za mabaraza yenye tija zimefupishwa katika sehemu hii. Kanuni hizi zinaweza kuwasaidia viongozi katika mabaraza ya Kanisa na vilevile wazazi katika mabaraza ya familia zao.

4.4.1

Makusudi ya Mabaraza

Makusudi ya msingi ya mabaraza ni kuwasaidia waumini kufanya kazi pamoja katika kutafuta mwongozo wa kiungu kuhusu maswala ambayo yatawabariki watu binafsi na familia (ona Mafundisho na Maagano 43:8–9). Mabaraza yanatoa mkazo wa kipekee kwenye kuwasaidia waumini kupokea ibada na kuweka maagano yanayohusika. Washiriki wa baraza pia wanatafuta msukumo kuhusu kupanga na kuratibu kazi ya Bwana katika maeneo yao ya uwajibikaji.

Baadhi ya shughuli za kiutawala, kama vile kupanga kalenda, zinaweza zisihitaji majadiliano katika mpangilio wa baraza. Mengi ya haya yanaweza kushughulikiwa kupitia mawasiliano kabla na baada ya mikutano.

Washiriki wa baraza wanatoa uangalizi mahususi kwa watu binafsi na familia zenye mahitaji muhimu. Mabaraza yanasaidia kuratibu msaada. Kwa taarifa kuhusu baadhi ya mahitaji haya, sambamba na nyenzo kwa ajili ya kuelewa na kusaidia, ona Life Help katika Maktaba ya Injili.

4.4.2

Matayarisho kwa ajili ya Mikutano ya Baraza

Urais na Mabaraza wanatarajiwa kukutana mara kwa mara. Kila urais na baraza lina kiongozi ambaye ameitwa na kusimikwa. Viongozi hawa wanatafuta mwongozo wa Bwana katika kupanga mikutano ya baraza. Pia wanatafuta mawazo kutoka kwa washiriki wa baraza katika kuamua nini cha kujadili.

Viongozi wanaruhusu washiriki wa baraza wajue juu ya mada za kujadili mapema. Washiriki wa baraza wanajiandaa kushiriki umaizi kuhusu mada hizi. Kwa ajili ya mabaraza ya kata na ya kigingi, mengi ya maandalizi haya yanatokea katika mikutano ya urais.

Washiriki wa baraza wanajiandaa wenyewe kiroho kushiriki katika mikutano ya baraza. Wanatafuta kuwa wasikivu kwa misukumo ya Roho.

4.4.3

Majadiliano na Maamuzi

Bwana alisema,“Bali azunguze mmoja na wengine wote wasikilize maneno yake, ili wote watakapokuwa wamezungumza wote wapate kujengana, na kwamba kila mmoja apate kuwa na nafasi sawa” (Mafundisho na Maagano 88:122). Kanuni hii inatumika katika mabaraza ya Kanisa.

Wakati wa mkutano wa baraza, kiongozi (au mtu yeyote anayechaguliwa na kiongozi) anaelezea mada inayofikiriwa. Kiongozi kisha anahimiza majadiliano miongoni mwa washiriki wote wa baraza, akiuliza maswali na kuomba mawazo.

Kiongozi anawahimiza washiriki kuzugumza kwa uwazi na uaminifu. Hali tofauti za tamaduni, umri, uzoefu, na maoni ya washiriki wa baraza hustawisha baraza. Washiriki wanatoa mapendekezo na kusikilizana kwa heshima. Wanapotafuta kujua mapenzi ya Mungu, roho wa mwongozo na umoja anaweza kuwepo.

Katika baraza ambalo linajumuisha wanawake na wanaume, kiongozi anatafuta umaizi na mawazo kutoka kwa wote. Wanawake na wanaume mara nyingi wana mitazamo tofauti ambayo inatoa usawa unaohitajika. Wanaume na wanawake wanafikia maamuzi mazuri zaidi na kuwa na mafanikio makubwa mno katika huduma ya Bwana wakati wanapothamini michango ya kila mtu na kufanya kazi pamoja.

Kiongozi anaongoza majadiliano ya baraza. Hata hivyo, yeye anapaswa kusikiliza zaidi kuliko kuzungumza. Wakati kiongozi wa baraza anaposhiriki mtazamo wake mapema sana, inaweza kuzuia michango ya wengine. Inapokuwa lazima, kiongozi wa baraza kwa upole anabadili uelekeo au anatoa fokasi mpya kwenye majadiliano.

Baada ya majadiliano, kiongozi anaweza kuamua nini cha kufanya au kuahirisha maamuzi wakati akitafuta taarifa na mwongozo wa ziada. Maamuzi yanapaswa kujulishwa kwa majadiliano na kuthibitishwa na Roho. Mchakato wa baraza unasaidia kuleta maamuzi yenye mwongozo ambayo ni mazuri zaidi ya maamuzi bora ya kiongozi. Kiongozi anaweza pia kupeleka mada kwenye baraza tofauti.

Wakati mwingine washiriki wa baraza wanaweza kuwa na hisia za kutia wasiwasi kuhusu maamuzi muhimu. Hii inapotokea, kiongozi anaweza kungojea mkutano mwingine kwa ajili ya kufikiria mada zaidi na kutafuta uthibitisho na umoja wa roho. Katika baadhi ya hali, mshiriki wa baraza anaweza kutaka kukutana na kiongozi yeye binafsi ili kujadili dukuduku lake.

4.4.4

Umoja

Bwana aliwaelekeza wafuasi Wake kuwa na “umoja” (Mafundisho na Maagano 38:27). Washiriki wa baraza wanatafuta kuwa na umoja katika matamanio na lengo kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Wanajitahidi kwa ajili ya umoja katika majadiliano na maamuzi. Wanajitahidi pia kuwa “wa moyo mmoja na nia moja” pale wanapofanya kazi pamoja (Musa 7:18).

Washiriki wa baraza wanapaswa kuepuka mabishano, hukumu zisizo za haki, na masengenyo (ona 3 Nefi 11:28–30). Wanapotenda katika umoja, Baba wa Mbinguni atabariki juhudi zao.

4.4.5

Hatua na Uwajibikaji

Washiriki wa baraza wanafanya karibu kazi zao zote kabla na baada ya mikutano ya baraza. Wakati wa mikutano, wanatafuta mwongozo katika kukuza mipango na kutekeleza maamuzi. Kiongozi wa baraza anawaalika washiriki kutimiza kazi inayohusiana na mipango hii. Washiriki wa baraza kwa kawaida wanawaalika wengine kwenye vikundi vyao ili kusaidia. Watu binafsi hawapaswi kulemewa na majukumu.

Washiriki wa baraza wanaripoti juu ya majukumu yao. Maendeleo kwa kawaida yanahitaji uangalifu endelevu na kufuatilia majukumu.

4.4.6

Usiri

Taarifa zote binafsi lazima zishughulikiwe kwa heshima. Viongozi wanatumia busara pale wanaposhiriki taarifa binafsi na baraza. Kwa kawaida wanaomba ruhusa ya muumini ili kushiriki taarifa hii.

Baraza linaheshimu matamanio ya yoyote anayeomba usiri. Washiriki wa baraza hawapaswi kushiriki taarifa binafsi nje ya baraza isipokuwa iwe inatakiwa kutimiza jukumu kutoka kwa kiongozi wa baraza.

Baadhi ya mada ni nyeti mno kuzileta mbele ya baraza zima. Kama inafaa, viongozi wanarejea upya mada hizi na washiriki binafsi wa baraza. Au wanaweza kupeleka baadhi ya mada kwenye baraza tofauti.