Seminari na Vyuo
Fundisha kupitia Roho


“Fundisha kupitia Roho,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi: Kwa Ajili ya Wote Wanaofundisha Nyumbani na Kanisani (2022)

“Fundisha kupitia Roho,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi

4:17

Fundisha kupitia Roho

Mwokozi alipowaamuru Joseph Smith na Sidney Rigdon kuhubiri injili Yake, Yeye aliwaahidi, “Roho Mtakatifu atamwagwa katika kutoa ushuhuda kwa vitu vyote mtakavyosema” (Mafundisho na Maagano 100:8; ona pia Mafundisho na Maagano 42:15–17; 50:17–22). Ahadi hiyo hiyo inatumika kwa wote wanaofundisha injili, ikijumuisha wewe. Unapofundisha injili ya Yesu Kristo, unaweza kuwa na Roho Mtakatifu ili kukuongoza na kukushuhudia juu ya ukweli kwenye akili na mioyo ya wale unaowafundisha (ona Mafundisho na Maagano 8:2). Hauko peke yako wakati unapofundisha, kwani “sio wewe unayezungumza, bali ni Roho Mtakatifu” (Marko 13:11).

Roho Mtakatifu ni mwalimu wa kweli. Hakuna mwalimu mwenye mwili wenye kufa, hata kama ana ujuzi na uzoefu kiasi gani, anayeweza kuchukua nafasi Yake katika kushuhudia juu ya ukweli, kushuhudia juu ya Yesu Kristo, na kuibadilisha mioyo. Lakini walimu wote wanaweza kuwa vyombo katika kuwasaidia watoto wa Mungu wajifunze kupitia Roho.

Fundisha kupitia Roho

  • Jiandae mwenyewe Kiroho.

  • Daima kuwa tayari kuitikia misukumo ya kiroho kuhusu mahitaji ya wanafunzi.

  • Tengeneza mazingira na fursa kwa ajili ya wanafunzi kufundishwa na Roho Mtakatifu.

  • Wasaidie wanafunzi watafute, watambue na watendee kazi ufunuo binafsi.

  • Shuhudia kila mara, na kuwaalika wanafunzi kushiriki hisia zao, uzoefu wao na shuhuda zao.

Mwokozi Yeye Mwenyewe Alijiandaa Kiroho ili Kufundisha

Ili kujiandaa kwa ajili ya huduma Yake, Mwokozi alitumia siku 40 nyikani “ili kuwa na Mungu” (Tafsiri ya Joseph Smith, Mathayo 4:1 [katika Mathayo 4:1, tanbihi b]). Lakini maandalizi Yake ya kiroho yalianza kitambo kabla. Shetani alipomjaribu, Yeye alikuwa na uwezo wa kuvuta kutoka kwenye “maneno ya uzima” ambayo alikuwa ameyaweka kwenye hazina kwa ajili ya “saa ile” ambapo angeyahitaji (Mafundisho na Maagano 84:85). Fikiria kuhusu jitihada zako mwenyewe za kujiandaa kiroho ili kufundisha. Je, unajifunza nini kutoka Mathayo 4:1–11 kuhusu jinsi unavyoweza kufuata mfano wa Mwokozi katika maandalizi yako ya kiroho?

Roho ni mwalimu halisi na chanzo cha kweli cha uongofu. Ufundishaji injili wenye nguvu hauhitaji tu kuandaa somo bali pia kujiandaa mwenyewe kiroho kabla hujaanza kufundisha. Kama umejiandaa kiroho, utakuwa mwenye kuweza vyema kusikiliza na kufuata mwongozo wa Roho pale unapofundisha. Njia ya kumwalika Roho Mtakatifu katika ufundishaji wako ni kumwalika Yeye katika maisha yako. Hii inajumuisha kujitahidi kufuata mfano wa Mwokozi na kuishi injili Yake kwa moyo wako wote. Na kwa kuwa hakuna yeyote kati yetu anayefanya hili kikamilifu, inamaanisha pia kutubu kila siku.

Maswali ya Kutafakari: Inamaanisha nini kwako wewe kujiandaa mwenyewe kiroho ili kufundisha? Unahisi kushawishika kufanya nini ili kuboresha namna unavyojiandaa kiroho? Ni kwa jinsi gani unadhani maandalizi ya kiroho yanaweza kuleta tofauti katika ufundishaji wako?

