Muungano wa Usaidizi na Akidi ya Wazee
Kufundisha, Kujifunza, na kutumia jumbe kutoka kwenye Mkutano Mkuu


Njoo, Unifuate

Kufundisha, Kujifunza, na kutumia jumbe kutoka kwenye Mkutano Mkuu

Akidi ya Wazee na Muungano wa Usaidizi hutoa mchango mkubwa katika kazi ya wokovu na kuinuliwa. Wakati wa mikutano yao ya Jumapili, wanajadili namna ya kutumia mafundisho kutoka katika jumbe za mkutano mkuu wa karibuni kwenye jitihada zao katika kazi hii. Urais wa Akidi ya Wazee na Muungano wa Usadizi huchagua ujumbe kutoka mkutano mkuu ili kujifunza kwenye kila mkutano wa Jumapili, kulingana na mahitaji ya waumini na msukumo kutoka kwa Roho. Mara moja moja, askofu au rais wa kigingi anaweza pia kupendekeza ujumbe. Kwa ujumla, viongozi wanapaswa kuchagua jumbe kutoka kwa washiriki wa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Hata hivyo, ujumbe wowote kutoka kwenye mkutano mkuu wa hivi karibuni unaweza kujadiliwa.

Walimu hufokasi kwenye namna ya kuwasaidia waumini kutumia mafundisho kwenye jumbe za mkutano mkuu katika maisha yao. Viongozi na walimu hutafuta njia za kuwahimiza washiriki kusoma jumbe zilizoteuliwa kabla ya mkutano.

Kwa taarifa zaidi kuhusu mikutano ya akidi za wazee na Muungano wa Usaidizi ona General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, 8.2.1.2, 9.2.1.2, ChurchofJesusChrist.org.

Kupanga Kufundisha

Maswali yafuatayo yanaweza kuwasaidia walimu wanapopanga kutumia ujumbe wa mkutano mkuu ili kufundisha. Kulingana na mahitaji, walimu hushauriana na akidi ya wazee au urais wa Muungano wa Usadizi wakati wanapotafakari maswali haya.

  • Kwa nini urais wa akidi ya wazee au uraisi wa Muungano wa Usaidizi walichagua kujadili ujumbe huu? Je, wanatumaini waumini watafahamu nini na kufanya nini baada ya kujadili ujumbe huu?

  • Je, mzungumzaji anataka waumini waelewe nini? Ni kanuni zipi za injili anazozifundisha? Ni kwa jinsi gani kanuni hizi zinatumika kwenye akidi yetu au Muungano wa Usaidizi?

  • Ni maandiko yapi mzungumzaji aliyatumia kutegemeza ujumbe wake? Je, kuna maandiko mengine ambayo waumini wanaweza kusoma ambayo yatafanya uelewa wao kuwa wa kina? (Unaweza kupata baadhi katika maelezo ya mwisho ya ujumbe au kwenye Mwongozo wa Maandiko [scriptures.ChurchofJesusChrist.org].)

  • Je, ni maswali gani naweza kuuliza ambayo yatawasaidia waumini kutafakari na kutumia mafundisho yaliyo katika ujumbe? Ni maswali yapi yatawasaidia kuona umuhimu wa mafundisho haya katika maisha yao, familia zao, na katika kazi ya Bwana?

  • Nini naweza kufanya ili kumwalika Roho katika mkutano wetu? Ninaweza kutumia nini ili kuchochea mjadala, ikiwa ni pamoja na hadithi, analojia, muziki, au kazi ya sanaa? Mzungumzaji alifanya nini kuwasaidia washiriki kuelewa ujumbe wake?

  • Je, mzungumzaji alitoa mialiko yoyote? Ni jinsi gani naweza kuwasaidia waumini wahisi hamu ya kufanyia kazi mialiko hiyo?

Mawazo ya Shughuli

Kuna njia nyingi za walimu kuwasaidia waumini wajifunze kutoka kwenye jumbe za mkutano mkuu na jinsi ya kutumia jumbe hizo. Hii hapa ni mifano michache; walimu wanaweza kuwa na mawazo mengine ambayo yatafanya kazi vizuri zaidi katika akidi zao za wazee au Muungano wa Usaidizi.

