“Daudi na Goliathi,” Hadithi za Agano la Kale (2022)
“Daudi na Goliathi,” Hadithi za Agano la Kale
1 Samweli 17
Daudi na Goliathi
Kukabiliana na changamoto ya shujaa
Wafilisti walikuwa wakiwashambulia Waisraeli. Kila asubuhi shujaa Mfilisti aliyeitwa Goliathi alimpa changamoto Muisraeli yeyote kupigana naye. Goliathi alikuwa mkubwa na mrefu kuliko mtu mwingine yeyote, na alikuwa katili. Alivaa vazi zito la vita na alibeba upanga, mkuki na ngao kubwa. Hakuna aliyethubutu kupigana naye.
Daudi alikuwa mchunga kondoo kijana aliyekuwa na imani katika Bwana. Kaka zake wakubwa walikuwa askari katika jeshi la Israeli. Siku moja, Daudi aliwapelekea kaka zake chakula. Wakati alipofika kwenye kambi ya jeshi, alisikia changamoto ya Goliathi.
Daudi aliwauliza askari kwa nini hakukuwa na mtu aliyeitetea Israeli. Kaka zake walikasirika na kumwambia aende kuchunga kondoo. Lakini Daudi alijua Bwana angeitetea Israeli.
Mfalme Sauli alifahamu juu ya imani ya Daudi, hivyo aliomba kuonana na Daudi. Daudi alimwambia Sauli kwamba yeye hakuogopa kupigana na Goliathi. Daudi alifafanua kwamba siku moja wakati akichunga kondoo wake, aliua simba na dubu. Bwana alimlinda kipindi hicho, na Daudi alijua Bwana angemlinda sasa.
Sauli alimpa Daudi vazi lake la vita. Lakini halikumtosha, kwa hivyo Daudi alilivua. Aliamua kupigana bila vazi la vita.
Daudi alikusanya mawe laini matano na kuyaweka ndani ya mkoba. Alichukua kombeo lake na fimbo ya kuchungia na kutoka kumkabili Goliathi.
Wakati Goliathi alipomuona Daudi, alipiga kelele na kumdharau. Alisema kijana mchunga kondoo asingeweza kumpiga. Daudi alijibu kwamba alimwamini Bwana kwa ajili ya kumlinda! Daudi alisema angempiga Goliathi ili kuonyesha ukuu wa Bwana.
Daudi alikimbia kumwelekea Goliathi. Kwa haraka alirusha jiwe kwa kombeo lake. Jiwe lilimpiga Goliathi kwenye paji la uso, na mwanamume shujaa akaanguka chini. Bwana alimsaidia Daudi kumshinda Goliathi bila upanga wala vazi la vita.
Wakati Wafilisti walipoona kwamba Goliathi alikuwa amekufa, walikimbia kwa hofu. Waisraeli walishinda vita. Daudi alimwamini Bwana, na Bwana aliilinda Israeli.