Kutoka kwenye maandiko: Ezra 7:10; Luka 6:12; Alma 17:2–3, 9; Mafundisho na Maagano 11:21; 42:13–14

Mwokozi Daima Alikuwa Tayari Kuitikia Mahitaji ya Wengine

Yairo, mtawala wa sinagogi, alianguka miguuni pa Yesu, akimwomba amsaidie binti yake aliyekuwa mahututi. Yesu na wanafunzi Wake walikuwa wakitembea kwa shida kupita mitaa iliyojaa watu kuelekea nyumbani kwa Yairo wakati ghafla Yesu aliposimama. “Nani aliyenigusa?” Aliwauliza. Lilionekana kama swali lisilo la msingi—katika umati mkubwa wa watu, ni nani ambaye hakuwa anamgusa? Lakini Yesu alitambua kwamba katika umati ule, kuna mtu alikuwa amemwendea akiwa na hitaji maalumu na akiwa na imani ya kupokea uponyaji ambao Yeye ndiye aliutoa. Bado kungekuwa na muda wa kumtembelea binti wa Yairo. Lakini kwanza alizungumza na yule mwanamke ambaye alikuwa amegusa mavazi Yake, “Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani” (ona Luka 8:41–48).

Kama mwalimu, unaweza wakati mwingine kujikuta kwenye haraka ya kukamilisha kitu fulani ulichojiandaa kufundisha. Wakati hilo laweza kuwa muhimu, hakikisha kwamba katika hiyo haraka yako, wewe pasipo kukusudia hupiti hitaji muhimu la mtu unayemfundisha. Katika ziada ya mwongozo wa kiroho uliotafuta ulipokuwa ukijiandaa kufundisha, tafuta pia kuongozwa na Roho wakati ukiwa unafundisha. Jaribu kuwa mwenye ufahamu wa mahitaji, maswali, na mapendeleo ya wanafunzi. Roho Mtakatifu anaweza kukusaidia utambue jinsi mwanafunzi anavyopokea au kuelewa kitu ulichofundisha. Yeye anaweza kukupa msukumo, nyakati zingine, wa kubadilisha mipango yako. Kwa mfano, unaweza kuvutiwa kutumia muda zaidi kuliko ulivyokusudia kwenye mada au kuacha baadhi ya majadiliano kwa ajili ya baadaye ili kukipa kipaumbele kitu ambacho kina umuhimu zaidi kwa wanafunzi sasa.

Maswali ya Kutafakari: Ni lini ulihisi kwamba mzazi au mwalimu mwingine alijua juu ya mahitaji yako kama mwanafunzi? Je, wale unaowafundisha wanajua kwamba wewe unavutiwa zaidi katika kujifunza kwao kuliko kukamilisha somo? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwasiliana nao vyema kuhusu kuvutiwa kwako?

Kutoka kwenye Maandiko: 1 Petro 3:15; Alma 32:1–9; 40:1; 41:1; 42:1

Mwokozi Alitoa Fursa kwa Watu ili Wafundishwe na Roho Mtakatifu

Ilikuwa vigumu kwa wengi katika wakati wa Yesu kuelewa Yeye alikuwa nani hasa, lakini kulikuwa na maoni mengi. “Wengine wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji,” Wanafunzi Wake waliarifu, “wengine, Elia; na wengine, Yeremia, au mmoja wa manabii.” Lakini kisha Yesu aliuliza swali ambalo liliwaalika wanafunzi Wake waweke kando maoni ya watu wengine na kutazama ndani ya mioyo yao wenyewe: “Ninyi mwasema Mimi ni nani? Yeye aliwataka watafute majibu yao siyo kutoka “nyama na damu” bali moja kwa moja kutoka kwa “Baba yangu aliye mbinguni”. Ilikuwa aina hii ya ushuhuda—ufunuo binafsi kutoka kwa Roho Mtakatifu—ambao ulimwezesha Petro kutamka, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” (ona Mathayo 16:13–17).