  • Tumia kweli katika maisha yetu. Waalike waumini kupitia ujumbe wa mkutano mkuu wakitafuta kweli zitakazowasaidia kukamilisha kazi ambayo Mungu amewapa wao kama watu binafsi au kama akidi ya wazee au Muungano wa Usaidizi. Kwa mfano, ni kitu gani tunajifunza kinachoweza kutusaidia sisi kama wahudumu? Kama wazazi? Kama waumini wamisionari? Ni kwa jinsi gani ujumbe huu hushawishi mawazo yetu, hisia, na matendo yetu?

  • Jadilianeni katika makundi. Wagawe waumini katika makundi madogo madogo, na lipangie kila kundi kipengele tofauti cha ujumbe wa mkutano mkuu ili wasome na wajadiliane. Kisha liombe kila kundi lishiriki ukweli walioupata na jinsi gani unatumika kwao. Au unaweza kutengeneza makundi ya watu waliojifunza vipengele tofauti vya ujumbe na uwape nafasi ya kushiriki wao kwa wao kile walichogundua.

  • Tafuta majibu ya maswali. Waalike waumini wajibu maswali kama yafuatayo kuhusu ujumbe wa mkutano: Ni kweli zipi za injili tunazipata katika ujumbe huu? Ni kwa jinsi gani tunaweza kutumia kweli hizi? Ni mialiko ipi na baraka zipi zilizoahidiwa zilitolewa? Ni nini ujumbe huu unatufundisha sisi kuhusu kazi ambayo Mungu anataka tuifanye? Au tengeneza maswali machache ya kwako mwenyewe yanayowahamasisha waumini kufikiri kwa kina kuhusu ujumbe au jinsi ya kutumia kweli zake. Kisha waruhusu waumini wachague moja kati ya maswali haya na watafute majibu katika ujumbe.

  • Shiriki dondoo kutoka katika ujumbe. Waalike waumini washiriki dondoo kutoka kwenye ujumbe wa mkutano mkuu ambazo zimewapa msukumo wa kutimiza wajibu wao katika kazi ya wokovu na kuinuliwa. Wahimize wafikirie jinsi ambavyo wanaweza kushiriki dondoo hizi ili wambariki mtu fulani, ikiwa ni pamoja na wapendwa wao na watu wanaowahudumia.

  • Shiriki somo la vitendo. Kabla ya muda, waalike waumini wachache walete vitu kutoka nyumbani ambavyo wanaweza kutumia kufundishia kuhusu ujumbe wa mkutano mkuu. Wakati wa mkutano, waombe washiriki waeleze jinsi vitu hivyo vinavyohusiana na ujumbe na jinsi gani ujumbe unatumika kwenye maisha yao.

  • Tayarisha somo la kufundisha nyumbani. Waombe washiriki wafanye kazi katika jozi ili kupanga somo la jioni ya nyumbani kutokana na ujumbe wa mkutano mkuu. Wangeweza kujibu maswali kama haya: Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kuufanya ujumbe uwe wa kufaa kwa familia zetu? Je, ni kwa jinsi gani tunaweza kushiriki ujumbe huu na watu tunaowahudumia?

  • Shiriki uzoefu. Someni kwa pamoja kauli kadhaa kutoka katika ujumbe wa mkutano mkuu. Waombe waumini washiriki mifano kutoka katika maandiko na kutoka katika maisha yao ambayo inaonyesha au inaimarisha mafundisho yaliyofundishwa katika kauli hizi.

  • Tafuta kirai. Waalike waumini wachunguze ujumbe wa mkutano wakitafuta virai ambavyo vina maana kwao. Waombe washiriki virai hivyo na kile wanachojifunza kutokana navyo. Waombe washiriki ni kwa jinsi gani mafundisho haya huwasaidia kukamilisha kazi ya Bwana.

Kwa mawazo zaidi kuhusu jinsi gani ya kujifunza na kufundisha kutoka kwenye jumbe za mkutano mkuu, ona “Mawazo kwa ajili ya Kujifunza na Kufundisha kutoka kwenye Mkutano Mkuu.” (Bonyeza “Mawazo ya kujifunza” chini ya “Mkutano Mkuu” katika Maktaba ya Injili.)