Ili kunusurika kiroho katika siku za mwisho, watu unaowafundisha wanahitaji ushahidi wa kiroho juu ya ukweli. Huwezi kuwapatia wewe, lakini unaweza kuwaalika, kuwatia moyo, kuwashawishi, na kuwafundisha kuutafuta. Unaweza kuweka wazi—kupitia maneno yako na matendo—jinsi gani Roho Mtakatifu alivyo muhimu katika kujifunza injili. Zingatia, kwa mfano, mazingira ya kujifunza ambayo wewe unayatengeneza na kuyahimiza. Kitu rahisi kama upangaji wa viti katika chumba au jinsi unavyosalimiana na kuchangamana pamoja na wanafunzi inaweka toni ya kiroho kwa ajili ya uzoefu watakaoupata wanafunzi. Unaweza pia kuwaalika wanafunzi wajiandae wenyewe kiroho ili kujifunza, kama vile wewe unavyojiandaa kiroho kufundisha. Waombe wawajibike kwa ajili ya roho wanayemleta darasani. Na wewe unaweza kutoa fursa kwao wamhisi Roho akishuhudia juu ya Yesu Kristo na injili Yake. Ushuhuda huo utakuja kuwa “mwamba” kwao, na “malango ya kuzimu haitawashinda [wao]” (Mathayo 16:18).

Maswali ya Kutafakari: Je, umegundua nini ambacho kinachangia mazingira ya kiroho kwa ajili ya kujifunza injili? Ni nini kinavuruga? Ni kitu gani kinawasaidia watu unaowafundisha wajifunze kutoka kwa Roho? Fikiria kuhusu mazingira ambayo kwayo mara nyingi unafundisha. Unahisi vipi unapokuwa hapo? Ni kwa jinsi gani unaweza kwa tija zaidi kumwalika Roho awepo hapo?

Kutoka kwenye Maandiko: Luka 24:31–32; Yohana 14:26; 16:13–15; Moroni 10:4–5; Mafundisho na Maagano 42:16–17; 50:13–24

wamisionari wakiifundisha familia

Tunapofundisha, tunaweza kuwaalika wanafunzi watafute ushuhuda wao wa kiroho juu ya ukweli.

Mwokozi Aliwasaidia Wengine Watafute, Watambue na Watendee Kazi Ufunuo Binafsi

Bwana anataka kuwasiliana na sisi—na anataka tujue kwamba Yeye anawasiliana na sisi. Katika mwaka 1829, mwalimu wa shule mwenye umri wa miaka 22 aliyeitwa Oliver Cowdery alikuwa akijifunza kuhusu mafundisho thabiti, ya kusisimua kwamba mtu yeyote anaweza kupokea ufunuo binafsi. Lakini alikuwa na maswali sawa na yale ambayo wengi wetu tumejiuliza: “Je, Bwana hakika anajaribu kuzungumza na mimi? Na, ninawezaje kujua kile Yeye anachokisema?” Ili kujibu maswali haya, Yesu Kristo alimwalika Oliver Cowdery kufikiria nyuma wakati alipokuwa na maswali ya udadisi wa kiroho. “Je, sikusema amani akilini mwako kuhusiana na jambo hili?” Yeye aliuliza (ona Mafundisho na Maagano 6:21–24. Baadaye, Yeye alimfundisha Oliver kuhusu njia zingine ambazo kupitia kwazo Roho anaweza kusema naye (ona Mafundisho na Maagano 8:2–3; 9:7–9; ona pia Mafundisho na Maagano 11:12–14).

Kuishi katika ulimwengu ambao mara nyingi hautambui mambo ya kiroho, sisi sote tunahitaji msaada wa kuitambua sauti ya Roho. Yawezekana tumewahi kumsikia Roho pasipo sisi kumtambua. Na sote tunaweza kujifunza zaidi kuhusu jinsi ya kumtafuta Roho, kutambua ushawishi Wake, na kutendea kazi misukumo Yake anayotupatia. Unapofundisha, wasaidie wanafunzi wagundue njia ambazo kupitia kwazo Roho anaweza kuwasiliana—na jinsi ambavyo Yeye amewasiliana nao. Moja ya zawadi kubwa zaidi unayoweza kutoa kama mwalimu ni kuwasaidia wale unaowafundisha wapige hatua katika safari hii ya maisha yote ya utafutaji wa ufunuo binafsi.

Maswali ya Kutafakari: Kwa nini ni muhimu kujifunza kupokea ufunuo binafsi? Je, kuna mtu yeyote amekusaidia uelewe jinsi ya kutafuta na kutambua ufunuo? Unawezaje kuwahimiza wale unaowafundisha watafute, watambue na watendee kazi ufunuo kutoka kwa Roho Mtakatifu?

Kutoka kwenye Maandiko: Wagalatia 5:22–23; Alma 5:45–47; Mafundisho na Maagano 42:61; 121:33; Joseph Smith—Historia ya 1:8–20

Mwokozi Alitoa Ushuhuda kwa Wale Aliowafundisha

Katika wakati mahususi sana wa kufundisha na kuhudumu, Yesu alitafuta kumfariji rafiki Yake aitwaye Martha, ambaye kaka yake alikuwa amefariki. Alishiriki naye ushuhuda rahisi juu ya ukweli wa milele: “Ndugu yako atafufuka” (Yohana 11:23). Ushuhuda Wake ulimsukuma Martha naye kutoa ushuhuda wake mwenyewe: “Ninajua kwamba atafufuka katika siku ya mwisho” (Yohana 11:24). Angalia jinsi mpangilio huu unavyojirudia katika Yohana 11:25–27. Nini kinakuvutia kuhusu mfano wa Mwokozi? Kwa nini kushiriki ushuhuda juu ya kweli za injili ni sehemu muhimu ya kufundisha?

Ushuhuda wako unaweza kuwa na ushawishi wenye nguvu kwa wale unaowafundisha. Hauhitaji kuwa wa ufasaha wa lugha au mrefu. Na hauhitaji kuanza na “Ningependa kutoa ushuhuda wangu.” Kwa urahisi kabisa shiriki kile unachokijua kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Ushuhuda juu ya ukweli unakuwa na nguvu zaidi unapokuwa wa moja kwa moja na wa kutoka moyoni. Toa ushuhuda mara kwa mara juu ya Mwokozi, injili Yake, na nguvu Yake katika maisha yako, na wahimize wale unaowafundisha wafanye vivyo hivyo. Na kumbuka kwamba wakati mwingine ushuhuda wenye nguvu zaidi hautolewi na mwalimu bali mwanafunzi mwenzao.

Maswali ya Kutafakari: Tafuta mifano katika maandiko ambayo inafafanua ushawishi wenye nguvu wa mtu anayetoa ushuhuda. Je, unajifunza nini kutoka katika mifano hiyo? Je, ni lini umebarikiwa kutokana na ushuhuda wa mtu fulani? Ni kwa jinsi gani kushiriki ushuhuda wako kuliwashawishi wale unaowafundisha? Ni kwa jinsi gani kulikushawishi wewe?

Kutoka kwenye Maandiko: Matendo ya Mitume 2:32–38; Mosia 5:1–3; Alma 5:45–48; 18:24–42; 22:12–18; Mafundisho na Maagano 46:13–14; 62:3

Baadhi ya Njia za Kutumia Kile Unachojifunza

  • Waombe wanafunzi washiriki kile Roho Mtakatifu alichowafundisha walipokuwa wakijifunza neno la Mungu.

  • Jiandae mapema kupokea misukumo ya kiroho wakati ukifundisha.

  • Andika misukumo ya kiroho inayokujia wakati unapojiandaa.

  • Toa fursa za mara kwa mara kwa washiriki wa darasa kukaa kimya huku wakitafakari kile Roho anachowafundisha.

  • Tumia muziki mtakatifu na picha ili kualika ushawishi wa Roho.

  • Sikiliza misukumo wakati unapopanga na unapofundisha, na uwe tayari kurekebisha mipango yako.

  • Toa fursa kwa wanafunzi wote kutoa ushuhuda wao juu ya kile wanachojifunza.

  • Wasaidie wengine watambue wakati Roho anapokuwepo.

  • Ishi kweli unazozifundisha ili kwamba uweze kuzitolea ushuhuda.

  • Fuata misukumo ya kufundisha katika nyakati zinazojitokeza zenyewe, na zisizo rasmi.